Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi ili kwa uchache kabisa niweze kuchangia katika hoja ambayo ipo mbele yetu, hoja ambayo ni hotuba ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, sambamba na hotuba ya Bajeti ya Wizara ya TAMISEMI.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, ninaomba kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha na kuniwezesha kusimama siku ya leo kwa mara nyingine kwa ajili ya kuleta sauti ya Wanajimbo la Segerea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ninayo pia historia ambayo ningependa kuieleza ndani ya Bunge hili Tukufu. Kwa mara ya kwanza kabisa katika maisha yangu jana nimeweza kushiriki katika mbio za Mwenge ndani ya Jimbo langu la Segerea na nimekesha mpaka asubuhi, niseme nimejifunza mengi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa moja kwa moja niungane pamoja na Waheshimiwa Wabunge wengine ambao wameweza kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa yale ambayo anayafanya yeye kama Rais, ambayo yanaonekana kuwa na tija kwa maslahi mapana ya wananchi wote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niweze pia kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na hotuba yake nzuri, lakini nikiri kama Mbunge kwamba ameanza vizuri. Tumemwona akifanya ziara za hapa na pale, ziara ambazo kwa namna moja ama nyingine zimeleta faraja kubwa sana kutoka kwa wananchi wakiamini kwamba sasa wanaweza kupata faraja na tabasamu lile ambalo Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amewaahidi kuwapatia Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa baada ya hapo kwa harakaharaka nimpongeze Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI, niwapongeze sana Manaibu wote kwa maana ya Naibu unaye-deal na masuala ya elimu na afya na Manaibu wote waliopo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, hakika wanafanya kazi nzuri sana ambayo kwa kweli wanapaswa kupongezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Mama Samia Suluhu Hassan, anafanya kampeni zake, alisema na aliwaambia Watanzania kwamba pale atakapokuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, zipo changamoto ambazo ndani ya siku 100 atakwenda kusimama kuhakikisha kwamba anatatua ili kuleta faraja na tabasamu kwa Watanzania. Pamoja na mengi aliyoyaahidi alisema moja kwa moja kwamba ndani ya siku 100 atakwenda kuhakikisha anamtua mwanamke ndoo kichwani. Wote tunafahamu dhana ya Mheshimiwa Rais, ya kumtua mwanamke ndoo kichwani haijaanza leo imeanza kipindi akiwa ni Makamu wa Rais.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awamu hii alisema kwamba ataenda kuweka nguvu sana kuhakikisha kila mwanamke wa kitanzania habebi tena ndoo kichwani bali maji yanamkuta ndani ya nyumba yake. Wakati Waheshimiwa Wabunge wengine wakiwa wanalalamika na kusema kwamba katika majimbo yao wanapata maji kwa mgao, ninaomba nimwambie Waziri, ndani ya Jimbo la Segerea hatulilii mgao kabisa, tunalilia upatikanaji wa maji safi na salama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Wabunge wengine wanasema kwamba wanapata maji mara mbili kwa wiki, ninaomba nikwambie kwamba ndani ya Jimbo la Segerea kuna wananchi ambao mpaka hivi ninavyoongea wana miezi sita hawajaona maji safi na salama, lakini kuna wananchi wengine ni miezi 10 hawajaona tone la maji katika mabomba yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, haya ninayoyaongea mbele ya Bunge lako Tukufu, Mheshimiwa Waziri wa Maji Aweso, atakuwa ni shahidi kwamba hiki ninachokisema ni ukweli mtupu na Mwenyezi Mungu anafahamu kwa sababu yeye mwenyewe ambaye amebeba ndoto za Mheshimiwa Rais, za kumtua mwanamke ndoo kichwani, ameiona hiyo changamoto ndani ya Jimbo la Segerea na alikuja mwenyewe kuweka kambi ndani ya Jimbo la Segerea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri alijionea kwa macho, alisikia kwa masiko na akaelekeza kwamba, DAWASA iweze kuweka kambi ndani ya Jimbo la Segerea kwa sababu kero ya maji ndani ya Jimbo la Segerea imekuwa ni kubwa ukilinganisha na maeneo mengine. Kwenye hili ninaomba nimpongeze Mheshimiwa Waziri Aweso, ni kwa bahati mbaya sana simwoni, lakini amefanya kazi kubwa sana. Mheshimiwa Aweso, akisikia sehemu yoyote kuna changamoto ya maji hata kama jambo hilo lipo nje ya uwezo wake kwa wakati huo atafika kusikiliza na atatoa mwelekeo. Ninaomba nimpongeze sana Mheshimiwa Aweso lakini niwapongeze watendaji wote wa DAWASA, engineer Bwire na mameneja wote ambao wapo ndani ya kanda hii ya Jimbo la Segerea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeanza kwa kuelezea hiyo tathmini ili kuweka kumbukumbu sawa kwamba ndani ya Jimbo la Segerea wananchi wanalia na wana kiu wanahitaji maji safi na salama, kwa sababu Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliwaahidi kuwatua ndoo kichwani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa harakaharaka nina ombi kwa upande huu wa maji. Kutokana na hali ilivyo kwa sasa, uzalishaji wa maji imekuwa ni changamoto kubwa sana na majuzi hapa nimemwona Mheshimiwa Waziri, akiwa kule China akifuatilia pump kwa ajili ya kuja kuzifunga ili kuhakikisha uzalishaji wa maji na usukumaji unakuwa na nafuu kubwa sana na hivyo wananchi kuweza kupata maji safi na salama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa taarifa nilizonazo, pump nne tayari zimewasili ndani ya Nchi yetu ya Tanzania, ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam. Ombi langu pamoja na kazi nzuri hiyo, niwaombe Mheshimiwa Waziri na niseme nipo chini ya miguu yao kwa niaba ya Wanajimbo la Segerea, zile pump nne wanazosema kwamba zikifungwa zitakwenda kuleta nafuu kwa wananchi wa Dar es Salaam na hususan Jimbo la Segerea niwaombeni chonde chonde ziende zikafungwe ili akinamama wa Jimbo la Segerea wasiweze kubeba ndoo kichwani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sambamba na hilo nina ombi. Kuna ufumbuzi mwingine wakati mwingine unaweza ukawa wa dharura na mwingine ukawa ni wa muda mrefu. Ndani ya Jimbo la Segerea ukosekanaji wa maji safi na salama kwa sababu ni kilio kikubwa sana, ninaomba kwamba Mheshimiwa Waziri akubali kuja kutuchimbia visima vya kisasa virefu ndani ya kata zote 13. Kwa kuwa kazi hii wameshakwishaanza ndani ya kata mbili; Kata ya Kisukulu na Kata ya Segerea, ambao hawajapata maji zaidi ya miezi sita, niwaombe na nimwombe Mheshimiwa Waziri aje akatuchimbie visima kwenye kila kata wakati tunasubiri miradi mikubwa ambayo hatuna uhakika kwamba ni lini itakwenda kukamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo ninaomba niende moja kwa moja katika suala zima la TARURA kwa maana ya barabara. Wakati Wabunge wenzangu wanasema kwamba wanahitaji barabara za kuunganisha kutoka jimbo moja kwenda jimbo lingine, kutoka kata moja kwenda kata nyingine. Ninaomba nimwambie Waziri, ndani ya Jimbo la Segerea lenye mitaa 61, mitaa yote 61, hakuna mtaa hata mmoja unaopitika ndani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi tunavyoongea maeneo mengi yamefungwa, njia hazipitiki kabisa, ni barabara zote kiasi kwamba ninashindwa hata kukutajia kwamba ni barabara ipi na ipi ambayo ina changamoto kubwa zaidi. Kwa sababu nikianza kutaja barabara moja baada ya nyingine nitakuwa ninajichonganisha mwenyewe na wananchi wa Jimbo la Segerea, kwa sababu wanafahamu mitaa yote 61 haipitiki kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona katika hotuba hii ya TAMISEMI, bajeti imeongezeka ya TARURA imekuwa sasa shilingi trilioni 1.2 na wameelezea katika hotuba yao, wamesema kwa sasa hawana madeni kabisa kwa wakandarasi. Ombi langu Mheshimiwa Waziri, ninajua ni msikivu, chonde chonde hii fedha shilingi trilioni 1.2 ielekezwe kwenye majimbo ambayo njia hazipitiki kabisa. Mfano, nimwambie ndani ya jimbo langu tumepoteza watoto watatu kwa sababu mvua iliponyesha mafuriko yamekuwa ni mengi wameondoka na maji Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kata ya Kimanga tumezika mtoto mdogo, Kata ya Kinyerezi watoto wawili. Mheshimiwa Waziri, nimwombe chonde chonde hii shilingi trilioni 1.2 ielekezwe kwenye majimbo ambayo changamoto yake ni kubwa, ninamwomba aanze na Jimbo la Segerea. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Mheshimiwa....
MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Mwenyekiti...
MWENYEKITI: Mheshimiwa muda wako umekwisha.
MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nimalizie.
MWENYEKITI: Malizia kwa haraka, wind up.
MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati namalizia kwenye Kata ya Kipawa katika Mtaa wa Kipunguni; kuna wananchi waliopisha ujenzi wa airport mpaka leo ninavyoongea hawajalipwa fidia, wanaishi katika mazingira magumu, hata huduma za kijamii hawazipati kwa sababu mazingira ni mabaya, ni mabaya. Ninaomba kwa haraka niseme kama ifuatavyo...
MWENYEKITI: Aaah! Usianze kutaja majina, Waziri ameshasikia compensation, malizia bila ya kwenda kwenye list.
MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Jambo la mwisho sasa ni kuhusiana na stahiki za Waheshimiwa Madiwani pamoja na Wenyeviti wa Serikali za Mitaa. Kwa dakika moja ninaomba niseme, Waheshimiwa Wabunge, wote wanafahamu wakati mimi ni Mbunge wa Viti Maalum sikujua kama kuwa Diwani ni kazi kubwa sana na kuwa Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa ni kazi kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe, Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI, aangalie namna ya kuwasaidia hawa Madiwani, Diwani kulipwa shilingi 350,000 halafu unampelekea mradi wa mabilioni na mamilioni ukiamini atausimamia wakati ana njaa kali, haiwezekani kabisa Mheshimiwa Waziri...
MWENYEKITI: Haya, ahsante.
MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, wenyeviti wa Serikali za Mitaa wanapewa shilingi 100,000 kwa mwezi Mheshimiwa Waziri, hii siyo sawa...
MWENYEKITI: Ahsante...
MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, na haiendani na kauli ya Mheshimiwa Rais, anayosema: “Utu na Kazi, Tunasonga Mbele”, utu utangulizwe kwa Wenyeviti wetu pamoja na Waheshimiwa Madiwani...
MWENYEKITI: Haya, shukuru....
MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)