Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tanga Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. KASSIMU A. MBARAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, shukrani sana kwa kupata fursa hii ya kuchangia katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa siku hii ya leo. Jambo kubwa la msingi zaidi, ninamshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutujaalia sote kuwepo hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawapongeza Waheshimiwa Wabunge wote kwa michango yao mizuri waliyoiwasilisha hapa Bungeni kwenye hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, michango yenye kujenga, kuonyesha mwelekezo na kutoa njia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuchangia kuna machache ambayo nimeyaona nikasema nichangie ili hatimaye niweze kuunga mkono hoja juu ya hotuba hii. Jambo la kwanza ni kuhusiana na mikopo ya 10%. Kwanza tuipongeze Serikali kwa kutoa mikopo hii kwa muda mrefu sana ya 10% kwa makundi ya vijana, akina mama na walemavu. Ni jambo kubwa na jambo zuri sana. Tukiangalia kwa muhtasari na muktadha tulionao sasa na kule tunakokwenda, tunahitaji kufikiria upya suala hili la mikopo ya 10%, hususan kwa kundi la vijana (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa muda mrefu sana vijana wamekuwa wakipata asilimia nne kwenye mikopo hii ya 10%. Sasa, tunatakiwa tubadili fikra kwa kule tunakokwenda. Idadi ya vijana sasa hivi ndani ya nchi yetu ni kati ya 60% hadi 70%. Ukiangalia katika taasisi mbalimbali za fedha utabaini kuwa kuna programu nyingi sana za uwezeshaji za mikopo ya akina mama, au tuseme wanawake; lakini kundi hili la vijana limeachwa nyuma kwa namna moja ama nyingine, liko kwenye mikopo hii ya 10% ambao wanaambulia asilimia nne. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa, ninaomba tubadili fikra na mtazamo kwa kushauri kwamba, tuanze kufikiria kuwa na Benki ya Maendeleo ya Vijana ndani ya Taifa hili la Tanzania. Vijana hawa 60% hadi 70%, ambayo ndiyo idadi ya population ya Tanzania ni muhimu sana kuwalea, kuwajengea uwezo kwa sababu hawa ndiyo mabilionea na wawekezaji wa kesho ndani ya Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa harahaharaka ukiangalia utaona kuna takribani milioni moja ya vijana au tunazungumzia rural-urban migration. Kila mwaka nguvu kazi inatoka vijijini inakuja mjini, lakini wakati huo huo kuna wanaohitimu shuleni na ambao wamefikia umri wa kuajiriwa takribani nao milioni moja. Yaani wako tayari kuingia kwenye soko la ajira. Hawa wote tunawapeleka wapi? Hatuwezi kuwaajiri wote, lazima tuwe na benki itakayowalea. Isiwe benki kama benki zilivyo za sasa hivi, iwe benki ya ulezi katika kusimamia startups za hawa vijana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitatoa mfano mdogo, kijana ana andiko mradi zuri, ana wazo zuri, anapokwenda kwenye financial institution yoyote leo hii atahitajika collateral. Amehitimu chuo huyu kijana, hana collateral yoyote ataweza kuanzia wapi? Jambo kubwa na la msingi zaidi linalohitajika kufikiriwa upya, benki hiyo ianzishwe, ikishaanzishwa ifanye kazi ya kushirikiana na hawa vijana katika ufanyaji wa biashara. Haya yatasaidia vijana na itaweza kuwajengea uwezo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesikia pia suala zima la matumizi ya vyeti wanapohitimu, viweze kutumika kuweza kuwapatia fedha. Sasa, idadi kubwa hii ya vijana tusipoitengenezea mazingira mazuri leo, kesho yao itakuwa ngumu na inaweza ikawa bomu la Taifa. Kwa hiyo ninaomba sana, katika hoja hizi zilizotolewa, ushauri wangu Serikali ianze kufikiria upya sasa kuleta Benki ya Maendeleo ya Vijana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuanzisha Wizara ya Vijana. Wizara hii ya Vijana imeanzishwa imetengewa takribani shilingi bilioni 200 ziko pale. Leo tungekuwa na benki ya maendeleo ya vijana fedha hizi zote zingewekwa pale, za kwenye kilimo kama kuna zinazowahusu vijana zingewekwa pale, asilimia nne za halmashauri zingewekwa kwenye Benki ya Maendeleo ya Vijana. Hatimaye vijana wa Taifa hili wakanufaika na wakaweza kujiajiri na kuja kutengeneza ajira nyingi kwa hapo baadaye. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nukta nyingine ya msingi ninayotaka kuchangia ni kuhusiana na suala zima la sekta binafsi. Sekta binafsi imekuwa ikifanya vizuri sana ndani ya nchi yetu na imekuwa ikichangia sana maendeleo ya nchi yetu na pato letu la Taifa, lakini yapo mambo ya msingi ambayo tunahitaji kuyaangalia kwa upana na kwa sura ambayo ni nzuri zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwa kiwango gani Watanzania wanaofanya kwenye sekta binafsi wananufaika, ambapo kundi kubwa bado ukienda huko ni vijana? Tarehe 13 Oktoba, 2025 Wizara ya Utumishi wa Umma ilitoa tangazo la kuongezeka kwa kima cha mshahara katika sekta binafsi, lakini ukiangalia kwa harakaharaka ukifuatilia mchanganuo uliowekwa kwenye lile Gazeti la Serikali, tangazo lile lililosainiwa na Mheshimiwa Waziri wa Utumishi wa Umma, ukipitia na ukiangalia hali halisi ilivyo huoni utekelezaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niishauri Serikali, sekta binafsi wakati inakua na maisha ya watu wanaofanya kazi ndani ya sekta binafsi, basi tuhakikishe nayo yanakua na mishahara ile iliyotangazwa kuongezeka ifuatiliwe iongezeke. Nitatoa mfano katika hili; Bandari ya Tanga kumefanyika uwekezaji mkubwa takribani shilingi bilioni 423, lakini kwa muda wa miaka 10 vibarua walioajiriwa pale kuna kampuni zimechukua tender ndani ya TPA (Tanzania Ports Authority).
Mheshimiwa Mwenyekiti, zile kampuni baada ya kuchukua tender kwa muda wa miaka 10, vijana wale wanalipwa kati ya shilingi 9,500 mpaka 11,000 na wapo vijana takribani 17,000. Tangazo la Serikali limetoka, TPA inazilipa zile kampuni vizuri kabisa, wale watu wanachelewesha mishahara kwa wale vijana, lakini mwisho wa siku kilichokuwepo ni kwamba mpaka leo wale vijana bado hawajaongezewa mishahara wala hawajaongezewa ujira wao kwenye vibarua. Hii ni changamoto wakati maelekezo ya Serikali yametoka na yametolewa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mawaziri wetu wanafanya kazi kubwa nzuri sana. Katika hili ninaomba waamke, wapite kwenye viwanda na kwenye sekta mbalimbali za binafsi waangalie maelekezo yaliyotolewa kutoka kwa Waziri wa Utumishi wa Umma, je, yanatekelezeka ili hali za maisha ya wananchi wetu yazidi kustawi na kuboreka? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nukta nyingine ya msingi ninayotaka kuchangia ni sehemu ya uvuvi. Niipongeze Serikali kwa kutoa boti na kuwasaidia wavuvi hususan watu wa ukanda wa bahari na sehemu ya maziwa; wanafanya kazi nzuri sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, ninataka niliambie Bunge hili Tukufu, zaidi ya 80% ya uvuvi wa Tanzania ni traditional. Boti zilizopelekwa kule ni modern: boti zimepelekwa zina rangi nyeupe, wavuvi wanaenda kuvua usiku baharini wana karabai zao, kunatokea reflection ya light samaki wanatawanyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi watu wa Pwani, unapoenda kuvua basi unapaka lile dau lako au mashua yako inaitwa sifa, iwe na rangi nyeusi kama rangi ya lami ili itengeneze kiza samaki wakusanyike karibu kwenye mwanga ili mwisho wa siku upate samaki wa kutosha ili mambo yaweze kwenda vizuri. Matokeo yake boti zile zimepelekwa, watu wanafukuzana na waliopewa boti kwa ajili ya marejesho, kumbe ukiangalia watu wameshindwa ku-consider point moja kwamba, uvuvi wetu 80% ni traditional, tunawapelekea vifaa ni modern. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashauri katika hili ikiwezekana Wizara husika ikae na wavuvi kwanza iangalie modality kwenye maeneo yao husika ni aina gani ya boti wanazozihitaji kuliko kutumia gharama kubwa ya pesa na kuleta boti ambazo kwa namna moja ama nyingine mwisho wa siku zinakuwa hazina tija kwa wavuvi kulingana na ile sekta ya uvuvi jinsi ilivyo. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante sana.
MHE. KASSIMU A. MBARAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuzungumza haya, ninaunga mkono hoja. Shukrani sana. (Makofi)