Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. GRACE E. MKOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii katika Bunge lako Tukufu ili nichangie hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Kwa kuanza ninaomba nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa nafasi hii, kwa kunifikisha siku ya leo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba pia nichukue nafasi hii kumpongeza na kumshukuru sana Mwenyekiti wetu wa Chama Cha Mapinduzi, Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan kwa kura nyingi ambazo alizipata na zimepelekea Chama Cha Mapinduzi kuwa na Wabunge wengi katika Bunge hili Tukufu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nichukue nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutuona sisi watu wa Singida; kwa maana ya kutuchagulia au kumteua Waziri Mkuu Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba ambaye anatokea Mkoa wa Singida. Tunashukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutuamini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachukua nafasi hii pia kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kuaminiwa na Mama Samia Suluhu Hassan. Sisi wananchi wa Singida tunampongeza sana. Tunamwombea kwa Mungu aendelee kuchapa kazi, Wanasingida tunamwamini, lakini na Taifa la Tanzania linamwamini; aendelee kuchapa kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nichukue nafasi hii pia kumshukuru mama yetu mlezi wetu wa UWT, Mama Mary Chatanda. Ametulea vizuri wanawake wa UWT na ametuweka pamoja na wanawake wote tumekuwa na umoja. Ninaomba nichukue nafasi hii kuwashukuru sana wanawake wa Mkoa wa Singida ambao wao sasa walinichagua kwa kura nyingi na wamesababisha mimi kuwepo kwenye Bunge hili Tukufu kwa ajili ya kuwawakilisha. Ninawaahidi kwamba nitawawakilisha vyema na kwa weledi mkubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaipongeza sana Serikali kwa kazi nyingi ambazo inazifanya, pia kwa kuleta fedha nyingi katika Mkoa wetu wa Singida na kusababisha miradi mingi kutekelezeka; ninaipongeza sana Serikali yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kuleta fedha nyingi hizo, bado katika Mkoa wetu wa Singida kuna changamoto nyingi sana. Ninaiomba Serikali, kwa mfano kwenye suala la barabara; ninaona kila Mbunge akisimiama hapa analalamikia habari ya barabara. Vilevile, kila Mbunge akisimama hapa analalamikia maji na kila Mbunge akisimama hapa analalamika kuhusu elimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nichukue nafasi hii kutaja changamoto mbalimbali ambazo ziko katika Mkoa wangu wa Singida, hasa nikianza katika barabara. Katika Mkoa wetu wa Singida, hasa katika Wilaya ya Iramba, tuna changamoto kubwa sana ya barabara. Tuna barabara inayoanzia katika Kijiji cha Misigiri. Barabara hiyo inapita Ndago inaenda mpaka Singida Mjini. Barabara hiyo inaunganisha wilaya tatu za Mkoa wetu wa Singida. Barabara hiyo ni muhimu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hiyo imeanza kujengwa tangu miaka miwili iliyopita, lakini bado inasuasua; mpaka sasa barabara hiyo haijakamilika. Ninaiomba Serikali itusaidie kuikamilisha barabara hiyo ya Mkoa wa Singida ambayo inaunganisha wilaya tatu; iwasaidie wananchi wa Mkoa wa Singida ili sasa na wao waweze kufaidika na barabara hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mikoa yetu iliyoko Tanzania Mkoa wa Singida ni moja ya mikoa kongwe na mikoa ya zamani sana, lakini mpaka hivi sasa ninavyozungumza katika Mkoa wa Singida hatuna chuo kikuu. Ninaiomba Serikali itusaidie kutujengea chuo kikuu katika Mkoa wetu wa Singida; ukizingatia kwamba population ya Mkoa wa Singida sasa inakuwa kubwa, ili sasa na sisi wananchi wa Mkoa wa Singida tuendelee kunufaika na chuo kikuu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna changmoto nyingine kubwa sana ambayo inafanya wanawake wa Mkoa wa Singida kukosa amani na hata familia sasa zinakuwa na manung’uniko. Changamoto hiyo ni maji. Katika Wilaya ya Iramba ambalo ndilo jimbo la Mheshimiwa Waziri Mkuu, katika Kitongoji cha Kiomboi tuna changamoto kubwa sana ya maji na wanawake wa wilaya hiyo hasa katika Kitongoji cha Bomani wanateseka sana. Ninaiomba Serikali itusaidie sana kututatulia changamoto hiyo ya maji ambayo imekuwa kero sana kwa wanawake wa Wilaya ya Iramba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama unavyojua, maji ndiyo uhai, maji ndiyo kila kitu, lakini katika Wilaya ya Iramba tuna changamoto kubwa sana na hiyo imekuwa kero kubwa sana kwa wanawake wa Wilaya ya Iramba. Ninaomba sana sana Serikali itusaidie kutatua changamoto hiyo ili sasa hawa wanawake waondokane na hiyo changamoto ya maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia, ninashukuru sana, ninaishukuru Serikali yangu. Ninaamini Serikali yangu ni Serikali sikivu, itaenda kusaidia kero hizi na kutatua kero hizi za watu wa Mkoa wa Singida, ili sasa watu wa Mkoa wa Singida waifurahie Serikali yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)