Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Christina Solomon Mndeme

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. CHRISTINA S. MNDEME: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii. Ninaanza kwa kumshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi, kwa kuniteua na kuruhusu mimi kugombea nafasi hii kuwawakilisha wanawake wa Mkoa wa Tabora. Kwa namna ya pekee ninawashukuru sana Wanawake wa Mkoa wa Tabora kwa kunipigia kura ya ndiyo na leo hii ninawawakilisha hapa Bungeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya pekee ninatoa pongezi nyingi sana kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kutunukiwa Shahada ya Uzamivu ya Heshima kutoka Chuo Kikuu cha Jimbo la Nasarawa Keffi kilichopo Nchini Nigeria. Shahada hiyo ya uzamivu ya heshima kwa kutambua mchango wake, kama kinara wa nishati safi ya kupikia, afya ya mama na mtoto, taswira nzuri katika masuala ya uongozi kwa wanawake Afrika na kusimamia masuala ya biashara, hususan kwa vijana wa Kiafrika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hongera sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, dunia inatambua kazi zako na uongozi wako mzuri, bora na thabiti. Tunampongeza sana Mheshimiwa Rais wetu kipenzi na chaguo la Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachukua nafasi hii vilevile kumpongeza Mheshimiwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Waziri Mkuu, Mheshimiwa Spika wa Bunge letu, Mheshimiwa Naibu Spika na Waheshimiwa Wenyeviti wa Bunge. Mwenyekiti wa Wanawake wote wa Tanzania, Mary Pius Chatanda, Makamu Mwenyekiti Zainab Shomari na vilevile Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa wote nchini, pamoja na Mkuu wangu wa Mkoa, Mheshimiwa Paulo Chacha wa Tabora. Tunawapongeza sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wakuu wa Wilaya, Maafisa Tarafa, Watendaji wa Kata, Watendaji wa Vijiji, Watendaji wa Mitaa, Waheshimiwa Madiwani, Wenyeviti wa Serikali za Mitaa na wananchi wote kwa ujumla kwa kazi kubwa wanazozifanya. Hongera sana, kwani wao wanamuunga mkono Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa vitendo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya pongezi hizi tunasema Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kazi zake anatekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi kwa vitendo. Ninachukua fursa hii tena kwa dhati ya moyo wangu kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Daktari huyu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, kwa uongozi wake mahiri na bora wa kuwatumikia wananchi wa Tanzania na dunia inashuhudia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunasema Rais huyu ana mapenzi ya dhati kwa Watanzania, ana moyo wa dhati kwa Watanzania, anafanya kazi kwa uhodari wa dhati, ili Watanzania hawa waweze kufurahia matunda ya nchi yao. Sisi sote ni mashahidi wa kazi kubwa anayofanya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuwaletea wananchi maendeleo. Tunashuhudia Tanzania ya leo, siyo Tanzania ya jana, imepiga hatua sana ya maendeleo, kila sekta imeguswa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunashuhudia kila mkoa umeguswa kimaendeleo, kila wilaya imeguswa, kila tarafa imeguswa, kila kata imeguswa, kila kijiji kimeguswa, kila mtaa umeguswa na tabasamu la mama linaonekana. Tabasamu la mama tunaliona kwenye madarasa, tabasamu la mama tunaliona kwenye vifaa vya afya, tabasamu la mama tunaliona kwenye hospitali, tabasamu la mama tunaliona kwenye barabara, tabasamu la mama tunaliona kwenye ma-culvert, tabasamu la mama tunaliona kwenye madaraja, tabasamu la mama tunaliona kwenye ruzuku ya pembejeo na tabasamu la mama tunaliona kwenye chanjo za mifugo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tabasamu la mama pia tunaliona katika ujenzi wa VETA katika kila Wilaya. Tabasamu la mama tunaliona kwenye ajira, tabasamu la mama tunaliona kwenye ujenzi wa masoko, tabasamu la mama tunaliona kwenye mikopo ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu. Tabasamu la mama tunaliona kwenye umeme, tabasamu la mama tunaliona kwenye SGR, tabasamu la mama tunaliona kwenye uchumi wa bluu, tabasamu la mama tunaliona kwenye utalii, tabasamu la mama tunaliona kila sekta; nani kama Mheshimiwa Samia? Hakuna wa mfano wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Waheshimiwa Wabunge na wananchi wote kwa ujumla tuna kila sababu ya kumwombea Mheshimiwa Rais wetu huyu, ili Mwenyezi Mungu aendelee kumpa afya njema, Mwenyezi Mungu aendelee kumpa ulinzi, Mwenyezi Mungu aendelee kumpa nguvu, ili aweze kuwatumikia Watanzania hawa. Insha Allah Mwenyezi Mungu anasikia dua na sala zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi kubwa anazozifanya za kuwafikia Watanzania. Ninamshukuru sana na kumpongeza kwa hotuba yake nzuri iliyoakisi hali halisi ya maendeleo ya Taifa letu. Hotuba yake nzuri ambayo inaakisi hali halisi ya bajeti na mpango wa maendeleo wa bajeti kwa Watanzania. Tunaliona tabasamu la mama katika hotuba yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunawapongeza pia, viongozi wote wakiwemo Waheshimiwa Mawaziri chini ya Wizara yake, kwa kazi kubwa wanayoifanya. Mheshimiwa Rais ameleta tabasamu kila sekta kupitia falsafa yake ya “Kazi na Utu, Tunasonga mbele”. Ni kwa sababu, Mheshimiwa Rais wetu anathamini kazi, Mheshimiwa Rais wetu anathamini utu na Taifa linasonga mbele. Mheshimiwa Waziri Mkuu, yeye akiwa msimamizi wa shughuli zote za Serikali, sisi tunamwombea dua. Mwenyezi Mungu akusimamie kwani tunaona kazi zako na tunazithamini sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi wewe umekuwa ukiwafikia wananchi, leo hii tunashuhudia maendeleo makubwa nchini kwetu. Sisi Wanatabora tunashuhudia Reli ya SGR kutoka Tabora – Isaka, Tabora – Kigoma inajengwa, maji kutoka Ziwa Victoria tumepata, ili kumtua mwanamke ndoo kichwani na hususan mwanamke wa Tabora. Ushauri wangu kwa Serikali ni, sisi Wanatabora tunaomba kujengewa hospitali ya kanda…

MWENYEKITI: Malizia Mheshimiwa Mndeme.

MHE. CHRISTINA S. MNDEME: …ili tuweze kusogeza huduma za afya karibu, lakini vilevile tunaomba TARURA waongezewe fedha ili wawe na fedha za kutosha na kuondoa changamoto ya barabara. Barabara zikiwa nzuri, mnufaika mkubwa ni mwanamke na mtoto. Tunaomba semina iendelee kupanuliwa wigo kwa wanawake kupitia mikopo na uwezeshaji wananchi kiuchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashauri Serikali pia kupitia TAMISEMI, iendelee kuboresha mfumo mzuri wa kuhamasisha halmashauri kujiunga na biashara ya carbon, ili Serikali ipate fedha nyingi kupitia biashara hii iweze kuzalisha credit nyingi. Biashara ya carbon siyo kupitia tu misitu, biashara ya carbon, halmashauri inaweza kupata fedha kupitia nishati safi ya kupikia, nishati mbadala, majengo endelevu, green buildings, usimamizi wa takangumu (waste management), kama ilivyo Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, kilimo himilivu (climate smart agriculture), usafiri endelevu, uhifadhi wa ardhi oevu (waste land conservation) ili sasa hamashauri zetu…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. CHRISTINA S. MNDEME: …ziweze kupata fedha, kwa ajili ya kuzalisha credit nyingi na kupata fedha nyingi…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mndeme.

MHE. CHRISTINA S. MNDEME: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na ninaunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)