Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Asha Ramadhani Baraka

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. ASHA R. BARAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza kabisa ninakushukuru kwa kunipa nafasi hii na pia ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kuwa salama na kuendelea na shughuli za Bunge kama kawaida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakishukuru Chama changu Cha Mapinduzi hususan Kamati Kuu bila kusahau UWT Taifa - Mkutano Mkuu wa UWT ambao uliniwezesha kunipa kura nyingi chini ya Mwenyekiti wetu, Mama Mary Chatanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru Raisi wetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuweza kuiongoza nchi yetu mpaka tumefikia hapa tulipo na Bunge linaweza kufanya kazi zake kama kawaida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kumpongeza Waziri Mkuu kwa ziara zake ambazo amekuwa akizifanya mikoani. Ningependa zile ziara ziendelee ambapo wananchi wengi wanatoa kero zao kwa Waziri Mkuu kwa kuonana naye hapo kwa hapo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninarudia mapendekezo ya bajeti ya hotuba ya Waziri Mkuu, ninaipongeza Serikali yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwanza kabisa ninasema Serikali yetu ambayo imejenga shule pale Kibaha DC, hii shule ni ya watoto wenye ulemavu wenye uhitaji maalum, ni shule ya primary ambayo inakwenda kwa jina la Kawawa Primary School.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kumpongeza Waziri wa TAMISEMI kwa kuhakikisha kwamba ile shule imekuwa vizuri na iko nzuri na salama kabisa; ni shule ya boarding school inategemea kuingiza watoto 495 wa boarding. Sasa niiombe Serikali, kwenye bajeti hii kumekuwa na malalamiko sana ya watu wenye uhitaji maalum. Ile shule kwa sababu ni primary school, waweze kuwekewa vifaa vya kisasa na rafiki ili waweze kufanya mafunzo yao pale. Hata ikiwezekana waongezewe na chuo cha pili cha VETA ili waweze kujifunza pale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niko hapohapo Kibaha DC, ninampongeza Waziri wa Kilimo kwa mikakati yao ambayo ameiweka na Mheshimiwa Waziri Mkuu ameichakata vizuri. Pale Kibaha DC kuna kilimo ambacho kinaanzishwa, ni kilimo cha kisasa, ni kilimo cha mbogamboga ambacho kitasaidia ajira kwa vijana wetu na wanawake. Ninaomba tu kwamba kile kilimo cha mbogamboga kinategemea kulisha Mkoa wa Dar es Salaam na Kibaha yenyewe, hususan Mkoa wa Pwani na mikoa ambayo iko karibu. Ninaomba tu kwamba waweze kupatiwa ile mikopo ya 10% bila masharti yoyote hawa akina mama pamoja na vijana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pale mbogamboga zitalisha Mkoa wa Dar es Salaam ni eka karibu 2,000 ambazo zimetengwa na Wizara ya Kilimo. Kwa hiyo, ninaomba hizi eka hizi 2,000 zigawiwe kwa uwiano, nikisema tuhakikishe kwamba vijana na wanawake wanapata na wanatengeneza hicho kilimo, kitakuwa tumenusuru ajira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaongezea jambo lingine ambalo liko chini ya taasisi zisizokuwa za Serikali. Taasisi Zisizokuwa za Kiserikali (NGOs) kutokana na matatizo ya vita na nini imekuwa ni ngumu kupata misaada na kuweza kusaidia jamii. Ninamwomba Waziri Mkuu afanye michakato kupitia hizi taasisi za mashirika tofauti tofauti ya umma au taasisi hizi za kifedha za kibenki na nini ziweze kuzisaidia hizi NGO. Kuziokoa zisiweze kufa na ziendelee kufanya kazi zake kama kawaida za kusaidia jamii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaenda kwenye AFCON ambayo inategemewa kufanyika mwaka kesho. Mwaka kesho kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu ni karibu sana. Ukiangalia barabara ambazo zinakwenda kwenye AFCON, kwenye viwanja ambavyo vimetumia pesa nyingi sana, barabara bado hazijakuwa nzuri na siyo rafiki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia hata Barabara ya Uwanja wa Mkapa kama unatoka Dar es Salaam pale kwenda Uwanja wa Taifa, utaona kuna makontena mengi sana ambayo ni hatari kwa wageni wetu ambao watakuja kwenye AFCON. Tunaomba barabara hiyo iachwe wazi na yale makontena yatafutiwe sehemu nyingine ambayo ni rafiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninazungumzia pia hivi vilabu vyetu. Vilabu vyetu vimekuwa vikicheza mashindano ya kimataifa, tunamshukuru Mheshimiwa Rais kutoa lile goli moja la mama, imekuwa ikivipa motisha hivi vilabu vyetu vinaweza kufanya vizuri na kujitahidi kuweza kusonga mbele kwa ajili ya Taifa letu. Pia, nilimwona pale Mheshimiwa Makonda alikuwa amekaa na Mheshimiwa Waziri Mkuu, nikakumbuka kitu. Mheshimiwa Makonda alivyokuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam alitoa kiwanja kwa Young Africa na ameacha kumbukumbu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ninamwomba tu Waziri Mkuu kwa heshima na taadhima. Waziri Mkuu ni mwanamichezo, lakini ninamwomba, Klabu ya Simba huko nyuma (zamani) ilikuwa inafanya mazoezi Jangwani, vilabu vingi vilikuwa vikifanya mazoezi Jangwani, kuna Tololo sijui Pan - African na nini, pale karibu na Klabu ya Yanga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi Yanga wamepata uwanja mwingine na wamepewa hati hapohapo. Kwa hiyo, ninamwomba Waziri Mkuu ni mwanamichezo, afumbe macho na aweke historia kwenye Simba Sports Club na yeye atupe uwanja wetu kama alivyofanya Mheshimiwa Makonda, yeye ni Simba lakini hakuwa na ubaguzi wowote, akasema hii ni michezo kwa ajili ya nchi yetu. Kwa hiyo, ninamalizia na ninakuomba kwa heshima na taadhima, tulishaandika barua Serikalini, kiwanja kile Simba hawajakabidhiwa na timu nyingine. Kwa hiyo, tunaomba Simba nao wapewe kiwanja ambacho kitaweka kumbukumbu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono hoja. Ahsante. (Makofi)