Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Aziza Sleyum Ally

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. AZIZA S. ALLY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachukua nafasi hii kukushukuru kwa kunipa nafasi ya kuongea, lakini kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa siku ya leo kusimama hapa jioni hii na kuweza kuongea machache ambayo niko nayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba yake nzuri yenye mpangilio na yenye utaratibu mzuri uliotulia. Pia ninampongeza katika hotuba yake mwanzo tu alipoanza alianzia kuongelea kuhusu masuala ya afya. Waziri Mkuu nina imani na Mheshimiwa Rais katika Ilani ya Uchaguzi aliahidi kuwajali wananchi wake katika idara ya afya hasa kwa magonjwa sugu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii nimesimama hapa ninapenda niseme katika Mkoa wetu wa Tabora tunasimama kifua mbele wa kumpongeza Rais wetu na kumshukuru mpaka hivi sasa tumeshapokea mashine za kusafisha damu na mashine za kusafisha figo. Ahadi yake amekamilisha ndani ya siku mia moja. Hongera sana Rais wetu tunakupongeza kwa kazi kubwa unayofanya na tuna hakika uongozi wako umetoka kwa Mwenyezi Mungu. Ndio maana unayafanya haya ambayo unayoyafanya kwa kuwa Mungu anakuongoza kwa yale mema ambayo unayafanya na nia yako ni njema na ni nzuri kwa wananchi wako. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba niwashukuru wanawake wa Mkoa Tabora kwa kunichagua na kuniamini na kunipa kura za kutosha. Pamoja na hayo niweze kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa pesa alizotenga kwa wanawake ili waweze kupata mkopo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tumefanya zoezi moja kubwa hapa Dodoma kupitia Mbunge mwenzetu Neema kwa kuwashukuru sana CRDB Foundation kwa Dr. Tuli msichana ambaye ni mwanamke; amefanya vizuri kupitia foundation yake. Amemuunga mkono Rais wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa Dodoma wanawake wamepata shilingi bilioni moja wanazokwenda kufanyia kazi za mkopo; ambao mkopo huo hautakuwa na riba hata kidogo. Ninapenda kuwaambia wanawake wa Tabora tumeanza na Dodoma kinachofuata ni Tabora. Huyo ndio Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, mama yetu kiongozi wetu jemedari wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mkoa wetu wa Tabora katika kipindi ambacho Rais ameingia madarakani ameweza kupeleka pesa katika halmashauri zetu shilingi bilioni 12.2 hizo ni za vifaa tiba, lakini amepeleka shilingi bilioni 37 ambazo hizo ni kwa ajili ya majengo. Mheshimiwa Rais ameyafanya haya kwa ajili ya kuwajali wananchi wake katika huduma za afya, lakini Waziri Mkuu huyu yeye alikuwa ni Waziri wa Fedha na aliyaona haya na yeye pia alielekeza pesa hizo kwa namna yoyote kuweza kuzitafuta ili zikafanye kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapata shida sana na lazima niseme ukweli pesa nyingi zinapita kwenye halmashauri zetu, lakini bado shida ipo kule katika hospitali zetu za chini. Je kuna utaratibu gani Mheshimiwa Waziri Mkuu wakaangalia hili dudu la halmashauri, pesa hizi kama za Wizara ya Afya ziweze kutafutiwa mfumo mzuri, akafanye kazi huduma kwa wananchi wale wa chini ikafanye kazi vizuri na huduma ipatikane bila malalamiko yoyote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kila fedha utakayoiona inatengwa katika halmashauri zetu. Kwa hiyo, hili ni tatizo ambalo kwa nini iende moja kwa moja kwenye halmashauri kule wanawawekea mzigo mkubwa zaidi. Tuje tubadilishe mfumo sasa tuweke mzuri ambao utapeleka kule na kwa usimamizi ambao utakuwa mzuri zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina imani Serikali ina imani kubwa na halmashauri na hata sisi Wabunge tuna imani kubwa na halmashauri zetu, lakini je, kwa utaratibu huu huduma kule kwa wananchi wetu zitafika kwa utaratibu mzuri? Tunajua wafanyakazi wanafanya kazi yao vizuri, lakini lazima tuseme ya kwamba waweze kupata usimamizi uliokuwa imara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nichangie kuhusu madaktari wetu bingwa na madaktari na manesi ambao wanahudumia binadamu. Leo ningependa kuwa balozi wa kujipa mimi mwenyewe ubalozi wa madaktari. Tunao madaktari bingwa katika nchi yetu; lakini madaktari wetu bingwa hao stahiki zao zikoje? Ni ndogo sana. Madaktari wetu bingwa huwezi kukutwa sehemu yoyote wanapewa kipaumbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi wanasiasa tuna nafasi yetu, wacheza mpira wana nafasi yao, wasanii wana nafasi yao, lakini hawa wanaojali wananchi, wanaotusaidia tukiwa na afya legelege humu ndani mtu akipata tatizo lazima akimbie pale hospitali. Je, wale nani anayewasimamia na kuwasemea? Kweli kazi ya udaktari ni kazi ya wito, lakini lazima tukubali tuwajali sasa hivi na kuwasemea na kuangalia stahiki zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vijana wetu wamesoma, vijana wetu wamesoma miaka minne Serikali imewahudumia lakini bado mapato yao ni madogo. Tukichukua tu overtime ya daktari ambaye yuko hapa Benjamin leo, ule muda wake wa overtime analipwa shilingi elfu ishirini na mbili, overtime yake ni elfu ishirini na mbili hapa Benjamin. Hapo ana mgonjwa ambaye ni wewe, mimi au ndugu yako. Yeye anamfanyia operation muda wa kazi umekwisha, lakini anaokoa uhai wake akitoka pale anapewa elfu ishirini na mbili ndiyo overtime yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati huo umepita na hatutoweza kuvumilia. Nilikuwa ninaomba wakija kuja kutoa majibu waje kueleza namna gani tunawainua madaktari wetu. Hawana nyumba hata za kukaa, nyumba ni chache. Mheshimiwa Waziri Mkuu ninamwamini ni kijana anayefanya kazi na anayebuni mambo mengi kwa nini tusiwajengee nyumba madaktari wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia Benjamin Mkapa hapa kuna nafasi kubwa ambazo tunaweza kutafuta hata ubia na sehemu nyingine yoyote wakafanyiwa hata apartment waweze kukaa wakiwa karibu. Hiyo Mheshimiwa itawasaidia sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuliwaahidi madaktari vijana wetu waende wakasome, watakaposoma tutawalipia ada na hatutowadai tena, Serikali itawasomesha, lakini sasa hivi kwenye kile kidogo cha mshahara anachopata hapo hapo anaenda kukatwa pesa itakayolipa ule mkopo ambao amesoma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili linasikitisha sana kwa vijana wetu madaktari wetu na manesi wetu. Wengi tunachukua nafasi hii kuweza kuwalaumu kwa kila siku hakuna tutakaowapa nafasi. Mheshimiwa Waziri Mkuu unashindwa nini siku moja ukawaandalia vijana wetu madaktari bingwa, ukakaa nao na kunywa nao hata maji; wao soda hawanywi kwa sababu wanaogopa sukari, lakini hata maji ya mia tano watakunywa. Kaa nao wasikilize shida zao watatulie matatizo yao. Utapata nafasi yako kwenye chama na Serikali, lakini pia utapata nafasi yako kwa Mungu pia kwa ajili ya kuwasikiliza watu na shida zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanawake wa Tabora pia wameniagiza. Hawajapata pesa zao ambazo wameuza tumbaku, bado hawajalipwa pesa zao. Je, Serikali ina utaratibu gani wa kuwalipa hawa wakulima wa tumbaku pesa zao wanazodai. Hivi sasa wananunua tumbaku nyingine ambayo tayari wana madeni ambayo bado wanadaiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nichukue nafasi hii kuunga mkono hoja. Ahsante. (Makofi)