Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Esther Lukago Midimu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia. Kwanza kabisa nimpongeze Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba yake nzuri iliyosheheni matumaini ya Watanzania. Mheshimiwa Waziri Mkuu amefanya kazi nzuri sana. Tunamwona anazunguka, anaenda kwenye mikoa, anapita wilaya zote, anasikiliza kero za wananchi na kuzitatua. Hongera sana Mheshimiwa Waziri Mkuu, lakini pia ninawapongeza Mawaziri wote na Manaibu Waziri kwa kazi nzuri wanazofanya, Mwenyezi Mungu awabariki sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, anafanya kazi nzuri sana. Mheshimiwa Rais ni simba jike unayelinda watoto wako, unafanya kazi nzuri sana. Mwenye macho haambiwi tazama. Mheshimiwa Rais ni nahodha, usibabaishwe na mtu, kanyaga twende. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Mkuu wangu wa Mkoa, Anamringi Macha, anafanya kazi nzuri sana pamoja na cabinet yake anafanya ziara majimbo yote kukagua miradi ya maendeleo lakini pia na kusikiliza kero za wananchi na kuzitatua. Hongera sana Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa Simiyu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaendelea kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kuboresha hospitali ya Muhimbili. Mheshimiwa Rais ameboresha hospitali ya Muhimbili, upasuaji wa kichwa unafanyika hapa hapa Tanzania Muhimbili, upandikizaji wa figo hapa hapa Muhimbili, upasuaji wa moyo unafanyika hapa hapa Muhimbili, amepunguza adha ya wananchi kufuata matibabu India, vipimo vyote vipo. Hongera sana Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri unazozifanya mama; wewe ni simba jike hakuna mtu atakayepinga. Mwenye macho haambiwi tazama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaendelea kumpongeza Mheshimiwa Rais, kwa mkoa wetu ametupatia fedha tumejenga hospitali ya mkoa. Pia, akatutengea zaidi ya shilingi bilioni saba tukajenga majengo manne; jengo la kutakasa vifaa, jengo la kufulia, jengo la mochwari na jengo la mama na mtoto tena ghorofa la kisasa limekamilika na linafanya kazi; Mheshimiwa Rais Mungu akubariki. Ombi langu kwa Hospitali ya Mkoa Simiyu haina uzio; tunaiomba Serikali itupatie fedha ili tuweze kujenga uzio. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaendelea kumpongeza Mheshimiwa Rais wangu kipenzi, Mama yetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri. Ametutengea shilingi bilioni saba tukajenga Hospitali Mpya ya Itilima pamoja na kununua vifaa tiba, hongera sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali ya Itilima nayo haina uzio. Niombe Serikali ifanye utafiti hospitali zote za wilaya na za mkoa ambazo hazina uzio itoe fedha zijengewe uzio kwa sababu ni hatari sana hospitali kukaa bila uzio. Utoroshwaji wa dawa na vifaa tiba ni rahisi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, ninaendelea kuomba kwa Itilima, tuna Kituo cha Afya cha Zagayu; hakina wodi za kulaza wagonjwa. Tunaiomba Serikali itusaidie fedha ili tuweze kujenga wodi; kuna ujenzi wa Kituo cha Afya Itilima Mwanhunda unaendelea, lakini unasuasua. Tunaiomba Serikali itupatie fedha ili tuweze kukamilisha ujenzi huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaendelea na pongezi kwa Hospitali ya Busega, Wilaya mpya ya Busega tumejengewa hospitali mpya, tumetengewa shilingi bilioni nne na Mheshimiwa Rais. Ombi langu kwa Busega kuna Kituo cha Afya cha Mkula jengo la OPD limekamilika, lakini halina wodi za kulaza wagonjwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaiomba Serikali iendelee kututengea fedha ili tuweze kujenga wodi katika Vituo vya Afya vya Mkoa Simiyu ambavyo havina wodi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaishukuru Serikali kwa kuboresha jengo la hospitali ya Maswa, theatre nzuri ya kisasa, wodi zote zimejengwa na jengo la ICU limejengwa. Tunamshukuru Mheshimiwa Rais, ila nina ombi Kata ya Buchambi na Kata ya Sukuma; hatuna vituo vya afya. Kata hizo zina wakazi wengi tunaomba tupatiwe fedha ili tuweze kujenga vituo vya afya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunamshukuru kwa ujenzi wa Hospitali ya Wilaya Bariadi mpya alitupatia shilingi bilioni nne. Hongera sana Mheshimiwa Rais na kuendelea kuboresha hospitali ya Meatu. Kuna Kituo cha Afya cha Mboboko kiko kwenye ilani. Tunaiomba Serikali itupatie fedha ili tuweze kujenga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu maji ninamshukuru Mheshimiwa Rais kwa kutupatia shilingi bilioni 440 kwa ajili ya mradi wa maji. Mradi wa Maji wa kutoka Ziwa Victoria kuja Mkoa wa Simiyu na wilaya zake; Busega, Bariadi, Itilima, Maswa na Meatu. Mradi huo umeshaanza kujengwa, lakini bado unasuasua. Ninaiomba Serikali ije na majibu ni lini mradi huu utakamilika kwa sababu wananchi wa Simiyu wanasubiri kwa hamu maji ya Ziwa Victoria ili iweze kutimiza azma ya Mheshimiwa Rais ya kumtua mama ndoo kichwani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaenda ujenzi; kuna Barabara ya kutoka Bariadi kwenda Itilima, Meatu, Sibiti na Singida kwa Waziri Mkuu, hii barabara ni shortcut. Hii barabara ikikamilika ijengwe kwa kiwango cha lami itafungua uchumi, lakini na barabara nyingine ya kutoka Bariadi kwenda Magu na hiyo tunaomba ijengwe kwa kiwango cha lami. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaendelea kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kununua ndege, mpaka sasa ndege zimefika 16, hongera sana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu sasa ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Mkoa Simiyu uko kwenye ilani. Eneo tayari limeshatengwa liko Igegu Sapiwi. Hilo eneo liko jirani na Mbuga ya Serengeti na Ngorongoro. Uwanja huo ukijengwa ukikamilika hata watalii watakuwa wanashuka pale. Hata sisi wananchi wa Mkoa wa Simiyu tuna hamu sana uwanja ule ukamilike. Sisi ni wachapakazi, wakulima na wafanyabiashara tutapanda ndege: ndege zitajaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu 10% ya akina mama, vijana, na walemavu. Bahati nzuri Wilaya ya Itilima walipata kibali fedha zipitie benki na akina mama, vijana na walemavu wakaendelea kukopa. Wilaya ya Itilima imefanya vizuri sana. Ombi langu; ninaiomba Serikali itoe vibali na wilaya zingine ili fedha zile ziwe zinapitia benki. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Midimu, hebu malizia.

MHE. ESTHER L. MIDIMU: Nimalizie?

MWENYEKITI: Muda wako umekwisha.

MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, ninampongeza mama yetu Mheshimiwa mama Chatanda, mwanamke wa shoka ametuunganisha wanawake, anatupenda na anatushauri vizuri. Mama siyo siri unachapa kazi, tunakupenda mama yetu wanawake wote unatuunganisha tunapendana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, ninaunga mkono hoja. (Makofi)