Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kigoma Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. CLAYTON R. CHIPANDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia katika Hotuba ya Waziri Mkuu na bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa ninaipongeza Serikali ya Awamu ya Sita ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Moja, kwa kutupa nafasi vijana. Nimeona Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amemaliza lawama kuhusiana na vijana katika Bunge hili. Asilimia kubwa ni vijana. Ametupa nafasi twende tukawasaidie wananchi. Lawama yoyote ambapo tulikuwa tunalaumu kwamba vijana hatupewi nafasi, haya Bunge hili hapa, tuko wengi kuliko watu wenye umri mkubwa. Sasa huu ni muda wa sisi kuweza kuonyesha Tanzania kwamba vijana tunaweza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia idadi kubwa ya Mawaziri wamepewa vijana. Mama amemaliza kwenye hilo. Ni muda wetu wa kufanya kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa, nimeangalia 97% ya Wabunge wote ambao wameongea katika Bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuchangia Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, wameongelea barabara. Tafsiri yake ni kwamba suala la barabara ni tatizo, ni kama janga lingine. Ni kwa nini tusifanye maamuzi Bunge hili tukaliweka suala la barabara kama janga la Taifa na tukatafuta namna bora ya kuweza kutatua shida ya barabara? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukimpelekea mkulima mbolea shambani halafu usipompa barabara ya kufikisha hayo mazao ambayo anayatoa shambani kuyaleta mjini, ni sawa na kazi bure. Ukijenga hospitali ya wilaya, usipowapa wagonjwa njia ambayo watapitishwa na hiyo ambulance kwenda hospitali, hiyo ni sawa na kazi bure.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Kigoma Mjini, hospitali ya wilaya ilipojengwa, hakuna barabara ya kuwafikisha watu pale. Ni mashimo, mabonde na kuinama. Tafsiri yake ni nini? Utampeleka mzazi kwenda kujifungua wakati unampeleka unampiga kwenye mashimo, afike kwanza atengenezwe kwanza nyonga uliyovunja kwenye mashimo; haiwezekani. Lazima tufanye maamuzi. Vijana tuko humu ndani, tufanye maamuzi kuhusiana na suala la barabara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka nimwambie ukweli Mheshimiwa Waziri Mkuu. Suala la TARURA kuna mtego huo huwa wanatuingiza; mkenge. Ukisikia wataalam wanakushauri upeleke barabara ya vumbi kwenye jimbo lako, tafsiri yake ni kwamba wamejitengenezea kitengo cha kuwa wanakutana na mkandarasi kila mwaka kuchukua 10%.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni kwa sababu utatengeneza barabara ya vumbi mwaka huu kwa shilingi milioni 400, ikifika mwezi Desemba mvua zikinyesha, zinazoa milioni 400 yote zinaipeleka ziwani au kwenye mto. Mwaka kesho wanatenga tena milioni 400 kwa ajili ya kujenga barabara ile ile. Wale watu wa TARURA wanakutana na mkandarasi kila mara wanachukua 10%, maisha yanaendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni muda wa kufikiria kujenga barabara za lami na tuachane na barabara za vumbi. Wamerahisisha lugha kuiita barabara za vumbi. Mzee ni barabara za vumbi wakati wa kiangazi, ikifika wakati wa masika ni barabara za tope. Nadhani tuzibadilishe jina tuziite barabara za tope.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Kigoma Mjini, tulipata ufadhili wa Nchi ya Belgium mwaka 2018 mimi nikiwa Diwani. Belgium walikubali kutujengea kilometa 42 za barabara za pavement blocks ambazo zingeenda kufuta shida yote ya barabara katika Jimbo la Kigoma Mjini, lakini mpaka leo hakuna kinachoendelea na mkandarasi alikuwepo, upembuzi yakinifu ulishafanywa na kila kitu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi nilienda kwa Mheshimiwa Profesa Shemdoe, nyumbani kwake, sikumkuta. Nilienda kwake sikumkuta, nikauliza hata shemeji yangu nae sikumkuta. Nilikuta watoto wake, maana niliona sura zinafanana na Profesa Shemdoe mtupu, nikajua ni watoto wake. Lengo nilikuwa ninataka nikae na Profesa Shemdoe tuongee kifamilia kuhusiana na barabara za Kigoma Mjini. Jimbo la Kigoma Mjini ndio jimbo la mjini ambalo lina barabara za vumbi kuliko jimbo lolote duniani, siyo Tanzania, dunia nzima. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka nikuhakikishie, ukienda Kata ya Mwanga Kaskazini, kuna barabara inaitwa Barabara ya Serengeti ambayo inaunganisha Kata ya Mwanga Kaskazini na Kata ya Gungu. Hiyo barabara ina makorongo ambayo ukifika Mheshimiwa Waziri Mkuu, utasema Inna lilahhi wa inna ilahhi raji'un. Ukienda Kata ya Buzebazeba, kutokea uwanja wa Lake Tanganyika, ukipita barabara hiyo ambayo inaenda ku-connect mpaka soko la Buzebazeba, ina-connect Kata ya Rusimbi, ina-connect Kata ya Kasingirima, ina-connect Kata ya Majengo, ina-connect Kata ya Machinjioni, barabara zote hizo ni vumbi tupu. Ifikie hatua watusaidie watu wa Kigoma na sisi tupate barabara ambazo zitaenda kuchochea maendeleo ya mji wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tunaenda pale na Mheshimiwa Waziri Mkuu ninadhani kesho kutwa kwenda kukutana na wafanyabiashara kutoka Congo, Burundi na sehemu nyingine tofauti tofauti. Wanaenda kuona aibu iliyopo pale Kigoma Mjini. Wanaenda kushuhudia barabara za vumbi zilizotaradadi pale ndani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa watu wakishaona hizo fursa, baadaye wataanza kuzinunua nyumba za wapiga kura wangu kwa bei ndogo kwa sababu nyumba iko kwenye korongo, utamuuzia nani bei kubwa? Watazinunua bei ndogo, baada ya kuja kujenga barabara, wananchi wetu watakuwa wamepoteza opportunity. Huu ni muda, wameniamini, kibarabara, mtoto wao. Nimekuja kuwaombea barabara kwa ajili ya Jimbo la Kigoma Mjini katika Bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. watusaidie barabara, watupe barabara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tukifanya maamuzi ya pamoja Wabunge wote, ninawaambia ukweli; mama alivyokuja kuhutubia Bunge hapa, Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wetu, alivyotaja tu barabara, Bunge zima likapiga makofi, akajua hapa kuna tatizo na ndiyo maana ameongeza hela kwenye upande wa barabara, lakini bado tunaomba sana utusaidie watu wa Kigoma tuweze kupata barabara. Hiyo ni tabu kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, shida ya pili, mafuriko. Jimbo la Kigoma Mjini limekumbwa na mafuriko. Yapo mafuriko ambayo yanatengenezwa na Mwenyezi Mungu; Mwenyezi Mungu analeta mvua nyingi, mafuriko yanatokea. Hilo hatuwezi kumlaumu mtaalam yeyote, lakini yapo mafuriko ambayo yanasababishwa na uzembe wetu sisi ambao ni viongozi tuliopewa nafasi ya kuwaongoza wale wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, sehemu ambapo maji yangefuata mtaro yangeenda ziwani moja kwa moja, hujajenga mtaro. Tafsiri yake maji yanachagua sehemu ya kupita, aidha yachague sebuleni au chumbani kisha yapitilize yaendelee na shughuli zake. Kwa hiyo, kuna makosa mengine hata mimi kwenda kuwapa watu pole ninaona aibu. Huwezi kwenda kuwapa watu pole sehemu ambapo ungejenga mtaro mkubwa, maji yasingeleta mafuriko kwenye nyumba za watu. Siwezi kwenda na nikimwona Waziri anakwenda aende yeye, wakamzomee yeye mwenyewe, mimi siwezi kwenda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachotaka niende na Mheshimiwa Profesa Shemdoe, twende tukazindue mitaro, tukazindue barabara, hapo tutashirikiana kwa pamoja. Ninawaomba sana, namwomba sana Mheshimiwa Waziri Mkuu atusaidie watu wa Kigoma tuweze kupata barabara, lakini pia suala la mafuriko ya Bwawa la Katubuka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Bwawa linaitwa Katubuka. Hili Bwawa liko miaka yote tangu tumezaliwa, halikuwahi kufurumia kiasi kile, lakini wataalam wetu walitengeneza mitaro wakaelekeza maji yote ya mji kwenye hilo bwawa. Sasa hivi limebadilika limekuwa ni bwawa ambalo linaleta mafuriko kwenye Mji wetu wa Kigoma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kuna mtu alikuja kutudanganya siku aliyosema ni uongo au ni ukweli akasema Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ameelekeza shilingi bilioni nne kwa ajili ya kwenda kutengeneza mtaro wa kuyatoa maji pale Katubuka. Tukamwona mkandarasi anaanza kazi, nami nikaenda kuitisha mkutano, nikasema mnaona kazi ya mama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya mwezi mmoja na nusu mkandarasi ametoa vifaa vyote anasema hana hela. Nikamuuliza shida ni nini? Akaniambia pesa nilizokuwa ninazitumia kujenga hapa ni pesa ambazo nilipewa kwa ajili ya Barabara ya kutoka Katonga kwenda Ujiji. Sasa barabara ile inatakiwa kwisha na hapa siwezi kuendelea kwa sababu hela ya huu mtaro sijapewa. Mzee wangu Prof. Shemdoe, anisaidie. Mimi ni mmoja kati ya mashabiki wake, ninamkubali, anatusikiliza, tunamheshimu, anatuheshimu na hata 2030 akichukua fomu yoyote tuko nyuma yake mzee wangu.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante. Malizia kwa kuunga hoja.
MHE. CLAYTON R. CHIPANDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamalizia suala la mwisho, ni suala la fidia. Wananchi wa Kata ya Majengo pamoja na Machinjioni walikubali kupisha upanuzi wa airport pale Kigoma Mjini na wakazuiliwa baada ya kufanyiwa valuation, wakazuiliwa wasijenge tena kwenye nyumba zao kwa sababu wanasubiri kulipwa. Sasa tunakwenda mwaka wa pili; tofali liking’oka mtu anashindwa kurudishia kwa sababu anaamini kwamba hilo tofali litaongeza gharama ambayo hatalipwa. Ni muda umefika sasa twende tukawalipe wale wananchi fidia pale Kigoma Mjini ili maisha mengine yaweze kuendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kusema hayo machache, ninamalizia na hili la wavuvi mzee wangu; ninaomba Mwenyekiti wangu anisaidie Wabunge wenzangu si wanaona kama kidogo mambo ni mazuri?
MWENYEKITI: Malizia, ninaomba umalizie kwa kuunga mkono hoja, ninadhani nimekuongezea muda wa kutosha.
MHE. CLAYTON R. CHIPANDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, sawasawa kwenye suala la wavuvi, ninaunga sana mkono hoja baada ya kuona Ziwa Tanganyika ni moja ya...
MWENYEKITI: Mheshimiwa Chipando.
MHE. CLAYTON R. CHIPANDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)