Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Magu
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nishukuru kwa kunipatia nafasi hii na mimi niweze kuchangia hotuba ya Waziri Mkuu. Nimshukuru sana Mwenyezi Mungu ambaye ametuwezesha sisi sote kusimama mahali hapa tukiwa salama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, nipongeze Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo inaendelea kutatua changamoto za Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze pia Waziri Mkuu kwa hotuba yake nzuri na namna ambavyo anaendelea kushughulikia matatizo ya Watanzania pamoja na Mawaziri wote walioko chini ya Wizara yake, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu, Manaibu Makatibu Wakuu na Wakurugenzi wa Wizara hii ya Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti ya Waziri Mkuu ni shilingi trilioni 12. Kule nje, Watanzania wanadhani ni hela ya mfukoni ya Waziri Mkuu kuweka kwenye mambo yake. La hasha! Inabidi Serikali ijielekeze pia kuwaeleza wananchi kwamba fedha hizi zinatumika kwa namna gani. Mfano, tuna miaka 10 TAMISEMI ilikuwa Ofisi ya Rais na sasa TAMISEMI imerejeshwa Ofisi ya Waziri Mkuu. Maana yake huko TAMISEMI ndiko kuliko na mzigo mkubwa wa watumishi wa Serikali wanaowahudumia wananchi wa kwetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo lazima bajeti iongezeke na iwe ya kutosha. Kwa sababu mwananchi huduma nyingi anazipata kwenye ngazi za chini kabisa za Serikali. Kama ni afya, kuna zahanati; watumishi wa zahanati ni wengi. Kama ni elimu, kuna shule, watumishi wa elimu ni wengi. Kama kuna watendaji wa vijiji wako wengi, kama ni kilimo wako wengi. Kwa hiyo, Ofisi ya Waziri Mkuu shilingi trilioni 12 ni fedha nyingi, lakini zinakwenda kutatua changamoto za Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo tulilonalo sasa hivi ni barabara. Niungane na wewe wakati unachangia hapa asubuhi na wengine, tuna matatizo makubwa ya barabara. Tuone namna ambavyo tunaweza kutatua. Nimesoma bajeti ya TARURA, ni fedha kidogo bado ukilinganisha na mahitaji ya Watanzania kwenye maeneo yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ulipokuwa unazungumzia jimbo lako lina mjini na vijijini. Mimi nina Mji wa Kisesa pamoja na Mji wa Bujora, hauna barabara kabisa, zimekufa zote. Kuna maeneo ni mji, lakini wananchi wanapaki gari zao kwenye sheli. Kuna maeneo akifariki mtu, wananchi wakibeba mwili kwenda Igeye kutokea uwanja wa Mkapa, wanabeba kwa mabega, si sawa. Kuna maeneo, Mwaholi, hawawezi kufika wananchi. Kwa hiyo kama mtu anabeba mwili kwa mabega kwa karne hii, si sawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakubaliana kwamba kazi nyingi zimefanyika, lakini bado kuna kazi nyingi zinatakiwa kufanyika. Kwa hiyo, alivyokuwa anachangia asubuhi lazima tuangalie, hii ni miji iliyokua sasa hivi. Mji wa Bujora una barabara moja tu ya lami ambayo imejengwa kilometa 1.7 ambayo inakwenda kwenye makumbusho ya Wasukuma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mji wote wa Bujora, Mji wote wa Kisesa, hauna barabara ya lami hata moja. Hapo mwisho wakati tunakwenda kwenye uchaguzi, tuliahidiwa hapo na Serikali kwamba tutaleta fedha za dharura, wakaleta na barua. Manunuzi yakaandaliwa, mikataba ikaandaliwa, mikataba mpaka leo haijasainiwa. Tumewaeleza wananchi hapo tutajenga kilometa 1.2, tutajenga kwa mitaro, tutajenga kwa lami. Mambo mengine haya tunatakiwa lazima tuone namna ya kumaliza matatizo ya wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, humu mjini hata kama utajenga barabara za kupanguka weka gravel, kama hujaweka mitaro ni kupoteza fedha. Hatuna sababu ya kuwa tunapoteza fedha kila mwaka badala ya kutengeneza mitaro tukatengeneza barabara ikaimarika angalau hata miaka miwili watu wakaitumia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapata tabu sana. Barabara za TANROADS zinaimarika, barabara za TARURA haziimariki, lakini nimepiga hesabu kwa Jimbo la Magu au ukiangalia Mkoa wa Mwanza mzima na mikoa mingine, barabara za TARURA ni nyingi kuliko barabara za TANROADS. Kwa hiyo, lazima tuangalie kwenye mgawanyo wa fedha hapo ama tutoke kwenye 30% TARURA, 70% TANROADS, twende 50/50 ili tuweze kutekeleza vizuri barabara zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukitoka kona ya Kayenze leo kwenda Shule ya Mwanza Girls, kwenda Kayenze kule kilometa 19, wananchi hawapiti. Ukionyeshwa kwa drone, unaweza ukashangaa kwamba hii barabara iko wapi. Kwa hiyo, yako mambo lazima tuyakabili, lakini wakati mwingine wilaya zetu zinaungana na wilaya nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda Itilima nilitegemea Waziri Mkuu siku amekuja Bariadi kule Itilima, akitokea Bariadi apite Mahaha, tukutanie pale Mwamnemha, hakuna barabara. Kwa hiyo kama anakuja Magu lazima aende Lamadi, si sawa. Kama anataka kutokea Bariadi, kuna ule Mto Gudama, unahitaji daraja, Gudama pale Mahaha kwenda Itubukilo, likipata kuunganishwa; halina gharama zaidi ya shilingi milioni 500. Nimekuwa nikilizungumza humu kila mwaka, lakini tuna barabara ya kutoka Kabila kwenda Nyasato, Nobola, Kabale kwenda Mahaha kilometa 25.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna miaka mitatu hatujaitengeneza hiyo barabara. Kwa hiyo, uhitaji wa fedha za barabara zinahitaji fedha nyingi. Tuangalie Serikali namna ya kuweza kurekebisha, kuongeza fedha ili tuweze kurekebisha barabara hasa za vijijini. Hizi barabara ni vikwazo vya kiuchumi. Kuna maeneo mchele ulipaswa kununuliwa 1,800 lakini kwa sababu ya barabara, mchele unauzwa 1,300. Kwa hiyo, maana yake ni kwamba ni vikwazo vya kiuchumi kwenye maeneo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapo ndipo ninapotaka kujenga hoja yangu. Fedha za tozo tunazozipata shilingi bilioni 1.5 kila jimbo, lazima tuangalie namna ya mgawanyo. Huwezi kulinganisha mwenye dumu la lita 20 na mwenye pipa, namna ya ujazaji wa maji lazima uende tofauti. Kwa hiyo, lazima tuangalie wenye majimbo makubwa, fedha hizi ziongezwe tusilinganishe na majimbo madogo. Ninataka kusema kwamba, tukifanya hivyo hakuna atakayelalamika humu kuhusu ukubwa wa jimbo au ukubwa wa wilaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, kuna fedha inaitwa fedha ya service levy. Inaweza kuwa kubwa sana kwa Njombe, inaweza kuwa kubwa sana kwa Jiji la Mwanza, inaweza kuwa kubwa sana kwa Jiji la Dodoma. Fedha hii ni mapato ya ndani. Ushauri wangu…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Mheshimiwa malizia, muda wako ulikuwa umekwisha.
MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini fedha hii tusiitenge kama fedha maalum kwa ajili ya kwenda kwenye barabara? Ikawa fedha lindwa, mapato lindwa kama ambavyo yako mapato ya Wizara ya Afya lindwa, ili fedha hizi zikaenda moja kwa moja kutengeneza barabara ambazo zinaonekana ni kichocheo cha uchumi kwa nchi yetu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ninaunga mkono hoja. (Makofi)