Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Mhe. Dickson Nathan Lutevele

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafinga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. DICKSON N. LUTEVELE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia. Kwanza kabisa nianze kumshukuru Mwenyezi Mungu; na nijielekeze moja kwa moja kwenye kuchangia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kwa heshima na taadhima niipongeze sana hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ambayo kusema ukweli imesheheni mambo mengi sana. Tayari kwenye hotuba hii Waheshimiwa Wabunge wengi wamechangia, hasa wakipongeza sana kazi kubwa ambayo tayari viongozi wetu wanaendelea kuifanya. Sasa ninaomba nijikite kwenye maeneo matatu muhimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa, ninaomba nimpongeze sana Rais wetu kwa kuendelea kuchapa kazi. Anachapa kazi kubwa na sisi tunaiona. Rais wetu ametuteulia Waziri Mkuu ambaye kwa kipindi hiki ndiye tuliyekuwa tunamtaka; Dkt. Lameck Mwigulu Nchemba, kwa sababu sote tumeona namna anavyofanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika maeneo mengi ambayo yamechangiwa na Waheshimiwa Wabunge wenzangu; sisi kwa ujumla hatuna mashaka na utendaji kazi wa Serikali yetu. Tumeona namna ambavyo Mawaziri wanafanya kazi usiku na mchana, wanafanya ziara wakienda maeneo yote katika idara zote kuhakikisha kwamba Watanzania tunaendelea kupata huduma kama ilivyo katika lengo la Serikali la kutupatia huduma. Tumemwona yeye mwenyewe Waziri wetu Mkuu akienda katika maeneo kadhaa na kutenda kazi kubwa sana katika kuibua na kujibu kero za Watanzania. Sasa, yako maeneo ambayo ninaomba nishauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tukirejea kwenye namna ambavyo tunaona kwenye maeneo yetu; viongozi wakubwa wanafanya kazi kubwa sana lakini wale wanao deliver zile huduma kule chini utendaji kazi wao kila Mheshimiwa Mbunge humu ndani anaulalamikia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, unakuta Afisa wa Kilimo amepewa kishikwambi, amepewa pikipiki lakini akiondoka asubuhi ofisini kwa Mkurugenzi, akifika kule kijijini kuna sehemu maalumu ameweka, pale wanamjua, huwa anafika saa mbili na nusu, atakunywa supu, chakula cha mchana huwa anakula saa nane, hajaenda kule ambako Serikali imemuwezesha na imemnunulia vifaa kwa ajili ya kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa mtindo huu hatuwezi kusubiri hadi Waziri Mkuu aje, au hadi Mkuu wa Mkoa ashuke kule chini. Tutafute namna ya kuwafanyia tathmini ya namna wanavyofanya kazi hawa wataalam wetu. Sisi kule kwetu yako maeneo ambayo wananchi wanahitaji ng’ombe watibiwe; lakini Mganga wa kutibu ng’ombe mpaka apigiwe simu na pengine atoe ratiba mwezi mzima hajakanyaga; ng’ombe wanakufa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nitoe ushauri kwa Serikali. Kwa kuwa tuko kwenye mpango wa dira ya miaka hamsini, yawezekana Mheshimiwa Waziri Mkuu tuanze kuangalia; mfumo tunaoutumia wa ajira unamfanya mtu asiwajibike. Kumbe sasa, ikiwezekana tuweke mfumo kwenye dira yetu. Tuweke mfumo wa ajira ya mkataba. Mtu akifanya kazi miaka mitatu, amefanya vizuri, ataendelea. Hajafanya vizuri, wasomi wako wengi nje wanasubiri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfumo huu tunaoutumia sasa hivi ulifaa sana wakati ambao wasomi ni wachache. Sasa hivi kila nyumba ina mtu anamiliki masters. Watu wafanye kazi kwa mikataba, wasisubiri kustaafu (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nijielekeze katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Ameeleza kwamba katika pato la Taifa sekta binafsi inachangia pato la Taifa kwa 70%. Sasa, ni lazima tuangalie kwamba 70% hii tunaiendeleza vipi? Ninaomba nitoe ushauri kwamba; katika kuziendeleza sekta binafsi, lazima tupunguze utitiri wa mamlaka zinazokwenda kwenye sekta binafsi. Tutengeneze one stop center. Kama ni tozo, mtu anatakiwa alipe laki moja na nusu, basi ijumulishwe alipe mara moja, siyo kila baada ya siku imekuja mamlaka hii, kila bada ya siku imekuja mamlaka hii. Hii hapana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine kubwa. Ni kweli kwamba Mamlaka yetu ya Mapato, TRA, inapongezwa na imekuwa ikifanya vizuri sana. Kila baada ya msimu wanapotutangazia wanakuwa wamevuka lengo na wameenda asilimia kubwa sana. Ni lazima kama Serikali pia tuangalie, asilimia kubwa hii je, wale kule wanakokusanya kodi maendeleo yao yakoje? Isije ikawa inakusanywa sana kodi, halafu kule wananchi wanafilisika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatoa mfano, leo hii, wafanyabiashara pale Kariakoo lazima takwimu zipo, tutazame miaka 10 nyuma biashara ilikuwa inafanyikaje? Watanzania walikuwa wana import kontena ngapi? Leo hii pale Kariakoo tunaanza kuwashangilia mawinga, kumbe wale mawinga kwa asilimia kubwa ni biashara ya wafanyabiashara wageni, wafanyabiashara wenzetu wenyeji wamefunga biashara wameondoka kwa sababu mitaji yao imekufa. Kwa hiyo ninaomba Serikali, pamoja na ukusanyaji mzuri wa mapato, lazima tuhakikishe ng’ombe huyu anaendelea kupata majani na furaha, anaendelea kufurahi kukusanya kodi. Vinginevyo tutajikuta tunazidi kubomoa kile ambacho tumekijenga jana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, ninaomba nitoe ushauri. Kama ikimpendeza Waziri, ninashauri mamlaka zetu zipite kuangalia namna ambavyo wafanyabiashara wetu nchi nzima wanavyofanya biashara zao. Wachukue hata rekodi ya miaka mitatu nyuma, waangalie ili tunapokusanya kodi tukusanye kwa watu ambao wanafurahi kulipa kodi kwenye nchi yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, ningeomba na ningeshauri; Watanzania wanafurahishwa sana na kasi ya Serikali, wamefurahi, wanafurahi mno, lakini wana jambo moja ambalo wanaliomba, kwamba kazi kubwa zinafanyika matibabu, afya, barabara na kila kitu. Barabara zetu za vumbi zitengenezwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho, Watanzania wanaomba mtaani kidogo shilingi iongezeke. Mtu akifanya biashara basi aone hela inapatikana kwa wingi mtaani. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante sana. Nilimwita Mheshimiwa...

MHE. DICKSON N. LUTEVELE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuunga mkono hoja.