Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Emmanuel John Khambay

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Babati Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. EMMANUEL J. KHAMBAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa kunipa nafasi ili niungane na wachangiaji waliokwishatangulia kuchangia hotuba ya Waziri Mkuu. Awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema ambaye amekuwa akiturehemu sote kwa kutujalia afya njema; lakini zaidi kuniwezesha kusimama hapa kuwawakilisha wananchi wa Jimbo la Babati Mjini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii kutoa pole za dhati kwa ndugu zangu wa Jimbo la Babati Mjini, hususani Kata mbili, ambao wamefiwa na wapendwa wao. Kata ya Bagara na Kata ya Maisaka ambapo jana asubuhi mwanafunzi wa kidato cha kwanza alipata ajali na akapoteza maisha na mwenzake na mmoja yuko Hospitali yetu ya Rufaa anaendelea na matibabu kwa kuvunjika mguu. Nitumie nafasi hii pia kutoa pole kwa familia moja ya kada mashuhuri wa Chama Cha Mapinduzi ambaye pia amekuwa akituvisha sare za chama katika Ofisi yetu ya CCM Babati Mjini na Mjumbe wa Baraza la Umoja wa Wazazi wa CCM, Wilaya ya Babati Mjini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii kumpongeza Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake za dhati kabisa za kuwaletea Watanzania maendeleo. Sisi watu wa Jimbo la Babati Mjini tunamshukuru kwa namna ambavyo alituletea fedha nyingi za maendeleo katika maeneo yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii pia kumpongeza Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ndugu yetu Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba kwa ziara zake ambazo amekuwa akiendelea nazo nchini; ziara ambazo zimekuwa na tija katika kutatua changamoto za wananchi. Binafsi ninamshukuru kwa ziara yake katika Jimbo la Babati Mjini ambapo baadhi ya changamoto zilizokuwepo ametusaidia zimeweza kupata utatuzi; hususani katika suala la ardhi ambapo Mheshimiwa Mkuu wetu wa Mkoa Queen Cuthbert Sendiga aliunda timu ya kushughulikia changamoto hiyo na changamoto hiyo imeendelea kutatuliwa. Tunaamini tutapokea ripoti mapema ya utatuzi wa changamoto hiyo na nini itakuwa njia ya kutatua mgogoro huo moja kwa moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo niendelee kuishukuru Serikali; katika sekta ya elimu sisi watu wa Babati Mjini tunaishukuru Serikali; kwanza kwa mitaala bora ambayo inakwenda kumwandaa mwanafunzi wa Kitanzania pindi amalizapo masomo kwenda kujiajiri. Ninaendelea kuipongeza hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kama ambavyo wenzangu pia wameipongeza. Ni hotuba ambayo inaakisi maendeleo katika sekta zote nchini. Kama hotuba hiyo na yale yaliyomo mle yatapata kusimamamiwa kwa weledi wa hali ya juu basi ni dhahiri maendeleo yatakwenda kuonekana katika nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na maboresho ya mitaala, tunapoelekea 2028 tutakuwa na ongezeko kubwa la wanafunzi. Sisi watu wa Babati Mjini tunatazamia kuwa na ongezeko la mwanafunzi 64,000. Tutakuwa na uhitaji wa madarasa 98. Hiyo kama haitoshi tuna shule ambazo zimezidiwa. Kwa mfano Shule ya Sekondari ya Komoto iliyopo Kata ya Bagara, ni shule ambayo kwa kweli imezidiwa kutokana na population kubwa katika kata hiyo, lakini pia kwa sababu mji wetu unakua kwa kasi. Hivyo, tutakuwa na uhitaji pia wa shule nyingine ya kui-support shule hiyo; eneo tayari tunalo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaendelea kuiomba Serikali katika bajeti hii ya awamu hii, katika yale maeneo ambayo tunahitaji mabweni katika shule zetu basi tuweze kupatiwa mabweni. Sambamba na hilo tuna shule mbili ambazo watu wa Babati tunatamani kuona kuwa zinaenda kutoa advance level. Shule ya FT Sumaye ina eneo la kutosha; Shule ya Sekondari Wang'Waray tunatamani pia na yenyewe iweze kutoa watoto wa kidato cha tano na cha sita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo nitumie nafasi hii kuishukuru Serikali. Tunatambua kuwa jitihada kubwa zimefanyika katika kulipa wakandarasi. Kwa hiyo ninaamini changamoto tulizonazo upande wa TARURA za uhitaji wa fedha katika bajeti hii tutakwenda kupata suluhisho. Sisi watu wa Babati tulikuwa tunapokea bilioni 1.8; tunaishukuru Serikali, lakini tumeongezewa imefika bilioni 2.5; tunaishukuru Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hivyo, Mji wa Babati ni mji ambao unakua kwa kasi, ndiyo Makao Makuu ya Mkoa wa Manyara. Hapa nyuma barabara nyingi zimevurugika kutokana na hali ya mvua. Hivyo, tunaomba ikimpendeza tuweze kuongezewa fedha hizi ziweze ku-double ili tuweze kutatua changamoto hizo na hivyo tuendelea kuboresha barabara ambazo zipo katika maeneo yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika fedha za maendeleo tunaomba pia tukumbukwe kupata fedha hizo ili tuweze kufuingua Barabara kutoka stendi mpya kuelekea Chuo cha Uhasibu ambapo ni Campus mpya ya Chuo cha Uhasibu cha Arusha katika eneo la Wang'Waray.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii pia kuishukuru Serikali. Katika sekta ya afya tumeendelea kupokea fedha nyingi na Hospitali yetu ya Mji wa Babati imeendelea kuimarika, ikiwa ni pamoja na vifaa tiba, vituo vya afya na zahanati. Tunaishukuru Serikali kwa kututengea bilioni moja na milioni themanini kwa ajili ya Kituo cha Afya cha Nangara, Zahanati ya Singi ambayo tunatazamia kwenda kupanda kuwa kituo cha afya, lakini na Hospitali ya Mji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii kuiomba Serikali, tutaandika ombi maalum kwa ajili ya kupata fedha za kuboresha majengo mengine katika hospitali yetu ya mji kwani Serikali imetupa zaidi ya bilioni 12, lakini bado tuna majengo mingine ambayo ni chakavu katika Hospitali yetu ya Halmashauri ya Mji. Ikumbukwe kuwa Mji wa Babati ni mji ambao unakua kwa kasi, hivyo tunahitaji kuboresha huduma ya afya katika maeneo haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongeze kuchangia kuhusu suala la Mfumo wa NeST. Ninaipongeza Serikali kwa kuwa na Mfumo wa NeST katika kwa ajili ya manunuzi ya umma. Lengo la Serikali ni kuweka uwazi, kuweka usawa katika competition ya tender, lakini ili pia fursa zilizopo wananchi wote waweze kuzipata au kushiriki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashauri kwamba, katika mfumo huu pawepo na ongezeko kidogo katika kubaini wakandarasi ambao mara pengine, wana tender zaidi ya moja na wanapopata zabuni zingine, wakati mwingine wanachelewa kukamilisha kwa wakati zabuni ambazo wamezichukua. Wakati mwingine wanaweza kuchukua fedha za zabuni mpya aliyopata akapeleka kuwenda kukamilisha zabuni nyingine ili apate certificate itakayowezesha fedha hizo; apatapo kwenda kumalizia tena mradi mwingine. Kwa hivyo, niombe Serikali kufanya maboresho katika mfumo wetu wa NeST, pia kuboresha mfumo wa TEHAMA ili maeneo yote watu ambao wana-bid hizo zabuni waweze kupata access ya mfumo wetu na kuondoa lawama ambazo pia sio za msingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo ninachangia ni katika suala zima la force account...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa muda wako umekwisha, kwa hiyo usichangie lingine.

MHE. EMMANUEL J. KHAMBAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba dakika moja. Katika suala la force account ni utaratibu mzuri ambao Serikali inautumia katika punguza gharama kwa kutumia vyanzo vya ndani pia. Kutokana na mfumo huu ninaishauri Serikali kuangalia ni miradi ipi ambayo tunapaswa kwenda kutumia moja kwa moja force account na miradi ipi ambayo tunaweza kuwaachia wazabuni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninasema hivyo kwa sababu tusipokuwa na monitoring ya majengo au uwekezaji ambao Serikali imetoa fedha ni vigumu kuweza kuona fedha hizo zinatumikaje. Kwa hiyo ni dhahiri kadiri itakavyotupendeza basi tuweze kuwa na mfumo wa ki-electronic wenye lengo la kuingiza, kutoa au kuweka udhibiti wa fedha zote ambazo zinakwenda kwenye ujenzi wa majengo ya Serikali. Kuwe na monitoring tusisubiri...

MWENYEKITI: Mheshimiwa Khambay ninaomba umalizie.

MHE. EMMANUEL J. KHAMBAY: ...tusisubiri kufanya postmortem wakati mtu ameshakufa. Majengo ya Serikali wakati mwingine ni chakavu, lakini fedha zimetumika za kutosha. Hivyo, tuwe tunafanya ufuatiliaji wa kina ili kuweza kubaini changamoto kuliko kusubiri mpaka tunapofikia mwisho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuunga mkono hoja. Ahsante. (Makofi)