Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Patrick Adkin Mwalunenge

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbeya Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. PATRICK A. MWALUNENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa kunipa fursa hii mchana na mimi niweze kuchangia bajeti ya ofisi ya Waziri Mkuu. Awali ya yote ninamshukuru Mwenyezi Mungu aliyetupa uzima nikapata fursa hii leo ya kuweza kutoa mchango wangu na mawazo kwenye bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Kwanza ninamshukuru Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya, alishajipambanua wazi kupitia hotuba yake aliyolihutubia Bunge, maelezo aliyoyatoa na kazi kubwa anazozifanya kwenye nchi hii, Wabunge wengi wamezungumza, sitaki kurudia huko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, ninampongeza Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa bajeti nzuri aliyoleta na kazi anazoendelea kuzifanya kwenye nchi hii, kwa ziara anazozifanya kwenye mikoa na kutatua kero za wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii inaleta matumaini makubwa kwa wananchi wa Tanzania kwamba sasa Serikali yao ipo kazini. Ninasisitiza tu Wasaidizi wa Rais kwa maana ya Mawaziri, wasaidizi wa Waziri Mkuu sasa waige ile njia anayoifanya Waziri Mkuu kutatua kero za wananchi na hiyo ndiyo njia pekee ambayo wananchi wetu wanataka. Wananchi wa sasa wanataka kuona matokeo tumeshazungumza sana, tumeshaandika sana makaratasi, hasa vijana waliopo sasa wanataka kuona matokeo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti ni nzuri, mambo ni mengi yamezungumzwa, nijikite kwenye Jimbo langu la Mbeya Mjini, pia niendelee kumpongeza na Dada yangu aliyetangulia kuzungumza hapa Mheshimiwa Suma Ikenda Fyandomo ametuwakilisha vizuri wananchi wa Mbeya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawashukuru wananchi wa Mbeya Mjini kwa kunipa imani hiyo ya kuwa mwakilishi wao hapa Bungeni. Wanambeya mjini pale shughuli zetu kubwa ni biashara, Ofisi ya Waziri Mkuu kwa maana Waziri Mkuu na Watendaji wake Mipango, TAMISEMI watakubaliana nami kwamba, umefika wakati muafaka sasa kwenda kuweka shughuli za biashara kwa maana kongani za viwanda kwenye Jiji la Mbeya, kwa sababu Jiji la Mbeya ni jiji la biashara na Jiji la Mbeya, ni barabara inayopitisha magari mengi na ndiyo lango la SADC kuelekea nchi zote za Kusini mwa Afrika, lakini hatuna viwanda Mbeya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye kujibu tatizo la ajira la vijana wetu kaka yangu Kitila atuletee kongani za viwanda Mbeya, atuletee uwekezaji Mbeya ili tunufaike na jiografia ya Mbeya ilivyo, kwa maana Mbeya ni lango la SADC, lakini kuna wakulima wengi wa mazao, basi tupate viwanda ambavyo vinatokana na uzalishaji wa mazao ya kule kama vile viazi, machungwa, ndizi, mpunga ili yale mazao tuweze kuyaongezea thamani na watu wetu waweze kupata ajira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ameongea sana hapo dada yangu na mimi ninakazia kwenye suala la miundobinu. Mbeya tunao utalii mwingi sana lakini bado hatujautangaza vizuri kwa sababu ya hali ya miundombinu. Nikiongea specific Mbeya Mjini, barabara nyingi za Mbeya Mjini hazipitiki vizuri. Ikiwa wakati wa mvua mifereji inajaa na wakati mwingine inaziba, wakati wa jua vumbi kali. Sasa huwezi kuwa na Jiji la aina kama ya Mbeya lenye wafanyabiashara wengi ambao wanajituma, vijana wanaweza kufanya kazi halafu barabara hazipitiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo ninaiomba Ofisi ya Waziri Mkuu watupatie barabara angalau hata kilometa 100 ya barabara za ndani ya Jiji la Mbeya, ninawahakikishia Mbeya itastawi na itashamiri na itavutia utalii na watu wa Mbeya ni wachapakazi wazuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasi tunajiongeza wakitupatia barabara hizo kilometa 100 tumeanza kuandika andiko hivi sasa kupitia viongozi wangu wa Mkoa kwa maana ya Mkuu wa Mkoa, Wakuu wa Wilaya na Mkurugenzi wa Jiji, tumeanza kuandika andiko ambalo kama watatukubalia Ofisi ya Waziri Mkuu kwa maana ya TAMISEMI waturuhusu tukope pesa kwenye taasisi za fedha ili tujenge hizo kilometa 100, kwa sababu Jiji letu linalo uwezo wa kukusanya mapato ya kulipa. Kwa hiyo, tutaandika hilo andiko na tutaliwasilisha kwao walione kama linakidhi vigezo waturuhusu ili sisi tuondoe vumbi Mbeya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunao uwezo kwa sababu mapato tunayo, tupate mkopo hata wa miaka 20 tunao uwezo wa kulipa, sisi Jiji letu la Mbeya tuisaidie Serikali yetu, wakati wanahangaika kutafuta fedha kwa ajili ya kujenga miradi mingine ya barabara ya njia nne, barabara za ndani ya jiji tunao uwezo wa kuzijenga kupitia vyanzo vetu vya mapato. Hilo linakuja na nitaomba waliangalie ili tuweze kuiweka Mbeya yetu katika hali nzuri na barabara ziweze kupitika vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni ukarabati wa masoko. Mimi ninajikita sana huko kwa sababu watu wa Mbeya ni wafanyabiashara, masoko yetu mengi yana hali chakavu na tumesema tunataka watu wetu wakajiajiri na maeneo ya kujiajiri ni maeneo ya masoko, lakini masoko yetu mengi ya Jiji la Mbeya yana hali mbaya sana. Wakati wa mvua wafanyabiashara wananyeshewa mvua, wakati wa jua wanapigwa na jua. Kwa hiyo, tunaomba kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu watuwekee bajeti kwa ajili ya ukarabati wa masoko yote yaliyoko kwenye Jiji letu la Mbeya ili yafanane na hadhi ya Jiji la Mbeya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, Mbeya ni lango la SADC, tunaomba pale na sisi siku moja tuje tu-host mikutano mikubwa kama wanavyo-host wenzetu wa Arusha mikutano – AICC, basi na sisi tuwe na ukumbi mmoja pale mkubwa utakaoweza ku-host mikutano ya SADC badala ya watu kutoka Nchi za Kusini mwa Afrika wanapita kwenye anga letu wanaenda kufanya mikutano Dar es Salaam. Tunaomba sana Wizara kwa maana Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI na Ofisi ya Mipango watusaidie jambo hilo ili siku moja nasi tuweze ku-host mikutano mikubwa na hiyo itakuwa njia pekee ya kuutangaza utalii wetu tulionao kwenye Mkoa wetu wa Mbeya na Mikoa yote ya Nyanda za Juu Kusini na Mbeya itakuwa ni center ya biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo michango yangu itajikita sana kwenye biashara kwa sababu sisi pale Mbeya tunafanya biashara. Pia suala la mikopo kwa vijana, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais ametuundia mpaka Wizara ya Vijana na tunaye Waziri machachali kabisa sina mashaka na yeye, hofu yangu inanijia kwa wale watu watakaokuwa wanamsaidia kazi, je ni watu wabunifu? Kwa sababu vijana wanayo staili yao jinsi ya kuishi nao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshapata Waziri mzuri, sawa Mheshimiwa Rais amefanya jambo jema ametuwekea pale bilioni 200 kianzio cha mtaji, lakini ninatamani ile bilioni 200 kuizalisha zaidi iwe mara tano ya ile bilioni 200, nayo inawezekana Wizara ya Vijana ijiongeze waweke vikao na hizi taasisi nyingine kwa maana hii Mifuko ya Hifadhi, ina pesa kule, lakini haiwekezi kwenye miradi ambayo itaongeza ajira kwa vijana wanawekeza kwenye kujenga majengo ambayo return yake ni ya muda mrefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ninawaomba kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Vijana ikae na hii Mifuko ya Hifadhi, wana pesa nyingi kule wawekeze kwenye miradi itakayoleta matokeo kwa vijana kujenga mabwawa ya umwagiliaji ambako kule vijana wengi watahitaji kwenye kilimo, kujenga zile skimu za umwagiliaji na masuala ya ufugaji wa samaki, ufugaji wa ng'ombe kule ndiyo kwenye matokeo. Maana yake unakuta Mifuko ya Hifadhi inaenda kuwekeza kwenye majengo ambayo unakuta return yake ni ya miaka 100 na wakati mwingine pesa hiyo hairudi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine kuna hawa watu wa TFS na TANAPA imekuwa ni tatizo kubwa, ni mgogoro mkubwa sana kila mahali kwenye nchi hii, hii tu inatokana na kwamba wao TFS hawazalishi wao ni regulator ili kufanya udhibiti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, siku moja nikawauliza watu wa TFS kwa nini ninyi mnawaambia wananchi waulinde msitu tu, wataulinda kwa miaka mingapi, badala ya ule msitu utumike kwenye kufuga nyuki, wale wananchi wa eneo husika wakafuga nyuki wakaulinda wao ule msitu, wakawa na chanzo kipya cha mapato badala ya kuwakataza kukata kuni, kukata mkaa lakini wakati huo hamuwapi njia mbadala ya kuzalisha lakini wakati huo TFS ataongeza mapato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, inasikitisha sana unaona juzi tu hapa niliongea na Waziri Mkuu, watu wa TANAPA, watu wetu wa Mbarali wamelima mpunga ekari karibu 2000, wanakwenda kuziteketeza wanasema wamelima maeneo yaliyotunzwa na ni eneo oevu. Sasa unajiuliza, yule mtu alipanda lini mpunga, wao walikuwa wako wapi? Tunamshukuru Waziri Mkuu aliliingilia kati akazuia, lakini wale watu walikuwa wamejiandaa, wanatumia fedha za Serikali kwenda kuteketeza mpunga ambao mwananchi anatakiwa avune baada ya miezi miwili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaona hili si jambo jema, tunaongea hapa watu wakajiajiri, tutengeneze ajira, watu wajiajiri kupitia kilimo, leo ekari 2000 zimelimwa, watu wanachukua pesa ya Serikali kwenda kuteketeza ule mpunga! Sasa hii ni namna ya kuichonganisha Serikali na wananchi na kuwachonganisha na Rais.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. PATRICK A. MWALUNENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono hoja na ahsante sana. (Makofi)