Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia kwenye bajeti hii ya Waziri Mkuu. Kwanza ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa kibali hadi nimeweza kusimama mahali hapa kwa ajili ya kuchangia. Ninakwenda moja kwa moja kwenye mchango wangu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Mbeya tunacho kilio na msiba mzito. Barabara ya Mkoa wa Mbeya kuanzia Igawa mpaka Tunduma ipo kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi iliyopita, barabara ile mpaka sasa hivi ina sintofahamu. Barabara ile tunamshukuru sana Rais aliongea kwa unyenyekevu na upendo mkubwa kwamba, barabara hii acha basi tuanzie Uyole mpaka tufike Airport Songwe, tulimshukuru sana Mheshimiwa Rais lakini ile barabara inakwenda kwa kusuasua sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba tumeanzia katikati Uyole, Rais ametujengea hospitali kubwa nzuri ya rufaa iko katikati ya Jiji la Mbeya, lakini pia bado ametujengea hospitali ya wanawake ambayo ni ya kujifungua wanawake wa Mkoa wa Mbeya kubwa sana ya Meta ukiachilia mbali vituo vya afya, Rais amejali sana wanawake, ameweka majengo ya mama na mtoto kwenye vituo vya afya vilevile.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya za Mkoa wa Mbeya ukianzia Mbalali ukienda Kyela, ukienda Rungwe, Jimbo la Busokelo, Mbeya DC, unapokwenda kuzifikia zile hospitali lazima upite katikati ya ile barabara. Barabara ile tunashukuru Serikali iliruhusu fedha kiasi cha shilingi bilioni 183 ili iende kujenga barabara ile. Mpaka sasa hivi miaka mitano ile iliyopita na sasa tumeingia awamu nyingine, barabara ile imejengwa kwa 44%. Ninaomba sana hiki kilio cha wananchi wa Mkoa wa Mbeya barabara sasa hivi katikati ya jiji pale ni vumbi tupu. Mvua ikinyesha ni matope matupu, jua likiwaka ni vumbi, yaani hakuna usalama wowote juu ya wananchi wa Mkoa wa Mbeya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Mkoa wa Mbeya tuna kilio kikubwa sana juu ya barabara ile, tunalia kilio hicho, ajali zinatokea za mara kwa mara, ndugu zetu wanapoteza Maisha, wanakufa, lakini pia wanaopata ajali wengine wanaumia wanabaki kuwa ni walemavu wanaugulia mahospitali mpaka sasa hivi. Ninaomba sana kwa ridhaa yako nimwombe sana Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan atuone wananchi wa Mkoa wa Mbeya, atuone kwa jicho la huruma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mama yetu huyu tunavyomjua, ana hekima ana busara wakati wowote, hapendi kuona wananchi wake wanateseka, tunaamini kwamba kwa kuliona hili atatusaidia wananchi wa Mkoa wa Mbeya ili tuache misiba pamoja na walemavu kwenye Mkoa wetu wa Mbeya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Mbeya tunajua Tanzania nzima inaombea Taifa amani, inaombea Serikali amani, inamwombea Rais, lakini Mkoa wa Mbeya ndiyo tunaongoza kwa maombi Tanzania nzima. Mkoa wa Mbeya una makanisa mengi sana tunapoanza kuomba lazima tumwombee Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, yeye pamoja na Serikali yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, achilia mbali makanisani hata misibani, wananchi wa Mkoa wa Mbeya misiba inavyotokea alfajiri tunapoanza kulia lazima tuombe sala, hiyo sala lazima wanawake wale wanavyoomboleza, wanamtanguliza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan wakimweka kwenye maombi, namna anavyoongoza Taifa hili la Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Mkoa wa Mbeya, kawaida yetu tunavyoomba, tunaomba kwa unyenyekevu tukipiga magoti.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwa sababu ninaheshimu Siwa ipo pale, nilipaswa niende pale nipige magotiā¦
MWENYEKITI: Mheshimiwa Suma, kuna taarifa. Mheshimiwa Musukuma.
TAARIFA
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka kumpa taarifa mzungumzaji kwamba suala la maombi ni siri ya mtu, akisema Mkoa wa Mbeya wanaomba sana, mimi kwa imani yangu ninaamini Mkoa wa Geita ndiyo tunaomba kuliko Watanzania wote.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Suma unaipokea hiyo taarifa?
MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo taarifa siipokei. Ninaomba sana Mheshimiwa Musukuma ninakuheshimu nipo serious hapa, kilio cha wananchi wa Mkoa wa Mbeya hajakijua na namna tunavyomwombea Rais hatuongei mdomoni tunamwombea kutoka moyoni, ninaomba sana atambue wananchi wa Mkoa wa Mbeya tukisema tunaomba, tunaomba kweli kweli, hatuombi kwamba tunafanya mizaha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeeleza kwamba hapa ninaheshimu Siwa kwa sababu ipo, Siwa isingekuwepo ningekuomba kwa imani yangu ningepiga nikuombe nipite pale mbele nipige magoti ili wajue wananchi wa Mkoa wa Mbeya tunaomba barabara ya Mkoa wa Mbeya kwa kumaanisha, tunaomba sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba Mheshimiwa Rais alichukue hili Mbeya jamani tuna kilio, tuna msiba, ninaamini Rais wetu kwa sababu ni msikivu amesikia, atatuondolea shida iliyopo katikati ya Jiji ambapo msongamano wa magari umekuwa mkubwa sana kwa sababu ya vumbi ile iliyopo pale, kwa sababu ya barabara mbovu na tope lililopo pale, ambulance zinavyotoka kwenye Wilaya zile kule kumkimbiza mgonjwa hospitali katikati ya Jiji hazipiti kwa wakati, sina namna ya kuongea zaidi ya hili ninaloliongea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Dkt. Samia Suluhu Hassan ni Mama msikivu, wakati wote ninamwongelea hilo kwa sababu ninamwelewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Rais alihamasisha nishati safi kwa ajili ya kupikia, wanawake ndiyo sisi wapishi wakuu, Mama yetu Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ndiye Mheshimiwa Rais wetu, yeye Rais katika hili kulikuwa na kilio kwa upande wa mbolea. Kilio kikubwa mfuko wa mbolea ulikuwa unauzwa zaidi ya 155,000. Rais alivyosikia hili jambo alitoa ruzuku mpaka sasa hivi mbolea inauzwa kwa bei ya pungufu karibu 75,000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba sana Rais hii nishati safi ambayo ameshatuzoesha kwa sababu tuliitikia sana, wanawake wa Tanzania waliitikia hasa wa Mkoa wa Mbeya, tunaomba ruzuku kwenye gesi ili nishati safi hii iendelee kutumika.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante.
MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona umewasha taa, ninaomba nisipoongea hili pengine ninaweza kuugua, ninaomba nijibu kuna swali moja la Watanzania ninaomba sekunde moja tu nijibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipindi cha uchaguzi tulikuwa na kikao wanawake, Mwenyekiti wetu Mheshimiwa Mary Chatanda, Ndugu Zainab Shomari pamoja na Katibu ambao ni viongozi wetu upande wa wanawake, kuna swali ambalo wanajiuliza Watanzania, ilikuwaje Dkt. Samia Suluhu Hassan apate 98% za ushindi. Ninataka niseme hivi, mwanamke akiwa na jambo lake hashindwi, hafeli, wanaume wanalijua hili, Mama jinsi ambavyo anaku-pet Baba, kukuomba kitu ambacho anakihitaji hajawahi ku-fail hata mara moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kina baba ambao ni wanaume zetu lakini pia watoto wetu tunakuwa tunawaheshimu na tunawapenda na heshima ni kubwa sana pale ndani, tulizidisha heshima, tulizidisha upendo, akina baba tuliwaomba kura walitusikia wakatupa kura za heshima za Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika wachache wale ambao wanajiuliza mpaka sasa, ninaomba niseme hivi kipindi kile hakukuwepo mama ambaye alikuwa mkali kwa baba kwamba, ulikuwa wapi? Kwa nini umechelewa? Hata baba akirudi saa sita za usiku alikuwa akipokelewa koti.
MWENYEKITI: Ahsante sana.
MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, akikaribishwa kwa upendo, ndivyo ambavyo tulipata zile kura na tulitegemea zingepatikana kura asilimia mia moja, kura mbili ndiyo zilipotea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)