Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mkinga
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. TWAHA S. MWAKIOJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, nitumie nafasi huu kumshukuru sana Muumba wangu kwa neema hii ya uhai, afya na baraka ya kuwepo katika ukumbi huu wa Bunge letu Takatifu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, ninakushukuru wewe kwa nafasi hii muhimu ya kuwasemea wananchi wenzangu wa Tanzania na kwa umaalumu wa kipekee wananchi wa Jimbo la Mkinga. Tatu, nitumie nafasi hii kumpongeza sana Rais wetu mpendwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna alivyotekeleza vyema Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi iliyoishia mwaka 2025.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza pia alivyomalizia utekelezaji wa Dira ya 2025 ambayo inamalizika Juni na alivyotekeleza kwa umahiri Mpango wa Tatu wa Maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo matatu ya mfano yaliyonigusa kufikia kusema, ninampongeza sana, eneo la kwanza, pamoja na changamoto nyingi za mwenendo wa uchumi duniani, lakini nchi yetu uchumi wake umeimarika na kuweza kufikia asilimia sita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili, ninampongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna alivyosimamia vyema ukusanyaji wa mapato, mapato yanayotokana na kodi na mapato yasiyotokana na kodi. Taarifa iliyopo katika hotuba ya Waziri Mkuu kuanzia Juni mpaka Februari, 2026, tuna ufanisi wa 103%. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la tatu, ninalompongeza Daktari ni kwa namna alivyoimarisha mahusiano ya Kitaifa na Kimataifa hadi miradi zaidi ya 927 yenye thamani zaidi ya shilingi trilioni 28, imesajiliwa. Kwa kweli pongezi kubwa kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Waziri Mkuu wetu kwa namna anavyotekeleza vyema majukumu yake, na kwa namna Wizara zake zilizopo katika ofisi yake zinavyotekeleza vyema majukumu yao na namna alivyotoa dira na mwelekeo wa nchi yetu wa mwaka 2026, katika hotuba aliyoitoa katika Bunge lako Tukufu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na maeneo mahsusi ninayoweza kuchangia, ninapenda nijikite katika maeneo matano yanayohusu Ofisi ya Waziri Mkuu ambayo mimi kwa maoni yangu ninatambua kwamba nchi yetu hatuna upungufu wa mipango mizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuna upungufu wa bajeti nzuri, hatuna upungufu wa mikakati, ila haya maeneo matano yakiimarishwa katika Ofisi ya Waziri Mkuu, ninaamini utekelezaji wa Dira inayoanza Julai na utekelezaji wa Mpango wa Nne unaweza kuleta matokeo tarajiwa makubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la kwanza ni namna ya kuboresha uratibu katika Ofisi ya Waziri Mkuu, uratibu ndani ya Bunge na uratibu nje ya Bunge. Serikali yetu imekuwa na changamoto kubwa ya coordination imekuwa na duplication ya effort ya sekta na sekta, imekuwa na mwingiliano wa majukumu, imekuwa na namna ya kunyang’anyana resources, imekuwa na namna ya kila mtu anavuta kwenye sekta yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili litawezekana tu pale ambapo Ofisi ya Waziri Mkuu itakapoweza kuunganisha kwa mfumo wa ki-digit usimamizi wa bajeti, usimamizi wa resources ili kuondoa utekelezaji wa majukumu uliopo kama vile kila sekta inafanya kama ipo kwenye kisiwa chake, kila mtu anafanya kama ni mpiga ngoma anawapigia watu wake peke yake ilhali sote tunamhudumia mwananchi mmoja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninatamani Ofisi ya Waziri Mkuu iwe kama Policy Coordination Hub yenye mfumo mmoja wa kidigiti unaoweza kuiangalia nchi moja, kwenye dashboard moja namna ya kutekeleza majukumu ya kila sekta ya MDAs na LGAs. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili ambalo ninataka nilizungumzie, ni eneo la ufuatiliaji na tathmini. Tumekuwa na utamaduni ambao kwa maoni yangu, ninauona siyo utamaduni mzuri. Tunaangalia ufuatiliaji na tathmini kwa kuangalia nimeweka fedha shilingi milioni 10, nimepata darasa moja hapo tumemaliza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatupimi matokeo yanayotokea kwa wananchi. Je, madarasa haya yanaleta matokeo gani kwa wananchi? Barabara hii tuliyoijenga inaleta matokeo gani? Kwa hiyo, hapa ninashauri tuimarishe mfumo wetu wa ufuatiliaji na tathmini ili kupima outcomes, kupima impacts na siyo kuishia kupima input na output kama inavyofanyika sasa hivi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo hili, ninashauri vipengele vitatu, tuimarishe au tutengeneze Mfumo wa Real Time Tracking System. Tuwe na mfumo ambao unakuonesha mradi huo uko sehemu fulani, uko hatua fulani, unatekelezwa na watu fulani, unaleta matokeo fulani mpaka wakati huu. Kuliko sasa hivi tunatumia sana physical monitoring ya kukimbizana, ya kukimbiza magari mengi, lakini tungekuwa na Mfumo ambao ni Real Time Tracking System, haya yote yangepungua, yangeleta ufanisi, yangepunguza gharama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine katika eneo la ufuatiliaji na tathmini, ninatamani tuwe na Performance Contracts za viongozi wetu mbalimbali wanaotarajiwa kutoa matokeo mbalimbali. Sasa hivi tunafahamu kiongozi fulani hajafikia matokeo yake, akifika Mheshimiwa Waziri Mkuu, au akifika Mheshimiwa Rais ndiyo tunaona kiongozi huyu hajakamilisha majukumu yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiwa na Performance Contracts ambazo zitakuwa zimeunganishwa na Mfumo wa Real Tracking System, hapa mapema kabisa ataonekana Mkurugenzi fulani, Mkuu wa Wilaya fulani, Waziri fulani hajatimiza wajibu wake, na hii inatosha kabisa kuchukuliwa hatua za wazi kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu katika eneo la Monitoring and Evaluation, ninashauri kwa miradi mikubwa ya kimkakati, tuwe na kitu kinaitwa Independent Evaluation. Tuwe na taasisi za nje ya mfumo wa Serikali ambazo zinaweza zikatufanyia tathmini ili tujione namna gani tunafikia matokeo, kuliko sisi wenyewe ni wachezaji na sisi wenyewe ni marefa na sisi wenyewe tunasema kwamba tumefikia hatua fulani. Kwa hiyo, jambo la pili ninashauri tuimarishe mfumo wetu wa Monitoring and Evaluation. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la tatu ninaloshauri katika Ofisi ya Waziri Mkuu ni eneo la kukabiliana na maafa, majanga na matukio ya dharura. Mfumo wetu umekuwa ni reactive sana kuliko proactive. Tunasubiri janga litokee halafu tunaanza kukimbizana resources zote zinaelekezwa huko badala ya kutekeleza bajeti iliyopangwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tukiwa reactive, tukiimarisha mfumo wetu wa Early Warning System tukawekeza hapo, basi tutaweza kukinga zaidi kuliko kuwekeza resources pale majanga yanapotokea. Eneo hilo la Waziri Mkuu ninashauri liweze kuimarishwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la nne ni urasimu, ucheleweshwaji wa maamuzi na uwajibikaji wa wazi. Kweli ninatambua urasimu ni sifa nzuri ya Serikali, lakini kwa maoni yangu urasimu umezidi, tunachelewesha utekelezaji, na maamuzi. Unakuta bajeti imefika katika taasisi husika ndani ya miezi mitatu hakuna hatua hata moja iliyochukuliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaona fedha za Serikali, Mheshimiwa Dkt. Samia anapeleka nyingi, tunasingizia Mfumo wa NeST kwamba unatuchelewesha siyo kweli, watendaji wetu hawachukui maamuzi. Tuimarishe eneo la maamuzi, tuimarishe eneo la kupunguza urasimu na uwajibikaji wa wazi. Hili tutaweza kwa kutumia takwimu sahihi, kwa kutumia teknolojia na watu wachukuliwe hatua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la tano kwa Ofisi ya Waziri Mkuu na la mwisho, na kisha nitasema eneo mahsusi kwa Ofisi ya TAMISEMI, ni namna gani tunaisimamia sekta binafsi? Tumeipa sekta binafsi jukumu kubwa sana la kutoa ajira zaidi ya 85%. Tumeipa jukumu kubwa katika utekelezaji wa dira itutafutie fedha zaidi ya 70% ili tufikie uchumi wa kati wa juu wa zaidi ya shilingi trilioni moja, tufikie uchumi wa mtu mmoja wa dola 7,000. Je, sekta hii binafsi tunaiamini kwamba inaweza kuyafanya hayo? Je, sekta hii binafsi tunaiwezesha?
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, sekta hii binafsi tunaiweka kwamba ndiyo mhimili; tuipunguzie milolongo ya urasimu, tuipunguzie tozo, tuipunguzie namna wawekezaji wanavyobambikiwa kodi, tuipunguzie mambo mbalimbali ili iwe mhimili mkubwa wa uchumi ...
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante.
MHE. TWAHA S. MWAKIOJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, bila sekta binafsi kuwa imara, hatutaweza kufikia matokeo tarajiwa ya utekelezaji wa Dira yetu. Haya ni maeneo matano nilitamani niyachangie katika Ofisi ya Waziri Mkuu. Nijielekeze katika eneo moja katika Ofisi ya TAMISEMI ...
MWENYEKITI: Mheshimiwa ahsante sana, kengele ya pili imelia.
MHE. TWAHA S. MWAKIOJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba dakika moja, nimalizie eneo moja, la elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua Mheshimiwa daktari ameajiri walimu wengi zaidi ya 40,000 kwa miaka yake, madarasa mengi yamejengwa, shule nyingi zimejengwa, lakini tuna changamoto ya ubora wa elimu. Tujikite sasa kwenye ubora, miundombinu iboreshwe, walimu wetu wapewe stahiki zao, shule zetu zinavuja, watoto wanakaa chini, vyoo, madarasa na kadhalika ili tupate elimu bora. Bila elimu bora hatutaweza kuondoa umaskini ...
MWENYEKITI: Mheshimiwa ahsante sana.
MHE. TWAHA S. MWAKIOJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuwasilisha, na ninaomba kuunga mkono hoja. Ahsanteni sana. (Makofi)