Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Dr. Catherine Canute Joachim

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. DKT. CATHERINE C. JOACHIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia hotuba ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka 2026/2027.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema kwa kutufikisha sote siku ya leo. Kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza kuchangia katika Bunge Tukufu la Kumi na Tatu, nianze kwa heshima na unyenyekevu kumshukuru Mwenyezi Mungu, na pia nimshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuridhia nikaweza kuchaguliwa kuwa Mbunge wa Viti Maalum Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ninawashukuru Wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalum wa Wazazi kwa kuweza kunichagua. Ninaomba kutumia fursa hii kuwaahidi uadilifu mkubwa, usikivu na ushirikiano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naungana na Wabunge wengine kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba nzuri, lakini pia ninampongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa mafanikio makubwa ya Serikali kwa mwaka huu wa fedha. Pia ninampongeza kwa kuweza kutoa hotuba ambayo imesheheni vipaumbele vya Serikali vinavyokwenda kutekelezwa tunapokwenda kuanza utekelezaji wa dira. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu katika hoja hii utajikita katika ukurasa wa 66 hadi 68 wa hotuba hiyo ambayo imejadili au imewasilishwa masuala yanayohusu lishe na mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa lishe, nianze kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wetu, kwa kuendelea kuwa kinara wa lishe. Tumemwona Mheshimiwa Rais kuanzia mwaka 2017 ameweka msukumo mkubwa katika masuala ya lishe, lakini kikubwa zaidi msukumo wake umekuwa katika masuala ya kutatua changamoto kubwa ya udumavu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais ameendelea kuweka mikataba na Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa na kuweka viashiria mbalimbali ambapo tulipomsikiliza Mheshimiwa Waziri Mkuu, imeonekana kwamba tatizo la udumavu limepungua kutoka 34% mwaka 2015/2016 hadi 30% mwaka 2022. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, Mheshimiwa Rais wetu, ametambulika kama kinara wa masuala ya lishe katika Bara la Afrika, na pia ni miongoni mwa Marais sita waliopo katika Presidential Dialog Nutrition. Jukwaa hili nimeleta lishe kama ajenda kuu ya maendeleo ya rasilimali watu na uchumi Barani Afrika. Ushiriki huu unaipa nchi yetu nafasi kubwa ya uongozi unaosukuma mabadiliko ya kisera na utekelezaji katika lishe katika ngazi ya kikanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ninampongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwani sote tunafahamu uratibu wa kisekta ya lishe unafanyika katika ofisi yake vilevile, Ofisi ya Rais, TAMISEMI ambaye ndiye msimamizi mkuu wa masuala ya lishe katika utekelezaji wa ngazi ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. Wamefanya kazi hii ya usimamizi kwa mafanikio makubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mafanikio ambayo yamepatikana. Tunaona kwamba Tanzania ina watoto takribani 3,400,000 ambao bado wana changamoto ya udumavu. Hii ina maana kwamba katika kila watoto watatu tunaowaona, mtoto mmoja ana changamoto ya udumavu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, bila kushughulikia changamoto za lishe kwa uzito unaostahili, tunaweza tusilifikie lengo la Taifa, lenye uchumi shindani unaotegemea rasilimali watu yenye afya, ujuzi na uwezo wa kushiriki katika uzalishaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, kwa kuwa changamoto hii iko na watoto, inakwenda kuathiri watoto hao ambao wana udumavu, watashindwa kufuatilia masomo yao vizuri. Pia tafiti zinaonyesha, watoto ambao wamekuwa na hali ya udumavu, mchango wao katika uzalishaji unapungua kwa 20%.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo ninapenda kushauri maeneo ya kisera ambayo yamewekewa msukumo mkubwa. Tunafahamu kwamba halmashauri inatakiwa kutenda shilingi 1,000/= kwa kila mtoto kwenye halmashauri husika. Hivyo, nilikuwa nashauri takwa hili liwe la kisheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, changamoto ya udumavu iko katika halmashauri ambazo zina changamoto, zinazalisha chakula kwa kiwango kikubwa. Hivyo, nilikuwa nashauri, uzalishaji wa chakula ufungamanishwe na masuala ya lishe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, nilikuwa nashauri tafiti za masuala ya lishe zitengewe fedha, kwani mila na desturi katika mikoa zinatofautiana. Takwimu hizi zitaweza kuelezea nini mikoa ifanye ili kutatua changamoto za udumavu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa haraka haraka, nitakwenda kujielekeza katika mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI. Nianze kuipongeza Serikali kwa kuendelea kutoa huduma bure kwa watu wote ambao wana maambukizi ya VVU na UKIMWI, kuanzia mwaka 1983 janga hili lilipogundulika hapa nchini. Vilevile, ninaipongeze Serikali kwa kuweza kuanzisha tozo kwa ajili ya kugharamia gharama za UKIMWI. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sote tulisikia mwaka 2026 kwa mara ya kwanza, Serikali imeanzisha tozo ili kuweza kukabiliana na changamoto ya kupungua kwa fedha. Hivyo, ninaipongeza sana Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwani suala hili limekuwa likifanyiwa kazi kwa takribani miaka kumi iliyopita. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, pamoja na mafanikio ya kupunguza maambukizi mapya na vifo vitokanavyo na UKIMWI, bado tuna changamoto kubwa ya maambukizi mapya kwa vijana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa utafiti uliofanyika mwaka 2022 maambuki ya UKIMWI kwa mwaka yamekuwa kwa watu 56,000, lakini tukiangalia katika taarifa ile 70% ya watu wanaopata maambukizi mapya ni vijana wa kike. Hivyo, kundi hili liko katika hatari ya kutoweza kuchangia katika shughuli za uzalishaji mali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine kikubwa ambacho tunakiona ni gharama kubwa za dawa. Mgonjwa anayetumia dawa za UKIMWI, gharama yake ni shilingi 550,000 kwa mwaka. Hivyo, ukiangalia kwa sasa hivi, katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ilionesha tuna watu takribani 1,500,000 wanaohitaji dawa hizi za Virusi vya UKIMWI. Hivyo, kama nchi tunahitaji zaidi ya shilingi bilioni 800 kugharamia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, nilikuwa nina ushauri wa kisera katika maeneo makubwa matatu. Cha kwanza, ni kuongeza vyanzo ili tuweze kujitegemea zaidi; cha pili, ni kuweza kuwa na mkakati maalumu wa kinga ili kuweza kuzuia vijana wetu wa kike kupata UKIMWI; cha tatu, ni kuweza kufungamanisha huduma za UKIMWI katika bango kitita la mafao la Mfuko wa Bima ya Afya kwa Wote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)