Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. SHEILA E. LUKUBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii niweze kuchangia hotuba ya Waziri Mkuu ya Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka 2026/2027.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, ninapenda kumshukuru Mungu Mwingi wa Rehema kwa kutujalia afya njema nami leo nimeweza kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kumshukuru kwa dhati ya moyo wangu Rais, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi na vikao vyake vyote anavyoviongoza kwa kuniteua mimi na hatimaye nikachaguliwa kuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ninasema, ahsante sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawashukuru wananchi wa Mkoa wa Morogoro hususan wanawake wa Mkoa wa Morogoro kwa kumchagua Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kura nyingi za kishindo na mimi kunituma Bungeni kuwa mwakilishi wao. Ninawaahidi sitawaangusha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nitoe shukrani zangu za dhati kwa Mwenyekiti wangu wa Kamati ya Ulinzi na Usalama, gwiji wa mapinduzi ya uchumi wa kilimo Adam Kighoma Malima. Huyu Mkuu wa Mkoa anafanya kazi usiku na mchana bila kuchoka kumsaidia Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa aliyoifanya na anaendelea kufanya makubwa chini ya uongozi wake, miradi mingi imetekelezwa.
Mama piga kazi, wewe ni nguvu ya wanawake, tumaini la Taifa na chachu ya maendeleo endelevu. Mama ninakupa mstari kwenye Biblia ambao utakutia nguvu. Isaya 41:10, “Usiogope, maana mimi ni pamoja nawe, usifadhaike maana mimi ni Mungu wako, nitakutia nguvu nami nitakusaidia.” Mheshimiwa Rais ninakutia nguvu, sisi ni jeshi kubwa. Tutakulinda chini ya Mwenyekiti wetu mama Marry Chatanda. Piga kazi Mama tupo pamoja na wewe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba pia nimpongeze sana Waziri Mkuu, ndugu yangu, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba kwa kuonesha mfano wa kuigwa wa kuwafuata wananchi kwenye maeneo yao na kuwasikiliza kero zao na kuzipatia majawabu hapo kwa hapo. Hongera sana Mheshimiwa Waziri Mkuu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, viongozi wanaomsaidia Mheshimiwa Rais, hasa wale wateule, Mheshimiwa Waziri Mkuu ameonesha njia. Njia hii itawafanya wananchi kuendelea kuwaamini viongozi wao na Serikali kwa ujumla, pia itawasaidia wananchi kupata suluhisho sahihi la matatizo yao, na pia itasaidia kusikiliza kero mara kwa mara na kupunguza migogoro hiyo. Ameonesha mfano wa kuigwa, kwa hiyo, nanyi Wizara ninawaomba msibaki nyuma, fuateni nyayo zake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaungana na Wabunge wenzangu wa Mkoa wa Morogoro ambao wameshachangia. Sisi Mkoa wa Morogoro kipaumbele chetu cha kwanza kwa sasa ni barabara, hasa ukizingatia Morogoro ni ghala la chakula na sasa tumepata ghala la pili, Bwawa la Kidunda ambalo litahudumia Mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na maeneo ya jirani na mradi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo ninaomba Mheshimiwa Waziri Mkuu, Morogoro iangaliwe kwa jicho la kipekee kuhusu suala zima la barabara. Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan alikuja na falsafa zake nne za 4R, lakini Waziri wa Maendeleo ya Jamii pia naye ana kauli mbiu yake, “kaza kazawa” (kasi zaidi, karibu zaidi na wananchi).
Mheshimiwa Mwenyekiti, nami leo ninakuja na kaulimbiu yangu ya 4K kwenye suala zima la mikopo. ‘K’ ya kwanza, ni kutenga fedha za mikopo kwenye bajeti. Kuhakikisha halmashauri zetu zinatenga fedha za mikopo kama ilivyoelekezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ‘K’ nyingine ni kutoa mikopo yenye tija kwa walengwa. ‘K’ nyingine ni kufuatilia wakopaji ili kufahamu maendeleo yao na pia waweze kusaidiwa kupata masoko ndani na nje ya nchi. ‘K’ nyingine ni kuhakikisha kurejeshwa kwa mikopo hiyo kwani mikopo hiyo ni revolving fund. Ameonesha mfano wa kuigwa, kwa hiyo, nanyi Wizara ninawaomba msibaki nyuma, fuateni nyayo zake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuchangia Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu na Watu wenye ulemavu. Mheshimiwa Waziri Mkuu, kama ulivyoshuhudia katika ziara zako, matatizo mengi yaliyowasilishwa kwako na wananchi ni masuala ya ustawi wa jamii. Mfano migogoro ya ndoa, mirathi, matunzo ya watoto na vitendo vya ukatili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, nimefanya utafiti wangu usio rasmi na nimegundua kwamba kada hii ya ustawi wa jamii ina watumishi takribani 2,238, lakini pia ina upungufu wa watumishi takribani 18,000. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaiomba Serikali yangu Tukufu iweze kuiangalia kada hii ya ustawi wa jamii waweze kuongeza na wakishaongeza, watu hawa watakwenda mpaka kwenye kata na vijiji kufanya kazi na ustawi wa jamii. Pia watatusaidia katika suala zima la mmomonyoko wa maadili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ilhali tumeshuhudia kwenye maafa mbalimbali Maafisa Ustawi wa Jamii hawa wakitumika, mfano mafuriko ya Hanang’, janga la Kariakoo na mafuriko ya Kibiti, kada hii ni muhimu sana kwa makundi maalum ikiwemo watoto walio katika mazingira magumu, wazee na watu wenye ulemavu. Wote hawa wanahudumiwa na Maafisa Ustawi wa Jamii katika ngazi mbalimbali ikiwemo Serikali za Mitaa, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Wizara ya Afya na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kukosekana kwa mamlaka moja inayosimamia huduma za ustawi wa jamii kuanzia ngazi ya juu hadi ya chini, kunapunguza ufanisi wa huduma hizo. Je, Serikali sasa haioni umuhimu wa kuwa na Idara ya Ustawi wa Jamii katika ngazi za mikoa na mamlaka za Serikali za Mitaa ili kuweka vipaumbele vyao na bajeti zinazotekelezeka ili kuimarisha huduma za ustawi wa jamii? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu kwa sasa hivi wanategemea bajeti ya DMO ambaye naye anazidiwa anakuwa na vipaumbele vyake. Hivyo, ninaiomba Serikali ione umuhimu wa kuanzisha Idara ya Maafisa Ustawi wa Jamii.
MWENYEKITI: Ahsante sana.
MHE. SHEILA E. LUKUBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba dakika moja nimalizie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Maafisa Ustawi wa Jamii wanafanya kazi zao chini ya Ofisi ya Mganga Mkuu. Wengi hawana ofisi na wanashughulikia masuala mbalimbali na kusikiliza masuala nyeti ya kijamii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba basi, kwenye halmashauri zetu Maafisa Ustawi wa Jamii hawa wapewe ofisi ili waweze kufanya kazi zao vyema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono hoja. (Makofi)