Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Zena Maulidi Katambo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. ZENA M. KATAMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia fursa na mimi kuchangia leo katika hotuba ya Waziri Mkuu. Kwa kuwa leo ni mara yangu ya kwanza, ninaomba nitumie fursa hii kuwashukuru wanawake wa Mkoa wa Lindi ambao wameniwezesha kunifikisha hapa leo hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatumia jukwaa hili kuwaeleza kwamba nitawapa uwakilishi ambao umetukuka na nipo tayari kuwatumikia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo, kwa dhati ya moyo wangu ninampongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anayoifanya kwa kujitolea kwake kwa hali na mali kuhakikisha kwamba nchi yetu inapata maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee, ninamshukuru Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, tumemwona katika kipindi ambacho yupo kwenye nafasi hii amezunguka katika maeneo mbalimbali nchini na kufanya ziara ambapo katika ziara hizo amefanya shughuli mbalimbali na kutatua kero mbalimbali za wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie fursa hii kumtia moyo Waziri Mkuu, nimweleze kwamba wananchi tunafurahishwa na kasi yake ya utendaji kazi na kwamba aendelee hivyo hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo, mchango wangu kwa siku ya leo katika Wizara hii ninauelekeza kwenye barabara. Mkoa wa Lindi tunazo changamoto kubwa sana za miundombinu ya barabara. Barabara hizi changamoto inaanzia barabara kuu ambayo inaunganisha Mkoa wa Lindi na Dar es Salaam.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika barabara hii tumepitia changamoto mbalimbali ambapo katika msimu wa mvua wa mwaka 2024 ambao nchi yetu tulikumbwa na Kimbunga Hidaya, Mkoa wa Lindi, barabara hii iliathirika kwa kiasi kikubwa na kuharibika kwa madaraja, na pia sehemu kubwa ya barabara kuharibika vibaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hali hiyo, ninaipongeza Serikali kwa jitihada zake ambazo imefanya kwa kurekebisha yale madaraja makubwa ambayo yalikuwa yanaathiri matumizi ya barabara ile ambapo kwa kipindi cha mwaka 2025 wananchi wa Mkoa wa Lindi ni mashahidi kwamba baadhi ya nyakati tulilazimika kukaa kusubiri kungojea maji yapungue ili tuendelee na safari zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa Serikali imemaliza changamoto ile ya upande wa madaraja na kwamba sasa angalau tuna uhakika wa kusafiri moja kwa moja kutoka Dar es Salaam mpaka Lindi. Hata hivyo, tunayo changamoto nyingine katika barabara hiyo ambapo ile athari ya mvua iliharibu maeneo mengi ambapo barabara ile ina mashimo mengi, kwa kweli haipitiki vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, katika changamoto hii Serikali imejitahidi kuziba viraka katika barabara ile ili angalau wananchi waendelee kuitumia. Kutokana na uharibifu ule mkubwa, ninaiomba Serikali, sisi wananchi wa Mkoa wa Lindi suluhisho la kudumu tunaomba tujengewe barabara mpya ili kusudi iendane na mahitaji ya sasa tuliyonayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba barabara hii mpya kwa sababu tunafahamu kwamba Mkoa wa Lindi kwa sasa kuna miradi mbalimbali ya kimkakati ambayo inafanyika. Miongoni mwa miradi hiyo ni pamoja na bandari ya uvuvi iliyopo Wilayani Kilwa. Bandari hii Serikali imewekeza shilingi bilioni 280.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na uwekezaji huo, tunaiomba Serikali itutengenezee hii barabara kuu ili jitihada ambazo zimetumika kuwekeza kwenye mradi ule ziendane na miundombinu yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo, tunazo changamoto za barabara za ndani ya mkoa. Mkoa wa Lindi hauna wilaya ambazo zimeunganishwa kwa lami kati ya wilaya na wilaya. Hivi hapa tunavyozungumza, wananchi wa Wilaya ya Liwale ambao wanapitia barabara ya Nangurukuru kwenda Dar es Salaam hawawezi kusafiri siku ya leo, tangu jana barabara zimeharibiwa na mvua kubwa ambazo zinaendelea kunyesha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa Wilaya ya Nachingwea, wananchi wa Kilimalondo - Mbondo, wananchi wa Kilimalondo - Kiegei - Namapwia - Nero Mission hawawezi kusafiri kati ya maeneo hayo kwa sababu mvua hizi zinazoendelea zimekata madaraja katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa Wilaya ya Kilwa tunazo kata za Kandawale, Njinjo, Kipatimu, Kibata ambapo katika kata hizi wananchi hawawezi kuingia wala kutoka nje ya maeneo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Wilaya ya Ruangwa tunazo changamoto katika kata ya Matambalale, Chunyu, Nambilanje na Mandawa. Kwa ujumla tunaomba Serikali itusaidie kupitia TARURA kujenga madaraja na kwa awamu ya kwanza ituletee madaraja katika barabara hizi kwa sababu kiujumla hizi changamoto zimekuwa ni zile ambazo zinaendelea. Hizi changamoto ni zile ambazo zinatokea kila mwaka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, katika harakati za kutibu tatizo hili, tunaomba Serikali itujengee madaraja ili wananchi waendelee na shughuli zao za maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni umeme. Utakubaliana na mimi, Mkoa wa Lindi huenda ndiyo mkoa pekee au labda imebaki mikoa miwili mitatu ambayo bado haijaunganishwa kwenye gridi ya Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na kutokuunganishwa na gridi ya Taifa mkoa wetu una changamoto kubwa ya ukosefu wa umeme wa uhakika. Kwa Mkoa wa Lindi, umeme kukatika mara 10 mpaka 20 kwa siku ni jambo la kawaida. Hali hii inatuathiri sana wananchi wa Mkoa wa Lindi, lakini pia tunapata athari za kiuchumi ambapo tunakosa wawekezaji ambao wapo serious kwa ajili ya kufanya miradi mbalimbali ya maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaiomba Serikali, kwa kuwa sasa hivi nchi yetu tunazalisha umeme zaidi ya mahitaji yetu, ninaiomba Serikali ituunganishe na sisi wananchi wa Mkoa wa Lindi ili kusudi na sisi tuweze kunufaika na hii keki ya Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo, nimalizie kwa kuipongeza Serikali katika mradi wa LNG. Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa sasa hivi ipo kwenye hatua za mwisho za kusaini makubaliano ya utekelezaji wa uzalishaji wa gesi ya asilia kupitia mradi wa LNG Mkoani Lindi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi huu una thamani ya shilingi trilioni 100. Huu ni mradi mkubwa kuliko mradi wowote ambao nchi yetu ya Tanzania imewahi kuutekeleza. Mradi huu unasubiriwa sana na wananchi wa Mkoa wa Lindi, kwa sababu hii ilikuwa ni ahadi tangu Serikali ya Awamu ya Nne; ilituahidi kutekeleza mradi huu, lakini hatukufanikiwa, Serikali ya Awamu ya Tano na mpaka sasa ya Sita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi wananchi wa Mkoa wa Lindi kwa kweli tumeusubiri sana mradi huu, tunatamani na tunaiomba sana Serikali iharakishe zoezi la usajili na kusaini documents za makubaliano ili kusudi mradi uanze kazi, na pia uweze kuchangia kwenye Taifa na dunia kwa ujumla kwa sababu unalenga kuuza gesi ndani na nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ninaunga mkono hoja. (Makofi)