Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Zuena Athumani Bushiri

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. ZUENA A. BUSHIRI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na mimi kwa kunipa nafasi ya kuchangia hotuba hii ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, ninamshukuru Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema kwa kutufikisha sote siku hii ya leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa ambayo anaifanya katika hali ya kulijenga Taifa hili la Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze pia Waziri Mkuu kwa kazi kubwa ambayo anaifanya ya kumsaidia Rais na ziara ambayo ameifanya katika halmashauri zetu zote ambayo imeleta tija kubwa sana, bila kuwasahau Mawaziri wote na Manaibu Waziri kwa kazi kubwa ambazo wanazifanya za kumsaidia Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo katika hotuba ya Waziri Mkuu nitachangia mambo matatu kama muda utaniruhusu. Nitaanza na afya, nitakuja na shilingi bilioni 200 kwa vijana na nitakuja na mikopo ya 10% ya halmashauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na afya. Hakuna Taifa bila afya. Ili Taifa liweze kusonga mbele kwa kazi zake zote, ni lazima wananchi wake wawe na afya ya kutosha. Tumemwona Mheshimiwa Rais kazi aliyoifanya katika sekta ya afya, kuanzia ngazi ya zahanati hadi hospitali za kikanda. Hii inaonesha wazi kwamba Mheshimiwa Rais anawajali sana na anazijali sana afya za Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ukurasa wa 64 imeeleza, kwamba mwaka 2024 tulikuwa na wastani wa 80% katika vituo vya kutolea huduma. Hadi Februari, 2026 tuna wastani wa 89%. Hii ni hatua kubwa sana. Watanzania tumpongeze sana Mheshimiwa Rais. Mheshimiwa Rais amehakikisha tiba za kibingwa na bingwa bobezi zinapatikana hapa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zamani tulikuwa tunasafiri kwenda nchi za nje, hasa India, kwenda kutafuta matibabu na vipimo, lakini kwa sasa hivi Mheshimiwa Rais amejitahidi sana. Kwa mfano, kipimo cha saratani aina ya Pet/CT scan, bei yake ni shilingi bilioni kumi na nane na pointi. Mheshimiwa Rais ameguswa na shida za Watanzania ambao wanaumwa ugonjwa huu wa saratani, akahakikisha kipimo hiki anakileta katika nchi yetu, ambacho kimesaidia sana Watanzania. Tumpongezeni sana Mheshimiwa Rais kwa hatua hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna huduma ya upandikizaji wa figo. Mwanzo ilikuwa inapatikana katika nchi za nje. Tulikuwa tunaenda Nairobi na nchi nyingine za nje kupata huduma hii, lakini kwa sasa hivi huduma hii iko Muhimbili, na hapo Benjamini Mkapa. Ni hatua kubwa sana. Watanzania tumpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anayofanya katika sekta hii ya afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii imefungua njia mpaka nchi za nje sasa zinakuja kupata matibabu nchini kwetu, ikiwemo nchi za Comoro, Congo, Malawi Zambia, Burundi na nchi nyingine. Ni hatua kubwa sana kwa Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu kwa Serikali, ninaiomba sana Serikali iongeze ajira ya watumishi katika kada hii ya afya ili iendane na vituo vya kutolea huduma, iweze kuwasaidia. Pia ninaomba mfumo wa tiba mtandao ushuke kutoka katika hospitali za rufaa na mikoa hadi katika hospitali za wilaya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu wa pili, utakuja katika shilingi bilioni 200 za vijana. Tarehe 5 Februari, 2026 Serikali imetoa shilingi bilioni 200 kwa ajili ya mikopo kwa vijana. Vijana wetu wametafutiwa kila njia ya kujikwamua kiuchumi. Ukiingia katika mikopo ya halmashauri ya 10%, vijana wapo. Hata hivyo, Mheshimiwa Rais akaona haitoshi, atakawatafutia shilingi bilioni 200 ili kuwawezesha kiuchumi waweze kufanya biashara zao. Hongera sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombe vijana wakiwemo vijana wangu wa Mkoa wa Kilimanjaro wachangamkie sana fursa hii. Kazi aliyoifanya Mheshimiwa Rais ya kutafuta hizi fedha ni sababu ya kuhakikisha kwamba kila kijana anajikwamua kiuchumi. Watumie fursa hii ili walete maendeleo katika familia zao na Taifa kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu katika fedha hizi, tumeona changamoto iliyokuwepo mwanzo katika fedha za 10% za halmashauri. Utaratibu ule wa mwanzo haukuwa mzuri mpaka Mheshimiwa Rais alifika mahali akaona abadilishe utaratibu ukaja utaratibu wa pili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa fedha hizi shilingi bilioni 200 ninaiomba Serikali isimamie na iratibu utoaji wa fedha hizi ili zikatumike vizuri kwa lengo lile ambalo limekusudiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije sasa katika 10% za halmashauri, wenzangu wameongea, zipo changamoto. Changamoto kubwa ambayo inaonekana ni ujazaji wa lile dodoso.
Mheshimiwa Mwenyekiti, dodoso lile ni wachache ambao wanaweza kulitumia. Ukizingatia kuwa asilimia kubwa ya walengwa wa mikopo hii ni wale akina mama wanaoishi vijijini ambao hawawezi hata kufanya biashara kubwa, lakini utakuta Maafisa Maendeleo ya Jamii wanawatuma na kuwaambia waende wakajaze dodoso, kitu ambacho hawawezi. Matokeo yake wanaondoka wanaenda kwenye stationery wanatozwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwanamke wa kijijini wakati mwingine hata fedha ya kununua mchicha hana, ukimwambia habari ya kwenda kulipa stationery ili apate mwongozo wa kujaziwa lile dodoso kwake ni msalaba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaiomba Serikali yangu sikivu isimamie kwa makini suala hili na kuwatoa Maafisa Watendaji wa kata maofisini washuke chini wakiiga mfano wa Waziri Mkuu alichokifanya juzi. Waende wakawaone wananchi makundi yote, vijana, walemavu na wakina mama wawasaidie ili waweze kupata fedha hizi kwa ajili ya kufanya biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais amegusa sana mikopo hasa kwa vijana. Sasa kama sisi Serikali tukiisimamia vizuri, hawa vijana wetu ambao wanazunguka mitaani kila siku hawana kazi za kufanya, wakitumia mikopo hii watajikwamua kiuchumi na hatimaye Taifa kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo ninaunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)