Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Mwamengo Ulimboka Baraka

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kyela

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. BARAKA A. U. MWAMENGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kukushukuru kwa kunipa nafasi hii kuchangia Ofisi hii ya Waziri Mkuu. Kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, aliyetufikisha siku ya leo tukiwa wazima, wenye afya njema na leo tupo Bungeni hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii pia kuipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kupitia kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais na jemedari wetu kwa jinsi ambavyo ameendelea kuisimamia Serikali na malengo mazima ambayo yanatufanya tunaendelea kupanga bajeti hizi na fedha zinatolewa katika Majimbo yetu. Ninaishukuru sana Serikali na ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, ninamshukuru mwasilishaji wa bajeti hii ambaye ni Waziri Mkuu, kwa jinsi ambavyo amefanya ziara ndani ya majimbo yetu na katika wilaya zetu mbalimbali, ameendelea kusimamia kile ambacho aliahidi hapa kuwa anaenda kusimamia katika utekelezaji wa majukumu ya Serikali. Kama Mtendaji Mkuu wa Serikali, ameendelea kufanya haya kwa kumaanisha na kuendelea na ziara ambazo tunaamini zinaleta tija ndani ya majimbo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamwomba tu, kwa sababu ndani ya Jimbo langu aliahidi kurudi tena, basi ninaomba, kwa sababu hakufanya mkutano, aliahidi kurudi tena, ninamwomba pale atakapopata nafasi, aweze kurudi ili akafanye mikutano kama alivyokuwa ameahidi alipokuwa ameshindwa kufanya mkutano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maneno hayo, nianze kuchangia pia kutoa pole kwa maeneo mbalimbali ambayo yamepata mafuriko kwa mvua ambayo ni neema ya Mungu, ametupatia, lakini pale ilipozidi, tutoe pole sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee sana nitoe pole kwa wananchi wa Jimbo langu ambao kwa sehemu kubwa wameathirika na mafuriko hayo ya mvua zinazoendelea. Nitoe pole sana kwa walioathirika, baadhi ya Kata za Katumbasongwe, Bujonde, Ngonga, Kanjunjumele, Lusungo na baadhi ya maeneo ya Mapwale ambayo yameathirika sana na mvua hizi zinazoendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kutoa pole hizo, ninaomba kutoa mchango kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hotuba aliyowasilisha Waziri Mkuu, ninapongeza pia kwa jinsi ambavyo TARURA wamekuwa wakifanya kazi nzuri sana, na Mheshimiwa Prof. Shemdoe, Waziri wetu wa TAMISEMI, lakini baada ya mvua hizi na maeneo mengi yameathirika na mvua hizi, hasa Jimbo langu la Kyela, kwa sababu ni Jimbo ambalo lipo ukanda wa chini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kipekee sana TARURA wapewe fedha za dharura ili kuweza kwenda kuirekebisha ile miundombinu ambayo imeharibika kwa sehemu kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika majimbo yetu na hasa katika Jimbo langu, Kata za Nkokwa, Katumbasongwe, Lusungo ambazo mpaka sasa hivi baadhi ya maeneo kama daraja la Ngana - Ushirika ambapo wanafunzi wamelazimika kuahirisha kusoma eneo moja na wamehamia shule nyingine kwa sababu ya kushindwa kuvuka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaiomba Ofisi ya Waziri Mkuu, ichukue jambo hili na iipe udharura wa pekee ili tuweze kujenga lile daraja la Ngana na wanafunzi wa Ushirika waweze kwenda masomoni kama ambavyo walikuwa wanaendelea na masomo kama kawaida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninafahamu kuwa kuna mpango mkubwa wa TARURA kupewa fedha za dharura, lakini nilikuwa ninaiomba Serikali kuwa ichukue kipaumbele katika yale maeneo ambayo yana athari kubwa kwa wananchi ili kuweza kurudisha ile furaha ya wananchi wa maeneo husika hasa katika majimbo ambayo yameathirika na mvua hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulingana na mvua ambazo zinaendelea kunyesha kila wakati, Jimbo letu la Kyela linakuwa inaathirika kwa ukanda wa kusini. Kuna mradi mmoja ambao kama Serikali itauwekea kipaumbele na kuanza kuutekeleza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaamini kabisa kwamba tutaondoa kero kwa wananchi wa Jimbo la Kyela. Mradi huo ni wa Songwe Basin ambao uko chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Ninaomba sana ule mradi wa Songwe Basin ambao una components nyingi ndani yake, ambao tukizungumza, leo utakuwa mkombozi kwa sehemu kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninafahamu kuwa Serikali ipo katika hatua za kumtafuta mkandarasi au tunamwita transaction advisory. Ninaomba katika ile PPP, tuangalie zile components ambazo zinaweza zikawa zinakubalika kwa watu ambao wanataka kuwekeza kwenye PPP, ili twende haraka, ule mradi uanze kufanya kazi kwa sababu unahusisha ukanda wa kwetu na nchi jirani ya Malawi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi ule tukiusimamia vizuri, ninaamini kabisa utakuwa ni suluhisho la mafuriko ya kata zote ambazo ziko ukanda wa Katumba Songwe na mpaka wa kati ya Malawi na Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba mradi huo upewe kipaumbele, kwa sababu sasa hivi walikuwa wanaendelea na mchakato huo. Nilikuwa ninaomba waongezewe nguvu kwa sababu mradi huo utakuwa ni ukombozi kwa Wilaya ya Kyela na wilaya nyingine nne ambazo zitakuwa zimepitiwa na mradi huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaiomba Serikali kupitia kwa Waziri Mkuu, na alivyofika Kyela, tulimwambia na tulimshauri kuwa mradi huo upewe kipaumbele katika miradi ambayo Serikali itatoa kipaumbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa muda wetu unakimbia, ninaomba nizungumzie upande wa zao letu la kokoa. Zao letu la kokoa tunaendesha kwa Mfumo wa Stakabadhi Ghalani, lakini kupitia stakabadhi za ghala, bei imeendelea kushuka kwa jinsi ambavyo huko nje wanaendelea kupigana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba Serikali angalau waone uwezekano, kama alivyoahidi Mheshimiwa Rais katika hotuba yake na katika kampeni za uchaguzi wa mwaka huu kuwa atatujengea kiwanda cha kuongeza thamani zao la kokoa. Zao la kokoa lilifika zaidi ya shilingi 32,000 kwa kilo moja. Sasa hivi ninavyozungumza, mnada wa jana ulikuwa shilingi 7,020. Hivyo, wananchi wa Kyela wamekuwa wakiathirika sana kwa kushuka kwa bei ya zao hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kwa kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, waone uharaka wa kujenga kiwanda ndani ya Jimbo la Kyela ili zile tani 9,000 mpaka 10,000 tunazozalisha za zao la kokoa ziongezewe thamani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaamini, kwa kuongezewa thamani kule, kutafanya kuwa wakati pale ambapo bei zitakuwa zinashuka katika soko la dunia, zao liweze kuendelea kupatikana na kuwasaidia wananchi wa Kyela kuendelea kupata bei nzuri ya zao lile. Hii ni kwa sababu kwa uchumi na biashara kubwa, sisi Kyela zao la kokoa ndilo dhahabu yetu na ndiyo uchumi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika baadhi ya maeneo sasa hivi Tanzania yameanza kulima zao lile kwa sababu limekuwa likiingiza fedha nyingi za kigeni, hasa kwa wakati ule ambapo bei inakuwa juu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba jambo hili lipewe kipaumbele kikubwa ili angalau kuweza kuanza ujenzi. Maeneo yapo tayari ambayo ni kwa ajili ya uwekezaji wa kiwanda cha zao la kokoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ninakushukuru sana. Ninaunga mkono hoja. (Makofi)