Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Njombe Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia kwenye hoja iliyopo mbele yetu inayohusiana na hotuba ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya njema ili kuweza kusimama hapa leo na kuweza kutoa mchango wangu angalau kwa kifupi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza sana Waziri wetu Mkuu kwa kuwasilisha bajeti nzuri sana, bajeti ambayo inatoa mwelekeo wa utendaji wa Serikali. Siyo utendaji tu, lakini na makadirio ya matumizi na mapato kwa kipindi cha 2026/2027.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Watu wa Njombe, tumekuwa ni wanufaika wakubwa wa miradi mbalimbali ambayo tumeipata katika kipindi hiki cha bajeti iliyopita, lakini katika kipindi cha miaka mitano ya Serikali ya Awamu ya Sita. Tuna kila sababu ya kumshukuru sana Rais kwa mambo mengi makubwa ambayo ametufanyia wananchi wa Njombe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mambo ambayo yamefanyika katika maombi ya kawaida ya kibajeti, lakini kuna mambo yamefanyika kwa sababu tumemwomba Rais moja kwa moja alipotutembelea Njombe, na tuna mifano mingi ya mambo hayo na ndiyo maana tuna kila sababu ya kusema ahsante kwa mambo hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuwa hatuna Chuo Kikuu Njombe, na tumekuwa na kiu ya muda mrefu sana ya kuwa na Chuo Kikuu, lakini Mheshimiwa Rais alitoa kibali cha haraka, leo tunavyoongelea Chuo Kikuu cha UDOM, campus ya Njombe inajengwa kwa speed kubwa sana, na mwaka huu intake ya kwanza inaingia pale Njombe kwa ajili ya kujifunza masuala ya ujasiriamali yanayoendana na rasilimali zilizopo Njombe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuwa hatuna uwanja wa ndege wa kisasa, tumemsikia Naibu Waziri, akijibu maswali hapa, akionesha namna gani Wananjombe tuliomba jambo hili na Serikali imelisikiliza na imeamua kulitekeleza, na sasa mchakato upo katika hatua nzuri ya kufanya tathmini ya eneo na kulipa fidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kero yetu kubwa kuliko zote Njombe, na nilisema, ilikuwa ni maji. Tumepata miradi mingi ya maji karibu mitano, uwekezaji wa shilingi bilioni 60 ndani ya Mji wa Njombe. Miradi ipo katika hatua mbalimbali na inaendelea vizuri, na kero ya maji muda siyo mrefu itakuwa historia kwa wananchi wa Njombe. Kwa hiyo, tuna kila sababu ya kuwa na shukrani kwa yanayofanyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo yote, bado tuna changamoto ambazo tunaendelea kuzipitia, na wananchi wa Njombe wangependa kuzisikia Mbunge wao waliyemchagua akiziongelea katika ukumbi huu wa Bunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Njombe ni Mkoa wa kiuchumi na wengi wanalifahamu hilo, na waliotembelea Njombe wanafahamu hilo. Njombe ni Mkoa ambao una baraka, Njombe inao mchango mkubwa kwenye uchumi wa Tanzania, Njombe ina potential kubwa sana ya kuchangia mara dufu, mimi nasema siyo maradufu labda mara mia ya kile inachochangia leo; lakini inachangamoto za msingi ambazo zikitatuliwa, tuna uhakika Njombe tunayoiongelea itakuwa ni Njombe tofauti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo barabara yetu ya Itoni – Lusitu yenye urefu wa kilometa 51. Barabara hii tunaendelea kumshukuru Rais, kwa sababu alipokuja katika barabara 14 za kwanza alizosaini ili ziingie kwenye mchakato wa manunuzi, barabara ya Itoni – Lusitu ilikuwemo shilingi bilioni 95, ukiongeza na VAT kama shilingi bilioni 110. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kwa furaha mkandarasi amepewa site, ameijenga kwa kipindi cha mwaka mmoja, kutengeneza tuta na kazi inaendelea, lakini kwa masikitiko, kwa kipindi cha miaka miwili barabara hii imesimama, lakini usimamaji wa barabara hii umekuja na maumivu makubwa kwa wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Njombe kwa sababu barabara hiyo inayojengwa ndiyo wanayotumia kupitisha mazao mbalimbali, mazao ya Njombe ya kilimo ni viazi, mazao ya misitu ambayo yanahitaji usafiri. Kwa hiyo, wamepitia vipindi viwili vya mvua ambavyo havikuwa vizuri kwao, ambavyo vimewarudisha nyuma na vingine vimewatia umaskini. Tunaiomba sana Serikali ilitilie maanani suala la barabara ya Itoni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii ndiyo inayokwenda kwenye migodi ya Liganga na Mchuchuma. Huwezi kuongea Liganga na Mchuchuma bila kuongelea barabara ya Itoni – Lusitu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaiomba Serikali, tunafahamu mkandarasi haidai Serikali kwa maana ya kwamba kazi iliyofanyika amelipwa, baada ya sisi kuweka nguvu kubwa, lakini tunachosema, tunaomba itakapoanza ujenzi baada ya hizi mvua kwisha, tunaomba barabara hii isisimame tena, kwa sababu ni barabara kubwa ya kipaumbele, ni barabara ya kiuchumi, na ni barabara inayofungua Liganga na Mchuchuma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niliseme hilo kwa udogo wake. Tuna barabara ya Makambaku – Songea ambayo tunahitaji iweze kukamilishwa. Barabara hii ina miaka 40, Kamati ya Miundombinu imeitembelea, ni barabara kubwa ya Uchumi. Kama ingekuwa ni katika mwili wa binadamu, ni mshipa mkubwa wa damu. Tunaomba sana Serikali ifanye utaratibu wa kutafuta fedha. Tunafahamu inaendelea na mchakato ili tupate barabara hii iweze kuanza kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la barabara za vijijini kwangu ndiyo eneo kubwa na la muhimu sana. Tuna mtandao mkubwa sana wa barabara Njombe, karibu kilometa 1,000 za Barabara, ambapo ni kilometa kama 40 tu za lami. Mazao yote ya viazi, parachichi, mazao ya mbao, mazao ya chai yote yanatoka katika maeneo ya vijiji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Njombe ni Jimbo la Mjini na Vijijini. Mazao yote yanatoka vijijini ambapo kuna uhitaji mkubwa sana wa barabara. Sasa mimi nasema kuna vicious cycle, kwa sababu Mwenyezi Mungu ametubariki na mvua nyingi na mazao mengi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mazao hayo yanahitaji magari makubwa yaweze kuyachukua. Magari hayo yanahitaji kuingia vijijini. Magari ya tani 10, tumeshasahau tunaongelea semitrailer tani 32, tani 40 ndiyo yanayokwenda vijijini kuchukua mizigo. Kuwalisha Watanzania sio Wananjombe peke yao, ni Watanzania wa Mikoa karibu yote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulitoa hoja hapa na Wabunge wengi walichangia. Katika mgawanyo wa fedha ya TARURA, kwanza tunaishukuru Serikali kwa kuongeza bajeti kufikia 1.2 trillion, lakini tulidhani kwamba ingekuwa ni busara, yale Majimbo ambayo yana mijini na vijijini yangeangaliwa kwa namna ya pekee ili angalau yaongezewe fedha ili ziweze kukidhi kusaidia kutengeneza hizo barabara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana mwaka 2021/2022 nilijenga hoja kubwa sana hapa ya barabara, tukapata fedha za kutosha, shilingi bilioni 3.8 kwa ajili ya ujenzi wa barabara za mji wa Njombe, lakini uhakika ni kwamba shilingi bilioni 1.5 ilikwenda kwenye barabara za mjini na iliyobaki ilikwenda barabara za vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli barabara za vijijini ambazo tulizijenga kwa zile fedha, leo hii ukienda hutaamini kama hizo barabara ni zile tulizotumia fedha nyingi. Kwa hiyo, ninakubaliana na hoja ya Waheshimiwa Wabunge hapa, ni bora twende pole pole kujenga barabara za vijijini kuliko kwenda kupoteza fedha kwa kujenga barabara ambazo zinaondolewa na mvua kila mwaka unapokuja. Ni hasara kwa nchi yetu na kwa Serikali. (Mkaofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho, Waziri Mkuu, hapa aliongelea kuhusu lumbesa, ninamshukuru sana. Ni kero kubwa sana kwa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini na mikoa mingine kama Kilimanjaro na Kagera. Maeneo ya mahindi, vitunguu na viazi, wananchi wamekuwa wakinyonywa kwa muda mrefu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunamshukuru Waziri Mkuu, kwa kulisema. Ninaomba nitoe ombi, jambo hili ili lifanikiwe, linahitaji lisimamiwe kwa ukaribu, Halmashauri zote. Wananchi wa Njombe wakiamua kutekeleza suala la lumbesa; kutokuwa na lumbesa, kufunga mizigo kwa kilogramu 100; wananchi wa Chunya wasipofanya, wananchi wa Njombe ndio watakaopata hasara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, linatakiwa lisimamiwe kwa ukamilifu, lifuatiliwe, kuwe na monitoring na wenzetu wa TAMISEMI wahakikishe kuwe na measures kwa Maofisa wa Halmashauri ambao hawatasimamia agizo la Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi, naunga mkono hoja. (Makofi)