Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Joseph Enock Tama

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kaliua

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. JOSEPH E. TAMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa ili niweze kuchangia hotuba ya Waziri Mkuu. Awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema ambaye amenipatia fursa ya kuiona siku ya leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie fursa hii kwa sababu ni mara yangu ya kwanza kuwashukuru wananchi wa Jimbo la Kaliua kwa kuniamini na kunichagua niwe mwakilishi wao humu Bungeni, hakika ninawaahidi kwamba, nitakuwa mwakilishi mwema kwa sababu ninazo sababu alizonipatia Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa miradi na fedha nyingi alizozileta kwenye Jimbo letu la Kaliua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninasema hivi, kwa sababu ukienda kwenye sekta ya umeme nishati tumeletewa umeme vitongoji takribani 22 na ninaamini ndani ya mwaka huu kabla hujaisha tutaongezewa vingine na maisha yetu tutaendelea kutabasamu kama jinsi ambavyo Majimbo mengine wameendelea kunufaika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye upande wa maji, ninaamini kabla ya mwaka kwisha wananchi wangu wa Jimbo la Kaliua watakunywa maji kutoka Ziwa Victoria na tutaendelea kutabasamu, hakika tunaendelea kumwombea kwa Mwenyezi Mungu, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuchangia hotuba hii ya Waziri Mkuu, niseme mambo machache kwenye sekta ya afya. Ninafahamu Serikali imefanya kazi kubwa kwenye Jimbo letu la Kaliua. Tumepata hospitali ya wilaya, hizi ni juhudi za Dkt. Samia Suluhu Hassan, tulikuwa hatuna hospitali ya wilaya, sasa tuna hospitali ya wilaya na vituo vya afya takriban vinne.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie fursa hii kuwaomba TAMISEMI, ipo Kata ya Igwisi ina wakazi zaidi ya elfu sabini na mbili (72,000). Kata hii haina kituo cha afya, lakini Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan, wote Wabunge wanafahamu, kwa miaka mitano ilikuwepo program ya kujenga vituo vya afya vya kimkakati katika kila jimbo, taarifa zilizopo ni kwamba yamebaki majimbo 93 ikiwemo Jimbo la Kaliua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba Waziri wa TAMISEMI, niombe tena kwa mara ya pili, niombe kwa mara ya tatu, wapeleke fedha hizi tuweze kupata kituo cha afya, wananchi waweze kutabasamu, mama zetu waweze kujifungua kwenye maeneo mazuri, safi, huku wakiwa wanapiga mluzi taratibu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatujabaki nyuma kwa sababu kupitia jitihada za wananchi kwenye Kata ya Ugunga, Kata ya Ukumbi Siganga, tumeanzisha ujenzi wa vituo vya afya, ninaomba Serikali kupitia Wizara ya TAMISEMI iweze kupeleka fedha ili kukamilisha vituo hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye eneo la barabara. Yamesemwa mengi, wananchi wanatambua ya kwamba kila msimu, kila mwaka mvua zinanyesha na mvua ni baraka, ni kweli, mvua zikinyesha tunalima, lakini ni kweli zina madhara yake barabara zimekatika. Niombe Wizara ya TAMISEMI basi iharakishe mpango wake wa kupata hizo fedha bilioni 98 kuweza kuwapelekea wananchi kwenye majimbo yote tuweze kutengenezewa barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye ujenzi wa barabara, lipo jambo ambalo nisipolisema wananchi wa Jimbo la Kaliua hawawezi wakanielewa, bahati nzuri na wewe umepita Jimboni kuninadi, tarehe 11 mwezi wa Septemba, 2025 alikuja Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mama mwenye huruma, Mama mchapakazi, Mama anayeipenda Tanzania yake, aliwaahidi wananchi wa Kaliua kwamba anakwenda kufungua Mkoa wa Katavi, Mkoa wa Tabora na Mkoa wa Shinyanga kwa kuijenga kiwango cha lami Barabara ya Mpanda – Ugala – Kaliua – Ulyankulu mpaka Kahama, barabara hii ina urefu wa kilometa 428.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninasema hivi kwa uchungu kwa sababu barabara hii ina muda wa takriban miaka 20 tunaiomba. Upembuzi yakinifu umekamilika, usanifu wa kina umekwishafanyika. Ukienda kwenye Ilani ya Chama Cha Mapinduzi 2015-2020, ukurasa wa 59 imeahidiwa, ujenzi bado haujaanza. Ukienda kwenye Ilani ya Chama Cha Mapinduzi 2020-2025, ukurasa wa 75, ahadi hii ilikuwepo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imefanya vizuri, imefanya na kukamilisha usanifu, ninaomba hata 2025 - 2030 kwenye Ilani hii imeahidiwa. Niwaombe sana Wizara ya Ujenzi na ninamwamini Waziri Mkuu na ninamwalika kwenye Mkoa wetu wa Tabora, akifika Tabora nitakuwa kiongozi wake wa msafara kumpeleka Kaliua aone jinsi ambavyo Serikali imefanya kazi kubwa ya kufungua uchumi. Dhamira ya Rais ni kufungua uchumi kwa kujenga barabara hii nina hakika pato la Serikali litaongezeka na kwa kujenga barabara hii mazao mbalimbali yatasafirishwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninafahamu Kaliua ndiyo "Toronto" ya Tabora, ninaomba sana Wizara ya TAMISEMI, hatuna stendi ya kisasa, ninaomba kwa sababu tayari tumeshatenga eneo na halina mgogoro na halmashauri yetu tumeshatenga milioni 150. Sisi tuko tayari tumeshaanza kukimbia kuunga juhudi za Dkt. Samia Suluhu Hassan. Tunaomba wakamilishe kibali ujenzi uweze kuanza na ikiwezekana mtu-support kwa kianzio kidogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwenye sekta ya kilimo. Kaliua pamoja na Mkoa wa Tabora, tumbaku ndiyo dhahabu yetu. Zao la tumbaku ndiyo kimbilio letu, zao la tumbaku ndiyo jicho letu, Wanakaliua na wananchi kwa ujumla. Sote tunafahamu humu ndani sekta ya kilimo ina mchango mkubwa katika Serikali, sekta ya kilimo ina mchango mkubwa kufikia Dira ya Taifa 2050.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana kwa takwimu Kaliua pekee tumezalisha kilo milioni 35, mauzo tumepata bilioni 212, lakini hizi zote tunampa maua Dkt. Samia Suluhu Hassan alipeleka ruzuku ya mbolea, alirahisisha mazingira safi na mbolea ilifika kwa wakati. Kwa msimu huu, zipo changamoto na ninaomba Wizara ya Kilimo isilale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza kuna ucheleweshaji wa pembejeo za kilimo kwa msimu huu, ambapo msimu wanaanza kuandaa mwezi Agosti, mbolea inafika mwezi Novemba, hii siyo sawa kwa mkulima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ya pili ni ongezeko la gharama za uzalishaji, ongezeko limetokea kwenye upande wa mbolea. Ukienda kwenye mbolea ya NPK mwaka jana msimu uliopita ilikuwa ni dola 60.7 sasa hivi ni dola 63.8. Ukienda kwenye mbolea ya muhimu CAN, mwaka jana ilikuwa ni dola 30.34, mwaka huu msimu huu ni dola 34.08. Kama kweli tuna lengo la kumkomboa mkulima, tutazame gharama za uzalishaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka huu kwa maana ya musimu huu bei ya tumbaku imeporomoka kwa kilo moja wastani ni dola 1.95. Msimu uliopita ilikuwa ni dola 2.15 kwa kilo moja. Naiomba Serikali yangu sikivu, Serikali ya Chama Cha Mapinduzi, Serikali bingwa na hakuna asiyefahamu makubwa na uwezo ni kuamua sisi tufanye, ninaomba tumtazame mkulima wa tumbaku ili basi tuweze kulisafisha eneo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia changamoto ya mwisho ambayo Serikali niombe iweze kuifanyia kazi ni ucheleweshaji wa malipo ya fedha za wakulima. Mpaka leo tunavyozungumza wakulima wamelima msimu uliopita wakamaliza, wanadai kuna makampuni kama MAGEFA, JFO, na OBAMACO zinadaiwa fedha nyingi. Fedha hizi Halmashauri ndiyo tunazotegemea kama cess. Kwa mwaka jana mauzo yale ya bilioni 212, cess pekee yake iliyoenda Halmashauri ni bilioni 6.3. Tafsiri yake ni nini? Wakichelewa kulipa maana yake tunacheleweshwa na maendeleo. Niombe Serikali yangu sikivu ya Chama Cha Mapinduzi iweze kulifanyia kazi na haya makampuni yaweze kulipa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia, mnyonge mnyongeni haki yake mpeni. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa ambazo amezifanya, kwa fedha nyingi ambazo amepeleka kwenye Majimbo yetu, hakika leo hii ninashangaa hata Ndugu yangu Mheshimiwa Ado kuomba Katiba, omba maji! Leo hii watu wanatabasamu kwa kuletewa maji ya Ziwa Victoria Tabora nzima na Majimbo mengine. Omba umeme! Tumepelekewa...

MWENYEKITI: Taarifa Mheshimiwa.

TAARIFA

MHE. JOSEPH K. MSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nataka kumweka sawa mchangiaji. Amesema "mnyonge mnyongeni haki yake mpeni’’, Sasa mtu umeshamnyonga unampaje haki? Ninataka arekebishe aseme mtu anayefanya kazi vizuri tumpe hongera zake. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Joseph unaipokea taarifa hiyo?

MHE. JOSEPH E. TAMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana nimeipokea taarifa hiyo kwa mikono miwili, ninaongezea na miwili mingine kwa sababu hakuna kama Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Hata vitabu vya Mungu vinasema, tumpate wapi mtu kama huyu? Hakika Mungu ametubariki Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)