Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Urambo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili nichangie hoja iliyoko mezani. Kwanza ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa uhai, lakini pia ninawashukuru sana wananchi wa Urambo na familia yangu kwa support wanayonipa ambayo imeniwezesha kufanya kazi mpaka wakati huo. Nichukue pia nafasi hii kuipongeza sana Serikali inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jinsi ambavyo wametupa miradi mikubwa Urambo ikiwemo Kituo cha Kupozea Umeme, Mradi wa Maji ambao unaendelea, Shule na kadhalika. Tunaishukuru sana Serikali yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mazuri yote yanayofanywa pamoja na TAMISEMI ambayo Waziri wake Mheshimiwa Shemdoe anafanya kazi nzuri akisaidiana na Naibu Mawaziri na Wakuu wa Idara wote, kwa kweli pamoja na shukrani, lakini bado tunarudi kwao kwa ajili ya maombi maalum kwa niaba ya wananchi wa Urambo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza Urambo tunategemea sana kilimo hasa cha tumbaku, mahindi na kadhalika, kwa hiyo tunahitaji barabara imara vijijini. Kazi ya TARURA ni nzuri, lakini tunaomba iongezewe ipewe uwezo zaidi ili barabara za vijijini ziweze kubeba mazao yetu kuyapeleka kwenye soko. Pia nichukue nafasi hii kuishukuru TANROADS kwa kazi kubwa inayofanya, lakini na yenyewe tunaiomba pia iimarishe barabara zake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Tabora katika Wilaya ya Urambo, Ulyankulu, Kaliua na Sikonge tuunganishwe na barabara ya lami ili tuweze kupeleka mazao yetu kwa utaratibu ambao utatusaidia kubadilishana mazao na kuinua uchumi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Urambo tuna changamoto pia kwa upande wa shule. Serikali yetu imefanya kazi kubwa sana lakini kuna shule kwa mfano ya mjini inayoitwa Shule ya Ukombozi ambayo ina wanafunzi 1,600. Tunaomba Serikali yetu itupe shule nyingine Urambo Mjini kwenye Kata ya Urambo ili wanafunzi 1,600 wapungue wapate shule nyingine. Hali kadhalika, tunaomba shule ya msingi ijengwe sehemu ya Imara Makoe ambayo wanafunzi wanashindwa kwenda shule ambayo iko kilometa nne kutoka pale walipo, wakitaka mbadala inabidi wavuke barabara ya kwenda Kigoma ambayo ni hatari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeomba sana pia kwa upande wa afya hospitali yetu ya Wilaya ya Urambo jengo la utawala ambalo liko karibu na jengo la dharura halijakamilika. Tunaomba tusaidiwe ni zaidi ya milioni 250 ambazo zinahitajika ili tuwe na jengo la utawala karibu na jengo la dharura. Wakati huo huo ninaomba, kuna Kata moja inaitwa Uyogo ambayo iko na kilometa 59 kutoka mjini tunaomba na yenyewe ipatiwe kituo cha afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikirudi kwa upande wa wafanyakazi hasa nikiwalenga walimu, ninaiomba Serikali kwa mara ya ngapi sijui, bado kuna haja ya kuangalia TSC inavyofanya kazi. TSC iliundwa kwa Sheria Namba 25 mwaka 2015, bado haina hela za kutosha, bado wafanyakazi hawatoshi, lakini kazi yake iliyoundiwa ya kufanya kazi ya ajira, maadili na maendeleo ya wafanyakazi haifanyi kazi vizuri. Ninaomba kwa heshima na taadhima Serikali iangalie Tume ya Utumishi wa Walimu TSC ili ifanye kazi iliyokusudiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukulie pia kwa upande wa wafanyakazi wote kwa ujumla, ninaomba sana walimu na wafanyakazi wengine wa afya na kadhalika wanapomaliza muda wao wa kazi yaani wanapokaribia kustaafu, wanapata tabu sana kwa sababu mishahara yao inakuwa haijarekebishwa hasa wale waliopanda madaraja. Hivi ninavyoongea hapa nina Walimu 20 na wafanyakazi wengine ambao wamestaafu bila kurekebishiwa mishahara yao. Kwa hiyo inawapa shida sana wakati wa kupata pension. Kwa hiyo, tunaomba sana mfanyakazi yeyote yule kabla hajastaafu, mshahara wake uwe umerekebishwa ili kumsaidia aweze kupata pension kwa uzuri zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa msingi huo kuwaacha wafanyakazi wanahangaika baada ya kufanya kazi kubwa ya kutumikia ndani ya nchi yetu inakuwa siyo vizuri wasaidiwe waweze kupata haki zao kwa wakati mwafaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ninashukuru sana, lakini watusaidie sisi hasa tunaotoka vijijini tupatiwe kwa kweli barabara nzuri. Ninarudia tena barabara nzuri! TARURA wanafanya kazi nzuri sana, TANROADS wanafanya kazi nzuri sana, lakini waongeze fedha ili ziweze kuwasaidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa suala la wajasiriamali. Tumeongelea hapa kuhusu akina mama kupewa mikopo, vijana kupewa mikopo, lakini kama hatutapata elimu ya ujasiriamali kwanza kabla hawajawapa hizi fedha, inakuwa shida sana. Kwa hiyo, ninafikiri Maafisa Maendeleo wawezeshwe kutembea kutoa elimu kwa hawa vijana wenye ulemavu pamoja na wanawake ili wanapopata fedha elimu ya uendeshaji wa shughuli zao za kiuchumi waweze kuzimudu vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na ninaunga mkono hoja. (Makofi)