Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Taska Restituta Mbogo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi kuchangia ya hotuba ya Waziri Mkuu. Kwanza kabisa ninapenda kumshukuru Mwenyezi Mungu muumba mbingu na dunia kwa kutujalia uhai.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda nitumie nafasi hii kwanza kabisa kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi nzuri ambazo anazifanya kwenye Taifa letu la Tanzania pamoja na Makamu wake Balozi Dkt. Nchimbi. Ninapenda pia kuwashukuru wananchi wa Mkoa wa Katavi kwa ushirikiano wanaonipa. Ninapenda nitumie nafasi hii kumpongeza Waziri Mkuu Dkt. Lameck Nchemba na Mawaziri wote ambao wameteuliwa kwenye nafasi mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba sasa nichangie hoja na hotuba ya Waziri Mkuu ambayo imesheheni pia mambo mbalimbali ya TAMISEMI na mambo mbalimbali yanayohusu nchi yetu ya Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa 2023 niliwahi kusimama hapa Bungeni nikasema kwamba kwenye Mkoa wetu wa Katavi tuna upungufu wa madarasa, madawati pamoja na vyoo. Tatizo hilo kwenye Mkoa wa Katavi bado ni tatizo kubwa kwenye shule za msingi, tukiwa tunakwenda sasa kuwa na shule za ufundi ambazo ni shule za amali kwenye Taifa letu la Tanzania, lakini tukiwa tumebadilisha sera ya nchi yetu ya Tanzania kwamba elimu ya shule ya msingi ni kutoka darasa la kwanza mpaka darasa la sita pia mpaka darasa la 12. Mkoa wetu wa Katavi bado unakabiliwa na upungufu wa madawati, madarasa pamoja na matundu ya vyoo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nizitaje takwimu kwa sababu zinatisha. Kwenye Mkoa wetu wa Katavi tuna upungufu wa wa madarasa, tunao uhitaji wa madarasa tunahitaji wa madarasa 6,671, lakini sasa hivi tuna madarasa 2,866, tunao upungufu wa madarasa 3,205. Pamoja na upungufu wa hayo madarasa tunao pia upungufu mkubwa wa madawati kwenye Mkoa wetu wa Katavi. Tuna uhitaji wa madawati 87,681 lakini kwa sasa hivi tuna madawati 61,332 na kuleta upungufu wa madawati 27,348.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Mkoa wetu wa Katavi tunao uhitaji wa matundu ya vyoo 9,122. Kwa sasa hivi, tuna matundu ya vyoo 3,762 na tuna upungufu wa matundu ya vyoo 3,762. Ukiangalia hoja ya elimu kwenye Mkoa wetu wa Katavi ukichukua upungufu wa madarasa, upungufu wa madawati na upungufu wa matundu ya vyoo, unakuta kwamba Mkoa unahitaji kupata madawati, kupata hayo matundu ya vyoo na kupata madarasa ili Mkoa wetu wa Katavi uende sambamba na mikoa mingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaiomba Serikali iweze kuwahimiza Halmashauri zilizoko kwenye Mkoa wetu wa Katavi nikiwa na maana Halmashauri ya Mlele, Halmashauri ya Tanganyika, Halmashauri ya Mpimbwe pamoja na Manispaa ya Mpanda kutoa tarehe maalum, lakini kutoa ratiba maalum kwenye hizo halmashauri ili ziweze kutengeneza hayo madawati na kukamilisha matundu ya choo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaweza nikatolea mfano shule ambazo zipo pale Mpanda Mjini katikati ya kitovu cha Mkoa wa Katavi ambazo zina wanafunzi ambao wamezidi. Tunayo Shule ya Nsemulwa ambayo inao wanafunzi takribani 1,523, lakini ina walimu 16, ina madawati 102. Unaangalia jinsi watoto wanavyobanana darasani. Watoto wanakaa takriban 191 mpaka 200 kwenye darasa moja. Tunazo Shule za Msakila zina wanafunzi takribani zaidi ya 2,000 lakini watoto wanaokaa kwenye shule hiyo watoto 100 mpaka 200. Ninaomba mambo haya yachukuliwe kwa uzito ili Mkoa wetu wa Katavi uende sambamba na Mikoa mingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ningependa kulizungumza hapa ni suala la halmashauri nchini kwetu Tanzania ambazo zimejitengenezea kitega uchumi cha kujenga Shule za English medium. Imezuka tabia kwenye halmashauri nyingi nchini kwetu Tanzania kuweka kitega uchumi cha kujenga Shule ya English medium ilhali inatumia walimu wanaolipwa na Serikali, lakini pia inawachukua wale walimu wazuri na kuwapeleka kwenye shule hizo na kusema kwamba wametengeneza kitega uchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zipo Halmashauri zaidi ya 40 nchini kwetu Tanzania zinafundisha elimu ya msingi.

MWENYEKITI: Mheshimiwa muda wako.

MHE. TASKA R. MBOGO: Ahsante naomba dakika moja. Zinafundisha elimu ya msingi kuanzia darasa la kwanza mpaka la saba kwa lugha ya Kiingereza, lakini sera ya elimu nchini kwetu Tanzania inasema nini? Inasema kwamba elimu ya msingi kutoka darasa la kwanza mpaka la sita au la saba inatakiwa ifundishwe kwa lugha ya Kiswahili. Je wanafuata sera gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi na ninaunga mkono hoja. (Makofi)