Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Musa Godfrey Mbuga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisesa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. MUSA G. MBUGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa nafasi ya kuchangia hotuba hii. Ninaanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyeniazima uhai na ninaendelea kumwomba aendelee kuniazima ninapotimiza majukumu ya Wana-Kisesa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapoelekea kwenye Hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ninaanza kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wetu, kwanza kwa fedha nyingi ambazo amezileta kwetu Kisesa na kwa maendeleo makubwa. Muda hauwezi kutosha kuelezea moja baada ya lingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawapongeza pia wasaidizi wake; Mheshimiwa Makamu wa Rais, Dkt. Nchimbi, Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na Waheshimiwa Mawaziri wote. Ninawapongeza sana Waheshimiwa Mawaziri kwa sababu, kwanza wamekuwa ni wasikivu, wanatupa muda wa kutusikiliza na wanatatua kero zetu. Kwa hiyo, Waheshimiwa Mawaziri tunawashukuru na tunawapongeza sana pamoja na Waheshimiwa Manaibu Waziri wote. Hotuba yetu au ya Mheshimiwa Waziri Mkuu imeeleza utekelezaji wa 2025/2026 na imeeleza mwelekeo wa Serikali yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninayo mambo machache ya kushauri kutoka kwenye Hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Ni hotuba ambayo imesheheni mahitaji ya Watanzania na ni hotuba, ambayo inajibu hoja na haja nyingi sana za Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza kwenye suala la uratibu wa maafa. Pamoja na mambo mengi mazuri ambayo yameelezwa kwenye hotuba, ninalo jambo la kushauri kwenye uratibu wa maafa ambayo kwenye Hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ni Ukurasa wa 95. Tumekuwa tunapitia maafa mengi na hata Jimboni kwangu Kisesa baada ya mvua hizi nyingi kutokea na hatuwezi kumlaumu yeyote, hizi mvua zilizonyesha ni baraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi baraka zimekuja na changamoto, Malaika wa awamu hii nadhani alipoambiwa kwenda kufungulia maji akafungulia zaidi ya kiwango kwa hiyo, kwa Kisesa ikaleta shida kubwa; yapo maafa makubwa maeneo mbalimbali, kwa mfano Kijiji cha Nh’anga na sehemu zingine nyingi. Sasa zinapotokea changamoto kama hizi tunajua upo Mfuko wa Maafa ambao uko chini ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, lakini hauna bajeti ya kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkuu wetu wa Mkoa, pamoja na DC; kwanza ninawashukuru na ninawapongeza, Mheshimiwa Namlingi Macha pamoja na dada yangu Fauzia Ngatumbura. Wamekuwa wanajituma sana kwenye mambo mengi, lakini changamoto ni linapokuja suala la maafa bajeti haitoshi. Kwa hiyo, hata mwananchi anapopata shida ni suala la kwenda kumpa pole, lakini pole inasaidiaje wakati mtu hana chakula? Pole inasaidiaje mtu hana pa kujihifadhi? Kwa hiyo, ninaishauri Serikali, ninaishauri Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, iongeze bajeti kwenye kipengele cha maafa, ili zinapotokea changamoto kama hizi iweze kuwa rahisi kukabiliana nazo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu nyingine ambayo ninataka nishauri ni suala la maendeleo ya vijana, ambayo kwenye hotuba iko ukurasa wa 84, maendeleo ya vijana; Serikali ya Awamu ya Sita imechukua hatua madhubuti kabisa ikaanzisha Wizara maalum ya Vijana na tumeona hatua mbalimbali ambazo zimetolewa ikiwa ni pamoja na hii mikopo ya shilingi bilioni 200, kwa ajili ya vijana na wanawake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu ambacho ninataka niishauri Serikali ni hizi fedha, ukiangalia zimetawanywa kwenye Wizara mbalimbali, zipo zilizoenda Wizara ya Mifugo tumeona wametoa shilingi bilioni saba na kitu, zipo zilizoenda kwenye Wizara ya Uvuvi huko na Kilimo na sehemu mbalimbali. Ninashauri hizi fedha zingekuwa centralized sehemu moja, pawepo na one stop center, kama ambavyo REA wamefanya kwenye ule mradi wa kujenga petrol station vijijini fedha zote zimepelekwa Azania kwa hiyo, yeyote anayetaka kujenga petrol station vijijini anaenda REA, anapata maelekezo, ana-comply na EWURA, anakutana na fedha Azania, inaondoa milolongo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashauri pia, kwenye suala la maendeleo ya vijana hizi fedha zinazotolewa, kwa ajili ya wanawake, kwa ajili ya vijana, ziwe sehemu moja ambapo mwananchi anapokwenda anakutana na huduma zote. Pamoja na kwamba Wizara ya Vijana haina technical team ya kutosha, wanaweza wakachukuliwa wataalam kutoka Wizara ya Mifugo, Wizara ya Kilimo na Wizara zingine wakapelekwa kwenye Wizara ya Vijana, ili kijana wa Kitanzania anapojkwenda kuomba mkopo akutane na huduma zote. Sehemu moja inaondoa mkanganyiko, inaondoa tafsiri mbalimbali kwa hiyo, ninashauri suala la hii mikopo ya shilingi bilioni 200 iwe sehemu moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo ninaishauri Serikali ni kilimo. Serikali imefanya vizuri sana kwenye mambo mengi. Ninajikita kwenye kilimo cha pamba maana wananchi wangu wa Kisesa ni walimaji wakubwa wa pamba na kilimo, kwenye hotuba yetu, kiko page ya 24 na 25.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imefanya juhudi kubwa kwenye zao la pamba ikaanzisha kilimo cha mkataba, contract farming, lengo ni kuleta tija kwenye kilimo, kwa maana ya Mfumo wa BBT. Changamoto ya huu mfumo inakuja inapofika kwenye suala la ununuzi; suala la kuwa na mnunuzi mmoja linaondoa ushindani. Ni kweli, bei ya pamba ni suala la global, it's a global price kwa hiyo, inakuwa determined na market force.

Mheshimiwa Mwenyekiti, panapokuwa na ushindani kwenye ununuzi hata bei inapokuwa imeshuka ni rahisi kwa mwananchi, ni rahisi kwa mkulima kuamini kuwa, bei imeshuka kuliko panapokuwa na mnunuzi mmoja. Kwa hiyo, ninaishauri Serikali, kwenye hiki kilimo cha mkataba waangalie component ya kuwa na wanunuzi wengi kuliko kata nzima kuwa na mnunuzi mmoja na ukiangalia Hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa muda wako umeisha.

MHE. MUSA G. MBUGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana, ninamalizia. Ukiangalia Hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ameeleza jinsi ambavyo wananchi wamekuwa wanakopa fedha zao kwa hiyo, ikiwa wataboresha hii sehemu tutaondoa hayo yote. Muda ungetosha ningeeleza mambo ya Tembwa, lakini itoshe tu kusema ninaunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)