Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Fagason Aron Nkingwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbogwe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. FAGASON A. NKINGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuzungumza yale ambayo kama Waheshimiwa Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tunaenda kuyazungumza leo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kukushukuru wewe lakini pia nimshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa namna ambavyo anaendelea kulipambania Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijazungumza mengi ninataka niseme jambo moja. Ninapenda nimshukuru sana Mwenyezi Mungu, muumba wa mbingu na nchi, aliyetusababisha Wabunge wote tuliokuwemo humu ndani tukiwa salama kwa sababu ni mapenzi ya Mwenyezi Mungu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami ni mara ya kwanza kusimama kwenye Bunge hili, lakini nimesimama kwenye Bunge hili kwa sababu ya wananchi wangu wa Jimbo la Mbogwe. Jimbo langu la Mbogwe lina wananchi takriban 362,825, walipo wananisikia, wananiona lakini Mwenyezi Mungu ananiona zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kwanza niunge hoja mkono kabla sijasahau. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nizungumze yale ambayo Rais huyu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ameyafanya kwenye Jimbo la Mbogwe. Jimbo la Mbogwe, kama nilivyozungumza mapema, lina wananchi 362,825, lakini yapo maendeleo makubwa aliyoyafanya kwenye Jimbo la Mbogwe, ikiwemo ahadi yake ya siku 100 ameweza kutupa watumishi zaidi ya 156.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye ahadi zake za siku 100, pia ameweza kunipa shilingi 1,500,000,000 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa kwenye shule zilizopo Wilaya ya Mbogwe, lakini Mama huyu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye Jimbo langu la Mbogwe, ameweza kujenga shule ya amali yenye zaidi ya shilingi 1,600,000,000 ambayo ipo pale kwenye Jimbo langu la Mbogwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Rais huyu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameweza kujenga shule ya VETA yenye zaidi ya shilingi 1,300,000,000 kwenye Jimbo la Mbogwe. Ninaomba nizungumze kuhusiana na hii shule ya VETA iliyojengwa kwenye Jimbo langu la Mbogwe. Tunafahamu na tunatambua kwamba, Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa mkopo wa zaidi ya shilingi bilioni 200 kwa ajili ya kuhakikisha tunawasaidia vijana, akina mama na watu wenye ulemavu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, kwenye Jimbo langu la Mbogwe tumeweza kupokea zaidi ya shilingi bilioni tatu kwa ajili ya kuhakikisha tunawabeba vijana pamoja na akina mama, tunawapa mikopo kuhakikisha wanajiendeleza katika maisha yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nitoe ushauri. Katika Jimbo langu la Mbogwe tunao vijana wengi sana, ninao vijana takribani 14,000, lakini vijana hawa wanahitaji mikopo inayotolewa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ameleta mikopo hii, lakini niiombe sana kama Serikali, kwa sababu tunazo shule ambazo zina mafunzo ya hawa vijana, hususan kwamba tumeletewa pikipiki nyingi ambazo zinakuja kwa vijana. Juzi nimepokea pikipiki zaidi ya 51 kwa ajili ya vijana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba sana, Serikali iliangalie hili tunawapa vijana wetu pikipiki, lakini hatuwapi mafunzo. Kutowapa mafunzo vijana wetu tunasababisha ajali nyingi zinatokea, watu wanavunjika miguu, watu wanapoteza maisha kwa sababu ya kukosa uzoefu kwa maana ya kwamba tunazo shule za kuwafundisha vijana wetu ili waelewe namna gani wataendesha vyombo hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niombe Serikali itusaidie, kwa sababu tunazo shule ambazo zitaenda kuwasaidia hawa vijana. Tunapowapa mikopo na kuwanunulia bodaboda tuwaombe sana watusaidie kuwalipia mafunzo ili waweze kujifunza kuhakikisha kwamba wanaendesha bodaboda hizi au pikipiki hizi, kwa sababu wasipofanya hivyo tutaingia kwenye changamoto kubwa ya kuwapoteza ndugu zetu, ajali zimekuwa nyingi kwa sababu hatuna mafunzo ya hawa vijana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe sana Waziri kwenye Jimbo langu kama nilivyozungumza ninao vijana wengi, lakini vijana hawa wanatamani na wanatambua kwamba Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anawapa vifaa kwa ajili ya kuhakikisha wanajiendesha. Ninaomba tuje tutengeneze mfumo wa kuwafundisha vijana wetu waendeshe pikipiki kwa kufuata mfumo wa kuepuka ajali. Kwa sababu ajali zimekuwa ni nyingi, ukizingatia vijana wetu kama tunavyojua tuna vijana wa aina mbili. Wapo vijana wanaojiita Gen-Z, lakini vijana hawa wa Gen-Z tunao wa aina mbili: tunao vijana wa Gen-Z wenye akili timamu, lakini tunao vijana wa Gen-Z ambao hawafai kabisa kwenye nchi hii. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini ninalizungumzia hili? Leo kuna changamoto ya kutolewa nyeti. Jambo hili la watu kutolewa nyeti limekuwa ni changamoto sana kwenye Taifa letu. Nimwombe Waziri jambo hili tunatakiwa tulichukulie serious sana kwa sababu jambo hili limekuwa ni kubwa, watu wameuawa na wamejeruhiwa. Kwa hiyo, nikiwa kama kijana niliyesimama hapa jambo hili haliwezekani, kwa nini? Ninamshukuru sana Mheshimiwa Waziri husika, leo ametupatia mfano kwamba wanaume wapange foleni washikane mabega. Sasa mwanaume akimshika mabega mtu mwingine ionekane ametolewa dhababu tunasema. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sana kwenye jambo hili kama Taifa tuwe serious sana kwenye mambo ya hovyo kwa maana ya kwamba jambo hili linatuumiza. Jambo hili limesababisha ndugu zetu wameuawa, wamejeruhiwa kwa sababu ya mambo ya hovyo. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa muda wako umekwisha.

MHE. FAGASON A. NKINGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Ninaomba unipe dakika moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka nilizungumzie hili jambo la nyeti. Jambo hili la nyeti, niwaombe hata Mawaziri, jambo hili ni kubwa, jambo hili linadhalilisha Taifa. Leo tunakaa kujadili… (Makofi/Kicheko)

MWENYEKITI: Mheshimiwa muda wako umekwisha.

MHE. FAGASON A. NKINGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na ninaunga mkono hoja. (Makofi)