Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. MVITA MUSTAFA ALI: Mheshimiwa Mwenyekiti ahsante sana. Kwanza kabisa nimshukuru Mwenyezi Mungu kunijalia afya ya leo kuweza kuhudhuria ndani ya Bunge lako hili Tukufu. Pia nikushukuru na wewe kunipatia nafasi hii ili niweze kuchangia Bajeti ya Waziri Mkuu iliyoletwa mbele yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwashukuru sana wanawake wa Mkoa wa Kusini walionipa ridhaa kuja kuwawakilisha, kuwasemea changamoto zao na kutoa maoni yao. Ninaahidi mbele yako kwamba, sitawaangusha na nitawatumikia ipasavyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikishukuru sana pia Chama changu Cha Mapinduzi kwa kunilea tangu nikiwa Mwenyekiti wa Tawi hadi kufika taifani na hivi leo nimekuwa Mbunge wa Viti Maalum, ninawasemea wanawake wenzangu wa Chama Cha Mapinduzi kutoka Mkoa wa Kusini. Ninakiombea kwa Mungu Chama hiki kiweze kushika madaraka awamu bila kutetereka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ninatoa pongezi zangu za dhati kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa namna anavyoipambania nchi yake, pamoja na wananchi wake kiujumla. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninathubutu kusema Mama huyu ni wa mfano, mwenye maono na mzalendo na ninamwombea pia abarikiwe yeye na kizazi chake, pamoja na familia yake na jamii ya Watanzania anaotuongoza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kumpongeza Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Rais wangu kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa namna anavyoipambania Nchi ya Zanzibar kwa kuleta maendeleo makubwa na kutuliza amani ndani ya Nchi ya Zanzibar. Insha Allah naye Mwenyezi Mungu atampa busara na hekima ya kuongoza vyema Zanzibar, Amina. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa umuhimu mkubwa ninapenda sana kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na wananchi wake wa Jimbo la Iramba Magharibi kwa upendo wao mkubwa waliouleta, walioufanya, kutuletea mchapakazi huyu ndani ya Bunge letu hili Tukufu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina furaha zaidi pale ninapomwona Mheshimiwa Waziri Mkuu akihudumia ama akifanya ziara kwenye mikoa tofauti tofauti na kuyachukua matatizo ya Watanzania akayaona kama ni matatizo ya kwake. Kitendo hiki cha Mheshimiwa Waziri Mkuu kinadhihirisha kwamba yeye ni mtu mwenye utu, mwenye ubinadamu na mwenye ustaarabu. Itoshe kusema kwamba ninamwombea naye dua kwa Mwenyezi Mungu Insha Allah Mungu ampe hatma njema na amuone mja wake. Amina. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu mimi ni mdogo nitajikita zaidi kwenye sekta ya uvuvi hasa uvuvi wa bahari kuu. Ninaipongeza sana Serikali yangu sikivu kwa kutambua umuhimu wa wavuvi wadogo hasa wale wanaovua ukanda wa bahari kuu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali hii imeamua kwa makusudi kuwaletea meli ambayo imefika Februari na ni meli yenye njia ya mshipi wa kina kirefu (mita 22) kwa lengo la kupunguza ukali wa wavuvi hawa, kwa lengo la kuwaongezea kipato wavuvi hawa na kwa lengo pia la kuongeza kipato cha nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kushauri Serikali yangu tukufu. Kwa kuwa Tanzania ni sehemu ambayo ina bahari kuu ndani yake; ni dhahiri kwamba wananchi wengi wa maeneo hayo ya bahari kuu, ni wenye kufanya shughuli za uvuvi hasa uvuvi wa bahari kuu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndani ya Zanzibar kuna maeneo yapo karibu sana na ukanda wa bahari kuu, takribani kutoka maeneo wanayoishi wavuvi hao unaweza ukatumia takribani masaa mawili au masaa matatu. Maeneo hayo ni machache ambayo ninayoyajua yapo Katika Mkoa wa Kusini, Wilaya ya Kusini Unguja. Maeneo hayo ni Vijiji vya Jambiani, Mtende, Kizimkazi, na Makunduchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo hayo wanayokwenda kuvua hujulikana kwa jina maarufu fungu mbaraka. Maeneo hayo ya fungu mbaraka ni maeneo ya bahari kuu kama tujuavyo bahari kuu kabisa (kina kirefu cha maji). Ninahurumia sana wavuvi hawa wadogo wadogo wanaokwenda kuvua bahari kuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza wanapoondoka kufikia eneo hilo la uvuvi la bahari kuu, kwanza kabisa kinachopotea kwa wao ni mawasiliano. Maeneo hayo hayana mawasiliano kabisa na tuangalie ukaribu wa kutoka kijijini wanakoishi na wanakokwenda kuvua takribani masaa matatu tu, lakini ndani ya masaa matatu wakifika mawasiliano yale hupotea kabisa. Hii inadhihirisha uchungu wanaoupata wakati wanapokuwa kwenye kazi zao za kutafuta riziki. Huwa takribani kwa muda wa siku tatu au nne wanapokwenda kuvua, wanashindwa kupata mawasiliano na familia zao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nyenzo zao pia wanazotumia kufikia huko haziridhishi na ni duni. Ni nyenzo za zamani, mara nyingi hutumia maboti ya mbao ama fibre ndogo. Kama tujuavyo bahari kuu ni sehemu ya hatari, lakini pia ni sehemu yenye kina kikubwa sana cha maji. Hata hivyo, vyombo vyao wanavyotumia ni vyombo duni kama tulivyosema. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu kubwa kwa Serikali, wavuvi hawa waweze kusaidiwa kwa hali na mali. Ingawa Serikali yetu imeshanunua meli nayo ni moja, lakini pia ninaiomba Serikali yangu inunue meli japo za size ya kati kuweza kuwapatia wavuvi hawa wanaovua sehemu ya ukanda wa bahari kuu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lazima tuwahurumie waume zetu hawa, kaka zetu hawa, ndugu zetu hawa. Maana kadhia wanayoipata inakuwa ni kubwa sana. Ninasema hayo kwa sababu mimi ni mdau, lakini pia ni mkazi wa maeneo hayo ambayo nipo karibu na bahari kuu. Hivyo, ninaiomba sana Serikali yangu sikivu iweze kuwasaidia, ishirikiane na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar waweze kusaidiwa wavuvi hawa wadogo wadogo wanapokwenda maeneo ya bahari kuu kwenda kuvua, wapatiwe boti angalau za size ya kati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukifanya hivyo, tutawasaidia sana kukuza kipato chao, lakini pia zile ajira kwa vijana nazo pia tutaziinua sana kwa sababu maeneo haya vijana wanapokuwa wamefanya mtihani na hawakufaulu, basi kazi yao kubwa wao hujishughulisha kuingia kwenye uvuvi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kama Serikali tunahitaji kuongeza ajira kupitia vijana na kupitia sekta hii ya uvuvi wa bahari kuu, basi lazima tuwasaidie wavuvi hawa kuwapelekea boti ndogo ndogo zenye miundombinu za kuwasaidia, za kuweza kuwapatia kipato zaidi, lakini pia kuongeza pato la Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimejaribu kusema hayo kwa sababu ni mara yangu leo ya kwanza, lakini nimeamua kuzileta changamoto za wenzangu. Ninashukuru sana kupata nafasi hii na ninashukuru sana kwa kuwasilisha changamoto za wenzangu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)