Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nyamagana
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JOHN F. NZILANYINGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia kwenye hoja ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Kabla sijasema ninaomba nianze kwanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema ambaye ametujalia afya na uzima na hata tumekutana hapa tukiwa salama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ni mara yangu ya kwanza ninachangia kwenye hoja hii na kusimama mbele ya Bunge hili, nitumie fursa hii sana kuwashukuru wananchi wangu wa Jimbo la Nyamagana kwa namna ambavyo wananipa ushirikiano na hivyo kuifanya kazi yangu ya Ubunge kuwa nyepesi sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuwa nimeyasema hayo ninaomba sasa nami nichangie kwenye maeneo machache ambayo yameguswa kwenye hoja ya Ofisi ya Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nitapita kidogo upande wa TAMISEMI. Kwa bahati njema nimekuwa Mjumbe wa Kamati ya TAMISEMI, nimepata fursa ya kuyachakata kwa upana masuala yanayowagusa Watanzania moja kwa moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee sana nitumie fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI Profesa Shemdoe. Kwa kipindi kifupi ambacho nimekaa naye Mheshimiwa Profesa ameonesha uhodari mkubwa sana. Sambamba na Profesa Shemdoe nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Mwigulu. Kwa kipindi ambacho ameifanya kazi ya kupita kwenye mikoa mbalimbali amefanya kazi nzuri sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, alipokuja kule kwetu Mwanza, Wanamwanza walimwona kama mtu wa tofauti sana kutokana na kazi njema alizokuja kuzifanya. Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kipindi kifupi ameleta matumaini pale ambapo Watanzania walionesha kukata tamaa, ameleta nuru pale ambapo Watanzania waliona giza. Mheshimiwa Waziri Mkuu ameleta matumaini na kuwaunganisha watu ndani ya kipindi kifupi sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mantiki hiyo nikubaliane na wenzangu; ya kwamba kazi zote hizi zinazofanywa na wasaidizi wa Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI pamoja na Mheshimiwa Waziri, Mkuu ni kazi ambazo zinaakisi mipango na nia njema ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ambayo imejielekeza kuleta maendeleo sawasawa na mapenzi ya Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, upande wa Wizara hii ya TAMISEMI nimeisoma bajeti hii kwa mapana, lakini nimeiona ipo changamoto kubwa sana upande wa TARURA. Waheshimiwa Wabunge wenzangu watakubaliana na mimi; ninapochangia kwenye mpango huu wa bajeti tumekaa sana na Profesa Shemdoe, lipo jambo la dharura kwenye upande wa TARURA. Barabara nyingi kwenye majimbo yetu zimeharibika sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maelekezo yalitoka yakapelekwa kwa Mameneja wa TARURA, wameleta maombi ya dharura, Wizara imekwishafanya tathmini ambapo tayari imebaini kinahitajika kiasi cha zaidi ya bilioni 90 kwenda kukabiliana na changamoto ya dharura ya mafuriko na kuharibika kwa miundombinu ya barabara kwenye majimbo yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachotaka kuishauri Serikali, kwa sababu kazi nzuri imekwishafanyika, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana ai-push Serikali iweze kutoa fedha ili tukaweze kupambana na kuondoa adha ya changamoto za barabara ambazo zimekatika katika majimbo yote. Hii haihitaji kuchukua muda mrefu sana kwa sababu fedha hizi ni kwa mpango wa dharura. Haitakuwa na maana kubwa sana fedha zimeombwa mwezi Machi wakati wa mahitaji halafu ziletwe mwezi Juni au Julai; dhana halisi ya dharura haitakuwepo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, upande huo huo wa TARURA ipo sheria moja ambayo pengine tuliipitisha kwenye Bunge hili hili ambayo inatufanya kurudi huko tulikotoka. Sheria hii ni kandamizi sana. Watendaji wa TARURA chini ya Waziri wa TAMISEMI wanafahamu. Ipo changamoto ya kuharibika kwa barabara. Unaweza ukakuta barabara imetoboka shimo kidogo tu, imeharibika sehemu ndogo sana, lakini kwa namna sheria hii ilivyo Meneja wa TARURA wa Wilaya ambaye si Meneja wa TARURA wa Mkoa hana mamlaka ya kuidhinisha fedha kwenda kufanya ukarabati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa ninajaribu kufanya analysis katika Jimbo langu la Nyamagana; kuna changamoto kubwa sana ya mashimo pale Liberty. Nilijaribu kuzungumza na meneja wangu wa TARURA akaniambia thamani ya fedha iliyokuwa inahitajika kuziba pale haivuki hata milioni tano; lakini kwa utaratibu ulivyo hata kama kingelikuwa ni kiraka cha shilingi milioni moja ni lazima aandikiwe Meneja wa Mkoa aletewe Waziri ije kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ndani ya Bunge hili ili ipitishwe kwenda kuziba kiraka cha shilingi milioni moja; kitu ambacho hatuwatendei haki Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo tukubaliane; maisha ya Watanzania wengi tunaowawakilisha kwenye majimbo yetu yanaguswa moja kwa moja kwenye suala la miundombinu ya barabara. Ninataka nikwambie, katika Jimbo langu la Nyamagana, mtandao wa barabara ni zaidi ya kilometa 1,225. Nilikuwa ninajaribu kufanya hesabu kidogo kwa haraka haraka, nikasema kama tutakwenda na utaratibu wa namna fedha zinavyokwenda kutengeneza hizi barabara itatuchuku zaidi ya miaka 150 Nyamagana kuenea lami kwenye mitaa yote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nini kifanyike; nimekwisha kushauri huko nje na hapa ninaomba nishauri. Jimbo la Nyamagana ambalo ndilo Jiji la Mwanza makusanyo yetu ya fedha za ndani ni zaidi ya bilioni 30. Nilikuwa ninataka kuishauri Serikali na kuiomba sana; sisi watu tunaotoka kwenye Majiji, tunaotoka kwenye Manispaa watupe vibali ili tuweze kukopa fedha tujenge barabara kwa wakati ili tuweze kuwasaidia wananchi wetu kuondokana na changamoto hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni simple logic tu, dunia ya leo nikirejea maneno ya marehemu Mengi, aliwahi kusema wakati anazungumza na moja ya makongamano ya vijana. Alisema kuwa huwezi kuwa tajiri bila kukopa na ndiyo maana hata sisi mradi wetu wa reli tulilazimika kukopa na hatimaye tunayaona manufaa yake leo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakitupa kibali sisi watu wa Mwanza wa Jimbo la Nyamagana tukaenda benki tukachukua fedha bilioni 50 au 60, kwa kuanzia, barabara ambazo tungezijenga kwa zaidi ya miaka 30, ninataka nikuhakikishie kuwa ndani ya kipindi cha miaka mitatu karibu robo ya barabara zote ndani ya Jimbo la Nyamagana zitakuwa zimejengwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nje na hilo nigusie kidogo upande wa 4:4:2; kwa maana ya fedha ya 10% ya vijana, akina mama na watu wenye ulemavu. Tunafahamu kuwa huko nyuma fedha hizi zilikuwa zinatoka kwa utaratibu maalum; lakini hapo katikati zikasimama. Kwa dhamira ya dhati na upendo wa Mheshimiwa Dkt. Samia kwa Watanzania fedha hizi zimerejeshwa tena.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka nikwambieni ukweli, kwamba malengo ya fedha hizi kwenda kuwahudumia wananchi wetu ili waweze kupata mikopo kwenye halmashauri zetu si sawa na vile ambavyo ilikusudiwa. Watanzania wengi wenye sifa hawapati hizi fedha; na mimi nimejaribu kufuatilia kwa research ndogo, takriban 75% – 80% ya waombaji hawapati hizi fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii yote ni kwa sababu ya ukiritimba. Lipo jambo moja ambalo wakati wa kupita pita lilikuwa linanisikitisha sana. Ukienda huko chini kwenye kila kata tuna Maafisa wa Maendeleo ya Jamii. Utaratibu wa kuzitoa fedha hizi unavyofanyika; wanaweka hayo matangazo, lakini hakuna taarifa inayopelekwa kwa wananchi kwenda kuwahamasisha na kuwapa elimu. Maafisa wetu wa Maendeleo ya Jamii wamebaki kuwa ni watu wa ofisini kusubiria kupokea maombi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa dhana halisi ya kuwatumikia Watanzania, jambo la kwanza wanapaswa watoke wawafuate wananchi walipo, wakaitishe mikutano, wawahamasishe wawaeleze masharti na namna gani wanaweza wakazipata hizi fedha ili ziweze kuwasaidia kuinua uchumi wa mmoja mmoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kundi letu la vijana linahangaika na ajira na hii ni ajenda ya nchi ama pengine ni ajenda ya dunia. Serikali haiwezi kuajiri watu wote. Namna pekee ya kuwasaidia vijana wapate ajira ilikuwa ni kupitia fedha hizi za 10% kwa vijana pamoja na watu wenye ulemavu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka niishauri sana Serikali, Profesa Shemdoe, waangalie namna mpya ya usimamizi wa hizi fedha, fedha hizi kwenye baadhi ya maeneo zinakwenda benki, zinakaa huko zaidi ya mwaka hazijawahi kuguswa wakati Watanzania wenye uhitaji wapo wengi. Kwa hiyo nitumie sana fursa hii kuiomba Wizara husika pamoja na Serikali, iangalie namna bora ambayo itaweza kuwasaidia Watanzania na hatimaye kijana wa Kitanzania, mama wa Kitanzania na watu wenye ulemavu waliopo ndani ya nchi yetu waweze kunufaika na mikopo hii ambayo Dkt. Samia Suluhu Hassan ameendelea kuitoa kwenye Taifa letu…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Muda wako umekwisha Mheshimiwa.
MHE. JOHN F. NZILANYINGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapohitimisha nitumie fursa hii kumpongeza sana Dkt. Samia, amefanya kazi nzuri, nchi imetulia, wananchi wanafanya kazi zao kwa amani. Niwahakikishie tu wananchi ambao wanatusikiliza, sisi wawakilishi wao tupo macho kuifanya kazi iliyo njema ya kuishauri Serikali. Zaidi ya yote nina uhakika, kwamba matumaini aliyoyaahidi Mheshimiwa Dkt. Samia ifikapo 2030 yanakwenda kuonekana kwa vitendo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema hayo, ninaomba kuunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)