Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Asha Salum Motto

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. ASHA S. MOTTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi nami ya kuchangia hotuba hii ya Waziri Mkuu. Kwanza kabisa ninampongeza Waziri Mkuu kwa hotuba nzuri, hotuba yenye matumaini kwa Watanzania, ninaomba mchango wangu nijielekeze kwenye sekta ya afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tunavyojua Serikali inafanya kazi kubwa sana katika kuendeleza sekta hii ya afya hasa kutengeneza miundombinu, lakini pia nitumie fursa hii kumpongeza sana Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kupewa tuzo bora iliyotokana na kuzuia vifo vya mama na mtoto, hongera sana Dkt. Samia Suluhu Hassan, kazi zake zinaonekana na jitihada zake zinaonekana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaipongeza pia Serikali kwa kutengeneza Kiwanda kikubwa sana cha Dawa kile cha Arusha, ifikapo 2030 kiwanda kile kinaenda kutuheshimisha, zamani dawa tulikuwa tunapata 80% zinatoka nje, 20% sisi wenyewe, ifika 2030, 80% itatoka ndani na 20% tutategemea kutoka nje. Hii ni hatua kubwa sana kiwanda hiki kinaenda kutuheshimisha Nchini Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Afya ina mambo mengi sana, ninaomba nijielekeze kwenye magonjwa sugu hususani suala zima la ugonjwa wa figo. Ugonjwa wa figo ni miongoni mwa magonjwa ambao unaendelea kukua kwa kasi sana, magonjwa haya hasa kwa sasa yanaathiri sana vijana kuliko miaka ya zamani. Takwimu ya ugonjwa wa figo Tanzania inaonesha asilimia saba ya Watanzania wana ugonjwa wa figo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu waliogunduliwa na ugonjwa wa figo wanafikia takribani 8,800, watu wanaotumia dialysis mpaka sasa wamefikia 3,800, watu 5,000 mpaka sasa hivi bado hawatumii hii huduma ya dialysis. Ukiangalia takwimu hiyo unaona kabisa idadi ya wagonjwa wanaohitaji huduma ya dialysis imeongeze kama mara tatu kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita. Mwaka 2019 wagonjwa wa figo walikuwa 1,017, mwaka 2023 wagonjwa hawa wa figo waliongezeka kufikia idadi ya watu 3,200, ukiangalia 2025 wagonjwa wa figo wamefikia zaidi ya wagonjwa 3,300.

Mheshimiwa Mwenyekiti, magonjwa haya yanayo visababishi mbalimbali, lakini visababishi hivi ukiangalia hasa kuna kisukari, pressure, mtindo wa maisha ambao ulaji wa chumvi, mafuta na pombe au sigara. Ukiangalia takwimu vijana wengi ndiyo wanaoathirika sana na ugonjwa huu, ninaomba niishauri Serikali ichukue ugonjwa huu wa figo kama agenda, niwashauri Wabunge wenzangu ugonjwa huu unaenda kuteketeza nguvu kazi ya Taifa. Baada ya miaka 10 ijayo kama hatutaweza kuthibiti ugonjwa huu wa figo vyanzo vinavyosababisha ugonjwa wa figo hakika nguvu tunayoitumia ndani ya Bunge hili kufanya uwekezaji mkubwa, kuwa-invite wawekezaji katika miradi mikubwa tutafanya kazi ya bure kwa sababu miradi inaenda kutekelezwa na nguvu kazi ambazo tunaenda kuzitegemea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninaomba nishauri ikiwezekana tuongeze bajeti kwenye Wizara hii ya Afya hasa kwenye kitengo hiki cha magonjwa sugu ili kufanya awareness ili tuweze kupambana na gonjwa hili na changamoto hizo ambazo zinasababisha ugonjwa huu. Kama ambavyo Serikali ilipambana na ugonjwa wa UKIMWI, kama ambavyo Serikali ilipambana na magonjwa haya ikiwemo kifua kikuu kutafuta kinga. Hivyo hivyo, ugonjwa huu wa figo tuchukue kipaumbele ili kunusuru nguvu kazi ya Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba pia nichangie katika sekta ya uchumi wa bluu. Mpango wa Maendeleo ya Taifa umeeleza kuwa uchumi wa bluu kuwa ni mpango wa mkakati katika kukuza uchumi wa Taifa kwa kutumia rasilimali zinazotokana na mito, bahari pamoja na maziwa. Kule Mkoa wa Mtwara tumebahatika kuwa na bahari ambayo ina rasilimali nyingi sana zinazotokana na bahari ile. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi Mkoa wa Mtwara una wafanyabiashara ambao tayari wameshaji-engage katika suala zima la kuvuna zao la mwani, kufuga majongoo, kusindika samaki, lakini wavuvi wadogo wadogo wapo wengi sana ambao wanavua samaki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, ninaomba nishauri Serikali, kwa kuwa pia tuna bahari kubwa ambayo ina pweza, ina prawns na samaki wengi, mazao haya ya bahari yanachochea kipato kikubwa sana Nchini Tanzania. Ukiangalia takwimu ya uchumi mwaka 2024, asilimia kubwa ya kipato kile ilitokana na mchango huu wa mazao haya ya Bahari. Ilichangia USD dola takribani 180.6. Unaona ni namna gani uchumi unaotokana na rasilimali za bahari unachangia kiasi kikubwa sana uchumi wetu wa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nishauri hapa sasa; kwa kuwa tuna uwezo wa kuvua samaki hao tunaomba Serikali kuongeza kupeleka vifaranga vya samaki na kutupatia vifaranga vya prawns ili tuweze kufuga kwa wingi zao hili ili liweze kuongeza tija. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wafanyabiashara wale wadogo wadogo ambao tayari wameshajiingiza katika kusindika vyakula vile wapewe mafunzo, mitaji, waongezewe elimu ya kutosha ili waweze kuongeza tija.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nichangie suala la mwisho linalohusu maendeleo ya jamii. Ninaipongeza sana Serikali kwa kutupatia mikopo ya 10% kwenye sekta hii ya maendeleo ya jamii. Kwenye hizi 10% kwa ajili ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu; wanawake wanapata asilimia nne, vijana asilimia nne na watu wenye ulemavu wanapata asilimia mbili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022, Mkoa wa Mtwara una jumla ya wanawake 158,165. Takwimu ya maendeleo ya jamii inaonesha kuwa Mkoa wa Mtwara Mwaka wa Fedha 2024/2025 ina jumla ya vikundi ambavyo ni rasmi 1,142. Kati ya vikundi hivyo vikundi 661 tu ndivyo vilivyopata mikopo; vikundi 481 havijapata mikopo kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo suala zima la NIDA, wengine walikuwa na mikopo sehemu nyingine, lakini pia kulikuwa na upungufu wa fedha ambazo zilisababisha vikundi vingine kutopata mikopo hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nishauri Serikali; lakini kabla sijashauri; hata ufuatiliaji wa Maafisa Maendeleo ya Jamii kwenda kuhamasisha vikundi bado kasi ni hafifu, kasi ni ndogo sana. Hii ninaona itakuwa ni changamoto ya Tanzania nzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Mtwara una kata 191. Nimefanya ziara kwenye kata zote 191 mwezi Januari. Kila nilipopita changamoto inakuwa kwamba hawamfahamu Afisa Maendeleo ya Jamii, wakati Waziri wa TAMISEMI mwaka jana alitoa tamko kwamba kila kata kuwe na Maafisa Maendeleo ya Jamii, lakini kila nilipokanyaga hawamfahamu. Kila nilipopita malalamiko ni kwamba hatupati mikopo, hatuna mikopo, wengine tumekosa vigezo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia takwimu ni kubwa sana, wanawake ni wengi, vikundi vilivyobaki ni vingi na vikundi hivi vilivyopata mikopo bado kiasi walichopata ni kidogo sana. Ninaiomba Serikali itie nguvu; hasa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, ninaomba iliangalie suala hili kwa mapana zaidi ili kuwawezesha wanawake hawa waweze kupata mikopo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)