Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Yagi Maulid Kiaratu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Singida Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. YAGI M. KIARATU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa nafasi, lakini nichukue fursa binafsi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu mtukufu na mwingi wa rehema. Vilevile nitumie fursa hii kukishukuru sana chama changu, Chama Cha Mapinduzi chini ya uongozi wa Mwenyekiti wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa namna ambavyo alisimamia mchakato wa uchaguzi kuanzia kura za maoni hadi uchaguzi mkuu na hatimaye leo niko hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawashukuru sana wananchi wa Jimbo la Singida Mjini kwa imani kubwa waliyoonesha kwangu wamenichagua kwa kura nyingi nami mbele yako ninawaahidi kwamba nitawatumikia kwa weledi mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesikiliza hotuba ya Waziri Mkuu nimeisoma mara kadhaa, nimeielewa. Taarifa hiyo imetueleza watu tumetoka, mafanikio tuliyoyapata, lakini nini makusudio na matarajio ya wananchi wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kupongeza kwenye makusanyo ya mapato, Serikali imefanya vizuri sana kipindi hiki. Kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 mpaka kufikia Februari tayari walishakusanya shilingi bilioni 26.63 dhidi ya bajeti ya makadirio ya mwaka huo ambayo ni trilioni 25.68 sawa na 103.7%. Haya ni mafanikio makubwa sana na hii inaonesha namna gani sasa nchi inajipanga kwenda kujitegemea na kupunguza utegemezi wa kutoka nje, vilevile uwezo wa kuhudumia jamii ya Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, halmashauri zetu pia zimechangia, ziko halmashauri 184, ziko zinazokusanya kwa kiasi kikubwa ziko zinazokusanya kwa kiasi cha kati, lakini ziko zinazokusanya kiasi kidogo. Miongoni mwao zipo zinazofikia malengo na zipo zisizofikia malengo kwa sababu mbalimbali. Ninaiomba sana Serikali izisaidie halmashauri ili ziweze kupata fedha na kuhudumia wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya eneo ambalo ninataka kuongelea ni fedha ambazo zinakusanywa na halmashauri kwa niaba ya Serikali, lakini sehemu inayotakiwa kurejeshwa huwa hairejeshwi kabisa au inarejeshwa kidogo au haipatikani kabisa. Nitoe mfano wa kodi ya ardhi, Halmashauri zinakusanya kodi za ardhi zinafikisha Serikali, zinapaswa kurudishwa 20%, lakini haijahi kurejeshwa hata siku moja, tukumbuke fedha hizi zinakuwa ziko kwenye bajeti na zinaathiri bajeti kwa maana ya kutofikia malengo. Vilevile, zinaathiri utekelezaji wa shughuli za halmashauri kwa maana ya kutoa huduma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe mfano wa Halmashauri ya Manispaa ya Singida ambayo imekusanya shilingi milioni 999.1, ambapo ilitakiwa irejeshewe shilingi milioni 199.8, sawa na shilingi milioni 200, lakini hazijawahi kurejeshwa. Shilingi milioni 200 kwenye bajeti ya halmashauri ni pesa kubwa sana. Ninaomba basi taratibu za kisheria zifuatwe na fedha hizo ziwe zinarudishwa kwa wakati ili ziweze kufanya kazi zilizokusudiwa kwa mwaka husika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ina kila sababu ya kuzisimamia halmashauri. Tunaona kabisa ziko halmashauri zinakusanya kidogo na hivyo kutoa huduma kwake ni shida. Ninaomba kupitia miradi mikakati halmashauri zipate fedha na miradi hiyo mara nyingi inakuwa imesimama mwaka mzima kuweza kukusanyika. Mfano, mzuri halmashauri zinajengewa stendi zinajengewa masoko. Ninaiomba Serikali Halmashauri ya Manispaa ya Singida ina soko kongwe sana, soko lililojengwa mwaka 1958 linahatarisha walaji, linahatarisha wanaofanya kazi katika eneo hilo lakini pia uwezekano wa halmashauri kupata mapato mazuri unakuwa mdogo. Ninamwomba Waziri Mkuu kupitia nafasi hii basi Serikali ione namna ya kusaidia wananchi wa Manispaa ya Singida kupata soko zuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee habari ya afya. Kwa muda mrefu Halmashauri ya Manispaa ya Singida ilikuwa haina Hospitali ya Wilaya, ni miaka miwili tu tuliachiwa ile ilikuwa Hospitali ya Mkoa kuwa Hospitali ya Wilaya lakini ikiwa haina kitu chochote. Historia ya hospitali hiyo imejengwa mwaka 1950 na kwa wakati wote imekuwa ikikarabatiwa tu, inakosa miundombinu mingi ya muhimu kama chumba cha wagonjwa mahututi, wodi zimechakaa, OPD ndiyo haifai kabisa. Ninamshukuru Naibu Waziri wa TAMISEMI alifika na amejionea, lakini niombe sasa tupate fedha tujenge hospitali nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu hospitali ndiyo imeanza ina mapungufu makubwa ya watumishi, kwa maana ya waganga na wauguzi. Tunaye Daktari Bingwa mmoja tu wa Magonjwa ya Wanawake, hakuna Daktari Bigwa wa Magonjwa ya Watoto, hakuna Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Ndani (physician) lakini hatuna wateknolojia wa madawa, hatuna wateknolojia wa mionzi, hatuna fundi sanifu wa vifaatiba, pia hatuna watalaam wa dawa za usingizi. Hospitali kubwa yenye hadhi kama hiyo kukosa wataalam wote hao siyo sawa. Tunaomba sana TAMISEMI watuangalie watuletee wataalam hao ili tuweze kufanya vizuri katika suala zima la tiba tutekeleze yale ambayo tumeahidi wananchi katika Ilani yetu ya Chama Cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiongelea suala la elimu tumefanya vizuri sana, tumejenga madarasa na shule mpya, tumejenga shule ya sekondari ya wasichana kila mkoa, tumejenga shule za amali, tumepata ajira mpya, lakini bado kuna mapungufu katika miundombinu. Nitoe mfano, Halmashauri ya Manispaa ya Singida mpaka kipindi kilichopita ilikuwa na Shule ya A Level moja tu ambayo ni shule kongwe ya Mwenge Sekondari. Ninamshukuru Rais leo tunavyoongea zimeongezeka shule tano za A-Level. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilichofanyika ni kujenga mabweni, na madarasa na matundu ya vyoo tu, lakini iko miundombinu muhimu iliyosahaulika. Watoto wale wanakaa boarding, hakuna dinning hall, wala hakuna jiko, vyakula vinapikwa mahali ambapo hapafai, lakini watoto wanakula ovyo nje, mara mabwenini mara madarasani, siyo sawa kwa afya za watoto wetu. Tunaomba tunapojenga shule hizi basi angalau miundombinu hii muhimu iangaliwe ili watoto wetu wakae katika mazingira mazuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee suala la TARURA kama ambavyo wamesema wenzangu. Kwa kweli tunayo shida kubwa ya barabara, hapa ninavyoongea Mji wa Singida unahudumiwa kwenye mtandao wa barabara za TARURA kilometa 523 tu, takwimu ambayo ni ya zamani sana. Mji wa Singida unakua kwa kasi, ukiangalia unavutwa na Mji Dada wa Dodoma, tuna zaidi ya kilometa 2,000 ambazo hazijaingia kwenye mtandao, tunaomba Serikali ifanye mapitio ya kila mara ili kupata uhalisia wa urefu wa barabara, lakini bajeti pia ni ndogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Waziri Mkuu kwa namna ambavyo ametoa tamko mbele ya Bunge hili kwamba sasa anaamrisha hela zote ziende kwenye Mfuko na tuzitungie sheria zisitumike bila kibali maalum ili lengo zima la kutengeneza barabara likamilike. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakiri maslahi, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Afya na Masuala ya UKIMWI; tumetembelea, tumeangalia lakini leo niongelee kidogo kuhusu UKIMWI. Hapa bado kuna shida, wote tunafahamu historia ya ugonjwa huu ulianza zamani, ukapewa majina mbalimbali slimfiti, Juliana na kadhalika, pia zamani watu walikuwa wanakonda watu wanaogopa UKIMWI, lakini leo hakuna anayekonda wala hakuna anayeonekana kwa macho kwamba ana UKIMWI. Hii inawafanya watu kupunguza kasi ya upimaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia takwimu ya Watanzania zaidi ya milioni 60 wanaopima hata robo hawafiki, hii maana yake elimu bado haijafika kwa wananchi au kuna kupuuza, hivi ni lazima Serikali ifuatilie kuhakikisha kila mtu anatambua hali ya mwili wake. Wale wanaobainika wana matatizo tayari wanapata tiba na kwa sababu ni tiba endelevu za kila siku walio wengi wameacha na hili ni tatizo kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe mfano, tulienda konga moja Ilala, maeneo ya Pugu, katika watu 700 waliacha matumizi ya dawa waliofanikiwa kurejeshwa ni watu 200 tu, sasa ni hawa walioonekana huko majumbani wako zaidi ya hawa. Kwa hiyo, tuna kila sababu ya kuongeza elimu, ufuatiliaji kuhakikisha wale wanaopatikana wanatumia dawa, kwa ajili ya nguvu kazi ya Taifa. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa, muda wako umekwisha.

MHE. YAGI M. KIARATU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nimalizie kidogo, hasa suala la uraibu wa dawa za kulevya na UKIMWI. Tumegundua kwamba hawa watu wanaendana na Dar es Salaam ni wengi mno, huko tunakoenda watakuwa wengi zaidi. Wako wasiofika kwenye vituo na wako wanaofika kwenye vituo. Serikali iliangalie vizuri na waathirika wengi ni vijana ambao ndiyo nguvu Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono hoja. (Makofi)