Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nanyamba
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi, ili nichangie hoja iliyo Mezani kwetu. Kwa kuanza ninachukua nafasi hii kumpongeza Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anayoifanya, lakini kwa miongozo anayoitoa kwa nchi yetu na hususani anaposhughulikia suala hili la mafuta ambalo tunaona kabisa nchi za jirani na mpaka Ulaya sasa hivi katika vituo vingi vinaandikwa “no fuel”. Hongera sana kwa Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru na kumpongeza pia mtoa hoja, Mheshimiwa Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, kwa kazi nzuri anyoifanya na kwa uratibu wa hii hotuba, ambayo imesheheni takwimu, changamoto zimebainishwa na ametupa matumaini nini kifanyike ili kutatua hizo changamoto. Ninawapongeza Manaibu Waziri wa Wizara hii, ninawapongeza vilevile Mawaziri wa Nchi katika Ofisi hii; tuna Profesa Kabudi na Profesa Shemdoe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sina wasiwasi na Mheshimiwa Waziri, TAMISEMI ameishi, alikuwa Mkurugenzi, akawa Katibu Tawala wa Mkoa, akawa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, TAMISEMI hana cha kujifunza, achape kazi. Vilevile, kama nilivyosema, ana Manaibu wachapakazi wazuri, lakini pia, kuna Manaibu wa Wizara nyingine ambazo zipo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema, kitabu hiki kimejaa takwimu. Nitatoa ushauri katika maeneo mawili, eneo la kwanza ni suala la Kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitabu hiki kimetupa matumaini makubwa sana kwamba, Serikali yetu itaenda kufanya maboresho na itaendelea kufanya maboresho makubwa katika sekta ya kilimo. Miradi ya umwagiliaji itaendelea kutekelezwa, utoaji wa pembejeo za ruzuku kwa mazao ya kimkakati utaendelea, utoaji wa mbegu na vilevile uimarishaji wa ushirika na masoko. Hili ni jambo jema sana kwa sekta yetu ya kilimo, lakini sehemu nyingine ni kuongeza thamani ya mazao yetu na hapa nitachangia kidogo; katika kuongeza thamani ni jambo la muhimu sana, ili tusiendelee kuuza nje mazao ghafi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kusini tuna zao la korosho, ninaipongeza Serikali kwa kuanzisha Kongani ya Viwanda vya Korosho pale Maranje, Halmashauri ya Mji wa Nanyamba. Kazi nzuri imeanza kufanywa, ujenzi umeanza, warehouse mbili zimekamilika, lakini kizuri zaidi ni utekelezaji wa Dira yetu ya 2050 kwa sababu, dira ile inasema kwamba, mipango mingi itekelezwe kwa kushirikiana na sekta binafsi. Hapa tunapoongea kuna kampuni mbili kubwa zimeanza ujenzi wa viwanda viwili vya kubangua korosho, ambavyo kimoja kinaweza kubangua tani laki moja kwa hiyo, kwa viwili vitabangua tani laki mbili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo zuri ni Serikali yetu imetoa fedha kwa Bodi ya Korosho kuanza ujenzi wa kiwanda ambacho kitabangua tani 30,000 kwa hiyo, mkononi tuna uhakika mwakani tutakuwa na tani 230,000. Sasa hivi uwezo wetu wa kubangua ni tani 120,000, kwa hiyo, tukijumlisha na hizi tani 230,000, tuna uhakika mwakani tunaweza kubangua nusu ya korosho ambazo zinazalishwa Tanzania. Hongera sana Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili nina ushauri mmoja tu kwamba, hawa wawekezaji wa sekta binafsi wamefika tayari na ujenzi umeanza. Ninaiomba Serikali yangu ifanye mambo matatu, la kwanza ni, lazima tuweke special incentive. Tuwape vivutio rasmi hawa wawekezaji, ili tusirudi nyuma kwa sababu, huko nyuma tuna historia ya viwanda vya korosho. Tumekuwa na viwanda 12, lakini vyote vilifungwa na uzalishaji ukasimama kwa hiyo, tusirudi tulikotoka, tuwape special incentive hawa wawekezaji ili kazi hii ya ubanguaji iendelee.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu, kazi wanayoifanya ni kubwa sana na korosho zetu zitaongeza thamani kwa sababu, hatutashughulika na korosho tu, hawa sasa watashughulika na ganda la korosho, watashughulika vilevile na tunda la korosho kiasi kwamba, mkulima sasa atapata fedha kwenye korosho yenyewe, atapata fedha kwenye ganda la korosho na atapata fedha kwenye tunda la korosho. Kwa hiyo, thamani ya korosho itakuwa imeongezeka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili, hao wawekezaji wanakuja kutoa ajira kwa nchi yetu kwa hiyo, lazima vilevile tuhakikishe kwamba, hii special incentive inahakikisha kwamba waajiriwa wengi watakaoajiriwa pale wawe vijana wa Kitanzania, wawe skilled au unskilled, wawe vijana wa Kitanzania. Hii itawezekana tu kama, nilivyosema, tutawapa special incentive, lakini vilevile suala lingine la msingi ni utaratibu ambao utawawezesha kupata malighafi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema, hawa watu wanatarajia kutupa ajira, tusiwape utaratibu wa kawaida, lazima wawe na utaratibu maalum wa kuhakikisha wanapata korosho nje ya utaratibu wa sasa na si utaratibu ule wa soko la awali kwa sababu, soko la awali viongozi wengine wa AMCOS wanatumia vibaya na hivyo kuwadhulumu wakulima. Lazima tuandae utaratibu maalum kuhakikisha viwanda vyetu hivi vinapata korosho ya uhakika, ili visije vikafungwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Kongani hii ya Viwanda vya Korosho ipo kilometa 30 kutoka mkuza wa gesi asilia kwa hiyo, ili tuwape motisha ni lazima tuwapelekee gesi kwenye eneo hili la uwekezaji. Kule Mtwara kuna maeneo mawili muhimu, lile Eneo la Malanje na Eneo la Msijute, Mtwara Vijijini, nao tuwapelekee gesi asilia ili wawekezaji waweze kutumia nishati hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili, nimefurahishwa sana na kauli ya Waziri Mkuu kwamba, Wizara ya Kilimo ishirikiane na Wizara ya Viwanda na Biashara kuhakikisha tozo za holela kwenye sekta ya kIlimo zinakomeshwa na kuagiza halmashauri ziache kuweka tozo holela kwenye mazao ya kilimo. Hapa isiwe tu kwa halmashauri, kuna taasisi nyingi zinapeleka tozo kwenye mazao yetu ya kibiashara na hivyo kushusha bei ya mkulima. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye zao la korosho kuna zaidi ya taasisi nane zinachota ushuru kule na hivyo kusababisha kushusha bei kwa mkulima. Kuna TMX wanachukua fedha kule, kuna hizi RS wanachukua fedha kule, kuna Bodi ya Korosho yenyewe inachukua fedha, lakini kuna TARI Naliendele wanachukua fedha na taasisi zingine. Hawa vilevile kwa sababu, hapa tunapitisha bajeti zao za matumizi mengine kwa nini wakachukue fedha kule kwa mkulima? Kwa sababu, hata kama wanaweka charge ndogo, lakini mfanyabiashara anapokwenda kununua anabebeshwa charge ile, anapunguza bei kwa mkulima. Tuondoe hizo tozo, ili mkulima apate bei ambayo ina tija kwa zao lake la korosho na mazao mengine ya kimkakati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesema mchango wangu wa pili utajikita kwenye Serikali za Mitaa. Ukisoma Ibara ya 146 ya Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imeeleza madhumuni ya kuanzishwa kwa Serikali za Mitaa kwamba, ni kupeleka madaraka kwa wananchi. Huko nyuma, kama walivyosema wachangiaji waliopita kwamba, kulikuwa na viprogramu mbalimbali vya kupeleka maboresho kwenye Serikali za Mitaa, hapa katikati tumejisahau, hakuna mipango hiyo na hivyo, suala la upelekaji wa madaraka kwa wananchi linakuwa ni changamoto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bado Serikali Kuu ina mkono mkubwa sana kwenye shughuli zinazoendelea kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa. Ndugu zangu hatuwezi kuendesha maendeleo ya nchi hii kwa kutegemea maagizo kutoka Dodoma, ni lazima tuziwezeshe Serikali za Mitaa na kuziwezesha Serikali za Mitaa ni lazima ziwe na maamuzi, ziwe na autonomy na vilevile ziwe na uwezo wa kifedha, ziwe na vyanzo vya uhakika vya mapato. Halmashauri zetu hazina vyanzo vya uhakika vya mapato; vyanzo vya uhakika vya mapato vimebaki Serikali Kuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninaomba na kwa sababu, Mheshimiwa Rais amefanya maboresho mazuri sana, ameihamishia Ofisi ya TAMISEMI kwa Waziri Mkuu, ninatarajia sasa Mheshimiwa Waziri Mkuu, kama ilivyosemwa kwamba, Waziri wa Nchi mwenye dhamana TAMISEMI, Mheshimiwa Profesa Shemdoe, ameishi katika mazingira haya, wataratibu haya mageuzi. Lazima kuwe na reforms ya kutosha kuhusu Sera yetu ya Ugatuaji. Hadi sasa hivi hatuna sera, lazima tuje na sera za ugatuaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuna Sheria ya Ugatuaji ndiyo maana leo tukiamka tunafanya hivi, kesho tukiamka tunafanya hivi. Lazima tuje na hiyo sheria, ili ugatuaji katika kupeleka mamlaka ngazi ya chini ufanywe kisheria na siyo kwa utashi wa mtu. Vilevile tubadilishe kanuni na miongozo ambayo inaendesha Mamlaka za Serikali za Mitaa; Sheria nyingi, kanuni nyingi zimepitwa na wakati, lakini vilevile ukisoma Dira yetu ya 2050 inasema, ili tufanikiwe ni lazima tutekeleze mambo kwa isivyo kawaida, tukiendesha Serikali za Mitaa kama business as usual hatuwezi kutekeleza malengo ya 2050.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni matarajio yangu TAMISEMI, Ofisi ya Waziri Mkuu, itayafanya mabadiliko haya. Ninakushukuru kwa kunipa nafasi na ninaunga mkono hoja. (Makofi)