Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Cecilia Daniel Paresso

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia hoja iliyoko mbele yetu, hoja ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Kwanza ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya uhai na afya njema ambayo anaendelea kutujalia na kutufikisha siku ya leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, ninakishukuru chama changu, Chama Cha Mapinduzi chini ya Mwenyekiti wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuniamini na kuniteua kuwa Mbunge wa Bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ninawashukuru sana kwa imani yao kwangu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachukua nafasi hii pia kumshukuru Mwenyekiti wetu wa UWT Taifa Mama yetu Mheshimiwa Mary Chatanda kwa kuendelea kutuongoza, kutulea na kutuimarisha ili tuendelee kuwa viongozi bora. Ahsante sana Mama Chatanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza sana Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoendelea kuwafanyia Watanzania, kazi zinazozingatia na kujali utu wa Watanzania. Katika kazi kubwa anazofanya, moja ni kuendelea kusimamia na kuimarisha amani ya nchi yetu kwa kuwa amani ni msingi wa maendeleo ya jambo lolote lile. Hongera sana kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, toka amekuwa kiongozi wa nchi yetu katika kipindi kilichopita na hata sasa, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ameendelea kuhakikisha Watanzania wanapata maendeleo na maendeleo yanawafikia kwenye vijiji vyetu, kata zetu, wilaya na hata katika miradi ya Kitaifa, kwa maana ya miradi kimikakati. Tunamshukuru sana kwa upendo wake kwa Watanzania na ndiyo maana wakati wa uchaguzi aliaminiwa na Watanzania na akapata kura nyingi za ndiyo za kishindo na za heshima kwa kazi kubwa anazofanya na anazoendelea kutufanyia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachukua pia fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi kubwa anayoendelea kuifanya ya kumsaidia Rais pamoja na Mawaziri na Naibu Mawaziri, pamoja na Serikali yote ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi wanayowafanyia Watanzania. Tuna imani wataendelea kuhakikisha kwamba ile dhamira ya Mheshimiwa Rais ya kuwaletea tabasamu Watanzania, wao kama wasaidizi wake wa karibu inaenda kuwafikia Watanzania kwa ari na kwa moyo na kwa nguvu kubwa zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia mikutano ya Mheshimiwa Waziri Mkuu tumeona kazi anayoifanya na kupitia ziara anazofanya ameendelea kurejesha imani ya Watanzania. Tunamwombea mafanikio, asonge mbele kwa kasi hiyo hiyo, aendelee kuwafikia Watanzania popote pale walipo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitajikita mchango wangu katika sekta ya elimu. Kufuatia mabadiliko ya mitaala, lakini kupitia mabadiliko ya Sera ya Elimu ya Mafunzo na Ufundi ya Mwaka 2014 pamoja na toleo jipya la mwaka 2023, sekta hii inaenda kukabiliwa na mabadiliko makubwa ambayo yanahitaji rasilimali fedha pamoja na rasilimali watu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni matumaini yangu kwamba tutakapoanza utekelezaji wa Sera hii mwaka 2028, Serikali itakuwa imeshafanya maandalizi yote muhimu na ya kutosha kuhakikisha kwamba wale wanafunzi wote wakimaliza darasa la sita, wanapoanza kidato cha kwanza, kwa kuwa sera inaelekeza kwamba sasa elimu ya sekondari itakuwa ni sehemu ya elimu ya msingi na itakuwa ni sehemu ya elimu ya lazima, basi wanafunzi hao waweze kupata masomo na kufika madarasani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na kupunguzwa kwa muda huo na kutokana na makadirio ya awali ya wanafunzi wanaotarajiwa kujiunga na kidato cha kwanza, kwa mujibu wa takwimu mbalimbali tunatarajia kwamba ifikapo mwaka 2028 kidato cha kwanza tutatarajia kuwa na wanafunzi 2,973,195. Hili ni ongezeko kubwa la mara moja na ongezeko hili litahitaji maandalizi ya kutosha na maandalizi haya yanapaswa kuanza sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yapi ambayo yanatakiwa kuanza na yapi ambayo ni mahitaji? Tunapotarajia wanafunzi hao ninaomba nitaje kwa uchache mambo ambayo yanahitajika. Tunahitaji vyumba vya madarasa 35,564 kwa uwiano wa darasa moja kwa wanafunzi 45. Tunahitaji walimu wapya 35,000 kwa uwiano wa mwalimu mmoja kwa wanafunzi 45. Pia, tunahitaji matundu ya vyoo kwa wanafunzi wa kiume 31,000 kwa uwiano wa tundu moja kwa wavulana 25. Vilevile, tunahitaji matundu ya vyoo kwa watoto wa kike 41,268 kwa wasichana na kwa uwiano wa tundu moja kwa wasichana 20.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunahitaji kuwa na maabara 9,366. Tunahitaji mishahara kwa ajili ya walimu wapya, tunahitaji vitabu, tunahitaji gharama za uendeshaji, pamoja na mambo mengine. Haya niliyoyataja ni kwa uchache. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa takwimu hizi, maana yake Serikali katika mwaka huu wa fedha tunaoanza kuujadili 2026/2027 tunahitaji kiasi cha shilingi trilioni 2.12 ili kuanza maandalizi ya kuingiza wanafunzi 2,973,195 kidato cha kwanza ifikapo mwaka 2028.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, ninaipongeza Serikali kupitia hotuba ya Bajeti ya Waziri Mkuu aliyoisoma hapa, wameshaanza hatua za awali ambazo ni hatua muhimu kwa kuweka matarajio ya kutenga kiasi cha shilingi trilioni 1.77 kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa Sera hii na kuhakikisha hawa wanafunzi wote ifikapo mwaka 2028, waweze kuingia kidato cha kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu, ni matumaini kwamba utengaji wa bajeti kwenye vitabu ni jambo moja, lakini utekelezaji ili sasa tuweze kwenda kutekeleza kujenga madarasa na mambo yote yanayohitajika ni hatua ya pili. Ni rai yangu kwa Serikali, tuone basi maandalizi yanaendelea kufanyika utekelezaji unaanza ili kuhakikisha hawa wanafunzi itakapofika mwaka 2028 wote waweze kuingia kidato cha kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa nafasi na huo ndiyo mchango wangu. Ninaunga mkono hoja. (Makofi)