Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Vwawa
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa na maono makubwa ambayo ameyafanya ambayo anaendelea kuyatenda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, ninachukua nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na taasisi zake na Wizara zote ambazo ziko chini yake kwa kazi kubwa ambayo ameifanya, pia kwa hotuba nzuri na uwajibikaji uliotukuka ambao ameanza kuuonyesha katika nchi yetu. Tunampongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachukua nafasi hii kumpongeza Mkuu wangu wa Mkoa wa Songwe, Mheshimiwa Jabiri Makame pamoja na viongozi wengine wote wa mkoa, lakini Mkuu wa Wilaya, Wakurugenzi na watumishi kwa ujumla, kwa namna ambavyo tumekuwa na ushirikiano katika kutekeleza na kuleta maendeleo katika Mkoa wetu. Ninawapongeza sana namna hiyo na tukiendelea hivi nina uhakika mkoa wetu utapiga hatua kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ninataka kuchangia maeneo machache tu, lakini ninataka nianze kwanza, Baba wa Taifa alituambia maadui wakubwa wa Taifa letu aliwataja watatu, na mimi leo nitaongeza ili wawe wanne, maadui wakubwa wa Taifa letu. Maadui hao alisema ni suala la umaskini, ujinga, maradhi na suala sasa la ukosefu wa ajira kwa vijana. Hawa maadui ni sumu kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka niseme ninaipongeza sana Serikali ya Awamu ya Sita imechukua hatua kadhaa kuhakikisha kwamba inapambana na hao maadui na tunawatokomeza. Mpaka sasa hivi tunaona ujenzi wa viwanda unaoendelea katika nchi yetu katika maeneo mengi. Hii ni kwa sababu tunataka kupunguza umaskini, tunataka kuongeza ajira kwa vijana, lakini pia tunataka kujenga uchumi ulio imara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaona jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita kuweka ruzuku kwenye kilimo, pamoja na sekta nyingine za uzalishaji, pamoja na bajeti zao kuongezeka ili tuweze kupunguza umaskini, ili tuweze kujenga uchumi imara, ili tuweze kuhakikisha tunaondokana na ujinga. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaona ukarabati wa bandari mbalimbali unaofanyika, uwekezaji mkubwa unaofanyika, lakini tunaona ufufuaji wa Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) yote haya yana msingi wa kutaka kupambana na kupunguza umaskini tulionao, lakini kutengeneza ajira kwa wananchi wetu wa Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaona utalii; Tanzania imebarikiwa kuwa na vivutio vingi vya utalii vizuri vya asili, lakini jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita katika kuvutia watalii, hili ni kwa sababu tunataka kupambana na hao maadui ambao nimewasema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaona ujenzi wa barabara mbalimbali unaoendelea katika nchi yetu na hasa katika maeneo mbalimbali. Ujenzi wa maghala unaoendelea, yote haya ni katika kutaka kukabiliana na umaskini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaona ujenzi wa shule na madarasa mbalimbali, vyuo, ujenzi wa zahanati, ujenzi wa hospitali, kuanzisha mambo mbalimbali. Yote haya ni katika kutaka kupambana na hao maadui wakubwa na sisi Wanajimbo la Vwawa tuko bega kwa bega katika kuhakikisha kwamba tunapambana na hao maadui wakubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunataka kupambana na umaskini. Hatufurahii tunapoona 25% ya Watanzania wanaishi katika umaskini. Hatufurahii kuona watoto wetu hawasomi na kupata elimu iliyo nzuri. Tunataka wapate elimu nzuri, wapate maarifa mazuri, wajifunze teknolojia za kisasa ili maisha yao yawe mazuri na yaboreshwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kufanya hivyo, sisi Wanavwawa tunaiomba sasa Serikali ya Awamu ya Sita iendelee kutuunga mkono Wanavwawa kwa kufanya mambo yafuatayo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza, tunaomba Manispaa ya Mkoa wa Songwe. Mkoa wetu ni wa mwisho kuanzishwa. Mkoa wetu ni mkoa pekee ambao hauna manispaa wala halmashauri ya mji hatujapata bado. Tunaiomba Serikali na Mheshimiwa Waziri Mkuu atusikie. Sasa ni wakati muafaka Mkoa wa Songwe tunastahili kupata manispaa ili iweze kuchochea kuleta maendeleo zaidi katika Mkoa wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana tuliahidiwa kujengewa stendi ya mkoa, lakini na Soko la Mazao la Kimataifa. Mkoa wetu ni wa kilimo, tunahitaji mazao yetu yauzwe kwa Watanzania, lakini pia kwa taasisi mbalimbali kutoka nje ya nchi. Tunataka soko pale, tunataka stendi pale. Ninaomba Mheshimiwa Waziri Mkuu atusikie sasa, mwaka huu ianze kujengwa. Ninajua iko kwenye bajeti, basi hela zikitoka mapema ikajengwa itatusaidia sana kupunguza umaskini na kuhakikisha kwamba Wanamkoa wa Songwe na Wanajimbo la Vwawa wanapiga hatua kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunahitaji barabara. Barabara ya kutoka Vwawa – Londoni – Isalalo – Msia – Isalalo tuliahidiwa kwamba itaanza kujengwa, tunaomba sasa mwaka huu ianze kujengwa tuone matokeo. Barabara ya kutoka Ihanda – Ipunga ni muhimu sana kwa uchumi kwa sababu kule ndiyo uzalishaji mkubwa unakotoka. Mahindi yanazalishwa kwa wingi, kahawa inazalishwa kwa wingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Barabara ya kutoka Vwawa – Ndolezi – Iyula, ni kiunganishi kikubwa sana. Zao la kahawa litaweza kupata manufaa na hizi barabara zikikamilika nina uhakika mkoa wetu utapiga hatua kubwa na tutatoa mchango mkubwa katika ujenzi wa uchumi wa Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunahitaji Bandari Kavu pale Mpemba. Bandari hii tumeimba kwa muda mrefu, ninashukuru kwa kuona jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita ilizozichukua katika kuhakikisha kwamba tunaanza kuijenga hii bandari. Sasa, ninaona kama tuko polepole sana, ninaomba tuongeze kasi ili ile Bandari Kavu ijengwe pale Mpemba mizigo isafirishwe na TAZARA, isafirishwe ifike pale, basi wananchi wale, wale wafanyabiashara wa kutoka sehemu mbalimbali nchi jirani wachukue mizigo yao pale. Tutakuwa tumechangia uchumi mkubwa, tutakuwa tumejenga uchumi mkubwa wa Mkoa wa Songwe na nchi kwa ujumla. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mkoa wetu tunahitaji vyuo vya elimu ya juu. Hatuna chuo hata kimoja hata cha ngazi ya kata hatuna. Ni wakati muafaka umefika kwa mkoa wetu uangaliwe kwa sura ya kipekee kabisa, ili tupate angalau chuo chochote cha elimu ya juu kiweze kuwaandaa vijana wetu wawe na ujuzi unaostahili, wawe mahiri waweze kushiriki katika ujenzi wa Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunahitaji maji katika kata mbalimbali. Pale Vwawa tuna changamoto ya maji. Ninamshukuru Mheshimiwa Rais alileta Mradi mkubwa wa Maji ule wa Mto Momba. Bado haujakamilika, ndiyo unaanza uko kwenye hatua ya awali, lakini pale pana changamoto kubwa ya maji. Ninaomba basi jitihada zifanyike ili kile Kisima cha Ichenjezya na maeneo mengine basi yaweze kupatiwa maji kwa kuangalia vyanzo vingine vilivyopo wakati tunasubiri huu mradi mkubwa kuweza kukamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukamilishaji wa maboma Serikali ya Awamu ya Sita imefanya kazi kubwa sana na sisi Mbozi katika Taifa hili ndiyo ninafikiri wilaya ya kwanza kuwa na maboma mengi ambayo wananchi walijitolea kwa nguvu zao wakaanza kujenga. Kulikuwa na maboma 1,520, mpaka sasa hivi bado mengi hatujayakamilisha. Ninaomba Serikali tuweke mkakati wa kuhakikisha kwamba haya maboma tunayakamilisha kadri itakavyowezekana. Pale Iboya tunajenga kituo cha kukagua mizigo mbalimbali, ambacho kitajengwa na TANROADS. Tunaomba kile kituo kijengwe haraka ili kupunguza foleni ya Tunduma ikaguliwe pale na mambo yaende. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kabla sijahitimisha niongezee mambo mawili. La kwanza, ninaishauri Ofisi ya Waziri Mkuu; tulianzisha madaraka mikoani, tulifanya ugatuaji wa madaraka. Hii sera ni ya muda mrefu, kuna haja sasa ya kuipitia vizuri kuangalia kama je, tumekidhi na kufikia matarajio tuliyoyatarajia? Ugatuaji wa madaraka mikoani ni muhimu sana, lakini tuone kwamba kweli namna tunavyokwenda namna tunavyoendesha TAMISEMI, tunavyoendesha Serikali za Mitaa tunafikia yale malengo tuliyokusudia kuyafanya. Hili ninafikiri ni muhimu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, ili kutatua tatizo la vijana, ninashauri waangalie uwezekano wa kuitisha kongamano la Kitaifa la kushirikisha wadau mbalimbali wa kujadili upungufu na ukosefu wa ajira, ili kusudi tuweze kutatua hili tatizo la Watanzania wote. Sekta binafsi zishirikishwe ipasavyo kuhakikisha hili tatizo tunalitokomeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi. (Makofi)