Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Rebeca Sanga Nsemwa

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. REBECA S. NSEMWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia bajeti hii ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Awali ya yote nimshukuru sana Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema ambaye ameweza kunipa afya njema ya kuwa mahali hapa siku ya leo. Nimshukuru sana pia Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi nzuri anayoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda nianze katika sekta ya afya kama ambavyo imeandikwa katika ukurasa wa nane na wa tisa, kama ilivyowasilishwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu. Tunaipongeza sana Serikali kwa kuanzisha huduma ya Bima ya Afya kwa watu wote na kwa awamu ya kwanza wameweza kutoa bima kwa watu milioni moja laki nne hamsini na saba elfu mia sita na mbili, tunaishukuru sana Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana Serikali kwa kuona umuhimu wa kuanza kugharamia magonjwa sugu kwa watu ambao hawana uwezo au wasiojiweza, magonjwa haya yameelezwa kama vile saratani, figo, moyo, kisukari na mifupa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe Serikali, nikijaribu kuangalia watu ambao tunasema hawana uwezo ni wale watu ambao watakuwa-addressed na Maafisa wetu wa Ustawi wa Jamii, watakuwa ranked kwamba hawana uwezo. Hata hivyo, nikijaribu kuangalia kwa magonjwa haya sugu ninaomba twende kwa ugonjwa wa figo, kulingana na mfumo wa maisha uliopo sasa hivi watu wengi sana wanapata matatizo ya figo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa najaribu kuangalia kufanya dialysis katika hospitali zetu za Serikali ina cost shilingi ngapi? Tukaja kuona kufanya dialysis mara moja ina range kuanzia 150,000 mpaka 180,000. Mara nyingi wagonjwa hawa wa figo hufanya dialysis at least mara tatu kwa wiki inategemea na accumulation ya sumu kwenye mwili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ukiangalia mtu ambaye anaweza akafanya dialysis mara tatu kwa wiki kwa range ya shilingi 150,000 ina maana kwa wiki anatumia shilingi 450,000, kwa mwezi atatumia 1,800,000. Gharama hii ni kubwa sana kwa Watanzania. Hivyo basi, niombe tunashukuru Serikali inasema itagharamia kwa watu wasio na uwezo, lakini hata kwa watu wa kati hata kwa watu wenye uwezo ambao hawako katika mfumo rasmi wa ajira jambo hili hawawezi kulimudu hata kidogo fedha hii nyingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sina shaka kwamba magonjwa kama haya yakiingia katika familia tayari yanaenda kuleta umaskini. Kwani mtu huyu ambaye anafanya dialysis tunamtegemea mara nyingi kuwa weak, hawezi kuwa active kama mwanzo na just imagine mtu huyu akifanya mara tatu kwa wiki ina maana hawezi kufanya kazi zake za uzalishaji kama ilivyokuwa mwazo. Hivyo, niombe Serikali itusaidie huduma zote za magonjwa sugu zigharamiwe na Serikali kwa watu wote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe kusema katika Mkoa wangu wa Njombe ninaotoka hakuna Kituo cha Kusafishia Damu (Dialysis) hivyo wananchi wanapata wakati mgumu aidha waende Mbeya au kwa sasa kuna Kituo kimeanzishwa Iringa, waende Iringa. Just imagine mgonjwa aliyefanyiwa dialysis atoke kijijini huko Makete ndani Kipagalo asafiri mpaka afike Iringa anafika amekwishachoka kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tafadhali tunaomba Kituo cha Kusafishia Damu katika Hospitali ya Mkoa wa Njombe kiwekwe, ugonjwa huu umeongezeka kwa kiasi kikubwa na kwa sehemu kubwa unatokana na life style ya wananchi wetu, hali ambayo imekuwa ikijitokeza katika eneo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nichangie suala la mikopo ya 10% kwa akina mama. Tunashukuru sana Serikali yetu kwa kuweka sera ya kuhakikisha kila halmashauri inatenga 10% ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya kuweza kuwakopesha wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba tujaribu kuwasaidia hawa akina mama. Mfumo wa kupata zile fedha ni mgumu mno kwao. Mfumo ule unaweza ukawa unawa-favor watu ambao wana exposure, watu ambao ni well educated, lakini kwa wale akina mama wa interior (ndani vijijini) ukimwambie aandike andiko, anaandikaje jamani? Hali hii inakuwa ni ngumu inawapa wakati mgumu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niishauri Serikali, tunaomba iwaelekeze Watendaji wetu wa Vijiji, wa Mitaa, waweze kuwasaidia hawa akina mama katika ku-structure yale maombi yao na wasiwa-charge kitu chochote, kwani wanakutana na changamoto. Akina mama wanapotaka kuandikiwa maandiko anatakiwa atafute mtaalam na amlipe. Sasa, atamlipa kwa hela gani? Mtu mwenyewe anaenda kuomba mkopo wenyewe wa shilingi 400,000. Andiko mtu anakwambia unisaidie nikulipe shilingi 200,000. Kwa hiyo, tutakuta azma nzuri ya Serikali inaweza isitekelezwe kwa sababu tu hatujaweka mfumo mzuri. Ninaishauri Serikali tuliangalie suala hili kwa namna nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaiomba Serikali iwasaidie akina mama ile mikopo yao kupata watu wa kuwaelekeza, itolewe kulingana na mazingira wanayotoka. Kwa mfano, wananchi wa Mkoa wa Njombe wao ni wakulima. Kwa hiyo, akina mama wengi sana wa vijijini wao ni wakulima. Basi, tupate Maafisa Kilimo ambao watawaelekeza wale akina mama na kuwasaidia kuweza kulima kilimo bora na chenye tija. Kwa hiyo, wakipata ule mkopo wanaweza kwenda kulima kilimo chenye tija and then waweze kupata mazao mengi zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mwisho ninaomba nichangie suala la uanagenzi. Tunashukuru sana Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kuweza kugharamia kozi za uanagenzi kwa wanafunzi 5,746 kwa mwaka huu wa fedha. Tunaomba, idadi hii ni ndogo sana. Vijana wengi wako mtaani na vijana ambao hawana ajira ni rahisi sana kutumika kufanya uovu wowote. Kwa hiyo, ninaomba, ili kujiepusha na hili Ofisi ya Waziri Mkuu iongeze idadi ya kozi ya uanagenzi kwa vijana. Iongeze ili wale vijana wawe wengi, lakini pia tukishawapa ile kozi tusiwaache mtaani. Tuwashike mkono tuwasaidie ili waweze kupata mikopo ya halmashauri na hatimaye waweze kujiajiri. Kwa kufanya hivyo kozi hii itakuwa ina tija. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna vijana wazuri pale wanasoma useremala, tuombe Serikali baada ya kutoka pale iwasaidie waweze kupata tender za ku-supply furniture katika ofisi za Serikali. Tusiwaache tu mtaani, kwamba tutajisifu tumetoa kozi ya uanagenzi lakini je, ina impact? Kwa hiyo, ninaomba tufuatilie impact ili wale vijana wakitoka pale tukawasaidie kuwashika mikono, tuwatafutie tender, tuwatafutie kazi ili wawe na kitu cha kufanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)