Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Segerea
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. BONNAH L. KAMOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nipende kuchukua nafasi hii kukushukuru kwa kuweza kunipa nafasi ili niweze kuchangia mchango wangu kwenye Hotuba ya Waziri Mkuu. Kwanza ninapenda kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa ambayo anaifanya katika Nchi yetu ya Tanzania kuhakikisha kwamba tunapata maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru pia Mheshimiwa Waziri Mkuu, nimshukuru Makamu wa Rais na viongozi wote wa Serikali ambao wanafanya kazi kwa juhudi kubwa kuhakikisha kwamba sisi Watanzania tunaendelea kuwa salama, lakini pia tunapata maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru mambo yaliyofanyika katika Mkoa wetu wa Dar es Salaam, Wilaya ya Ilala tumefanya mambo makubwa kipindi kilichopita tumejenga shule nyingi kwenye sekta ya elimu ambayo shule za mfano. Ukiangalia katika Wilaya ya Ilala tuna shule nyingi ambazo ni shule za kisasa na shule zenye lifti na shule ambazo zinawafanya watoto wetu ili waweze kukaa katika mazingira salama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya pongezi hizo nichukue sasa nafasi hii kutoa mchango wangu kwenye Hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Kama tunavyojua kwamba nchi yetu ina ugeni 2027 kwa ajili ya Mashindano ya AFCON, lakini watu wote tunajua kwamba Mkoa wetu wa Dar es Salaam kwa hali ulionao kwa sasa miundombinu ya Mkoa wa Dar es Salaam imeharibika sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi juzi tumeona mvua imenyesha kubwa barabara nyingi ambazo zinaweza kupitisha magari zilikuwa zimefungwa. Pia ukichangia na ujenzi ambao unaendelea wa miundombinu katika Mkoa wa Dar es Salaam hali ni mbaya sana. kwa hiyo, ninaiomba Serikali au ninashauri kwamba Mkoa wetu wa Dar es Salaam haiwezekani ukapangiwa mpango kama mikoa mingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza Mkoa wetu wa Dar es Salaam ukiangalia watu ambao wanaishi katika Mkoa wa Dar es Salaam ni watu wengi. Kwa sasa hivi siyo ajabu ukakaa kwenye foleni masaa mawili mpaka matatu, sasa nikiangalia tunakwenda kupata wageni 2027 na ujenzi wa barabara zetu au miundombinu ya barabara zetu za Mkoa wa Dar es Salaam, barabara moja meta 300 au meta 500 inajengwa kwa mwaka mmoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninaomba Serikali ije na mpango wa kuhakikisha kwamba tunapokwenda kwenye hii fursa ambayo tumeipata ambayo ni ya kiuchumi, ya kijamii pamoja na kidiplomasia kwamba sisi Mkoa wa Dar es Salaam tunakwenda kuonekana kwamba tuko vizuri, lakini pia tunakwenda kuitangaza nchi yetu kwa kuonekana kwamba ina miundombinu mizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Mkoa wa Dar es Salaam mindombinu yake ni mibovu sana. Pia ucheleweshwaji wa wakandarasi wetu, mkandarasi anaanza kutengeneza barabara. Tuna barabara ambazo zimeanza kutengezwa 2019/2020 mpaka leo hazijamalizika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiongelea Barabara ya Kinyerezi – Bonyokwa – Kibamba ambayo inakwenda mpaka Jimbo la Ubungo. Hii barabara ni barabara ya kilometa 6.3, tangu imeanza kujengwa 2020 mpaka leo haijawahi kumalizika. Hii barabara ni barabara ambayo wananchi wako karibu na barabara. Kwa hiyo, wananchi wameweza kutoa sehemu zao za nyumba zao ili barabara iweze kupita. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, kutokana na mvua zinazonyesha sasa hivi hizi nyumba ambazo ziko pembezoni mwa barabara zingine zimevunjika kuta zingine zimeharibika, lakini pia imeleta usumbufu mkubwa kwa wananchi, hawawezi sasa kuingia katika nyumba zao kwa sababu barabara haijakamilika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ninaomba kama kunakuwa bado hakuna pesa za kutengeneza hiyo barabara imalizike ni afadhali pesa zikusanywe kwanza halafu baadaye ndiyo barabara itengenezwe. Kwa sababu barabara inachukua muda mrefu miaka mitano na inaleta usumbufu kwa wananchi. Kwa hiyo ninaomba sana sana hilo jambo walizingatie. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, TAMISEMI ilianzisha mkakati wa kujenga barabara meta 300, meta 200 ili baadaye waweze kuunganisha. Barabara hiyo imejengwa Tabata Bima ambayo inakwenda mpaka stendi ya Kimanga, lakini sasa hivi naona wameacha huo mkakati. Hizi barabara ambazo zinapita kwenye hizi kata zetu ni barabara muhimu sana na zinapitisha watu wengi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninaomba, Mheshimiwa Waziri Mkuu ni lazima hizi barabara zetu ambazo zinapita kwenye kata zetu zina watu wengi, lakini pia ndiyo kata ambazo zinajishughulisha na mambo mengi. Mfano Dar es Salaam, mvua ikinyesha hakuna mfanyabiashara yeyote ambaye anafanya biashara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kutakuwa kuna foleni kubwa ya magari, lakini pia hata watu wa boda boda hawawezi kufanya kazi, hata mama ntilie wetu hawawezi kufanya kazi. kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri Mkuu tunakuomba katika suala la mipango ya bajeti tunaomba Mkoa wetu wa Dar es Salaam msiweze kuupangia mipango kama vile wanavyopangia mikoa mingine. Kwa sababu Mkoa wetu wa Dar es Salaam una watu wengi, lakini pia ndiyo mkoa ambao unachangia pato kubwa katika Nchi yetu ya Tanzania. Kwa hiyo, tunaomba Serikali ije na mpango maalum kwa Mkoa wa Dar es Salaam. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo la Kibamba nimeona Serikali inataka kujenga Kiwanda cha Madawa Mloganzila, lakini ukiangalia barabara ambayo inakwenda Mloganzila ambayo inapitia Kiswopa ni barabara ambayo siyo nzuri. Kwa hiyo, ili watu waweze kuona kule kwamba ni sehemu ambayo wanaweza wakaanzisha biashara zao na kwa sababu wanapeleka miradi ya Serikali ni lazima hii barabara iweze kutengenezwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu ni jambo la fidia, fidia ya watu. Maeneo ambayo wanayachukua Serikali kabla hawajaanza kufanya Miradi ya Kiserikali ninaomba wananchi walipwe, hili jambo Mheshimiwa Waziri Mkuu analijua. Alikuja Jimbo la Segerea – Kipawa mpaka sasa hivi Kipunguni hawajamaliziwa fedha zao na hao wananchi sasa hivi wako katika mazingira magumu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukizingatia sasa hivi kuna tatizo la mvua wameweka matenti, tunaomba sana sana, wamebaki wachache, tunapongeza hata hao waliolipwa, lakini hawa watu wengine waliobaki tunaomba walipwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ninataka kuongelea Mheshimiwa Waziri Mkuu ni jambo la Kariakoo. Tunajua kabisa kwamba Kariakoo kuna wafanyabiashara wengi na Kariakoo ndiyo sehemu ambayo inatuingizia mapato mengi. Hata hivyo, mvua ikinyesha pale, kuna mifereji ambayo ilijengwa muda mrefu kwa sasa hiyo mifereji imezidiwa ina maana ikinyesha mvua tu kwa saa mbili au saa moja Kariakoo haipitiki, maji ni mengi, watu hawawezi kwenda kununua vitu. Kwa hiyo, hiyo italeta picha mbaya ukizingatia sisi tunakwenda kupokea ugeni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu alikwenda katika Jimbo la Kawe, Kata ya Mabwepande pale kuna barabara ambayo inatoka Mabwepande inakwenda Bandari, tunaomba sana sana hiyo barabara ijengwe,ni muhimu sana kwa wakazi wa Kawe…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MWENYEKITI: Mheshimiwa kengele yake ya mwisho imelia hivyo, ninashukuru sana.
Tunaendelea na Mheshimiwa Rebeca Sanga, Mheshimiwa Japhet Ngailonga Hasunga ajiandae.
MHE. BONNAH L. KAMOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono hoja. (Makofi)