Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Masanja Kungu Kadogosa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bariadi Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. MASANJA K. KADOGOSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami ninakushukuru kwa kunipa fursa ya kuzungumza kwenye Bunge letu Tukufu. Nianze kwa kumshukuru na kumpongeza sana Waziri Mkuu kwa hotuba nzuri ya kibajeti vilevile ya mwelekeo wa kisera kwa Serikali, niungane naye pia katika kumpongeza Rais kwa kazi nzuri ya kutuletea maendeleo vilevile kuonesha dira ya mwelekeo katika Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ninamshukuru Rais kwa kutupatia watendaji wazuri sana katika Mkoa wetu wa Simiyu, Mkuu wa Mkoa ni mweledi wa hali ya juu sana, Mheshimiwa Annamringi Macha, RAS wetu na katika level ya Wilaya, Mkuu wetu wa Wilaya, Mheshimiwa Simon Simalenga na DED Ndugu Khalid Mbwana wanafanya kazi nzuri sana ya kumwakilisha Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo ningetaka nijielekeze zaidi kwenye kutoa shukrani kwa wananchi wa Wilaya ya Bariadi Vijijini. Wamenituma hapa nitoe shukrani zao za dhati kabisa kutokana na maendeleo tuliyonayo. Kwa upande wa miundombinu ya elimu tunafanya vizuri sana kwenye shule za sekondari na za msingi. Vile vile kwa upande wa miundombinu ya afya, tuna vituo vya afya vinne kwa sasa hivi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajua kwamba sera ya Serikali ni kuwa na kituo cha afya kwa kila kata. Tunaamini tumeanza na mwanzo mzuri, tuna vituo vinne sasa hivi ambavyo vimekuwa registered na kuna vingine viwili vinajengwa. Tuna zahanati 40, ukiangalia katika kata zetu 21 unaweza ukaona kwamba karibu kila kata ina zahanati mbili. Huu ni mwanzo mzuri. Tunaamini kwamba maendeleo ni hatua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumefaidika sana vilevile katika hii ahadi ya Mheshimiwa Rais ya siku 100, sisi tulipata wafanyakazi 113, si haba. Kwa upande wa afya wafanyakazi takriban 67, kwa walimu wafanyakazi 27; na tunaishukuru sana TAMISEMI kwa hilo. Vile vile, hata kwa upande wa umeme tumepata vitongoji 85 na kabla ya hapo tulipata vitongoji kama 15, kwa hiyo tuna vitongoji kama 100. Kwa mwanzo huu kwa kweli Ubunge wangu huu mpya unaanza vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hili suala la shilingi bilioni 200 pia ambalo limezungumzwa; sisi tunajiandaa kama jimbo ili kuhakikisha kwamba tunafaidika, kwa maana ya kuwasaidia vijana kwenye maandiko. Hiyo kama Mbunge nilikwishajitolea kwamba kwenye maandiko nitahusika moja kwa moja kwa vijana kuhakikisha kwamba tunakuwa na andiko ambalo linaweza kuwa na mashiko ya kupata zile fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa bima mpaka sasa hivi ndani ya jimbo letu tumefaidika sana; kwa maana mpaka sasa hivi tuna kaya 7,011 tayari zimeshapata namba na kupata zile kadi na hili zoezi linaendelea. Kwa hiyo, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa zoezi hili na ninaamini kwamba linatoa nafuu kubwa sana kwa wananchi. Vilevile, sisi tumekuwa wafaidika wakubwa sana, kwa maana ya ruzuku ya pembejeo, mbolea kwa wakulima wetu na ujenzi wa majosho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hayo ni mambo ambayo ni lazima tuyashukuru na kuonyesha kwamba Serikali inafanya kazi kubwa sana. Zipo changamoto ambazo TAMISEMI ni vizuri wakazielewa. Wakipita kule wawe wanajiongeza kidogo kwenda kwenye shule; kuna changamoto kubwa sana ya madawati. Sasa, hili katika level, kwa maana ya mkoa, katika level ya jimbo tunafanya juhudi zetu, lakini tunahitaji mkono wa Serikali katika hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vizuri kwamba tunapokuwa tunaongeza madarasa nafikiri kuwe na package, tusijenge tu darasa bila kufikiria madawati, matundu ya vyoo au vyoo. Ninafikiri tukiwa tunaongeza madarasa, lakini hatufikirii upande mwingine, tunaongeza crisis. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo lingine ambalo ni very common na ninajua inawezekana kwa Waheshimiwa Wabunge na wenyewe watakuwa nalo hili. Tunajenga shule hizi ambazo ziko karibu katika mkoa na pengine zimekuja, tumekuwa wafaidika wakubwa sana; shule za wasichana. Ninafikiri takribani shilingi bilioni nne plus, lakini unakuta ule ujenzi inajengwa shule ya wasichana lakini haina fence. Hili ninafikiri halijakaa vizuri sana. Ninajua si kwetu tu, kwa research niliyoifanya takriban shule zote ambazo zimejengwa zinakuwa hazina fence.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haileti mantiki kuwa na mradi wa bilioni nne halafu ukashindwa kujenga fence ya shilingi milioni 100; kitu ambacho kingeweza tu kuwa negotiated humo ndani katika ujenzi wakandarasi ambao ni wazawa, wakalifanya hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema, kwamba speech hii na Mheshimiwa Mbunge mwenzangu aliyetangulia, inatoa mwelekeo wa kisera; kwa maana ya bajeti ya kwanza katika utekelezaji wa Dira yetu ya 2050 na ndiyo mwanzo wa kuanza kuendea uchumi wa shilingi trilioni moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa, hili ni jambo kubwa sana katika Taifa letu, ambalo tumejiwekea shabaha. Ni lazima, hata tunavyofikiria katika utendaji wetu au katika approach yetu ya kufikiria namna tunavyoweza kufanya kazi ibadilike. Kwa mfano, kwa upande wa barabara, ninajua sasa hivi kwa ngazi ya mikoa tunaunganisha, tumebakiza sehemu ndogo sana; lakini wakati tunasema tuunganishe wilaya na mkoa ni vizuri vilevile kama Taifa tukajielekeza kufungua zile barabara ambazo zinaunganisha kanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sisi watu wa Simiyu, tuna Barabara ambayo imetajwa na Mheshimiwa hapo ambayo inatokea Magu, kwa maana ya Salama – Nguliati – Itilima – Mwandoya – Kisesa – Meatu na kwa ndugu zetu Singida kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu, Iramba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii barabara siyo tu ni kwa Simiyu, unazungumzia Mara, Mwanza, Simiyu, Shinyanga, Singida na inaenda kuunganisha vile vile na kaskazini. Kwa hiyo, ni barabara muhimu sana. Ninajua kwa upande wa kusini na wenyewe wana barabara zao. Ni muhimu sana tukajielekeza kufungua kanda kwa ajili za kiuchumi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ninataka nilizungumzie hapa, ambalo limezungumzwa na waheshimiwa wengi, ni hili suala la mafuta. Kwanza, tumshukuru sana Mheshimiwa Spika kwa sababu alilitolea maelekezo siku ya kwanza na ninajua mpaka sasa hivi Serikali inafanya kazi nzuri sana kuona kwamba tunaendaje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo ambalo ninataka kuwakumbusha Watanzania ni jambo moja, suala la mafuta halikuanza leo. Mwaka 1951 – 1954 tulikuwa na crisis ya mafuta; kwa wale ambao wanasoma historia. Nilikuwa sielewielewi wakati huo, lakini historia inaonyesha kulikuwa na Abadan Crisis, kulikuwa na tatizo kubwa sana. Mwaka 1973 tulikuwa na crisis ya mafuta kwa ajili ya issue za OPEC, kulikuwa na mgogoro mkubwa sana na Marekani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 1979 tulikuwa na crisis nyingine tena ya mafuta kutokana na lranian Revolution. Mwaka 1990 kwa wale ambao wanafuatilia historia tulikuwa na mambo ya Iraq kuivamia Kuwait, tulikuwa na crisis nyingine. Miaka kati ya 2003 – 2008 tulikuwa na crisis. Mwaka 2021 – 2023 kulikuwa na COVID, baadaye vita ya Ukraine ikaongeza tatizo hilo na sasa hivi tuna tatizo hili la Israel na Marekani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa, ninachotaka kusema ni nini hapa? Crisis ni namna utakavyoichukua lakini inatupa mwanya wa kufikiria tofauti. Kama Taifa ni muhimu sana tukaanza kufikiria kuwa na reserve ya mafuta. Mheshimiwa Rais katika hili ameonesha mwanga mzuri sana. Tumejenga farm tank pale Dar es Salaam lakini kuna nyingine ziko Mtwara; zile ni kwa ajili ya storage lakini kama Taifa ni lazima tuanze kufikiria kwa mawazo tuwe na reserve ya mafuta. Tunaweza tukaanza na miezi mitatu, lakini baadaye tukaenda miezi sita. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwa nini ni muhimu sana? Tunapoiendea hii dira yetu 2050 growth yetu ambayo tume-project ni lazima iwe kwenye 10 plus, maana yake ni kwamba, hatuwezi ku-afford shocks za mara kwa mara kwenye uchumi wetu au 100 percent. At least lazima kuji-cover may be 40% au 50%. Kwa hiyo, ni lazima tuwe na reserve.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili Mheshimiwa Waziri Mkuu atusaidie ku-coordinate; kwa sababu tusianze na kufikiria fedha, tuanze na mawazo. Kwa namna yoyote nature ya mafuta obvious hata financing yake itakuwa ni evolving, haitakuwa kwamba unaweka fedha pale, zitakuwa zinarudi. Kwa hiyo, kwa maana ya kujumuisha private sector, hili litawezekana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna lingine ambalo Mheshimiwa Waziri Mkuu alilitolea maelekezo; kwamba Wizara ya Ujenzi na Wizara ya Nishati wakae chini kutafuta specifications kwa ajili ya equipment zetu au vyombo vyetu vya Serikali, vianze kuona namna ya kutumia either gas au umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya ni maelekezo mazuri sana, lakini ningependa twende zaidi, lazima kama Taifa tujiwekee mpango kwamba, tunaanza pengine usafiri wetu wa public, mabasi haya. Pengine ndani ya miaka 10 – 15 tuone 50% 70% tuanze kutumia either gesi au umeme katika mabasi hayo. Hiyo itapelekea kuwa na tatizo kubwa ndani ya nchi inapotokea crisis. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, tuangalie kuanza na Serikali, magari yetu, kwa sababu kama tukipanga hivyo kwa miaka 10 – 15 tuna uwezo mkubwa wa kujenga miundombinu kwenye barabara zetu hizi ili tuanze kutumia umeme na gesi. Maana yake ni nini? Maana yake ni kwamba, tunapokuwa na tatizo hili; na kwa statistics ambazo nimezitoa, ni obvious kwamba it’s another thing coming. Yaani tatizo hili tutakuwa nalo tena.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kama Taifa ni lazima tuangalie namna ya kupunguza ukali. Pengine katika finding yake tunaweza tukaangalia; tuna reserve sasa hivi ya madini; tunaweza tukaunganisha na hii namna ya ku-create reserve ya mafuta kwa kutumia reserve yetu ya madini bila hata kuuza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine la mwisho, hili ni vizuri nikalizungumza, ni kuhusu madini. Tuna GST na tuna Mamlaka ya Madini. GST kazi yao kubwa ni kufanya research au kuangalia indicatives, kwamba sehemu gani kuna madini, halafu tufanye exploration ya ndani zaidi ili kujua yale madini yako kiasi gani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa, kuna shida moja, GST ukiangalia iko less funded, hawawezi kufanya kazi hiyo, lakini kuna Mamlaka ya Madini ambao wanakusanya zaidi ya trilioni moja kwa mwaka. Sasa, ni suala la kuangalia, kuna mambo mawili ambayo wanaweza wakafanya. Kwanza, wanaweza wakasema kwamba fedha inayokusanywa kiasi Mamlaka ya Madini i-fund GST iweze kufanya exploration zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, kama GST inaonekana ni ndogo sana iwe part, either iwe ni subsidiary company ya mamlaka ya authority au iwe department ndani ya authority ili iweze kuwa funded. Kwa sababu mategemeo yetu ya kupata madini zaidi na sasa hivi tunazungumzia 16% tu ndiyo tumefanya utafiti; kwa hiyo bado tuna potential kubwa sana. Sasa, tusipoi-fund GST maana yake hatuwezi kufika huko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ambalo ninataka kuzungumzia, Mheshimiwa Mavunde nimemfahamu kwa muda kidogo. Bahati nzuri sana Mheshimiwa Mavunde amekuwa advocate mkubwa wa wachimbaji wadogo wadogo. Miaka 15 iliyopita nilikuwa Mkurugenzi Benki, walikuja kufuatilia anawatafutia wachimba madini wadogo wadogo fedha. Kwa hiyo, ni mtu ambaye ni sahihi katika sekta hii kwa sababu amei-view miaka mingi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo ambalo ningeweza kuomba watu wa madini watusaidie na especially sisi watu wa vijijini; wanapokuta watu wa vijijini, wananchi wamegundua either kwa kupiga ramli au kwa namna nyingine yoyote ile, wako 1,000 au 2,000 wasiwaondoe; wawafanyie utaratibu ili wawe wachimbaji pale. Serikali kwa sababu wana muscles, wakatafute exploration sehemu zingine, kwa sababu hii inatuletea kelele kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuzungumza hayo ninaomba kuunga mkono hoja. Ahsante sana kwa kunivumilia. (Makofi)