Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Jang'ombe
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. ALI HASSAN OMAR KING: Mheshimiwa Mwenyekiti, Ahsante. Awali ya yote kwanza ninapenda kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kutujalia kuwa hai na pia kuwa na afya kutufikisha siku ya leo, kuja kutathmini, lakini pia kupanga matumizi na mipango ambayo tumeipanga kwa ajili ya nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda pia kumpongeza Waziri Mkuu, ninampongeza kwa maana yangu kwa sababu ninampa hongera lakini ninampa na pole. Hongera kwa sababu ni wa kwanza kusoma hotuba ya bajeti kwa ajili ya kutekeleza Dira ya 2050, kwa ajili ya kutekeleza Mpango wa Muda Mrefu wa Miaka 25, kwa ajili ya kutekeleza Mpango wa Kati wa Miaka Mitano. Hongera na pole, yeye ndiye wa kwanza kutekeleza Mpango wa Muda wa Kati na Mpango wa Muda Mfupi wa Mwaka huu 2026-2027. Ninampongeza pia kwa sababu yeye ndiye wa kwanza kutekeleza bajeti ya mwanzo ambayo ndiyo tunaanza kutekeleza Dira ya 2050.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo, kwanza ninanukuu maneno yake ambayo ameyasema katika paragraph ya 120 page ya 48. Waziri Mkuu amesema kwamba, "Ninaelekeza Wizara ya Fedha iimarishe vyanzo vya upatikanaji wa fedha kwa Mfuko wa Barabara, aidha ihakikishe fedha hizo zinapelekwa moja kwa moja kwenye Mfuko kama ilivyotengwa kwenye bajeti."
Mheshimiwa Mwenyekiti, kila Mbunge anayesimama hapa na Wabunge watatu waliotangulia kusimama kabla yangu, walikuwa wanaelezea barabara, barabara, barabara, barabara! Wabunge wengi waliozungumza wanazungumzia maji, Wabunge wengine walikuwa wanazungumzia umeme vijijini. Umeme vijijini kupitia ring-fenced fund, fedha zilizozingirwa imefanya vizuri kwenye umeme, lakini kwenye barabara tunajiuliza kuna kitu gani? Ndiyo maana na mimi nikasema nije na jambo hili nilizungumzie kwa kuwa Wabunge wengi wamezungumzia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, malengo ya kuweka ring-fenced fund ni kwa ajili ya kupata fedha za uhakika kwa ajili ya kutekeleza ahadi za Serikali, ahadi za Chama Cha Mapinduzi na ahadi za Rais. Ring-fenced fund hizi leo tumemwona Waziri Mkuu anasimama anatoa administrative measure kwamba, anataka kuli-solve hili tatizo kiutawala wakati sisi kama Wabunge kupitia Katiba ya Jamhuri ya Muungano Kifungu Na. 63(3)(d) kwamba tunaweza kutunga sheria pale ambapo utekelezaji wa jambo linahitaji kutunga sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasi tulitunga sheria, katika Sheria ya Bajeti, Kifungu Namba 41(2)(1) kwamba, tukiidhinisha matumizi ya ring-fenced fund tunasema kwamba ziheshimiwe. Leo Waziri Mkuu anazungumza ametoa mwongozo kwa Serikali, Bunge nalo linatoa mwongozo kwa Serikali, kwa nini sheria tulizozitunga zipo na Wabunge tuko kwa mujibu wa sheria, kwa nini hizi sheria zisifuatwe?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka kusema kitu kimoja ambacho ni muhimu sana, ninataka tukazie sasa kwa kuwa Waziri Mkuu amesema fedha hizi moja kwa moja ziende kwenye Mifuko iliyozingirwa, basi tutumie nafasi yetu kama Bunge kisheria tuliweke hili kisheria tuache kutoa miongozo wakati sisi tunaweza kutunga sheria na tunaona athari yake isipotekelezwa mambo hayakai vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninanukuu Ibara ya 135 ya Katiba ambayo iko Sura ya Saba, Sehemu ya Pili, Kifungu cha Pili, kwamba, "Fedha ambazo hazitawekwa kwenye Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali ni zile ambazo zimetajwa na sheria, kwamba zitumike kwa shughuli maalum au ziwekwe katika Mifuko mingine kwa ajili ya matumizi maalum."
Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha tulizoziweka mwanzo zilikutwa na changamoto na changamoto iliyokuwepo, zilikuwa fedha zinazokusanywa zinakuwa ni nyingi kuliko zinazowasilishwa katika Mifuko. Pili, uwasilishaji ulikuwa unachelewa na fedha haziendi kwa uhakika kwa sababu hii sheria tuliyoweka haikufuatwa vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine, matumizi ya fedha hizi yalikuwa yanahitaji lazima yapate idhini ya Mlipaji Mkuu wa Serikali, Paymaster General (Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha) na Wizara ya Fedha inapokuwa ina ukwasi wa fedha, hizi fedha haziendi! Ndiyo haya malalamiko tunayoyakuta yako hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mimi niseme kitu kimoja. Unapoweka bond, ukiona kwamba bond ile inalegeza unaweka na washes. Wakati mwingine kama hata hizi washes kwamba kila wakati unabadilisha washes zinakuwa nyingi kinachohitajika ubadilishe bond uweke nyingine ili ile bond iwe ina-fit na kile kilichopo pale. Sasa ninapendekeza kwamba tuweke bond ambayo ina-fit kutokana na hiki kipengele ambacho tunacho hivi sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna msanii mmoja anaitwa Juma Bhalo amesema: "Ukilegeza kukaza kifundo kinafunguka." Maana kama hujakaza vizuri kifundo kinafunguka. Sasa ninataka tukaze ili kifundo kisifunguke. Ninapendekeza tuweke sheria ambayo itampa mamlaka Kamishna wa TRA kupeleka fedha moja kwa moja katika Mifuko iliyozingirwa (ring-fenced fund) ili zisipite sehemu nyingine, zikipita sehemu nyingine leo haya malalamiko tumeyasikia hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, toka juzi tumeanza kujadili bajeti hii nilikuwa ninawasikiliza Wabunge wengi wanaongea jambo hili, ili tuondokane nalo tuondoe hivi vitu kwa sababu kuna jambo moja, tumewekea Mfuko wa Maendeleo ya Barabara, Mfuko wa Barabara ambao kwa Sheria Sura Na. 220 ili kukidhi matengenezo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo kila Mbunge anazungumza hapa barabara zetu mbovu, tukiwa na barabara mbovu maana yake uchumi wetu hautakwenda vizuri kwa sababu tuna bandari tunategemea usafirishaji, lakini tukaweka TARURA kwa sheria hiyo ili tuweze kukidhi kupata barabara hizo, leo Wabunge hapa wanazungumza kuhusu barabara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninanukuu mtu mmoja anasema: "Siasa ya sasa hivi inaweza ikaja ikahamia kwenye barabara." Kwa hiyo, kwa nini hizi ring-fenced fund tusiziwekee sheria ambazo zitatumika kama vile ambavyo Wabunge ambao ndiyo tumekuwa mamlaka ya kutunga sheria tunatakiwa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashauri Serikali tuje na sheria ambayo itasema hizi ring-fenced fund moja kwa moja ziende katika Mifuko. Katiba haijakataa, Kifungu 135(2). Sheria tuliyonayo ya Bajeti, Sura 439 Kifungu cha 41(2), ninaona kama kinahitaji washes, kila wakati tunatoa miongozo, miongozo lakini tuweke sheria tumeshajua matatizo yetu ni yapi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukumbuke Ibara ya Nane ya Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inasema: "Serikali inapata mamlaka na madaraka kutoka kwa wananchi." Wajibu wa Serikali itakuwa kazi yake ni kupeleka ustawi kwa wananchi, kama barabara ni mbovu na kama maji hayapatikani, huo ustawi utakuwa ustawi gani? Kwa hiyo, ili twende vizuri tufanye hicho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatolea mfano hapa mwingine kwa mara ya pili, kwa nini tumefanya vizuri kwenye umeme vijijini? Tulikuwa tuna Mfuko MCC. MCC tulivyozuiliwa tukaja tukatenga fedha zetu hizi ambazo tukaanza kutumia 2015/2016, leo imetusaidia vijiji tumemaliza, tunakwenda kwenye vitongoji. Kwa nini tusiheshimu na huku ili tukapata maendeleo ambayo yanafanana na haya?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nimalize kitu. Watu wengi sana wanataka wapewe miongozo wakati sheria ipo. Fabi ayyi hadithim ba'dahu yu'minun, watu wataamini nini wakati tayari sheria ipo? Wapewe maelezo gani mengine ambayo yako chini au juu ya sheria? Kwa hiyo, fabi ayyi hadithim ba'dahu yu'minun.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana. (Makofi)