Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Timotheo Paul Mnzava

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Korogwe Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kutoa mchango wangu kwenye hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu Rahim ambaye ametujalia uhai, ametupa uzima na ametuwezesha kuendelea kuwepo kwenye jengo hili kwa ajili ya kuendelea kuifanya kazi ya watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee nitumie nafasi hii kwa kuwa ni bajeti ya kwanza tangu Bunge hili la Kumi na Tatu limeanza, niendelee kumpongeza Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa na kazi nzuri anayoifanya kwenye nchi yetu. Pia nimpongeze na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na nimpongeze Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa na kazi nzuri anayoifanya kwenye nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii pia kwa dhati kabisa kuwapongeza Mawaziri na Naibu Mawaziri wote walioteuliwa kuhudumu chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, ambapo hotuba hii ni hotuba yao Ofisi ya Waziri Mkuu. Mawaziri tunawapongeza sana kwa imani kubwa waliyopata kwa Rais na tunawatakia kila la kheri katika kutimiza majukumu yenu ya kuwatumikia Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu unajikita kwenye maeneo mawili tu siku ya leo. Eneo la kwanza nitazungumzia kidogo kuhusu Serikali za mitaa; eneo la pili nitazungumzia usimamizi wa shughuli za Serikali. Nchi yetu miaka ya 90 tuliamua kuanzisha na kutekeleza sera ya ugatuzi wa madaraka. Ili sera hii ifanye kazi vizuri, tukaziboresha na kuziweka vizuri Mamlaka za Serikali kuzishusha kule chini kwa wananchi ili ziwe karibu na wananchi na ziweze kuwahudumia wananchi pia zifanye kazi ya wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na changamoto kadhaa, lakini sera hii imekuwa na mafanikio makubwa kwa sababu imewashirikisha wananchi katika maamuzi ya shughuli mbalimbali zinazohusu maisha yao na shughuli zao kwa ujumla. Pia, tumeendelea kuisimamia sera hii na kuitekeleza. Tunashukuru hata kwenye dira tuliyoizindua hivi karibuni, Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Mwaka 2050, tumeonyesha ni namna gani ambavyo Serikali yetu inakusudia kuendelea kupeleka madaraka kule chini kwa wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiiangalia pia bajeti hii ya Ofisi ya Waziri Mkuu ambayo ndiyo bajeti ya kwanza ya utekelezaji wa dira hii tuliyoizindua, kwa mujibu wa taarifa za ukomo tunatarajia bajeti ya mwaka huu itakuwa kwenye shilingi trilioni 62.9. Katika hizi shilingi trilioni 62.9, shilingi trilioni 12.5 zinakwenda Ofisi ya Waziri Mkuu. Katika shilingi trilioni 12.5, shilingi trilioni 12.2 zinakwenda Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI. Maana yake ni nini? Maana yake ni kwamba fedha nyingi tunazipeleka TAMISEMI ili zikafanye kazi za kugusa maisha ya watu wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu ni mdogo tu kwenye eneo hili, tunapeleka fedha nyingi sana TAMISEMI, tunapeleka fedha nyingi sana halmashauri, lakini lazima tujiulize maswali fedha hizi tunazopeleka tunampelekea nani? Nani mwenye jukumu la usimamizi wa fedha hizi? Wenye jukumu la usimamizi kwa kuwakilisha wananchi kule chini ni viongozi wetu wa vijiji, viongozi wetu wa kwenye kata na Mabaraza yetu ya Madiwani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali ya Mabaraza yetu ya Madiwani ikoje? Hali ya Halmashauri zetu ikoje? Ni ushauri wangu katika kipindi hiki cha miaka hii mitano, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI watengeneze programu nyingine ya maboresho ya Serikali za Mitaa tuziongezee uwezo Halmashauri zetu na Serikali za Mitaa kwa ujumla ziwe na nguvu na uwezo wa kusimamia fedha hizi na ziweze kutoa matokeo kule kwa wananchi wetu ambao tunawaongoza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili ambalo ninataka kulizungumza leo kwenye hotuba hii ya Waziri Mkuu ni eneo mahsusi la usimamizi wa shughuli za Serikali. Kazi ya usimamizi wa shughuli za Serikali ni kazi ya Waziri Mkuu na ni jukumu lake la Kikatiba. Ibara ya 52(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunampongeza Waziri Mkuu, tumemwona anavyofanya kazi, tumeona ziara anazozifanya na tumeona namna ambavyo wananchi wanamkimbilia. Pamoja na nia nzuri aliyonayo na aliyoanza kuionesha mapema, lazima tukubaliane bado Serikalini kuna ugonjwa. Bado kuna ugonjwa wa kuleana, bado kuna ugonjwa wa kufanya kazi kwa mazoweya na bado kuna ugonjwa wa kuvumilia mambo ambayo hayako sawasawa, pia, kuna ugonjwa wa kutokufanya maamuzi au kuchelewa kufanya maamuzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeiona dhamira ya Waziri Mkuu, ni ushauri wangu kwa Waziri Mkuu, aongeze nguvu, aongeze ukali. Tunahitaji tuone wananchi wa nchi hii wanatumikiwa na viongozi wao na wanatumikiwa na Serikali yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo maeneo mawili nitatoa mfano, Serikali ya Awamu ya Sita ilifanya kazi nzuri sana kwenye kufufua kilimo hasa kwenye maeneo ya mazao ya kimkakati. Kilimo cha mazao ya kimkakati. Tumeona Serikali ikifanya kazi kubwa kwenye korosho, tumeona ikifanya kwenye michikichi, imefanya kwenye mkonge na kwenye maeneo mengine. Kwa kweli tunaipongeza Serikali ya Awamu ya Sita, imeweka alama kubwa sana kwenye eneo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka niseme kazi hii kubwa ya Serikali ya Awamu ya Sita ambayo ilifanyika chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu na mtangulizi wa Waziri Mkuu wa sasa, Mheshimiwa Kassim Majaliwa aliifanya vizuri sana, ilirudisha matumaini kwa Watanzania wa nchi hii, hasa wakulima wale wa mazao yale ya kimkakati. Kwa mfano kwenye zao la mkonge, kutokana na kazi kubwa na nzuri inayofanywa na Serikali chini ya ofisi ya Waziri Mkuu, tumeongeza uzalishaji wa mkonge kutoka tani 36,000 mwaka 2020 mpaka tani 73,000 mwaka jana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kazi hii nzuri inayofanywa na Serikali kuna mahali tumeanza kupata ulegevu na kuna mahali pameanza kuwa na shida. Tumeanza kuwaruhusu, kuwavumilia na kuwaonea haya wahuni wanaokwenda kucheza na bei za mazao ya wakulima wetu. Leo tunavyozungumza zao la mkonge liko kwenye changamoto kubwa, bei za mkonge zimeporomoka na mkonge umekaa kwenye maghala kwa zaidi ya miaka mitano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni nani anaruhusu watu kucheza na bei za mazao ya wananchi wa nchi hii? Tunaiomba Ofisi ya Waziri Mkuu, jambo hili tusiachie Wizara ya Kilimo peke yake, Ofisi ya Waziri Mkuu iingie ilishughulikie na ilisimamie ili tuendelee kuboresha maisha ya watu wetu na waweze kupata maisha mazuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa nitoe ushauri kwenye maeneo mawili, ushauri wa aina mbili kwenye eneo hili la mkonge. Jambo la kwanza, tunaiomba Serikali ituletee mfumo mzuri na mfumo mpya utakaosimamia kazi ya uuzaji na ununuaji wa zao la mkonge ili kuondoa uwezekano wa watu kucheza na bei kwenye zao la mkonge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Rais alipokuja katika Mkoa wa Tanga aliahidi kwamba mashine zote za kuchakata mkonge ambazo zilikuwa kwenye Kampuni ya Sisalana ambayo ni kampuni ya Serikali, zitarudishwa kwenye AMCOS zetu ili wakulima chini ya Bodi ya Mkonge wakasimamie. Jambo hili limechukua muda mrefu, kampuni inayosimamia mashine hizo mpaka sasa hivi hazifanyi kazi, zimefungwa na wakulima wamekuwa na changamoto ya uchakataji wa zao lao la mkonge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili ambalo linaonesha ulegevu ni kwenye upande wa zao la chai. Kwa zaidi ya mwaka mmoja wakulima wa Tarafa ya Bungu, Kata Tisa, viwanda viwili vya chai mwekezaji amevifunga ameondoka na wakulima hakuna kazi wanayoifanya. Alipokuja Rais, tumemweleza alitoa maelekezo, alikuja Waziri Mkuu tulimweleza alitoa maelekezo, lakini mpaka leo zaidi ya mwaka mmoja, hakuna kinachoendelea na wananchi hawajui hatima yao ni nini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili linahitaji usimamizi madhubuti wa Serikali, tukawakwamue wakulima ili waendelee kufanya shughuli zao wapate kipato, watengeneze uchumi wao, na uchumi wa nchi na maisha yao yaendelee kwenda vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo ninakushukuru sana na ninaunga mkono hoja. Ahsante. (Makofi)