Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kiteto
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa nafasi na ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa afya njema. Ninawashukuru wananchi wangu wa Kiteto kwa heshima kubwa sana waliyonipa, kurudi Bungeni hapa. Ninawahakikishia nitaendelea kuwa sauti yao hapa Bungeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaipongeza Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Ndiyo iliyotujengea heshima kule majimboni, ndiyo maana Watanzania wale wametuchagua kwa nguvu nyingi sana. Kwa kweli, kwa miradi ya maendeleo iliyofanyika kwa kipindi cha miaka mitano kwa Kiteto tu peke yake ni kazi kubwa sana na kila Mwanakiteto popote alipo akitoka kwenye kata yake, kijiji chake, ataona mradi ambao umejengwa kwa kipindi cha miaka mitano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunampongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa ziara zake anazozifanya na anasikiliza wananchi sana. Tunamwomba aendelee na nguvu hiyo hiyo ya kuwasikiliza Watanzania hawa. Amekuja Kiteto, leo timu ya matumizi bora ya ardhi iko Kiteto kwa ajili ya vijiji karibu 20 kwa sababu ya ziara yake, lakini vilevile kero za wananchi zimeanza kusikilizwa, karibu kero 300 wakati wa ziara hiyo. Ziara hizi za viongozi wetu ni nzuri sana, zinawagusa Watanzania walio wengi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza Mheshimiwa Profesa Shemdoe na timu yote ya TAMISEMI. Ninamfahamu Profesa, ni mtu mwema sana, humble. Aendelee hivyo hivyo na timu yake yote, na Mawaziri walioko Wizara hii, kwa kweli, wanafanya kazi nzuri. Tunawaombea Mwenyezi Mungu awape nguvu ili waendelee kumsaidia Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wana-Kiteto safari hii wamenituma nizungumzie barabara peke yake. Barabara tu. Jimbo la Kiteto ni kubwa kidogo, ni square kilometa karibu 17,000. Ukitoka mwanzo wa Kiteto mpaka mwisho ni karibu kilometa 500, jimbo moja, na wako wakulima na wafugaji wanachapa kazi sana; wanalima vizuri, wanafuga vizuri, lakini miundombinu ya barabara imekuwa tabu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mtandao wa barabara. Barabara za TARURA ni kilometa 1,291 halafu zenye lami ni kilometa nne tu peke yake. Mheshimiwa Waziri Mkuu alipokuja Kiteto alipita kwenye Barabara ya Kongwa – Kiteto – Simanjiro, ambayo ni muhimu sana kwa sababu, kwanza magari karibu 533,995 yanapita kwa mwaka. Ni barabara inayounganisha Mikoa ya Dodoma – Manyara – Arusha na Kilimanjaro. Kwa kuwa, sera yetu ni kuweka kipaumbele kwa barabara hizi ambazo zinaunganisha mikoa na kufungua uchumi, barabara hii haikwepeki, yaani haikwepeki sasa!
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesema tu, nitawakera sana kipindi hiki kuhusu barabara. Wananchi wa Kiteto wamenituma, in fact wameniambia kila nikipata nafasi hapa nianze kuzungumza kuhusu barabara. Hata nikipata nafasi ya kuuliza swali kwenye Wizara ya Maendeleo ya Jamii, nizungumze barabara hapa. Namna ya ku-frame i-fit, hiyo mniachie mimi, lakini kwa kweli, Wanakiteto sasa wanataka barabara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii ilikuwa kwenye mradi ule wa EPC+F, tumesaini mikataba hapa, Wanakiteto walikuja. Tuliambiwa kuna shida imetokea kwenye EPC+F, tunafahamu, lakini kupitia Wizara ya Ujenzi mlisema kwamba, mmehuisha tena mikataba. Kwa hiyo, kwa kweli, kama mnataka kujenga heshima ya wananchi hawa wa Kiteto, Barabara hii ya Kongwa – Kiteto – Simanjiro – Arusha ni muhimu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati wa ziara, Mwenyezi Mungu alitusaidia, mvua ikanyesha sana na Waziri Mkuu akapita barabara yote hiyo mpaka Arusha. Mwenyezi Mungu alisaidia naye aone. Kwa hiyo, kwa kweli, umuhimu wa barabara hii ni mkubwa sana. Kwa hiyo, tungependa sana majawabu na Serikali ijipange kuleta fedha, kwa ajili ya barabara hii. Barabara hii ni muhimu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Barabara ya kutoka Handeni – Kibirashi – Kiteto inakwenda Chemba mpaka Singida, ni barabara nyingine muhimu inayounganisha Mikoa minne ya Tanga – Manyara – Dodoma mpaka Singida. Ni barabara ya wakulima na wafugaji, ni barabara ya kilimo, barabara ya mifugo, Itafungua sana uchumi wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu umuhimu wa bomba la mafuta na Bandari ya Tanga. Barabara hii itakuwa ni muhimu sana na magari karibu mia tano na themanini na ngapi yanapita kwa mwaka. Kwa hiyo, ni barabara muhimu sana. Ni vizuri Serikali ikajipanga kwa kweli, tupate barabara za lami zitakazofungua uchumi wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni ajira kwa vijana. Tumejenga shule nyingi sana, na ni kitu kizuri sana. Tumetoka kwenye shule za kata, sasa tunakwenda vijijini na vijana wasomi wamekuwa wengi sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna siku nilikuwa naangalia kipindi fulani hivi kinaitwa sijui, Watu-Back Jobs; kijana mmoja anazungumza anasema, siku hizi GPA ambayo tulikuwa tunafahamu kwamba, ni "Grade Point Average", siku hizi inaitwa ni "Gambling People Association", ile GPA kwa sababu ya frustration, ambayo vijana wanaipata kwa sababu ya kukosekana kwa ajira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona fedha nyingi hapa, zile shilingi bilioni 200 za Mheshimiwa Rais. Nia ya Mheshimiwa Rais ni kwamba, ifike kwenye majimbo yote, na vijana wengi sana wa Kiteto wameomba hizi fedha. Tunachoomba ni hizi fedha tuone kila kijana ameguswa kutoka kila mahali, siyo kutuletea namba tu kwamba, wameajiriwa vijana kadhaa, hapana. Nchi yetu ni ya ujamaa, ni lazima kazi hizi na fursa zinapojitokeza kila mahali tusikie mkono huu wa Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nawaomba sana Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kweli, mratibu wote walioomba kwenye sekta hizi. Tunachotamani ni kuona kwamba, kuna Vijana wa Kiteto, Vijana wa Simanjiro, Kilindi, Chemba huko, majirani zangu wote. Tukiwagusa itaendelea kuwapa courage vijana kwamba, yes, elimu yetu siyo Gambling People’s Association, ile GPA. It matters bado na kwamba, Taifa hili linajali elimu na fursa zipo; lakini lazima tuongeze uwazi katika utekelezaji wa ajira hizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimemwambia Profesa, ni kilometa 1,291 mnatuletea shilingi bilioni mbili tu, haiwezekani. Mtuongezee bajeti kwenye TARURA, the minimum ni shilingi bilioni sita. Tungetaka yote, ni shilingi bilioni 11, lakini sisi tunafahamu uchumi wa nchi yetu, angalau sasa ile bajeti itoke shilingi bilioni mbili, twende shilingi bilioni sita angalau, lakini shule za sekondari kidato cha tano na cha sita tunazo mbili tu; Shereta, Maombi, Lesoit, Dongo, Sunya, Dosidosi, Ndedo na Kibaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo haimshindi Profesa. Tumeleta maombi kwa ajili ya mabweni, kwa sababu ya mazingira ya shule zetu. Huko kwetu huko mazingira ya shule zetu lazima yawe bora, ili yawe motisha kwa watu wetu kusoma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna kazi kubwa sana ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Miaka 50. Hii dira wataalamu wanasema ni "ambitious" lakini ni "achievable." Ni achievable peke yake tukifanya mambo kama haya, kwa sababu, sisi kuandika document nzuri, tuko vizuri sana na hata baada ya dira kwisha tukiambiwa tuandike, kwa nini hatukufanikiwa? Tutaandika document nyingine nzuri sana. Sasa tabu yetu ni utekelezaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Hotuba ya Mheshimiwa Rais inasema hivi, ili kutimiza Dira ya Maendeleo ya 2050 ni lazima tujenge utamaduni wa utekelezaji na uwajibikaji, kwa hiyo, hapa lazima mchakamchaka uwepo kidogo. Utekelezaji uko kwa Ofisi ya Waziri Mkuu, tukimbizane wazee, tutoke huko sasa kwamba, sisi tunaambiwa tunaandika document nzuri, na tusipopata matokeo, tunaandika nyingine nzuri ya kusema kwa nini hatukupata? Hebu twende kwenye utekelezaji sasa, dira ni nzuri, itahitaji nguvu kubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, tumesema private sector. Private sector ni 70% tunatarajia, lakini wanachotaka private sector ni lazima tu-expand tax base, siyo tax burden. Watu wachache lazima tufungue tax na informal sector, lazima waingie, lakini wakati mwingine tunafikiri wawekezaji ni kuomba tu waje nchini. Wawekezaji waliopo nchini, kila mmoja akija hapa anataka aweke kwanza mtaji kidogo halafu jinsi unavyo-behave ndiyo ataongeza zaidi na zaidi na hao ndio wanaongea na watu wengine wote duniani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuache zile sheria ambazo ni unpredictable, zinabadilikabadilika tu, tuache bureaucracy, tuwe ni watu wa vitendo. Tukifanya hivyo, tuta-attract hiyo 7%0 ya private sector. Baada ya kusema hayo machache, nakushukuru na ninaunga mkono hoja. Ahsanteni sana.