Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tarime Vijijini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru kwa nafasi na ninaomba Mheshimiwa Waziri Mkuu unisikilize, ninataka nitoe software. Ninataka nizungumzie kwa niaba ya wananchi wa Tarime Vijijini pia kwa niaba ya Watanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, nimefurahi sana kutoa maelekezo kwamba halmashauri zote ambazo zilikaidi agizo la kununua dawa, majina yao yaletwe Jumanne ijayo, nimefurahi sana kwa jambo hilo. Jambo la pili ambalo nimefurahia sana, ni Mheshimiwa Spika kutoa maagizo kwamba Kamati ikae na ilete majibu namna ya kusaidia shida ya mafuta nchini na ninaomba niwaambie Watanzania kwamba jambo hili Wabunge tunaunga mkono pamoja na Serikali tutatafuta ufumbuzi kwa pamoja, ni jambo la kwetu ni jambo la Watanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme kwamba Bunge linaitwa Bunge la Tanzania. Kwa hiyo, kila Mbunge aliyeko humu anatakiwa afanye kazi ya Watanzania waliomleta kutokea eneo alikotoka, aidha mkoa au jimbo. Hilo jambo likieleweka vizuri maana yake Bunge hili tutafanya kazi ya wananchi. Kwa kusema hivyo, ninaomba nimpongeze Mheshimiwa Rais alipokuja kufungua Bunge hili alizungumzia mambo ya demokrasia ambayo ndiyo mambo ambayo wananchi wanataka kusikia. Alizungumzia mambo ya Katiba mpya, akazungumzia mambo ya maridhiano ya Kitaifa, akazungumzia pia kuunda Tume ambayo imefanya kazi na mimi nimehojiwa. Hayo ndiyo mambo ambayo Watanzania wanataka kusikia.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze Mheshimiwa Waziri Mkuu amefanya ziara na nimemfuatilia sana ameenda Tanga, Kilimanjaro, Katavi na Rukwa, kote alikopita kuna maagizo ametoa na kuna kero amepewa. Sasa ninataka nimwambie mambo ambayo watu wengi hawasemi na ninataka nimwambie kwa sababu tunafahamiana.
Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza, leo tunapozungumza hapa nchi hii ina vyuo vikuu vya umma na binafsi 57. Kwa hiyo, akifanya ziara anaongea na wasomi wenzake hata kama hawana PhD. Kila kijiji kuna wasomi wa level ya shule ya msingi, kuna sekondari, kuna degree na kuna masters. Ndiyo maana akisema jambo watu wanalifuatilia, wanasema anasema nini wanachanganua. Mheshimiwa Waziri Mkuu amepewa kazi ngumu, ninataka afanye kazi mpaka aote mvi kabla ya miaka mitano kwisha kwa sababu kazi aliyopewa ni ngumu na ni kazi ya kitaifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninataka nimwoneshe Mheshimiwa Waziri Mkuu. Sasa hivi ameleta mipango hapa ya mwaka mmoja, ametaja trilioni 1.7 mwaka 2028, hiyo ni kazi ifanyike madarasa na matundu ya vyoo yapatikane. Waziri wa TAMISEMI alikuwa Katibu Mkuu, tumemwambia kwenye Kamati ya TAMISEMI, leo kwenye hotuba ya Waziri Mkuu Bunge la Tanzania linakaa kujadili kwamba shule imefungwa eti hakuna matundu ya vyoo, watoto wanakalia mawe katikati ya utajiri huo. Hiyo ni kazi ya Waziri Mkuu (Mtendaji Mkuu), anayo kazi ya kufanya, tutamuunga mkono apambane.
Mheshimiwa Naibu Spika, Waziri Mkuu ametaja mambo ya kusisitiza pale, kwa mfano namba tano wakandarasi; aende wampe taarifa wakandarasi hasa wa maji na barabara, wazawa hawajalipwa, wamefilisika, wameuza nyumba na wamepoteza mwelekeo. Aende awalipe fedha zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala namba sita, ameelekeza wakuu wa mikoa wakashughulike na matundu ya vyoo, tunatakiwa bajeti ya mwaka huu, wakurugenzi wa halmashauri hizi waje watuoneshe mpango mkakati ndani ya miaka mingapi shida ya matundu ya vyoo, madawati, viti na meza, maboma ya msingi na afya yatakwisha, hiyo ni kazi ya kufanya.
Mheshimiwa Naibu Spika, namba saba amesema, maji yaende katika shule za msingi na sekondari, maeneo ya makanisa na maeneo ya umma. Wakandarasi wa miradi ya maji wanadai zaidi ya bilioni 600 hawajalipwa, wawalipe walete maji. Watu wa vijijini tunataka maji, watu wetu wanywe, akina mama wote watakate kama wa mjini.
Mheshimiwa Naibu Spika, iko hoja ya utawala bora imezungumzwa; uwazi, uwajibikaji na ameelekeza pia kwamba miradi iwe ya ubora. Sasa nimwambie Mheshimiwa Waziri Mkuu, madiwani waliongezewa posho mara ya mwisho mwaka 2012, nimeuliza mara kadhaa hapa. Kama unataka miradi yenye ubora unataka uwajibikaji, diwani unampelekea miradi yote itakayozungumzwa hapa na Wizara zote, itaenda kwenye vijiji na kata. Hao Wenyeviti wa Vijiji, Wenyeviti wa Mitaa, Waheshimiwa Madiwani wanatulalamikia Wabunge kila siku mpaka tunagombana nao. Sasa jambo hili lazima Waziri Mkuu alifanyie kazi hata kama hajaingiza kwenye bajeti ya mwaka huu. Ni vizuri aoneshe anawezaje kuboresha maslahi ya Madiwani, Wenyeviti wa Vijijj na Wenyeviti wa Mitaa ili anapowatuma kazi wanakimbia.
Mheshimiwa Naibu Spika, mtu anaenda kukagua mradi hata nauli hana. Mbunge ukienda wanakuomba hela ya matumizi, zile Kamati mbalimbali, haya mambo ndiyo uboreshaji wa huduma za kijamii na miradi itakuwa ya ubora.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna hoja ya kulimbikiza mali za umma na hili ninaomba nile pose kidogo. Mheshimiwa Waziri Mkuu alifanya ziara kwenye mikoa ile, ninataka nimwambie mikoa ile ina Wakuu wa Mikoa, ina Ma-RAS, ina wakurugenzi, ina Ma-DED, ina wakuu wa idara na watendaji wa kata, kwa nini aende yeye ndiyo waone shida? Kwa nini aende yeye ndiyo mwanya uonekane? Au kwa nini mwenge uende kwenye wilaya ambayo kuna mtu analipwa mshahara miezi 12, miaka 60, permanent and pensionable bila kum-assess (kufanya tathmini)? Hii kazi ni ya Mheshimiwa Waziri Mkuu aje na mpango.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nimuulize hizi za wakuu wa mikoa hawa, hivi kukiwa na vigezo kuna shida? Tunajua ili apate ukuu wa mkoa, apate U-RAS, apate U-DED, apate U-DC, apate ukurugenzi, hawa wafanye kama ma-CEO wa private. Wenyeviti wa bodi mbalimbali watendaji wakuu washindane.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni fedheha tukizungumza tutarudi kwenye ripoti ile, lakini ninataka nimwambie Waziri Mkuu, katika jambo ambalo Watanzania wanachukia ni kuja tunaomba hapa matundu ya vyoo, tunazungumzia maboma hapa, tunazungumzia habari ya maji, hospitali hakuna vitanda, hakuna dawa; kuna watu watumishi wa umma ambao tumetunga sheria wanatunzwa, wanalishwa, wanalindwa na wanatibiwa halafu eti wanawaibia Watanzania na Bunge hili likae kimya.
Mheshimiwa Naibu Spika, tutamuunga mkono Mheshimiwa Waziri Mkuu atakapokuja na mkakati ambao unaonesha watu wote ambao ni watumishi wa umma wana mali ambazo hazieleweki, hafanyi biashara, hafanyi chochote ila baada ya kupata cheo tu. Alisema uadilifu, sisi tunataka siyo kuandika makaratasi, tunataka viongozi wa umma wataje mali hadharani tuone namna ya kufanya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hayo ndiyo maneno ambayo Watanzania wanataka na Bunge hili linataka lifanye kazi ya Watanzania. Vyombo vyote kama ni Usalama wa Taifa, kama ni Jeshi la Ulinzi, hivyo hivyo kwa mahakama, watu wanataka haki wanataka maendeleo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Bunge hili lifanye kazi ya Watanzania na Mheshimiwa Waziri Mkuu ni wakati wake, ni kizazi chake, ana umri wa kutosha, ana elimu ya kutosha, amepewa wasaidizi aje na mambo ambayo watu wanayalalamikia, Bunge hili lionekane la maana. Hapo siyo mbaya Waziri Mkuu akifanana na akina Sokoine, walikuwa wakitangaza watu wanajificha, watu wanapoteza pesa. Ni kwa nini? Ni kwa sababu watu wanalalamikia mambo ambayo yanatakiwa yafanyiwe kazi na mtekelezaji ni Serikali, Mtendaji Mkuu ni Dkt. Lameck Mwigulu Nchemba, washauri, wasimamizi Bunge la Tanzania na kiongozi wao ni Mheshimiwa Zungu na Naibu Spika umekaa hapo na Waheshimiwa Viongozi wengine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, haya mambo Mheshimiwa Waziri akiyafanyia kazi tabasamu la Watanzania liko nje nje na sisi wakubali kwamba ni kioo. Sisi backbenchers ni kioo, unapokuwa unajiangalia nitakwambia tai imekaa vizuri, tai imekaa vibaya, hapo una doa nenda ukaoge, usinichukie. Penda wenye akili, pokea ushauri, tupambane kwa ajili ya Watanzania hawa. Waheshimiwa Wabunge, tumepata fursa kwa niaba ya Watanzania. Kuna watu milioni 65, jiulize Mbunge leo umekuja hapa kwa ajili ya nani? Hapa unamwakilisha nani? Watanzania wanasema nini? Sisi ndiyo tuamue Tanzania yetu kutoka hapa kwenda mbele iweje? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tukitaka iwe nzuri ni Bunge hili, tukitaka iwe mbaya ni Bunge hili, tukipenda nchi yetu kwa maelezo ambayo yamezungumzwa inawezekana. Rasilimali zipo, watu wapo na elimu wanayo na fursa wamepata na bahati ya kuingia kwenye Bunge hili Waheshimiwa Wabunge wanayo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mungu awabariki sana, ahsante sana. (Makofi)