Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Kiza Hussein Mayeye

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. KIZA H. MAYEYE: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi japo ilikuwa nafasi ya Mheshimiwa Ado Shaibu. Nimesikiliza Hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, lakini kipekee kabisa, ninampongeza kwa kazi ambayo amefanya kwa kupita kwenye majimbo na kutatua changamoto kwa wananchi, ninampongeza pamoja ya kuwa ninatoka upande wa pili, lakini haimaanishi kwamba ninatakiwa kupinga kila kitu. Kama anafanya kitu kizuri, nina kila sababu ya kumpongeza. Kwa hiyo, ninampongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu na kule Kigoma tunamsubiri ili aje atusaidie kutatua changamoto. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hotuba hii kwanza nijikite katika afya. Wote tunajua kwamba afya ndiyo kila kitu kwenye maisha ya mwanadamu na huwezi kuwa na Taifa bora kama hujaboresha afya. Tafsiri yake ni kwamba sisi kama Watanzania tunahitaji afya bora kwa Watanzania wote. Ninashukuru kwa hatua ya Mheshimiwa Rais ambayo sasa tunakwenda kwenye Bima ya Afya kwa Watanzania Wote.

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe zoezi hili likamilike kwa wakati, Watanzania wana shida ya afya. Katika majimbo yetu sote ni mashahidi, Sera ya Afya inasema watoto chini ya miaka mitano watatibiwa bure, lakini tunapokwenda katika majimbo yetu vijijini ni watoto hawa chini ya miaka mitano wakienda hospitali wanaambiwa hakuna dawa na wazazi wakati mwingine wanaambiwa watoe pesa. Kwa hiyo, kama kweli tumedhamiria tunasema tunataka kuboresha afya ya Watanzania hii huduma bure ya Watanzania ya afya iwe bure kweli kweli kwa Watanzania wote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Sera ya Afya inasema kila kata kutakuwa na kituo cha afya, lakini tunapokwenda katika majimbo yetu tuna kata ambazo hakuna vituo vya afya na Watanzania wanateseka kutembea umbali mrefu kutafuta huduma za afya. Mfano, katika Jimbo langu la Kigoma Kaskazini zipo kata ambazo mpaka leo tunapozungumza miaka 60 ya uhuru, hawana kituo cha afya na wananchi wanatembea umbali mrefu. Kwa mfano, Kata ya Kidahwe, Kata ya Matendo, Kata ya Ziwani, Kata ya Kagongo, na Kata ya Nyarubanda Mkigo wananchi hawana vituo vya afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe sana twende tukatekeleze sera hii ya kuwa na vituo vya afya kwenye kata zote. Shida ya Watanzania siyo kuwa na majengo peke yake Watanzania wanataka wakienda kwenye kituo cha afya wapate dawa, tunataka watumishi wa kutosha.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika jimbo langu juzi tumepata msiba, watu wa Wizara ya Afya wamefariki. Kwa hiyo, niombe sana tunapokwenda katika bajeti hii basi tuweze kupata watumishi wengine waweze ku-cover yale mapengo ambayo wenzetu wamefariki na kupoteza maisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninataka nizungumzie suala la watumishi. Sisi Wabunge tuko hapa, tunafanya kazi hapa Bungeni miaka mitano na miaka mitano ikiisha huwa tunatoka kwenye ule mlango pale watu wote pesa zimeingia kwenye akaunti za kiinua mgongo, lakini wapo wafanyakazi wa Serikali (ndugu zetu walimu, na manesi) ambao wanafanya kazi kubwa sana. Waziri Mkuu amefika hapa ni mwalimu; Waziri wa TAMISEMI, Mawaziri wote na Wabunge tumefika hapa ni kazi ya walimu, ni kazi ya manesi wanaotutibia watoto na kututibu sisi.

Mheshimiwa Naibu Spika, inasikitisha sana wapo watumishi ambao wanastaafu hata pesa ya mizigo kulipwa kwa wakati halipwi. Nina watu jimboni kwangu, mtu amestaafu miaka mitatu lakini mpaka leo anadai pesa ya mizigo kutoka Kigoma kwenda Sumbawanga. Hii inasikitisha sana na hawa watumishi ambao wanafanya kazi kubwa huko kwa wananchi hebu tufike mahali wastaafu wanastaafu, stahiki zao zilipwe kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wako watu wanahamishwa; mtu anatoka Kilimanjaro anakwenda Kigoma anatoka Kigoma anakwenda Kagera kwa mujibu wa Sheria ya Kazi anapaswa alipwe pesa zake za uhamisho. Anakwenda likizo anatakiwa alipwe pesa yake ya likizo, lakini wako watu wanahama vituo vya kazi hata saba hawapewi pesa zao za uhamisho, hawapewi pesa zao za likizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, hawa watu ambao wanafanya kazi kubwa huko hebu tufike mahali tuwahurumie wapate stahiki zao. Mbaya zaidi unakuta mtu ni mwalimu au ni nesi ameumwa amefanyiwa operation ya figo ametumia gharama zake Serikali hata kumrudishia pesa zake inakuwa ni kizungumkuti. Akienda halmashauri anapigwa danadana, akitafuta TAMISEMI danadana. Wako watu kwenye majimbo yetu, yuko mama amefanyiwa operation ya figo ametumia pesa zake vithibitisho vyote anavyo, lakini mpaka sasa hajalipwa pesa yake. Niombe sana tuwasaidie wananchi, kama kweli tumeamua kuwasaidia wananchi tuwasaidie. Yule anayestahili kupewa stahiki zake aweze kupewa stahiki zake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu ya muda nizungumzie suala la miundombinu. Sote tunajua kwamba miundombinu ni muhimu sana katika maendeleo ya Taifa letu. Ili kama Taifa tuwe na maendeleo hatuna budi kuboresha miundombinu yetu. Huko vijijini barabara zetu ni changamoto kubwa sana. Hizi barabara za TARURA na ninashukuru Mungu Mheshimiwa Rais amesema atawapelekea pesa TARURA. Niombe hizi pesa ziende kwa wakati, TARURA wakafanye kazi. Barabara za vijijini ni mbaya sana. Huko kwenye kata zetu huko kuna barabara ambazo mama mjamzito akipita kama sentimita zimesoma anakwenda kujifungua lazima atajifungulia barabarani kwa sababu ya ubovu wa barabara. (Makofi)

Kwa hiyo, niombe sana pesa ziende na sasa hivi mvua zimenyesha sana katika maeneo yetu, zichukuliwe hatua za dharura kukarabati barabara zote ambazo zimeharibika na wananchi waweze kupita bila changamoto yoyote.

Mheshimiwa Naibu Spika, ndani ya Jimbo langu la Kigoma Kaskazini kuna Barabara ya Mwandiga – Bubango - Chankele mpaka Kagunga. Barabara hii ni potential sana na siyo potential kwa Jimbo la Kigoma Kaskazini peke yake, kwa Mkoa wa Kigoma na Tanzania. Kwa sababu Kigoma tuko mpakani mwa Kongo, tuko mpakani mwa Burundi, barabara ile ikiweza kukamilika maana yake Wakongo na Warundi wataleta biashara, vijana watapata ajira, tutaondokana na umaskini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kiwanja cha ndege kinakwenda kukamilika, Liemba inakwenda kukamilika, Bandari kavu ya Katoshwe inakwenda kukamilika. Tukiwa na barabara hii, ninaamini kabisa tutaongeza mapato kama jimbo, kama mkoa na kama Taifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho ninataka nizungumzie suala la Ziwa Tanganyika. Nimezaliwa Kigoma na mpaka umri huu ndiyo kwetu, ndiyo ninaishi; ninalijua Ziwa Tanganyika. Ziwa Tanganyika automatic toka mababu na mabibi kuna wakati lenyewe linajaa, kuna wakati lenyewe samaki wanakuwa wengi na kwa lugha ya kwetu tunaita ‘ndenga’. kuna wakati inakuwa ndenga samaki wanatoka, kuna wakati samaki wanakuwa hawapo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jana Baba Levo aliibua hoja ya Ziwa Tanganyika kufungwa. Watu wa Kigoma si kwamba hatutaki mabadiliko au maendeleo, lakini maendeleo yoyote lazima tuwatazame na wananchi yanawaathiri kiasi gani. Yawezekana wamesaini mikataba Ziwa Tanganyika lifungwe, lakini tuangalie madhara kwa wananchi. Mheshimiwa Waziri jana amesema Ziwa lilipofungwa samaki waliongezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama kuna kipindi watu wa Kigoma tulikula mpaka dagaa wa Mwanza, ni wakati Ziwa Tanganyika limefungwa. Kwa hiyo, ninaomba hebu turudi kwa Wananchi wa Kigoma, tuwasikilize. Tusichukulie tu kwa sababu ni Serikali tuna mamlaka ya kufanya chochote tukafanya, inawaathiri vipi Watu wa Kigoma? Watu wakiacha kwenda kuvua tunakosa mboga, lakini hao wavuvi ambao wanategemea kutoka Ziwa Tanganyika wanakosa hata pesa na matokeo yake watu wataingia kwenye ujambazi na mambo yasiyofaa. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa muda wako umekwisha.

MHE. KIZA H. MAYEYE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.