Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Simai Mohammed Said

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

House of Representatives

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. SIMAI MOHAMED SAID: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote ninachukua nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu, lakini pia ninachukua nafasi hii kukupongeza wewe Mheshimiwa Naibu Spika pamoja na Mheshimiwa Spika na Waheshimiwa Wabunge wote kwa mapokezi mazuri ambayo tumeyapata jana mimi pamoja na wenzangu, kwa kweli tumefarijika sana. Ninaleta pia salamu kutoka kwa wenzangu Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi ambao sisi kwa ujumla tuko watano hapa kuliwakilisha Baraza la Wawakilishi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya wenzangu tunaahidi, tutajitahidi katika kuzishauri Serikali zetu na kutimiza malengo. Baada ya hapo, niende moja kwa moja katika mchango wangu ambao ninahisi pia utatusaidia.
Mheshimiwa Naibu Spika, hapa ukiangalia kiongozi wetu ambaye anaisimamia Serikali ni Mheshimiwa Waziri Mkuu na tunaweza tukasema kwamba Mheshimiwa Waziri Mkuu ni sawasawa na moyo. Kwa nini nasema hivyo? Kwa sababu moyo unachukua damu safi na chafu inapita pale moja kwa moja ili mwili uweze kusimama. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri Mkuu ni kiongozi wetu katika kuishauri Serikali na pia ni moyo wa Serikali na sisi kwa ujumla katika kuufikisha ujumbe wetu sisi kwako.

Mheshimiwa Naibu Spika, jana nimesikia michango katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu na Waheshimiwa Wabunge wengi wamempongeza katika ziara ambazo amezifanya katika mikoa mbalimbali ya ndani ya Jamhuri ya Muungano au katika upande wa Tanzania Bara, lakini niseme tu, katika kuishauri au kumshauri Mheshimiwa Waziri Mkuu; sisi tunaposema kwamba tuna muungano wetu na muungano wetu kweli ni muungano wa kipekee duniani, hakuna popote.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda popote ukisema Muungano huu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania upo wapi? Ni uko kwetu hata katika Bara la Afrika. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri Mkuu na sisi kwa upande wa Zanzibar, hata ukiangalia Katiba katika Nyongeza ya Kwanza, ukurasa wa 128 kuna maeneo mengi tu ambayo yanakugusa moja kwa moja kwa upande wako. Kwa hiyo, ninapenda kumshauri Mheshimiwa Waziri Mkuu pia katika ziara zake atakapozifanya, si vibaya basi akajipangia siku akipata na sisi kule Zanzibar yako maeneo nahisi tutaweza kuunganisha nguvu zetu kwa pamoja.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hili, hakuna mtu atakayesema kwamba sijui tunaingilia Mamlaka ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, hakuna. Sisi muungano wetu wa Serikali ni wa kipekee, wengine huzungumza ni muungano wa kisiasa, lakini muungano huu ni wa wananchi na tunaujua kabisa. Mtu akisema muungano huu maana yake sijui uko hivi au vile ninaona mwingine mtu anateleza tu. Ukienda kule Kigoma, ukipita Kagera, ukija Lindi, Mtwara, ukienda mpaka Tanga tunajijua sisi.


Mheshimiwa Naibu Spika, tutafurahi Mheshimiwa Waziri Mkuu katika ziara zake atakazopata, basi apite katika visiwa vyetu Unguja na Pemba na leo wengi wamezungumza, nimemsikia Mheshimiwa Mbunge wa Welezo akiuliza swali kuhusu masuala ya utalii. Utalii haumo, haujatajwa katika mambo ya Muungano lakini kila siku ya maisha yetu, Wazanzibari na ndugu zetu Tanzania Bara wanatugusa, ni muhimu sana, ni biashara kubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika muktadha huo, ninapenda kuishauri Serikali ya Jamhuri. Kwa muda mrefu sasa, ninaomba nieleweke kwamba mchango wangu ni wa jumla, sitaingia katika masuala ya bajeti kwa kuwa bado sijajifunza vitu vingi, lakini ninaamini huko mbele nitazungumza. Nikirudi kwenye hoja, utalii wetu tukiangalia kwa miaka mingi tunakwenda tunazungumza kuhusu kaskazini, Visiwa vya Zanzibar.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimekaa na dada yangu hapa nilikuwa ninampongeza kuhusu how beautiful this Western side is, ukienda Kigoma kule Mwamgongo kwenye Ziwa Tanganyika ukienda mle, karibu mita 1,400, maji yake meupe mazuri kabisa. Ukija huku chini mpaka Kagera, Katavi na Rukwa, bado tumepaacha tunategemea maeneo yale kila siku. Kwa hiyo, ninaishauri Serikali wala sitasubiri Wizara yenye dhamana, hapana, hii ni katika Dira ya nchi yetu na Ofisi ya Waziri Mkuu ni katika ofisi moja muhimu sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaishauri Serikali tuanze kujenga wigo, tuufungue upande huu wa magharibi. Sisi kwa upande wa Visiwa vya Unguja na Pemba tayari Mheshimiwa Rais Mwinyi amejipanga katika kuifungua Pemba: Pemba ikifunguka tukifungua na Tanga, tukija na Saadani upande wa huku tukafungua, tukajenga marine nzuri, tunashuka zetu moja kwa moja mpaka Lindi na Mtwara. Kwa hiyo, coastal yote hii lazima tutakuwa tunaiendeleza hasa katika fursa hiyo ili kuzalisha ajira mpya kwa vijana wetu, lakini pia kujenga uchumi imara na kutegemea utalii wetu.


Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, tumezungumza kuhusu Dira ya Nchi yetu ya 2050 na kwenda huko mbele, lakini ukiangalia kwa undani elimu yetu lazima tuiangalie kwa undani sana. Lazima elimu yetu tuiunganishe na hali halisi ya kila mwaka dunia inapokwenda. Hili linalozungumzwa suala la Artificial Intelligence (AI) lipo kweli, kwa uhakika by 2050, mawazo tunayozungumza hapa sasa hivi hayatakuwa yamefanana kabisa tukifika 2050. Aina ya fikra, mtazamo au ushauri kwa jambo lolote.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunachokizungumza hapa sisi Wabunge katika kuishauri Serikali, lazima tuiunganishe na elimu yetu. Wananchi wetu, vijana wetu, watoto wetu wanakwenda kwa kasi mno, hatuwezi kuwafikia. Unajua ninachoomba Mheshimiwa Mkuu, tunapo-review katika Mpango mzima wa nchi yetu tunapotaka kwenda navyo, basi tuangalie kwa undani. Sisi kule Mheshimiwa Rais Mwinyi amejitahidi sana kuboresha miundombinu ya Zanzibar.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunajua kwamba Serikali ya Jamhuri wanatujengea Barabara kutoka Tunguu kuelekea upande wa Makunduchi pamoja na Pemba, si vibaya pale panapotokea mfano Kisiwa cha Unguja ni kilometa 90, per kilometa nafikiri 54. Jamhuri ikiongeza nguvu ya kifedha kuboresha miundombinu ya visiwa vyetu, Wazanzibari na watazidi kuupenda muungano wetu, ni sehemu ndogo sana, lakini ina umuhimu mkubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho ninamalizia, katika kulishauri Bunge letu, jana wakati ninatoka usiku nikamuuliza mwenzangu hebu nipeleke sehemu ambapo ninataka nikaone. Ninajua kuna migahawa mingi, lakini ninapenda sisi kama viongozi, sijui kama kuna mpango huo, lakini ningependa kuona tuna Bunge Social Club yetu wenyewe ambapo tukienda tunapata stara zetu, kama kupigana vijembe au kupigana shoti tunapigana huko huko tunamalizana, hakuna haja ya kuingia mitaani.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini tusiwe na bendi yetu ya muziki ya Bunge? Kuna wasanii wengi sana. Nimefanya research na kuona Island, Waingereza wana bendi yao, Mheshimiwa Mwana FA ni mwimbaji, Babu Tale Meneja, pengine hata wewe Mheshimiwa Naibu Spika una kipaji chako hatukijui, Mheshimiwa Waziri Mkuu pengine siku mojamoja na yeye anapita, tuanzisheni bendi yetu na sisi wakati mwingine tunapotoka, tunaenda kuimba nyimbo zinazojenga uzalendo na nyimbo za kusherehekea. Hakuna ubaya; twende sambamba na wakati. Vijana wanasema tuungane nao, hivyo tuwe na bendi yetu ya Bunge.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana, ninaomba tena kwa niaba ya wale Waheshimiwa Wabunge wenzangu watano tuliokuja hapa, tunashukuru sana kwa mapokezi mazuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Ahsante sana. (Makofi)