Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Yahya Ally Mhata

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nanyumbu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi hii mchana huu. Awali ya yote ninaomba nichukue nafasi hii nimshukuru sana Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema, ambaye leo hii ameniwezesha kusimama ndani ya Bunge hili Tukufu kuchangia hotuba ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili; ninaomba nimshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuhakikisha kwamba jamii yetu ya Tanzania inasonga mbele na uchumi wa wananchi mmoja mmoja unaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tatu, ninamshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba yake nzuri aliyoitoa pale jana. Waziri Mkuu ameeleza mambo mengi sana ya msingi katika hotuba yake na kilichonifurahisha zaidi, aliongea taratibu na kwa umakini, kila mtu amwelewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri Mkuu wetu kwa kweli anarudisha tabasamu kwa Watanzania. Nilikuwa ninafuatilia anavyokwenda kwenye maeneo mbalimbali kule vijijini, watu mamia kwa mamia wanakwenda kupeleka hoja zao na hoja zao zinatatuliwa pale pale. Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kweli unaonyesha njia ya uongozi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, rai yangu, Mheshimiwa Waziri Mkuu, ametembea sehemu nyingi, hebu aje na Kusini, wananchi wanamhitaji aje awatatulie changamoto zao ambazo kwa kweli kwa uwepo wake ninaamini zitaisha. Karibu sana Kusini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba pia nichukue nafasi hii nimshukuru sana Mheshimiwa Spika wetu. Kwa kweli ameonyesha jinsi alivyoomba kura, alisema nipeni kura ili niwe Spika wa speed and standard. Nimeona tangu tumefungua Bunge letu hili amefanya maamuzi magumu sana mpaka nikawa ninamshangaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumefika tumekutana na changamoto ya mafuta, Mheshimiwa Spika ametoa maamuzi pale pale, ameitisha Kamati ya Nishati na Madini, amemwelekeza Waziri wa Nishati kwenda kulishughulikia jambo hili ambalo kwa kweli ni changamoto kwa Watanzania. Ninaomba niwaombe Watanzania, tuko hapa Bungeni kushughulikia changamoto zao na Spika yuko makini kuhakikisha kwamba shida za wananchi zinatatuliwa. hongera sana kwa Mheshimiwa Spika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii Wabungen ni mashahidi, Mheshimiwa Bahati, Mbunge wa Mbarali, alipokuwa anamuuliza Waziri Mkuu changamoto, kama sikosei ya vyandarua. Kama nitakuwa nimekosea Mbunge wa Babati au wapi alizungumza suala la halmashauri ambazo zimeshindwa kwenda kuchukua dawa ya kuua malaria wakati Serikali imelipa. Mheshimiwa Spika, ametoa maamuzi hapa hapa kwamba tarehe 8 ripoti ije, zile halmashauri ambazo wameshindwa kwenda kuchukua dawa ambayo imelipiwa, lengo ni kupambana na ugonjwa wa malaria, wameshindwa kwenda, ule ni uzembe, ripoti ije na wachukuliwe hatua. Mheshimiwa Spika, hongera sana kwa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo ninaomba na mimi nianze kwenye maeneo ambayo ningependa kuchangia. Kwanza kwenye kilimo. Kilimo ni moja ya maeneo ambayo yanaingiza fedha nyingi za kigeni. Sisi wananchi wa Kusini, kilimo cha korosho ni moja ya mazao ya kimkakati na sasa hivi zao hili halilimwi Kusini peke yale. Linalimwa Kusini, Pwani, Tanga mpaka hapa Dodoma na maeneo ya Manyoni mpaka kwa ndugu zangu Wanyakyusa huko mpaka Kigoma. Kwa hiyo, ni zao ambalo linaonyesha kwamba ni la kimkakati na endapo tutakuwa nalo serious litaongeza fedha nyingi za kigeni. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaona kabla ya Rais wetu, Mama yetu Samia Suluhu Hassan, hajaingia madarakani zao hili lilikuwa linakufa. Tulikuwa tunazalisha tani 100,000, leo hii ninavyoongea tunazalisha tani 600,000. Kwa nini tumefika hapo? Kwa sababu ya jitihada za makusudi za Mama yetu kuhakikisha kwamba anainua zao hili. Ameweza kutoa pembejeo za kilimo na viuatilifu bure kwa wakulima wote wanaolima zao la korosho. Kwa kufanya hivi ameweza kunyanyua zao hili la korosho. (Makofi)


Mheshimiwa Naibu Spika, sasa rai yangu kwa Waziri wetu wa Kilimo, kuna mambo asipoyaangalia yanaweza yakamwangusha. Zao la korosho ni zao ambalo linahitaji huduma ya mara kwa mara. Sasa hivi ni kipindi cha maandalizi ya zao la korosho. Wananchi wanahitaji pembejeo na viuatilifu viwe vimefika katika maeneo yao. Usipofanya hivi sasa hivi, ukaleta baadaye utakuwa umeua zao la korosho. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri hili aliangalie kwa sababu kuna wazabuni ambao wanafanya shughuli hizi wakati wanaleta viuatilifu na pembejeo nje ya wakati, wanatuangusha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, wanaleta viuatilifu na pembejeo ambazo zimepitwa na wakati. Mwaka jana tumeshuhudia ndani ya jimbo langu vimekuja viuatilifu ambavyo vime-expire. Tusipoliangalia jambo hili tunakwenda kuua zao letu. Sasa jambo la msingi ni Bodi yetu ya Korosho iwe makini katika kuhakikisha hili zao linasimamiwa kikamilifu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine, mabenki yetu. Nimewahi kuzungumza ndani ya Bunge lako kwamba mkulima wa zao la korosho hategemei tu ruzuku anayopewa na Mama bure, lazima awezeshwe kupewa mikopo ili aweze kuandaa mashamba yake. Kule Kusini utaratibu wetu wa zao la korosho tunanunua kwa Stakabadhi Ghalani na benki zetu hizi ndiyo zinazopitishiwa fedha zao.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninawaomba, ninatambua mchango mkubwa wa benki za NBC, CRDB na NMB kule Kusini. Wanatoa mikopo kwa wakulima wetu, ninawaomba, muda wa kutoa mikopo ndiyo sasa, wawawezeshe wakulima wetu kupata mikopo ili waweze kuandaa mashamba yao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, benki hizi zinafanya kazi kubwa sana na ninaheshimu jitihada inazozifanya. Katika jimbo langu, jitihada za Mama kutoa pembejeo bure na hizi benki kuweza kukopesha tumeweza kuongeza uzalishaji wa zao la korosho kutoka tani 15,000 hadi tani 21,000; zao ambalo kwa kweli limeingiza fedha nyingi za kigeni. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo tuna changamoto, kuna watu kule wanaitwa AMCOS. Hawa AMCOS Mheshimiwa Waziri wa Kilimo asipowaangalia watamkwamisha. AMCOS ndiyo wanaosimamia mauzo ya zao la korosho, lakini msimu unakwisha, baadhi ya wakulima hawajalipwa pesa zao. Kuna maeneo mengi sana wakulima wanadai fedha wakati wamepeleka mazao yao kwenye vyama vya msingi. Huwa najiuliza hizi fedha hawa wanakula wanapeleka wapi.

Mheshimiwa Naibu Spika, sheria ichukue mkondo wake, haiwezekani mkulima apeleke mazao yake kwenye AMCOS halafu fedha asipate, PCCB wapo, Polisi wapo, Mahakama ipo, kwa nini watu hawa wasichuliwe hatua? Hili jambo linahuzunisha sana. Zao la korosho siyo zao la kitoto, unakoswa na kuumwa na nyoka, unakoswa kuumwa na nyigu, mvua yako, jua lako, halafu mtu unalima hupati pesa zako, hili jambo halikubaliki. Ninaomba sana Mheshimiwa Waziri alifanyie kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine, ninaomba nielekeze kwenye wanyama waharibifu. Tumekuwa na changamoto kubwa sana sasa hivi ya wanyama waharibifu hasa tembo, haya ni maeneo yote. Leo Mheshimiwa Waziri Mkuu amejibu suala la wanyama waharibifu. Rai yangu, Mheshimiwa Rais alipokuja ndani ya jimbo langu, moja ya changamoto ambayo aliahidi kuitatua, ni kupambana na wanyama waharibifu. Aliahidi kuongeza Askari Wanyamapori ambaye Mheshimiwa Waziri Mkuu anasema, lakini aliahidi kuanzisha Kituo cha Ndegenyuki kupambana na wanyama waharibifu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kila mwaka wananchi mashamba yao yanaathirika na hawa tembo. Leo kila Kata kuanzia Masuguru, Sengenya, Nandete na kila mahali ndani ya kata yangu wananchi wanalia na uharibifu wa hawa tembo. Tusitegemee kwamba kutakuwa na kifuta jasho, zao la korosho linakwenda miaka mitano tangu upande…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Mbunge…

MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Naibu Spika, naam! Tumemaliza muda?

NAIBU SPIKA: umemaliza…

MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho kabisa, ninaomba kwa suala la watumishi, Mheshimiwa Waziri Mkuu watumishi wetu walipwe fedha. Leo kuna malimbikizo ya mishahara hawajalipwa, kuna fedha za uhamisho mpaka watumishi wapya ambao wamekuja ndani ya halmashauri zetu, hawajalipwa fedha za uhamisho. Hivi watumishi wale wapya wanapokuja kule tusiwalipe fedha za kujikimu, wataishi vipi? Ninaomba sana walimu na ndugu zetu wa afya, waganga, walipwe posho zao ili waende kufanya kazi kwa amani na utulivu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, ninaunga mkono hoja.