Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Buchosa
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kwanza nianze kwa kukushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kusimama ndani ya Bunge lako Tukufu. Pia, ninamshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu na Wizara zote zilizoko chini yake kwa kazi nzuri ambayo wanaifanya. Ninawapongeza sana TARURA kwa kazi nzuri waliyoifanya katika Jimbo la Buchosa kwa upande wa barabara. Profesa Shemdoe apokee pongezi zangu na timu yake yote kwa namna wanavyofanya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninampongeza sana vilevile ndugu yangu Mheshimiwa Ulega kwa alichotutendea watu wa Buchosa safari hii. Ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais, tumepokea shilingi bilioni 9.4 kwa ajili ya malipo ya awali ya mkandarasi wa Barabara ya Sengerema – Nyehunge. Mimi na kaka yangu Mheshimiwa Tabasam tulikuwa na wasiwasi kama tungegombea mwaka 2030, lakini kwa sababu ya jambo hili tunataka tuwaambie watu wa Buchosa na Sengerema, tunakuja kugombea tena. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninataka niongee mambo makubwa mawili. Jambo la kwanza ni namna ya kuifanya nchi yangu, Tanzania, iwe nchi ambayo haitegemei misaada kutoka kwa wageni kuendesha uchumi wake, kuongeza pato la Taifa. Jambo la pili itakuwa ni namna ya kupunguza matumizi yetu ili kama nchi tuweze kujitegemea.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikupe picha ndogo tu ambayo nimeshaiongea hapa ndani mara kadhaa nitapenda niirudie tena leo. Ninaishi katika Taifa tajiri sana, tajiri mno. Tanzania ni nchi tajiri sana na ninajivuna kuwa Mtanzania, kila mahali ninapokwenda ninawaambia ninatoka katika Taifa tajiri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa utalii wa natural destination Nchi yetu Tanzania ni nchi ya kwanza Afrika, lakini ni nchi ya pili duniani. Kwa makaa ya mawe ni nchi ya 50, kwa gesi asilia ni nchi ya 82, kwa dhahabu ni nchi ya 20, kwa helium gas ni nchi ya kwanza, kwa almasi ni nchi ya 10, kwa ukubwa wa ardhi, Tanzania ina ardhi yenye ukubwa wa kilomita za mraba 945,000. Inayolimwa peke yake ni kilomita za mraba 350,000 (arable land). Kwa uranium Tanzania ni nchi ya 10 duniani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hii inaonyesha kabisa kwamba nchi yangu ni tajiri na ina uwezo mkubwa sana. Si jambo sahihi hata kidogo kwa Taifa kama hili kuendelea kutegemea misaada ya wahisani kuendesha uchumi wa nchi yetu. Kwa hiyo, nimesimama hapa leo mbele ya Bunge lako Tukufu kwamba tufanye kila kinachowezekana kuhakikisha kwamba sekta hizi nilizozitaja na nyingine nyingi zichangie kwenye pato la Taifa letu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa uvuvi, kwa mfano, mchango wa uvuvi kwenye Pato la Taifa ni asilimia 1.7 lakini tuna maji mengi kuliko Uganda. Nchi ya Uganda mchango wake kwenye pato la Taifa ni karibu asilimia mbili kutokana na uvuvi. Upande wa mifugo, Tanzania nchi yangu ni ya pili kwa wingi wa mifugo katika Afrika ikiongozwa na Ethiopia, lakini kipato kinachotokana na mifugo katika nchi yangu ni asilimia 7.4.
Mheshimiwa Naibu Spika, Nchi ya Kenya ambayo ina mifugo kidogo kuliko sisi mchango wa mifugo kwenye pato la Taifa ni 12%. Hii inaonyesha kwamba tuna utajiri mkubwa sana ambao tunashindwa kuutumia kuongeza pato la Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninataka kuzungumza kwamba tunayo kila sababu ya kuhakikisha kwamba tunafanya kila kinachowezekana ili sekta hizi zichangie pato la Taifa letu. Pato la Taifa letu linakua, lakini mchango wa sekta ni mdogo. Nilishazungumza huko nyuma, ninazungumza tena leo ya kwamba Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameamua kwa nia moja kuhakikisha kwamba sekta za uchumi wa nchi yetu zinachangia pato la Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais amefanya hivyo kwenye utalii, tumeshuhudia pato la Taifa limeongezeka, amefanya hivyo kwenye madini, pato la Taifa limeongezeka na sasa anachanja mifugo nchi nzima ili mifugo iweze kuchangia pato la Taifa. Huu ni mwenendo mzuri sana na Taifa langu likichukua hatua hii nina uhakika pato la Taifa litaongezeka na pato la Taifa likiongezeka hakika tutaweza kuendesha uchumi wetu sisi wenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nchi za wenzetu wameanza kujitoa kwenye kusaidia nchi za Afrika. Marekani inajitoa na Jumuiya ya Ulaya inajitoa. Kwa hiyo, kuendelea kutegemea watu ambao na wao wana mambo yao kwa hivi sasa tutaendelea kuchelewa. Ninataka Tanzania iwe na uwezo wa kujitegemea yenyewe kuendesha uchumi wa nchi yake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mapato ya kodi kwenye pato la Taifa ni kidogo. Ratio ya tax to GDP ni ndogo na hapa kwetu Tanzania ni 12% tu kwenye pato la Taifa. Base ya walipaji wa kodi Tanzania ni ndogo. Katika nchi hii walipa kodi hawazidi milioni nane. Lazima kama Taifa tufanye kila kinachowezekana kuongeza idadi ya walipa kodi wetu. Utafanyaje kuongeza idadi ya walipa kodi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, moja, ni lazima pato la Taifa likiongezeka utaweza kupunguza baadhi ya kodi, compliance iweze kuongezeka. Jambo lingine la muhimu sana kufanya ni kuhakikisha kwamba kodi zetu zinakuwa rafiki ili watu wajitokeze wenyewe kwenda kulipa. Nina uhakika kabisa kwamba tukiweza kufanikiwa kuhakikisha watu wanalipa kodi wanavyotakiwa kulipa na wajitokeze wenyewe, Pato la Taifa litaongezeka na pato likiongezeka hakika tutaweza kuendesha uchumi wetu kwa urahisi zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, ni namna ya kupunguza matumizi yetu. Hata kwenye familia ya kawaida, baba mwenye nyumba unapokuwa nyumbani kwako, unapoingia kwenye wakati mgumu kuna mambo ya kupunguza. Ombi langu, kwa kuwa tunaingia kwenye hali ngumu ya uchumi kama Taifa, ninatamani kuona tunaendesha maisha yetu kama Serikali katika kujibana kutegemea na hali tuliyonayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, sitarajii kuona kwenye hali ngumu ya uchumi tuliyonayo, lakini watu wanaendesha uchumi kama vile hatupo kwenye hali ngumu, hilo halitakuwa jambo sahihi. Kwa hiyo basi, ninaomba tuhakikishe kwamba tunabana mianya yote ya kuvuja kwa mapato ya Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mapato yetu yanavuja, yanapotea. Fedha zetu zinapotea, tunakusanya fedha, lakini zinaingia mikononi mwa watu wasiokuwa sahihi, zinapotea. Juhudi ya Mheshimiwa Rais kukusanya kodi ni kubwa. TRA ninawapongeza sana, safari hii wamekusanya sana fedha kuliko wakati mwingine wowote, lakini fedha zetu zinapotea. Watu waaminifu wapo, lakini watu wabaya wapo. Tufanye nini kama Taifa?
Mheshimiwa Naibu Spika, nilishazungumza hapa ninarudia tena leo, hakuna tunachoweza kufanya zaidi ya kuhakikisha ya kwamba watu wawe mahali wanapostahili kuwa. Watu wanaoibia Taifa letu washughulikiwe kwa mujibu wa sheria. Tuna sheria nzuri kabisa lakini hatuzitumii kuwadhibiti watu wanaotuibia. Hatuwezi kwenda mbele, hata tukikusanya fedha kiasi gani kama wezi wanaendelea kuonekana mahiri kwenye Taifa letu. Watu wanaoiba waende mahali wanapotakiwa kuwa, tuna sheria nzuri sana. Tuna sheria tano nzuri kabisa, hatuhitaji sheria mpya katika nchi yetu, tuna sheria tano nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tuna Sheria ya Fedha, Sheria ya Uhujumu uchumi, Sheria ya TAKUKURU, Sheria ya Manunuzi pamoja na Sheria ya Utakatishaji wa Fedha. Sheria hizi zikisimamiwa vizuri, watu wote wanaoibia Taifa letu wanaotufanya tuendelee kuwa maskini wanajitajirisha wao wenyewe binafsi wakashughulikiwe kwa mujibu wa sheria hizi, hakika watu wataogopa mali ya umma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye Taifa hili watu hawaogopi mali ya umma, watu hawaogopi fedha za Serikali. Huko kwenye halmashauri zetu watu wanaiba, wanaiba, wanaiba lakini mwisho wa siku hakuna kinachotokea. Watu hawashughulikiwi. Ninataka kumwona mtu ameiba yuko jela ili wengine watakaofuata wasiweze kuiba. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tusipofanya haya, watoto wetu wanamaliza chuo kikuu leo, watakapoingia ofisini kufanya kazi wataona kumbe utaratibu ni kuingia na kuiba na kutajirika. Hatuwezi kujenga Taifa la namna hiyo. Ninataka kuona na ninatamani kuona Bunge hili la Kumi na Tatu lijijengee sifa ya kwamba chini ya Mheshimiwa Spika, Mussa Azzan Zungu na Naibu Spika, Baran Sillo, wezi walishughulikiwa walivyotakiwa kushughulikiwa. Hatuwezi kuwa na Taifa ambalo kila mwaka ikisomwa ripoti ya CAG mambo ya kututia aibu. Tujenge Taifa lenye reputation, mtu akiingia kazini ajue iko sheria, nikiiba nitashughulikiwa kwa mujibu wa sheria. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ya kusema ni mengi lakini ninaomba nimalizie kwa kusema hivi; kama Taifa hatuwezi kuacha kukopa, debt - GDP ratio bado ni ndogo. Sisi sasa hivi tunaweza kukopa kwa sababu ratio yetu bado tupo 47%, lakini bado threshold ni 50%. Ninaomba kama inawezekana kukopa tukope ili tuweze kuchochea maendeleo ya nchi yetu, lakini tukope pale tu ambapo ni lazima kukopa. Tofauti na hapo tutumie mapato yetu ya ndani kuendeleza nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)