Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Kunti Yusuph Majala

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru kwa kunipatia nafasi ili niweze kuchangia bajeti ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Awali ya yote, ninamshukuru sana Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema aliyetujaalia, na hatimaye leo tumeweza kukutana hapa kwa ajili kujadili mustakabali mzima wa Taifa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninamshukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi kubwa anayoifanya kwa ajili ya kulitumikia Taifa letu. Kwa pongezi hiyo kwa Waziri Mkuu, ninamwomba sana Mheshimiwa Waziri Mkuu, ziara zake anazoendelea nazo ndani ya Taifa letu ziwe na mwendelezo na ufuatiliaji wa maelekezo ambayo anaendelea kuyatoa kwenye ziara zake.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye suala zima la ziara za Waziri Mkuu, nimekuwa nikifuatilia, na jambo kubwa ambalo limeendelea kujitokeza kwenye mikutano yake ni migogoro ya ardhi kwa watumiaji wengi wa ardhi kwenye maeneo tofauti tofauti. Kila wilaya, kila mkoa na kila halmashauri alikokwenda Waziri Mkuu amekutana na changamoto ya migogoro ya ardhi.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la migogoro ya ardhi ndani ya Taifa letu limekuwa ni donda sugu ambalo tathmini, utafiti na wataalamu wetu hawataki kutoa namna bora ya kuweza kusaidia ili tatizo hili liweze kuondoka kwetu. Migogoro mingine ipo ambayo ni sisi Serikali tu tunatakiwa kukutana na kuamua na kutoa tamko, kwamba hiki ni A na hiki ni B.

Mheshimiwa Naibu Spika, migogoro mingine inasababishwa na sisi viongozi ambao tuko kwenye maeneo kule chini. Kiongozi fulani anasema jambo fulani na kiongozi fulani anasema fulani, na mwisho wa siku yote haya hayafuatiliwi na hayawezi kutolewa maamuzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, hatimaye tumekuwa tukitoa adha kubwa kwa viongozi wetu wa Kitaifa wanapofika, wananchi wanapanga msururu kwenda kutoa malalamiko yao ya migogoro ya ardhi. Nitoe mfano mmoja tu kwa Mkoa wa Dodoma, tumekuwa tukilia na tumekuwa tukilalamika migogoro baina ya watumiaji wa ardhi, wafugaji na wakulima na hifadhi zetu tulizonazo.

Mheshimiwa Naibu Spika, mgogoro wa Swagaswaga pamoja na watumiaji wengine, kwa maana ya wafugaji na wakulima, mgogoro huu umedumu zaidi ya miaka 20. Iliundwa Tume ya Mawaziri nane kwa ajili ya huu mgogoro, ikaenda, lakini mpaka leo mgogoro huu hauna suluhisho lililotolewa kwa watu hawa ambao ni wananchi wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri Mkuu amefanya kazi kubwa, na mimi nilitamani sana na watu wangu wapate huduma hiyo, kwani walikuwa wanafunga safari. Alipokuwa Tanga kuna baadhi ya watu walikwenda Tanga, wanatamani kukutana naye ili wapate hatma ya ardhi yao baina ya Hifadhi ya Swagaswaga pamoja na wananchi walioko pale. Kwa hiyo, ninaomba tamko rasmi la Serikali kuhusiana na mgogoro wa Swagaswaga pamoja na wananchi, watumiaji wetu wengine wa ardhi.

Mheshimiwa Naibu Spika, mgogoro mwingine ni wa Mkungunero ambao tunapakana na Kondoa Vijijini pamoja na Kiteto; na huu ni mgogoro wa kimipaka. Ninaiomba pia Serikali, hebu imalize hii migogoro. Tunashindwa kufanya shughuli za uzalishaji, wananchi wetu wanashindwa kutimiza wajibu na majukumu yao ya kufanya kazi kwa ajili ya kulijenga Taifa letu, wako busy kutembea kwenye ofisi za Serikali kwenda kutafuta hatma ya usuluhishi wa migogoro.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tuziombe Wizara zinazohusika, wao ni Serikali moja, tunaomba wakae watatue migogoro ya ardhi kwa watu wetu ili wananchi wetu waweze kulitumikia Taifa lao kwa kufanya kazi za uzalishaji kwa ajili ya ujenzi wa Taifa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo langu la pili ambalo ninatamani kulisema leo kwenye Bunge lako, ni suala zima la miradi ya kimikakati. Ninamshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu, wakati anajibu maswali asubuhi, amejaribu kutupa mwanga, kwamba nini sasa kinachofuata baada ya miradi mingine kuwepo iliyokuwa inaendelea, pamoja na ile ambayo ilikuwa imesimama kwa muda mrefu?

Mheshimiwa Naibu Spika, ni ukweli usiopingika, nchi hii tuna miradi mingi ya kimikakati na imekuwa ikisemwa kwa muda mrefu. Mpaka sasa wananchi wamekuwa wakiona kama Serikali yao inawalaghai na kuwadanganya.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba sana kwa kauli aliyoitoa Mheshimiwa Waziri Mkuu leo hapa akiwa anajibu maswali kwa Waheshimiwa Wabunge, kwamba sasa tunakwenda kukamilisha miradi iliyokuwepo na pili, tuweze kwenda kwenye miradi mingine mipya ili Watanzania wetu waweze kunufaika na rasilimali za Taifa letu, naomba niseme kwamba mradi wa barabara ya kutoka Tanga kimekuwa ni kizungumkuti kwa kipindi cha muda mrefu.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata Mheshimiwa Rais alipokuja kwenye Jimbo la Chemba wakati anaomba kura, wananchi walimwambia suala la barabara hiyo. Barabara hiyo, kati ya kilomita 462 Wilaya ya Chemba ndiyo tuna kilomita zaidi ya 160. Kwa hiyo, ukiangalia ukubwa wa hiyo barabara kwenye hii mikoa minne Wilaya ya Chemba ndiyo tuna eneo kubwa zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ombi langu kwa Serikali, tunapokwenda kwenye utekelezaji wa barabara hii, ninamwomba Mheshimiwa Waziri Mkuu, yeye kama Msimamizi wa Serikali na vyombo vyake vyote alivyonavyo, tuombe kila mkoa uweze kupewa mkandarasi ili barabara hii isije kuonekana inajengwa mahali fulani na maeneo mengine wameachwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kila mkoa katika mikoa yetu hii minne tuombe, mimi Mkoa wa Dodoma nitaomba mkandarasi wa Mkoa wa Dodoma ili barabara hii itakapokwenda kwenye utekelezaji, basi na sisi tuweze kuona huyo mkandarasi akiwa site na hatimaye anaweza kutekeleza majukumu kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya barabara hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi mwingine ni Daraja la Kilema Simba. Daraja hili lilipangiwa fedha tangu mwaka 2022; lilishatangazwa, mkandarasi akasaini mkataba na mambo mengine yakafanyika, lakini cha ajabu limekaa miaka mitano mkandarasi hakupewa senti tano ya Mwenyezi Mungu. Hali hii imepelekea mkandarasi kwenda kusitisha mkataba ule.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba daraja hili sasa litakapokwenda kutangazwa, fedha itolewe ili Watanzania wale waweze kuepukana na adha kubwa wanayoipata kwa ajili ya miundombinu ile ya lile daraja pale. Limeshakatika na mvua za safari hii tena limekatika zaidi. Kwa hiyo, kadri tunavyoendelea kuchelewa kwenda kulijenga litaenda kuleta madhara makubwa ambayo mwisho wa siku tutakuja kujilaumu sisi kama Taifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni kuhusiana na miundombinu ya TARURA. TARURA wana barabara nyingi za udongo. Ninaomba sasa tutoke kwenye barabara za udongo tuingie kwenye barabara za changarawe ambazo zitatusaidia kuwa na barabara imara zitakazokaa kwa muda mrefu badala ya kuendelea kuwa na barabara za udongo nyingi. Mvua kama hizi zinaponyesha barabara zetu zote zinaharibika kwa wakati mmoja kwa sababu tu ya ubora na uimara wa zile barabara.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninawashukuru sana Wizara ya TAMISEMI, kaka yangu Profesa Shemdoe ninamshukuru sana, kwani tulikuwa na adha kubwa sana kutokana na barabara hizi. Ninamshukuru kwa shilingi milioni 74 aliyonipatia kwa ajili ya barabara ya kutoka kwa Mtoro mpaka Sanzawa. Mkandarasi yuko site anafanya kazi. Wanachemba wanasema, ahsante sana, wanamshukuru sana kwa hicho ambacho amekifanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, bado tuna changamoto kubwa ya miundombinu ya barabara, inayopelekea mpaka Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI, anapowaleta watumishi kwenye Wilaya ya Chemba, wanashindwa kwenda kukaa kule kwa sababu gharama ya usafiri ni kubwa kutokana na mazingira mabovu ya miundombinu ya barabara. Kwa hiyo, ninawaomba sana, mwaka 2026/2027 majimbo ya vijijini wakatupe kipaumbele, watutengenezee barabara ambazo hata watumishi wetu tutakaowapanga kuja kuwasaidia, sekta ya afya na sekta ya elimu wanashindwa kukaa kule.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Chemba huwa ninaiita ni wilaya ambayo watu wanakuja kuchukua check number, kwa sababu akipelekwa, anachukua check number, anaomba uhamisho na kuondoka zake. Hatuhitaji kuwa wilaya ya watu kuja kuchukua cheque number. Tunahitaji kuwa wilaya ya watumishi watakaokuja wakae, watoe huduma kwa Watanzania wenzetu badala ya kuja kuchukua check number na kuondoka.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ninaomba sana miundombinu iimarishwe ili watu wetu ama viongozi wengine wanaokuja kufanya kazi na sisi, waweze kuona ni sehemu ya Tanzania na wanastahili kuwa Chemba na siyo vinginevyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo langu lingine ni suala la mawasiliano. Tunakwenda kutoka kwenye analojia na kuelekea kwenye dijitali, lakini mawasiliano kwenye maeneo na kwenye majimbo ya vijijini bado ni adha kubwa. Waziri wakati anajibu kwenye Wizara ya Vijana, wanasema kwamba wanatoa matangazo ya kuomba mikopo ya Mama ya bilioni 200.

Mheshimiwa Naibu Spika, kijana wa kijijini hana network, hana mawasiliano ya aina yoyote na hamiliki simu, anakwendaje kuomba hiyo mikopo ambayo Mheshimiwa Rais ameitoa kwa nia na dhamira njema ya kuwainua vijana?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tuombe Wizara ya Mawasiliano itusaidie kufikisha mawasiliano kwenye maeneo yetu ya vijijini ili watu wetu waweze kunufaika na fursa mbalimbali zinazotolewa na Serikali badala ya wao kubaki nyuma na hatimaye kuona watu wengine wananufaika.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana.

MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho kwa upendeleo wa dakika moja tu, nikuombe, ni muhimu sana.

NAIBU SPIKA: Malizia kwa sekunde 30.

MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kuhusiana na suala la maslahi ya Madiwani pamoja na Wenyeviti wetu wa Vijiji. Madiwani wetu leo posho yao ya mwezi ni shilingi 350,000, lakini Diwani huyu ndiye anayefanya kazi kubwa kuliko watu wengine wowote. Sisi leo tuko hapa Bungeni tumewaacha Madiwani wetu kwenye kata zetu, ndio wanafanya kazi hizo zote. Sasa, ukija kwenye posho zao, Diwani mshahara wa shilingi 350,000, hana uwezo hata wa kukopeshwa pikipiki.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ninaomba sana, Mheshimiwa Waziri Mkuu yeye ndiye msimamizi, alione hili kupitia TAMISEMI ili Madiwani wetu waweze kuboreshewa stahiki zao, na hatimaye nao waweze kuwa ni watu ambao wanafanya kazi kwa niaba yetu na kwa niaba ya Mheshimiwa Rais ya kuendelea kusukuma maendeleo kwenye maeneo yatu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana kwa muda wako na Mungu akubariki sana.