Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Jackson Gedion Kiswaga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kalenga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia asubuhi ya leo. Nianze kwa kumpongeza Waziri Mkuu kwa hotuba yake nzuri ambayo kwa kweli ime-cover maeneo mengi muhimu na ina mambo mengi mazuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaipongeza pia Serikali kwa namna ambavyo imeendelea kukuza uchumi. Katika taarifa yake imeonesha pato la Taifa limeendelea kukua kwa asilimia sita lakini mfumuko wa bei uko kwenye asilimia tatu nukta tano ambao uko kati ya ule wigo wa tatu mpaka tano. Vilevile, tumeona mapato ya fedha ya kigeni yameongezeka kwa takribani dola bilioni mbili kwa mwaka, ni kazi kubwa anayoifanya. Ndiyo maana mambo haya yanaleta attention. Ukuaji wa nchi hii uchumi wake unaleta tension sana kwa majirani.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninarudia kusema kile alichosema Shigeki Komatsubara ambaye alisema kwamba: “Ikiwa uchumi wa Tanzania utaendelea kukua kwa mwendo huu wa asilimia sita nukta sita sita tano saba na kuendelea, ndani ya miaka 10 ijayo Tanzania itakuwa ni nchi yenye uchumi mkubwa Afrika Mashariki kuliko uchumi mwingine wowote.” Kwa hiyo, taarifa hizi zinawashtua sana majirani.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama wenzangu walivyompongeza Waziri Mkuu kwa ziara zake za kuwasikiliza wananchi, kwa kweli na sisi wadogo zake tulio nyuma yake tuna mambo mengi ya kujifunza na kuendelea kufuata anachofanya kwa maana inaleta harmony kwenye Taifa na amani.

Mheshimiwa Naibu Spika na Ndugu zangu Watanzania, uchumi huu ambao tumeona sasa unakua vizuri utaendelea kukua endapo mambo mawili yatazingatiwa: kwanza, tuendelee kutunza amani yetu, na lakini utulivu wa kisiasa, huo ni wajibu ambao sisi Watanzania tunao, hakuna mwingine zaidi ya kwetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeona maneno mengi kwenye mitandao kuhusiana na bei za mafuta. Ndugu zangu Watanzania kwanza mkubali kabisa kwamba sisi kama nchi, Serikali yetu imeongeza bei za mafuta kidogo ukilinganisha na namna majirani walivyoongeza. Nilikuwa ninaangalia wenzetu hapo jirani Kenya, kwa mfano, Petroli wameongeza bei kwa sasa inafika shilingi 5,450, lakini ukiangalia Diesel ni shilingi 5,056 hivi, na mafuta ya taa ni shilingi 4,400.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninataka niwaambie Watanzania, nisiwape maneno ya faraja sana, ni kwamba mafuta haya inaonekana yataendelea kuongezeka ikiwa ule mfereji wa Hormuz hautafunguliwa. Wenzetu wa Ulaya wamesema hata kama vita itaisha leo, madhara yaliyojitokeza yanaweza kuendelea kwa muda mrefu, ndiyo maana wamewaambia wananchi wao (Umoja wa Ulaya) kwamba wengi wafanye kazi kutokea nyumbani na watumie zaidi magari ya umma kuliko magari yao binafsi ili kupunguza matumizi ya mafuta kwa sababu kuna uchache wa mafuta. Kwa hiyo, Watanzania wenzangu mambo ya mitandao myapuuze hayana maana.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inafikiria mambo mengi. Tumekaa na wenzetu wa Serikali, wanaangalia uwezekano kama hali ikiwa mbaya zaidi pengine mahali fulani waangalie kama wanaweza kuweka ruzuku, lakini nyongeza tuliyoongeza ni kidogo kwa hiyo, tupunguze mihemko tukabiliane na hali iliyotokea duniani, tuache haya mambo ya mitandao hayana sababu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kuishukuru sana Serikali kwa kupitia Waziri Mkuu kwa tamko lake la kusema fedha zinazokusanywa (shilingi 50) za mafuta kwa ajili ya Mfuko wa Barabara zitoke TRA kwenda moja kwa moja kwenye Mfuko wa Barabara. Ni jambo la kimapinduzi na ninatambua kwamba Waziri Mkuu asingesema mambo hayo bila kushauriana na mamlaka. Hivyo, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa hayo maelekezo, tunaomba yatekelezwe ili tuweze kufanya marekebisho ya barabara nyingi ambazo zimeharibika kutokana na neema ya mvua.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata mimi kwenye Jimbo la Kalenga ninazo Barabara maarufu kama Kalenga – Uwasa - Ulanda kwenda Magulilwa zimeharibika na sehemu nyingi hazipitiki, lakini niwaombe Watanzania wenzangu na Wanakalenga wenzangu kwamba tuwe na subira, ipo mipango madhubuti ya kuhakikisha kwamba mambo haya yanakwenda vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, niipongeze vile vile Serikali, ilifanya ukarabati wa shule kongwe pamoja na Shule yangu ya Tosamaganga ambayo mwezi Oktoba tutasherehekea miaka 100 ya kuwepo kwake. Zaidi ya shilingi bilioni tatu zimekwenda pale, lakini kuna majengo ambayo hayakumalizika. Ninaiomba Serikali, kwa kuwa ilianza kufanya kazi nzuri, basi iendelee na ukarabati wa shule kongwe tumalizie Shule yetu ya Tosamaganga, mwezi Oktoba tuwakaribishe na wote mliosoma Tosamaganga tutasherehekea miaka 100 pale, mje ili tuweze kusherehekea namna ile shule ilivyotoa viongozi wengi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ninaiomba Serikali, lile eneo lililobakia iweze kulimalizia, lakini pia na shule nyingine za msingi ambazo zimejengwa miaka ya 1960, 1970 na 1980 nyingi ziko katika hali mbaya. Tunaipongeza Serikali, inajenga shule nyingi nzuri, lakini mwaka huu tuone namna gani wataweka baadhi ya fedha kwenda kukarabati shule kongwe pamoja na Kijijini kwangu kule Nyamihuu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la upimaji wa ardhi limekuwa likiongelewa muda mrefu na wenzetu wa ardhi. Ndugu zangu mlioko ardhi mnapenda sana Serikali iwape fedha, ni jambo zuri, lakini kule kwenye sekta binafsi kuna kitu tunaita ROI (Return On Investment); kule kwenye sekta binafsi unaweza ukaomba, unapewa ilimradi unaihakikishia kampuni kwamba, hiki unachoomba utakirudisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye eneo la viwanja, pamoja na kuwa wanaomba fedha nyingi, ninaunga mkono, lakini ni lazima walete mkakati wa kuona namna gani Serikali inapata fedha kutoka kwenye viwanja.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza madeni mengi sana hayajakusanywa katika mwaka huu wa bajeti ambao tunakwenda nao. Lazima mkakati wa kuisaidia Serikali kukusanya fedha, ili zisaidie kwenye masuala ya maendeleo uoneshwe wazi na sisi tutawaunga mkono, ili Serikali iwape hiyo fedha nchi iendelee kupimwa, lakini at the same time ikusanye kodi kwa ajili ya masuala ya maendeleo. Misaada mingi imepungua, kwa hiyo, tunategemea sisi wenyewe tuongeze vipato vyetu na eneo hili la viwanja naomba tuliangalie kwa mapana yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo nchi tunatakiwa tuwekeze kwa nguvu kubwa ni eneo la utalii. Nchi yetu utalii unakua, kama ambavyo tumeona na tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa namna alivyoutangaza. Zile filamu alizotengeneza zimeleta matokeo makubwa, lakini kuna changamoto kubwa ya utoaji wa huduma katika nchi hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, watalii wengi wanalalamika, utoaji wetu wa huduma ni mbaya, hata ukienda kwenye hoteli. Wewe angalia, nenda kwenye hoteli ya kitalii, mtu atakuletea chakula, akishakuletea chakula anaenda kukaa jikoni. Jana nilikuwa hoteli moja hapa, nimekula, nimeletewa bili, hakuna Waiter, nikaamua kulipa tu kwa njia ya mtandao nikaondoka, nimekaa pale ninasubiri.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa huu ni mfano tu wa namna gani huduma zetu ni mbovu. Serikali ina wajibu wa kusimamia ubora wa huduma ambazo tunatoa kwenye hili eneo la utalii. Nimetokea kwenye utalii miaka ya nyuma na ninafahamu vizuri tu mambo ya utalii yanavyokwenda. Ikiwezekana Serikali iwe na timu ya kwenda kukagua, kuona aina ya elimu tunayotoa kwenye vyuo vyetu. Maana tukipunguza madini, eneo pekee ambalo litaendelea kwa muda mrefu ni eneo la utalii.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, huduma zetu ziangaliwe na kama wataunda hiyo timu ya kwenda kuangalia maboresho, namna gani tunaboresha huduma za kiutalii lazima waniweke kwa sababu, enzi ninafanya kazi huko, nilikuwa mmoja wa wafanyakazi bora sana kwenye eneo hilo. Kwa hiyo, hilo ni jambo la kutazama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye suala la mifugo, Tanzania tunaweza kunufaika sana na biashara ya kuuza mifugo yetu nje. Sasa hivi magonjwa mengi sana yameibuka. Ukiangalia South Africa tayari wamefungiwa kuuza nyama nje, na hapa Tanzania tayari kuna magonjwa kadhaa yamejitokeza kwenye mifugo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa, Serikali yenyewe ilisema ndiyo itakayoratibu masuala ya chanjo, tunaomba iweke projection ya kuona chanjo zinachanjwa kila baada ya miezi mingapi na kuwa na stock ya chanjo ambayo inaweza kutupeleka angalau miezi sita, ili tuhakikishe kwanza mifugo yetu haifi, mifugo yetu ina afya na tunatumia fursa ya vita inayoendelea huko kuwauzia nyama.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaweza tukakuza uchumi wetu katika eneo hilo kwa haraka endapo masuala haya ya chanjo yatazingatiwa. Tusiwe na kurukaruka, Serikali ihakikishe inawekeza fedha hapo na itaona return on investment katika fedha ambazo wameziweka.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali tunaipongeza, imekuwa na mikakati ya kuendelea kujenga vituo vya afya katika maeneo mbalimbali. Mwaka 2025 tulikuwa na vituo vya kimkakati, kama 186 hivi, lakini kwa sababu ya masuala mbalimbali Serikali imeweza kupeleka fedha ya vituo kama 90 au 93 na mimi chief nimekosa katika vile vituo vya kimkakati. Ninafahamu hatuwezi kujenga vituo vya afya kila mahali kwa sababu, kwanza itaongeza bili za Serikali, kata nyingine ziko karibu karibu, lakini vile ambavyo tunaona kabisa kata hizi ziko mbali, ziko porini kama kata yangu ya Kihanga, ni muhimu sana Serikali kwa kadiri inavyopata fedha iendelee kutuwezesha, ili wananchi waendelee kupata hii huduma ya afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho ninawapongeza sana kwa kuanza ile huduma ya Bima ya Afya kwa Wote. Ahsante sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)