Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. HAWA M. CHAKOMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia hotuba iliyo mbele yetu ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Nianze kwa kumshukuru Mungu kwa kuniwezesha kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu na kuchangia hotuba iliyopo mbele yetu. Pia, ninapenda sana kukushukuru wewe Mheshimiwa Naibu Spika kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia.
Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, ninapenda kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Rais Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo anafanya uwezeshaji wa kiuchumi kwa wananchi wa Taifa hili, lakini pia, anavyoendelea kustawisha maendeleo endelevu kwa wananchi wa Taifa lake la Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niruhusu pia nimpongeze Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba, Waziri wetu Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya kumsaidia Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunampongeza sana pia Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa ziara zake anazofanya za mkoa kwa mkoa, jimbo kwa jimbo, halmashauri kwa halmashauri, wilaya kwa wilaya na kata kwa kata. Hakika Mheshimiwa Waziri Mkuu anaitendea haki ile hotuba yake katika ukurasa wa 99 alipozungumzia mfumo wa uratibu wa malalamiko ya wananchi, hakika mfumo huu unaenda kufikiwa kwa 100%. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninapenda kumpongeza pia Spika wetu wa Bunge, Mheshimiwa Azzan Zungu, kwa kazi nzuri anayoifanya. Kama vile ambavyo alituahidi Waheshimiwa Wabunge, atafanya kazi ya speed and standard. Sisi tumeona kazi nzuri. Ukiangalia tu mic alizozileta ni mambo ya kisasa kabisa wala huhitaji kuisogelea wala kutumia nguvu kubwa. Sauti ndogo, mic inachuja, inaenea katika ukumbi mzima. Hivyo, tunampongeza sana kwa ubunifu huu mzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niruhusu sasa nianze kuchangia hotuba hii ya Waziri Mkuu na nianze na upande wa ustawi na maendeleo ya jamii na hasa nitapenda kuzungumzia ustawi wa wastaafu wetu nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninapenda sana kumpongeza Mheshimiwa Rais, kwani kwa makusudi ameamua kuboresha kiwango cha chini cha pension cha mwezi kutoka shilingi 100,000 na kufika shilingi 250,000. Hii ni kwa upande wa wastaafu wanaolipwa na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kwa utumishi wa umma.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwani ameangalia hali ya sasa, ameangalia mfumuko wa bei. Ni wazi kabisa kiasi cha shilingi 100,000 hakiwezi kukidhi, hivyo kimeongezeka mpaka kufikia kiasi cha shilingi 250,000/=. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kwa upande wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ya sekta binafsi na yenyewe kima hiki cha chini kimeongezeka kulingana na sekta zilivyo. Sambamba na hilo, suala hili la kustawisha wastaafu wetu, Mheshimiwa Rais kupitia Mifuko yetu ya Hifadhi ya Jamii, ni kwa makusudi sasa ameamua wastaafu wetu ile nenda rudi kufuatilia pension yao imepunguzwa ama imeondoka, kwa sasa ni siku 30 tu.
Mheshimiwa Naibu Spika, tarehe 25 ya mwisho wa mwezi, wastaafu hawa kama wamekamilisha vigezo vyote, basi wanakuwa wanastahiki kupewa mafao yao. Hivyo, tunamshukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nimeshatangulia kusema, Mifuko yetu ya Hifadhi ya Jamii inafanya kazi kubwa na kazi nzuri nchini. Wote tutakubaliana majukumu yake makuu ni kuingiza wanachama, kulipa mafao, na suala zima la uwekezaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mifuko yetu ya Hifadhi ya Jamii imekuwa ikiwekeza katika miradi mbalimbali ikiwemo Mradi wa Kiwanda cha Sukari Mkulazi na miradi mingine inayofanania na huo ambayo imekuwa iki-create ajira kwa wananchi, na pia imekuwa ikifanya mambo makubwa kwa Taifa letu la Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, hapa nitakuwa na ombi kwamba mifuko hii imekuwa ina madai. Inaidai Serikali kwa namna ya kugharamia miradi mbalimbali ya Kiserikali. Mathalani, katika Mfuko wetu wa NSSF unaidai Serikali takribani shilingi bilioni 951.29. Hizi fedha zikijumlishwa ndani yake kuna riba ya shilingi bilioni 757.97.
Mheshimiwa Naibu Spika, hizi fedha zisipolipwa kwa wakati, ndiyo zinakuwa zikitengeneza deni kubwa, lakini zimekuwa zikitengeneza riba kubwa kwa Watanzania. Tunamshukuru Mheshimiwa Rais, ameshaanza kuzilipa hizi fedha kwa kupitia hatifungani, tayari ameshalipa shilingi bilioni 433.71, lakini kiasi kilichobaki ni kikubwa, kama hakijalipwa kwa wakati, kitaendelea kutengeneza riba na deni kubwa. Itafika mahali itakuwa halilipiki. Kwa hiyo, tunaiomba sana Serikali iangalie namna bora ya kuendelea kupunguza madeni haya ili kuweza kuondokana na riba.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Mfuko wetu wa PSSSF na wenyewe umekuwa ukiidai Benki ya TIB shilingi bilioni 120. Tunaiomba sana Serikali kupitia Benki ya TIB kuhakikisha inaulipa Mfuko huu ili uweze kuendelea na majukumu yake ya msingi ya kuingiza wanachama, kulipa mafao na kufanya uwekezaji, ili hata zile actuarial valuation zikija kufanyika, basi Mifuko yetu iwe himilivu katika miaka inayokuja kuweza kulipa wastaafu wengi, pasipo kuwafanya wawe wanaenda na kurudi katika ofisi hizi za mifuko hifadhi ya jamii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa Mfuko wetu wa Fidia Kazini, tulikuwa tunaomba, ninadhani wakati umefika sasa Askari Polisi na wenyewe waweze kuingia katika Mfuko huu wa Fidia Kazini. Ukiangalia nature ya kazi yao, kuumia kazini ni rahisi na kupata majanga kazini ni rahisi. Kwa hiyo, ninaiomba Serikali ifikirie upya kuingiza Jeshi letu la Polisi, kwa upande wa maaskari katika Mfuko wa Fidia Kazini ili wanapopatwa na majanga wanapokuwa katika maeneo ya kazi, ili Mfuko huu uweze kuwagharamia na kuwasaidia kwa namna moja au nyingine. Hivi ndivyo ambavyo tunafanya Mifuko yetu iweze kuwa imara na thabiti kuendelea kulipa mafao haya ya utengemao kwa watumishi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho nitapenda kumalizia na Fungu 15 ya Wizara ya Kazi, Ajira na Mahusiano, Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA). Ninapenda sana kuipongeza Serikali kwa dhamira yake ya dhati, imeamua makusudi fedha zilizotengwa kwa mwaka 2025/2026 za upande wa maendeleo kiasi cha shilingi 276,046,000 kuzitoa zote kwa 100%. Tunaipongeza sana Serikali kwa kuamua kuzitoa fedha hizi. Fedha hizi zimeenda kufanya kazi nzuri kabisa ya kuanzisha ama kutengeneza Mfumo wa e-UTATUZI. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mfumo huu umekuwa ni mwarobaini wa migogoro iliyopo kati ya wafanyakazi au mwajiri na mwajiriwa. Miaka ya nyuma watumishi walikuwa wana kila sababu ya kusafiri umbali mrefu kufika katika ofisi za kazi kwa ajili ya kupeleka migogoro yao baina ya wafanyakazi pamoja na waajiri, jambo ambalo limekuwa likipunguza tija ya kuzalisha uchumi wa Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa tutakubaliana sote migomo na maandamano nchini imepungua kwa sababu ya kazi nzuri inayofanywa na Mheshimiwa Dkt. Rais Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)