Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mlalo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa nafasi hii kuwa mzungumzaji kwenye siku hii ya pili ya Hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Awali ya yote ninampongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa wasilisho lake ambalo limekuwa na takribani masaa mawili na nusu, ameweza kusimama hapo mbele, lakini ambalo limegusa maeneo mengi ya kimkakati na ambayo yanagusa jamii ya Watanzania kwa mapana.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, pia nimpongeze kwa kazi kubwa anayoendelea kuifanya katika maeneo mbalimbali hapa nchini kwetu. Kipekee, kwa ziara ambazo ameendelea kuzifanya katika mikoa mbalimbali, sisi Tanga pia tunashukuru, ni miongoni mwa mikoa ambayo ametufikia, na kwa kweli tunaridhika, na wema wake tumeuona, kwa sababu sasa mambo yanakwenda vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, ninawapongeza wasaidizi wake wote, Waheshimiwa Mawaziri; Mheshimiwa Prof. Shemdoe, pia ndugu yangu Waziri anayehusika na mambo ya mahusiano, Mheshimiwa Sangu na watendaji wote katika Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na idara zake zote.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitaanza na eneo ambalo ningependa kushauri. Kule katika awamu zilizopita, tumekuwa na program mbalimbali ambazo zinaratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu, lakini kadiri zile programu zilivyokuwa zinamaliza muda wake, tulikuwa hatuoni maendeleo na baadhi ya programu kwa kweli zilifanya kazi nzuri sana ambayo huenda tungeziboresha baada ya kumaliza muda, zingetupa tija kubwa zaidi ambayo leo tusingekuwa na matatizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, tulikuwa na mpango ule wa MKURABITA, Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara Tanzania, ulikuwa ni mpango mzuri sana umefanya kazi nzuri sana hasa kwenye sekta ya ardhi ambapo ulikuwa na jambo mahususi la kutoa hatiardhi za kimila katika maeneo mbalimbali. Sasa nishauri, kama Serikali itaona inafaa, basi ni vema ili uratibu huu ukaendelea kuongeza kasi ya utoaji hati za ardhi, hasa hati za kimila katika maeneo vijijini ambapo ndiyo kwenye shida kubwa sana ya migogoro ya ardhi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna programu nyingine ya ASDP ambayo imefika ASDP II; Agricultural Sector Development Program, hii ilikuwa imekusanya sekta zote, kwa maana hata barabara za vijijini, TARURA na usambazaji wa huduma vijijini.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia programu mbalimbali zinazohusu masoko vijijini zilikuwa ziko katika uratibu wa ASDP. Sasa tunaziona Wizara zikifanya program zake zenyewe, hakuna mafungamanisho na Ofisi ya Waziri Mkuu. Tunaoomba hili nalo liweze kuangaliwa upya na kuweza kuona namna ya kuzi-consolidate na kuziweka pamoja ili usimamizi uweze kuwa rahisi.
Mheshimiwa Naibu Spika, tatu, ni programu ya MIVARUF ilikuwa ni Marketing, Infrastructure, Value Additional, Rural Finance, na yenyewe ilikuwa inakwenda kuongeza mazao thamani kule vijijini. Tunatoa mazao mashambani, tunayapeleka kwenye masoko, tunaongeza thamani. Walianza na programu ya kujenga post-harvest centers na pia ku-control post-harvest loss. Yale majengo yapo, yamebaki, hakuna msimamizi, kwa sababu tumeondoa utaratibu mzima wa kusimamia miradi hii kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba sana programu hizi, Serikali izitazamie upya na Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana ya Mipango na Uwekezaji kwenye dira, hili ni jambo ambalo tungelitazama kwa mapana marefu, ninaamini kuwa litakuwa na mchango mkubwa sana kwa Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, sasa nirejee kule Jimboni Mlalo kwa mambo ambayo nimetumwa na wananchi wa Mlalo. Kwanza wananchi wa Mlalo wanamshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu. Alipokuja, alitoa maelekezo ya kusanifu barabara ya kutoka Lushoto kwenda Mlalo kilomita 36. Tunatambua kazi imeanza katika hatua za awali, lakini tunataka kasi iongezeke.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, kuna barabara ya kutoka Lushoto kwenda Lukozi, kwenda mpaka Mtahe pia kutoka Malindi kwenda Belei kwenda mpaka Mtahe na yenyewe tunaomba iingie katika mpango wa usanifu ili sambamba na barabara ile ya Umba Junction kwenda Mkomazi na Mabokweni kwenda Tanga, barabara zote hizi ziweze kufungua Jimbo la Mlalo na Halmashauri ya Lushoto kwa ujumla.
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi Lushoto tunasema barabara ndiyo kipaumbele chetu namba moja. Tunaporudia kipaumbele chetu namba mbili, ni barabara; na namba tatu ni barabara, kwa sababu sisi tunapata bidhaa mbalimbali kutoka maeneo mengine kwa gharama kubwa, kwa kuwa barabara zetu hazina uwezo wa magari makubwa yanayobeba tani nyingi kuweza kuingia katika Halmashari ya Lushoto na Wilaya ya Lushoto kwa ujumla.
Mheshimiwa Naibu Spika, mathalani, tunalo Shamba la Miti Shume ambalo tunazalisha miti na tunauza mazao ya miti katika maeneo mengine, lakini tunashindwa kushindana na soko la mbao zinazotoka Mafinga, kwa sababu tu ya gharama kubwa za usafiri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hata mtu ambaye ananunua mazao ya mbao kutoka Lushoto ambaye yuko Korogwe anapata kwa bei kubwa zaidi kuliko akiagiza kutoka Mafinga. Sababu ni kwamba magari yanayokuja kubeba mazao ya mbao, mwisho ni tani saba. Kwa hiyo, tungetamani sana barabara hizi tunapozungumza, ziboreshwe, ziwe pana ili magari makubwa (semi-trailers na truck and trailers) ziweze kupanda katika milima hii ya Usambara.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, mazao yetu yanaharibika kwa haraka sana kwa sababu sisi ni wakulima wa mbogamboga tunahitaji barabara ambazo zinapitika kwa mwaka mzima ili wananchi wetu wasiendelee kupata hasara.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili ni eneo la wanyamapori. Ninamshukuru sana Waziri wa Maliasili, alikuja, alifanya kazi kubwa angalau kusaidia kufukuza wanyamapori ambao walikuwa wanaharibu. Hata hivyo, tunazo ekari zaidi ya 5,266 zilizoharibiwa vibaya na uhakiki umeshafanyika, lakini wananchi wale bado hawajalipwa fedha zao za kifuta jasho.
Mheshimiwa Naibu Spika, tarehe 5 Aprili, 2025 na tarehe 17 Disemba, 2025 tathmini imeshafanyika, tunadai zaidi ya shilingi milioni 630 ambazo Wizara ya Maliasili inatakiwa iwafidie wananchi wa Halmashauri hii ya Lushoto hususan Jimbo la Mlalo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye hili hili eneo, wapo wananchi wamefariki. Pale kwenye kijiji cha Kikumbi kuna mwananchi anaitwa Samweli Saiko, tarehe 17 Juni, 2025 Kijiji cha Mkundi Mtae, alifariki; tarehe 29 Aprili, 2025 amefariki Yakobo Lombia; tarehe 11 Januari, 2026 Robert Nyalando Kijiji cha Lunguza alifariki; na tarehe 16 Machi, 2026 kuna mama anaitwa Fatuma Athumani katika Kitongoji cha Ngwalo alivamiwa na tembo.
Mheshimiwa Naibu Spika, hawa niliowataja mwanzo wamefariki na mpaka leo fidia zao hazijalipwa. Tunaomba sana jukumu hili Serikali ilitimize. Wamesema tuwalinde, sisi tunakubali, tunaendelea kuwalinda, lakini wanatudhuru. Sasa wakati wanatudhuru na wao wasituache peke yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ni sekta ya elimu. Hapa kwenye sekta ya elimu, sisi Wilaya ya Lushoto na Halmashauri ya Lushoto, ambayo pia ina majimbo mawili pamoja na Jimbo la Mheshimiwa Profesa Riziki Shemdoe, tuna shule 187 za msingi. Kati ya hizo, 179 ni za Serikali, lakini tuna upungufu ama uhaba mkubwa sana wa walimu. Walimu ambao wanahitajika ni 2,382, waliopo ni 1,272. Tuna uhaba wa walimu 1,110 sawa na 46.5% ya upungufu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Lushoto jiografia yake ina changamoto, kwamba walimu na watumishi wengi hawavutiwi kuja kufanya kazi kule, lakini wapo walimu katika maeneo mbalimbali wanaotoka Wilaya ya Lushoto. Ningetamani Mheshimiwa Profesa Shemdoe, hili kwa sababu yuko ndani ya Wizara hii, turatibu wale ambao wako tayari kuja kufanya kazi katika mazingira ya Lushoto, tuwape uhamisho kwa urahisi waweze kurudi kwenda kuwatumikia ndugu zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, inasikitisha sana kwamba Watanzania wengine hawataki kuja kufanya kazi Lushoto. Sasa kama wanataka watufanye sisi tuwe kisiwa, sisi tuko tayari. Kwa hiyo, na wale ndugu zetu wa Lushoto walioko maeneo mengine, wanaotaka kurudi nyumbani kuja kutoa mchango wao kwa Taifa hili, sisi tuwe na urahisi wa kuwaruhusu kuhama, kuja kuwatumikia Watanzania wengine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, lakini siyo kwa umuhimu ni kilimo. Sisi Mkoa wa Tanga tunalo zao letu la kimkakati ambalo ni la mkonge. Kwa masikitiko makubwa, ndiyo zao la kimkakati pekee ambalo mpaka sasa halina ruzuku. Ukifika kwenye korosho kuna ruzuku.
Mheshimiwa Chongolo ninaomba unisikilize kwa makini. Kwenye korosho kuna ruzuku, kwenye pamba kuna ruzuku, na mazao mengine ya kimkakati, lakini mkonge hauna ruzuku yoyote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hili ni zao ambao tunatakiwa tuliwekee ruzuku ili wananchi hata wakipato cha chini waweze kulima zao hili ambalo ni dhahabu ya kijani na tunaamini kwamba litakuwa na mchango mkubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, kule Lushoto tunalima sana mbogamboga na bei ya mbegu ya mbogamboga ni ghali sana, na bei ya pembejeo ni ghali sana. Ninaomba na lenyewe litazamwe kwa upekee tu kwa Lushoto peke yake, tupate ruzuku katika kilimo cha mbogamboga hasa kwenye mbegu pamoja na viuatilifu vingine. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana kwa nafasi.