Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Anna Richard Lupembe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nsimbo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa fursa hii ya kuweza kuchangia.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa ninaomba nimshukuru Mungu ambaye ameendelea kututetea na kutulinda leo ni tarehe Mosi Aprili tuko mahali hapa. Ninaomba nimpongeze sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa ambayo anaendelea kwa ajili ya kuwatumikia Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kipekee sana ninaomba nimpongeze Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mwigulu Nchemba kwa kazi kubwa ambayo anaifanya kwa Watanzania, ameleta imani kubwa kwa Watanzania kwa ajili ya Serikali yao, hongera sana Mheshimiwa Waziri Mkuu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba niwapongeze Waziri wa TAMISEMI pamoja na Naibu Mawaziri wake wote wawili, Naibu Waziri wa Afya pamoja na Naibu Waziri wa Elimu. Pia ninaomba nimpongeze Mkuu wangu wa Mkoa, Mwanamvua Mrindoko kwa kazi kubwa ya usimamizi wa shughuli zote za Mkoa wetu wa Katavi. Ninaomba nimpongeze Mkuu wetu wa Wilaya, Mheshimiwa Jamila Yusuf ambaye anasimamia maendeleo yetu na mipango yote ya Wilaya yetu ya Mpanda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nimpongeze Chief wa TARURA Ndugu yetu Engineer Victor H. Seff kwa kazi kubwa na usimamizi wa barabara zetu katika maeneo yetu ya vijijini, lakini ninawapongeza mainjinia wetu wa Mkoa wetu wa Katavi pamoja na mainjinia wa Wilaya yetu ya Mpanda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kila mtu atasimama hapa kwa ajili ya TARURA. Kwa Wabunge wa vijijini TARURA ni chombo muhimu sana. Nimesimama hapa tukiomba pesa za dharura kwa sababu hali imekuwa ngumu, madaraja, barabara zimekatika, vijito vyote vinatoa maji, chemchemi zimeibuka barabara hazipitiki. Maeneo ya vijijini tunaomba Serikali kwa unyenyekevu mkubwa, tunajua wametoa na wameongeza bajeti, lakini kwa kipindi hiki cha Mwenyezi Mungu ameleta neema kubwa ya mvua katika nchi yetu ya Tanzania, tunapokea neema hiyo kubwa, lakini kwenye neema hiyo kuna changamoto ambazo zimetokea, lazima tuzipokee tuzikubali. Tunaomba kwa sababu uharibifu umekuwa mkubwa, tunaiomba Serikali yetu kwa unyenyekevu itoe pesa za dharura. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninavyoongea kuna maeneo yangu, watoto sasa hivi hawaendi kabisa shule. Kumegawanyika kabisa hawaendi shuleni. Ninaomba Serikali yangu sikivu, tupewe pesa za dharura. TARURA wapewe pesa za dharura ili waweze kwenda kurekebisha barabara za muhimu ili watoto warejee katika maeneo yao ya shule. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, TARURA kwa vijijini ndiyo kiungo chetu kikubwa kwa uchumi. TARURA imefanya kazi kubwa sana, imetujengea madaraja, imetengeneza barabara vizuri sana, imewafikia wananchi kijiji kwa kijiji, kitongoji kwa kitongoji. Ninaomba niipongeze Serikali kwa kuiongezea bajeti TARURA, kwa sababu Wabunge wengi kilio chetu TARURA wakipata pesa wakiwa na bajeti nzuri watatengeneza barabara za vijijini kwa uhakika zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba niipongeze Serikali yangu kwa kuongeza bajeti ya TARURA kwa sababu tunajua sasa barabara zitakuwa nzuri, barabara zitatengenezwa, madaraja yatajengwa na wananchi wa vijijini wataongeza uchumi wao kwa sababu mazao yote tunayatoa vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nishukuru upande wa afya. Nimeletewa katika siku 100 za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, nimeletewa pesa za kituo cha afya, nimeletewa pesa kwenye shule za msingi na sekondari. Ninaomba niipongeze sana Serikali kwa kazi kubwa nzuri inayoendelea kuifanya katika nchi yetu. Watoto wanakwenda shule, watoto sasa hivi wanajivunia Serikali yao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa unyenyekevu ninaomba vituo vya afya, lakini katika hospitali yangu ya Halmashauri ya Nsimbo, nimejengewa hospitali nzuri ina kila kitu, nimejengewa theater kwa ajili ya akinamama wajawazito, lakini bado ninaomba kwa unyenyekevu nijengewe theater kubwa ya ujumla kwa ajili ya wagonjwa wote ili niweze kukidhi mahitaji ya hospitali yangu ya Wilaya yangu ya Nsimbo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kazi kubwa inafanyika kwenye vituo vya afya, zahanati, pamoja na shule ya msingi, pamoja na sekondari, lakini kuna miradi mbalimbali ambayo Waziri Mkuu tunaomba tumpongeze, amesisitiza sana kuwa shule zote zihakikishe zimejengwa vyoo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wabunge wenzangu waliopita na tunaomba tupongeze taasisi ambayo inasimamia PPRA, mpango mzuri unaoendelea katika nchi yetu kwa kuendelea kusimamia ununuzi lakini bado kuna tatizo. Hili tatizo changamoto tunaomba basi kwenye upande wa NeST, kuna vijiji ambavyo sasa hivi vina pesa lakini hawajui wafanye nini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunawaomba PPRA watoke kwa sababu huu mpango ni mzuri, tumeweza kuboresha mambo mengi na mafanikio makubwa, watoke sasa waende kwenye halmashauri zetu, kwa sababu Wenyeviti wa Vijiji, Watendaji wa Vijiji, wanagoma kutoa zile pesa na wakienda kwenye halmashauri zetu wanasumbuliwa njoo kesho, kesho mfumo haufanyi kazi, hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tulikuwa tunaomba basi PPRA sasa wachukue jukumu la kuwapatia semina Watendaji wa Vijiji, Watendaji wa Kata, ili waweze kuelewa jinsi ya mfumo unavyoenda kwa sababu pesa nyingi zinakwenda katika maeneo yetu ya vijiji. Sasa unakuta vijijini kule hela zote zimekaa zimeganda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba tumshukuru Waziri Mkuu alivyosema kuwa apate tathmini ya miradi yote iliyokwama ili waweze kujua watafanya nini, lakini ninaomba niishauri Serikali, PPRA sasa watoke waende wakatufanyie semina kwenye halmashauri zetu, kwa Watendaji wa Vijiji na wa Kata ili waweze kuelewa jinsi gani ya kuweza kuingia kwenye mfumo wa NeST. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye 10% ninaipongeza Serikali yangu kwa kazi kubwa nzuri, 10% Halmashauri zetu wanatoa, lakini kuna changamoto kwa upande wa walemavu. Ninaomba niishauri Serikali, hatuwezi kumpata mlemavu mmoja au kundi la walemavu katika eneo moja, ninaomba nishauri kwamba akipatikana mlemavu mmoja katika maeneo apewe huyo huyo mmoja katika eneo hilo ili ufanisi na yale malengo ya 10% yaweze kutimilika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunajua Rais ametoa ajira, tunaomba tushukuru tumepata ajira katika maeneo yetu, lakini bado kuna changamoto ya ajira, tunao upungufu, tunaiomba Serikali yetu iendelee kuajiri ili katika meneo yetu, vituo vya afya, zahanati, shule za msingi na sekondari tuweze kupata watumishi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nikushukuru sana, ninaendelea kumpongeza Rais kwa kazi kubwa ambayo anaendelea nayo. Vilevile Waziri Mkuu wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba tutaendelea kumwombea ili Mungu asimame naye kwa kazi hii kubwa ngumu aliyoibeba, kuhakikisha Watanzania wanapata amani na utulivu kwa Serikali yao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kuunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)