Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Dr. Wilson Charles Mahera

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Butiama

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. DKT. WILSON C. MAHERA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Ninaanza kushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika Bunge la Bajeti, kama mtu wa tatu. Nikiwa natokea Jimbo la Butiama naomba kwanza nianze kwa kumpongeza Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuendelea kutupatia dira ambayo inatuwezesha kulipeleka Taifa hili katika Dira ile ya Mwaka 2050. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninampongeza Waziri Mkuu kwa utendaji kazi wake mzuri, viongozi wote wa Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI na wasaidizi wao pamoja na Katibu Mkuu. Ukiangalia Hotuba ya Waziri Mkuu, ya leo kwa kweli, ina mikakati mizuri ya kutuonesha kwamba tunakwenda kuitekeleza Dira hii ya Mwaka 2050 na hasa mpango wa maendeleo wa miaka minne ambao tayari dhima yake ni kukuza uchumi na kuzalisha ajira. Lengo kwa kweli, ni itakapofika Mwaka 2050 tuwe na Taifa la watu ambao wanajitegemea kwa hiyo, mambo mengi ya msingi yameelekezwa hapa.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumpongeza pia, Rais kwa mambo yafuatayo; ukiangalia katika bajeti ya leo, hasa kipaumbele kinatolewa katika kuimarisha barabara za mijini na vijijini. Kwa hili pia, ninachukua nafasi hii kumpongeza Waziri Mkuu kwa kuielekeza Wizara ya Fedha kuimarisha upatikanaji wa fedha za Mfuko wa Barabara na kuelekeza zipelekwe moja kwa moja. Kwa hili ninaungana na Wabunge wenzangu waliotangulia kwamba, sasa angalau ile 30% ambayo ilikuwa inakwenda tena TANROADS halafu ndiyo ipelekwe TARURA sasa itaenda moja kwa moja TARURA na itawezesha utekelezaji wa barabara za TARURA kufanyika kwa umakini wa hali ya juu sana, kwa sababu, tatizo la TARURA, kama walivyosema watangulizi siyo kwamba, wana upungufu wa fedha bali fedha zilikuwa haziendi.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaamini sasa kwa agizo hili kwa kweli, mambo yatakwenda kuwa mazuri zaidi na hii tumeona kabisa hata katika Hotuba ya Mheshimiwa Waziri. Leo kuna baadhi ya barabara za kimkakati zinakwenda kujengwa, hasa barabara za kwenye majimbo, pamoja na madaraja yale 13 ikiwemo ile Barabara ya Suguti, Mkoa wa Mara kwa hiyo, ninapenda kuipongeza sana Serikali kwa hatua hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninapenda pia,kuipongeza Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuunganisha Mkongo wa Taifa katika wilaya 120 kati ya wilaya 139, hii ni 86%. Sasa ninashauri hizi wilaya 19 ambazo zimesalia nazo zikamilishwe. Hii itasaidia katika kuongeza utekelezaji wa shughuli za Serikali za kidigitali na kuongeza mawasiliano inavyotakiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninachukua pia, nafasi hii kuipongeza Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan na Hotuba ya Waziri Mkuu leo, hasa kwa kuendelea kujenga utekelezaji wa Sera ya Elimu ya Mwaka 2004, Toleo la 2023, ambapo mambo ya msingi yaliyoko mle ni pamoja na kuwapatia watoto wa kike elimu ya sayansi, teknolojia na ubunifu. Pia, lengo ni kuhakikisha kwamba, elimu ya amali inatolewa, lakini unaona shule 26 za wasichana zimejengwa kwenye kila mkoa na tayari shule saba zinajengwa, kwa ajili ya wavulana, lakini shule 103 za amali zimejengwa na kati ya hizo 29 ni zile za amali za ufundi na nyingine 74 siyo za ufundi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumesikia pia, shule 158 zinatekeleza mkondo wa amali. Sasa ushauri wangu hapa ni kwamba, tujitahidi kuhakikisha kwamba, tunakamilisha majengo yale yanayohitajika pamoja na kuajiri walimu wa masuala haya ya amali, pamoja na kununua vifaa vya kufundishia na kujifunzia, ili angalau mambo yaweze kwenda vizuri kwa sababu, hiyo ndiyo itakayokuwa njia pekee ya kusaidia kuhakikisha kwamba, ajira zinapatikana.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaipongeza pia, Serikali kwa kujenga VETA 64 ambazo zitasababisha kila wilaya iwe na VETA na ile moja ya Mkoa wa Songwe. Cha muhimu hapa ninachoshauri ni kwamba, tuongeze upatikanaji wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia. Pia, tuongeze kasi katika kuajiri Watumishi, ili angalau masuala ya amali vocational yaweze kufundishwa kwenye halmashauri zetu. Sasa tunazo VETA katika kila Wilaya, lakini ifikie mahali kwa sababu, tunayo VETA kila mkoa sasa twende kwenye VETA kila halmashauri, ili kila halmashauri iwe na mambo ya ufundi wanayofundisha kutokana na mazingira halisi ya huko.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninapenda pia, kushauri kwamba, tuwekeze sana katika ajira za walimu wa sayansi na mambo ya hisabati. Tujenge lab kwenye hizi shule zetu za sekondari ambazo zimejengwa maana kuna juhudi kubwa sana ya ujenzi wa madarasa na maabara, hivyo vitu vikikamilika vitasaidia sana kuhakikisha kwamba, elimu inayotolewa ni ile ambayo itasababisha tuweze kufikia malengo ambayo tunayataka.

Mheshimiwa Naibu Spika, tukumbuke kwamba, kuna campus 14 zimejengwa katika mikoa yote kwa hiyo, Tanzania kwa sasa, mikoa yote, inakwenda kuwa na campus za vyuo vikuu. Nadhani ni wakati muafaka wa kutumia hizi campuses kuhakikisha kwamba, zinatoa fursa za kufundisha masomo haya ya innovations kwenye maeneo yetu ya Mikoa, ili kuweza kuhakikisha kwamba, watu wanapata ujuzi wa kuweza kujiajiri wao wenyewe, ili tuweze kuhakikisha tunapunguza tatizo la ajira.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninapenda kuchukua nafasi hii pia, kuipongeza Serikali kwa kuhakikisha kwamba, katika kipindi cha mpaka Februari, 2026 zaidi ya shilingi bilioni 43.5 zimetolewa, kwa ajili ya kaya maskini. Pia, mikopo imetolewa kwa wanafunzi 3,179 wanaotoka katika kaya maskini na wanasoma katika vyuo vyetu; hilo ni jambo la kuipongeza Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ninashauri, kupitia TASAF, kama mnavyojua, malengo ya Mheshimiwa Rais sasa hivi ni kuhakikisha kwamba, Bima ya Afya kwa Wote inatumika. Sasa hili suala limeanza kutekelezwa, lakini linasimamiwa sana na Wizara ya Afya. Hivi karibuni walikuwa wanafanya ubainishaji wa kaya maskini ambazo zitanufaika na hili suala la Bima ya Afya kwa Wote, wanaokwenda ni watu wa NHIF, wakifika kule wanashirikiana na wale waratibu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninashauri kwamba, kwa sababu, zaidi ya 80% ya Watanzania wanatibiwa katika huduma ya afya ngazi za msingi, hapohapo ni TAMISEMI, nadhani ni vizuri tukaboresha ubainishaji wa wahusika watakaopata hii Bima ya Afya kwa Wote kwa kushirikiana na Watendaji na Wenyeviti wa Vijiji. Kwa maana nyingine ni kwamba, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI ishirikiane kwa karibu sana na Wizara ya Afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kwenye suala la mikopo nadhani 10% hii, tunaishukuru tena Serikali kwa kuleta zile kanuni, imeboresha kanuni. Tunadhani ifike mahali fulani majiji nayo ya-graduate kusudi zile fedha ambazo wanapeleka kwenye vikundi wapeleke chache, nyingine wapeleke kwenye miradi ya maendeleo, ili Serikali iweze kuwa na uwezo wa kupeleka fedha kwenye halmashauri ambazo ni za hali ya chini. Huo nao ni ushauri ambao ninajaribu kuutoa.

Mheshimiwa Naibu Spika, masuala ya fedha za mikopo ya madeni ya watumishi. Hapa napo tumeona kwamba, bado watumishi wengi sana wa halmashauri, Mamlaka za Serikali za Mitaa wanadai fedha. Kwa hiyo, tunashauri hapa Serikali, kwa kushirikiana na Mamlaka za Serikali za Mitaa, wajitahidi sana kadri inavyowezekana kutathmini haya madeni na kuyalipa kwa kadri inavyowezekana kwa haraka iwezekanavyo kwa sababu, tumeona hiyo ni changamoto ambayo ni kubwa kwa kweli.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu matundu ya vyoo; ninadhani vilevile hii moja kwa ishirini na tano kwa wavulana na moja kwa ishirini kwa wasichana iangaliwe kati ya Wizara ya Elimu na Wizara ya TAMISEMI kusudi tuwe na uhalisia. Hii itasaidia kupunguza gharama hizi au kuonekana kwamba, tunadaiwa matundu mengi sana kumbe hali halisi ya Watanzania ni, labda tundu moja wanaweza wakatumia wanafunzi 30 au 40.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile madarasa; ifikie mahali hii one to forty nadhani bado ni requirement ya hali ya juu sana. Tuangalie, hiyo nayo itasaidia kupunguza upungufu mkubwa ambao unaonekana upo wa madarasa. Kwa hiyo, ninapenda kuchangia hayo na pia, kwa sababu tuna changamoto ya walimu kwenye masuala haya ya amali, ninaishauri Serikali iweze kuajiri watumishi zaidi na ikiwezekana waende kwenye Nchi za Ulaya Mashariki kupata walimu ambao watakuja kusaidia kufundisha kwenye masomo haya ya sayansi, teknolojia pamoja na amali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu masuala ya afya, hotuba inaonesha kwamba tutawekeza zaidi katika maboma ya zahanati, lakini zaidi ya akinamama waliofanyiwa upasuaji wanapojifungua, 75% wamejifungua kwa wamefanyiwa upasuaji katika vituo vya afya. Kwa hiyo, ninashauri kwamba bajeti hii tuwekeze sana katika ujenzi wa vituo vya afya badala ya kukamilisha maboma ya zahanati.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kuwasilisha. (Makofi)