Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Benjamin Lukubha Ngayiwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kahama Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. BENJAMIN L. NGAYIWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana kwa kunipatia nafasi kuwa mchangiaji wa pili kwenye Hotuba hii nzuri ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Ninampongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi nzuri, tumemwona anazunguka katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu na kwa kweli, amesaidia sana kurudisha tabasamu kwa wananchi wetu. Hongera sana Mheshimiwa Waziri Mkuu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninawapongeza pia, Mawaziri wote waliowasilisha leo na Wenyeviti wote wa Kamati ambazo ziko chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Kipekee zaidi ninamshukuru Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuwa mtulivu na focused kwenye ile mipango yake ya miaka mitano kuhakikisha kwamba, wananchi wetu wanaenda kupata maendeleo kama ambavyo tumeweza kujipangia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninapenda kupita katika eneo la TARURA kwa udharura na umuhimu wake. Mheshimiwa Rais wakati anafungua Bunge letu alieleza kwamba, anaenda kuongeza bajeti. Tumesikia pia, katika Hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kwamba, Serikali inaenda kuongeza bajeti, sasa ninaendelea kusisitiza na kuiomba Serikali kwamba, bajeti hizi zielekezwe upande wa TARURA, ili waweze kukidhi na kutekeleza ile miradi yote ya maendeleo ambayo ipo huko imekwama kwa muda mrefu kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninapenda pia, kutoa maoni hapo kama ambavyo tumeweza kujadili katika Kamati yetu ya TAMISEMI kwamba, tumeshuhudia kila mwaka wa fedha, Serikali imekuwa inatenga fedha, kwa ajili ya kukarabati na kutengeneza barabara hizo kila mwaka. Unakuta ndani ya miaka mitatu, miaka minne, barabara moja imetumia shilingi milioni mia wakati mwingine zaidi ya shilingi milioni mia moja, lakini mwaka unaofuata unakuta barabara hiyo bado ni mbovu na haipitiki.

Mheshimiwa Naibu Spika, tukashauri kwamba, kama ambavyo tumekuwa tunatenga fedha za 10% za mikopo, halmashauri hizi zetu pia, zielekezwe kutenga kiasi cha fedha, kwa ajili ya kuhudumia hizi barabara, kuzijenga na kuzikarabati, ili ziwe imara na ziweze kupitika msimu mzima wa kiangazi na msimu wa mvua. Pia, hapa kama inawezekana itungwe sera, ili kuziwezesha hizi halmashauri zikope fedha, kwa ajili ya kuzipeleka katika hii sekta ya miundombinu; tutajikuta kwamba, tunapunguza gharama ya kutengeneza barabara hizi kila mwaka kwa kukopa hizo fedha, tunapata wakandarasi wanatengeneza hizi barabara kwa uimara kwa kuweka mifereji na barabara zetu zikawa nzuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukifika pale Jimboni kwangu Kahama, Jimbo ni zuri sana, Mji wa Kahama ni mzuri sana, lakini changamoto ya barabara inaweza ikakufanya utamani kuondoka kesho yake kwa hiyo, hali iko hivi katika maeneo mengi. Pale Kahama tuna mtandao wa barabara karibu kilometa 923, hizi ziko chini ya TARURA, lakini lami tunayo kilometa 14 tu. Kuna halmashauri zingine zina kilomita saba, mbili kwa hiyo, kwa kweli, TARURA tuiongezee uwezo wa kuangalia uwezekano wa kuweza kuzifanya halmashauri zetu zikope, ziweze kuzielekeza katika maeneo haya au ziweze kutenga 10% nyingine, kwa ajili ya kuhudumia barabara zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, najielekeza pia, katika 10% ya mikopo kule kwenye Local Government. Kama alivyotangulia kusema mchangiaji aliyepita, Mheshimiwa Wambura Chege hapa, zile idara zetu za maendeleo ya jamii kwa kweli, inabidi waongeze uwezo na wapite kuelimisha vikundi hivi vya vijana, vikundi vya akinamama na watu wenye ulemavu, ili waweze kukopa na kuweza kurejesha ile mikopo kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati tunapitia taarifa kutoka mikoa mbalimbali tumeona tangu Juni, 2024 mpaka Februari, 2026 halmashauri imekopesha fedha nyingi sana, lakini vilevile fedha hizo nyingi hazijarejeshwa. Hii ni kwa sababu gani? Inaonyesha kwamba, ama vikundi hivi na watu hawa waliokopa hawajapata elimu nzuri ya kwenda kutumia hizi fedha ili warejeshe au ufuatiliaji wa madeni haya, ili waweze kukopesha tena hauendi vizuri. Sasa tulikuwa tunajiuliza, tutaendelea kutenga hizi fedha mpaka lini?

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ina nia njema ya kukopesha watu wetu, wananchi wetu wafanye biashara, waweze kuinua vipato vyao, lakini fedha zinazodaiwa ni nyingi sana. Pia, fedha nyingi zinazotengwa wakati mwingine unakuta hazikopeshwi, zinakaa benki wakati watu wetu kule wanalalamika; vikundi viko safi vinatimiza masharti, lakini havikopesheki, havikopeshwi fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba sana hilo eneo twende tukaliboreshe, elimu itolewe na watu waweze kukopesheka. Wakati mwingine tukawa tunatamani hata wasikopeshwe fedha labda, wakopeshwe vitu vya kwenda kufanyia ile biashara; kama mtu anataka kwenda kufanya biashara ya kutotolesha mayai anunuliwe mashine ya kutotolesha mayai na aweze kuendelea kuliko kupewa fedha ambazo wakati mwingine anaishia kuzitumia katika matumizi mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninamalizia eneo la bakaa. Tumeona halmashauri nyingi zimekuwa zinavuka na bakaa nyingi sana na kisingizio chake wakati mwingine watu wanasema mtandao au huu mfumo wetu wa NeSTS. Kwa kweli, NeSTS pamoja na mazuri yake mengi na ninaunga mkono kwamba, hali ilivyokuwa hapo nyuma na kwa sasa tulivyo na huu Mfumo wa NeSTS unahitaji kuboreshwa tu, ni mfumo mzuri unaotakiwa kuboreshwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaweza nikakwambia baada ya ziara yetu ya Kamati ya TAMISEMI tumeweza kushuhudia kwamba, mkandarasi mmoja anapewa miradi zaidi ya saba kwenye mkoa mmoja. Wakati mwingine kwenye nchi nzima ukifuatilia ana barabara kilometa tatu Geita, ana barabara kilometa saba Kahama, ana barabara kilometa nne Songea. Sasa ukiangalia katika kutengeneza barabara inahitaji mobilization ya mitambo, upeleke kule wataalam, upeleke capital, sasa unakuta wakati mwingine mashine hizi na mitambo inakuwa ni michache. Kwa hiyo, unakuta huyu mkandarasi anagusa kidogo Mradi wa Songea, anagusa kidogo Mradi wa Geita, anagusa kidogo Mradi wa Kahama na yote haikamiliki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunapendekeza pale kwenye NeSTS, ule mfumo uweze kuwekwa vizuri. Kwamba, uweze kuwezesha hii miradi midogomidogo ya kilometa mbili, kilometa tatu, wachukuliwe wakandarasi wa eneo husika waweze kufanya hiyo kazi kwa umahiri na kwa muda, ndani ya muda ambao unatarajiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hizi bakaa pia, tunaomba Serikali iweze kupeleka hizi fedha timely. Halmashauri nyingi zinapokea fedha baada ya nusu ya mwaka kupita, sasa wakianza kutangaza tender; kwa mfano, tuliona Mkoa wa Lindi kule unakuta mkandarasi ameomba tender, anaenda mpaka site, halafu akifika anaona ile kazi haimlipi ana-withdraw, halmashauri inaamua kutangaza upya, inatangaza mpaka mara tatu. Kwa hiyo, tuangalie pia, hii michakato ya ku-award tender tusiende tu kwa ku-award hawa wanao-tender, kwa wale low bidder wanaotenda kwa chini halafu na hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mfano, huwezi kumpa mtu a-supply apple kwa shilingi mia mbili wakati linauzwa shilingi mia tano na wewe unampa huyo kazi, unajua kabisa atafeli. Kwa hiyo, tuangalie kabisa tathimini ifanyike vizuri hata mtu anayepewa hiyo tender tunajua kabisa anaenda kufanikisha hiyo kazi na kuifanya kwa umahiri mkubwa. Ninakushukuru sana na ninaomba niunge hoja mkono. Ahsante sana. (Makofi)